The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto

Hii ni muhimu kwani ukuaji wa kimwili na kiakili wa mtoto unaathiriwa na afya ya akili ya mama.

subscribe to our newsletter!

Mjadala uliofanyika Machi 3, 2023, katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) kuhusu afya ya akili baada ya kujifungua, umenikumbusha mbali. 

Siku moja napita pita katika wodi ya watoto wachanga nawahimiza akina mama kunyonyesha watoto, mama mmoja aliniita, “Dokta, ukimaliza njoo.”

Nilipoenda akamchukua mwanaye akanikabidhi mkononi akasema, “Shoga yangu, hebu niangalizie mwanangu, maana mimi sijielewi.” 

Nikamuuliza anajiskiaje, nikidhani labda ana shida ya mwili ili tuwaite watu wa wodi ya akina mama waje kumhudumia. 

Akasema, “Yaani, nikimbeba hivi mtoto kumpa maziwa, kuna sauti zinaniambia kabisa nimnyonge. Yani nawaza nimzibe pumzi afe. Sasa mimi sitaki kumdhuru mwanangu, naomba unilelee tu.” 

SOMA ZAIDI: Afya Moja Ni Nini Na Kwa Nini Ujali Kuhusu Ufanisi Wake?

Unajua hivi vitu ukivisoma kwenye vitabu vinaonekana kama utani fulani hivi hadi siku unakutana navyo. 

Baada ya yule mama kuniambia hivyo, nikawasiliana na mtu anayehusika, tukatoa taarifa kwa kitengo cha magonjwa ya akili, tukampeleka akapata msaada. 

Baada ya muda yule mama akaruhusiwa na mpaka muda huu naandika haya mwanaye yupo vizuri kabisa, hana shida, huku akiendelea kuhudhuria kliniki.

Siyo kesi ya kipekee

Hata hivyo, huyu siyo mwanamke pekee aliyepitia hali hii, au inayofanana na hiyo. Kuna wengine wanawachukia kabisa watoto wao na hawataki hata kuwagusa. 

Magonjwa ya akili kwa akina mama waliojifungua ni hatari sana kwani yanahatarisha afya yake na ya mtoto pia. 

Juzi hapa huko nchini Marekani, kulikuwa na yule mama aliyewanyonga watoto wake watatu. Ni vile alikosa huduma za afya ya akili. Pengine kama huduma hiyo ingepatikana, tukio hilo lisingetokea.

Lakini pia kuna yule mama aliyewazamisha watoto wake watano kwenye maji bafuni kwa sababu alikuwa anasikia sauti zinamwambia afanye hivyo na alishatafuta msaada akakataliwa. 

Kwanza, suala hili linatukumbusha umuhimu wa kujifungulia hospitalini lakini pia umuhimu wa kuongeza juhudi za huduma za kliniki baada ya kujifungua. 

SOMA ZAIDI: Walazimika Kujifungulia Nyumbani Baada ya Kituo cha Afya Kukosa Wahudumu

Mama pia apewe kipaumbele

Kuna video moja kwenye mtandao wa Tik-Tok wanaonyesha ukiwa mjamzito namna unavyojaliwa na ukishajifungua macho yote yanaelekezwa kwa mtoto. 

Mara nyingi utaulizwa maziwa yanatoka, mtoto anashiba, kidonda kimepona, bado unatokwa uchafu na vitu kama hivyo. 

Tena, kiukweli, sehemu nyingine wataulizia masuala ya mtoto tu; wewe mzazi labda utaulizwa uzazi wa mpango. 

Pili, unyanyapaa unaokuja na masuala ya afya ya akili. Mara nyingi mawazo ya kujiua au kumuua mtoto wamama hawa hawasemi kwa sababu hebu pata picha unamwambia, kwa mfano, baba watoto au mama yako kitu kama hicho? 

Cha kwanza, utaambiwa una mapepo kama siyo umepandisha majini! Jamii yetu bado haina elimu ya kutosha kuhusu haya mambo. Utaambiwa wewe ni mchawi kabisa. 

Lakini pia uwaambie huna raha, yaani hutaki hata kumgusa mwanao, utaambiwa huna shukrani, kwamba mtoto ni baraka. Utaambiwa wewe siyo mama bora na maneno mengi kama hayo.

Kwa hiyo, mtu anajua kabisa nikisema vile nitaishia kuonekana mbaya. Kwa hiyo, anaamua kumezea tu na mwisho inakuwa balaa. Inasikitisha. Inasikitisha mno. 

Hali hii inaweza kumkuta mtu hata kama anapokea msaada mkubwa kiasi gani kutoka kwa mwenza na familia yake. Naamini MEWATA wamefungua njia ya mjadala muhimu sana. 

Huduma za afya ya akili ziingizwe kwenye huduma za mama na mtoto. Maana, ukuaji wa kimwili na kiakili wa mtoto unaathiriwa na afya ya akili ya mama kwani mara nyingi yeye ndiyo mlezi mkuu wa mtoto. 

Saa nyingine unakuta mtoto mchanga lakini mama anamfokea na hata wakati mwingine anapiga kidogo aue. Wakati mwingine shida ipo kwenye akili. 

Naamini matokeo ya mjadala huu yataleta mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za mama na mtoto.

Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya afya ya umma. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kuduzekudu@gmail.com au kupitia Twitter kama @Kudu_ze_Kudu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi. 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts