The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Mtaalamu Aeleza Kila Kitu Unachopaswa Kujua Kuhusu Saratani ya Shingo ya Kizazi

Ni ugonjwa ambao huwaathiri zaidi akina mama walio na umri wa miaka 30 na kuendelea, daktari asema unatibika.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Wito umetolewa kwa akina mama, hususan wale walio na umri wa miaka 30 na kuendelea, kuhudhuria vituo vya afya mara kwa mara kwa lengo la kupima afya zao, hali ambayo imetajwa kuweza kuwakinga na ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.

Wito huo umetolewa na Dk Johnson Katanga, daktari kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alipokuwa akizungumza na The Chanzo kwenye mahojiano maalumu yaliyofanyika ofisini kwake hapo Machi 17, 2023.

Kwenye mahojiano hayo, Dk Katanga alisema ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi unatibika, akibainisha kwamba kitu muhimu ni kuugundua mapema kabla haujawa sugu kwenye mwili wa mtu.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa Dk Katanga anaanza kwa kuelezea ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ni nini haswa:

Dk Johnson Katanga: Kuhusiana na saratani ya shingo ya kizazi, labda kwa kifupi naomba niwafahamishe watu kwamba shingo ya kizazi ni kitu gani, pengine wakipata hiyo picha itaweza kurahisisha kujua saratani ya shingo ya kizazi ni nini. 

Shingo ya kizazi ni kiungo ambacho kinapatikana katika mwili wa mwanamke na inapatikana katika mfumo wa uzazi wa mwanamke, ambapo kwenye ule mji wa mimba–kuna mji wa mimba ambapo ndipo mtoto anakaa halafu kuna ile sehemu ya mji wa mimba inakua kama kashingo inachungulia kwenye uke ambapo ndipo mtoto anakuwa anatokea. 

Ndiyo maana wengine wanaita ni mlango, wengine wanaita shingo, kutokana na jinsi ilivyo. Kwa hiyo, hicho kiungo kama kikitokea kikipata saratani ndiyo inakuwa inaitwa saratani ya shingo ya kizazi au hata ukisikia watu wanasema saratani ya mlango kizazi na yenyewe pia usishtuke, wanakuwa wanazungumzia kitu hicho hicho kimoja.

Sasa, saratani tunasema zinakuwa ni chembechembe hai za miili yetu lakini zinakuwa zinahasi, au zinakuwa hazifuati ule utaratibu kama chembechembe hai nyingine za mwili zinavokuwa zilivyo. Kwa hiyo, zenyewe zinakuwa bila ya kufuata mpangilio wa mwili, zinatengeneza uvimbe na zinakuwa haziwezi kudhibitiwa na mfumo wa kawaida wa kimwili. 

Kwa hiyo, ikitokea hii hali ya hizo chembechembe zikahasi na zikaanza kuishi maisha yake yenyewe bila ya kufuata mfumo wa kawaida wa kimwili tunasema huo uvimbe unakuwa ni saratani. Kwa hiyo, ikitokea hiyo hali kwenye shingo ya kizazi hiyo inakuwa ndiyo saratani ya shingo ya kizazi.

The Chanzo: Ni nani sasa yupo hatarini kupata ugonjwa huu?

Dk Johnson Katanga: Kiujumla, tukiangalia kimaumbile, hii shingo ya kizazi inapatikana kwa mwanamke pekee, kwa mwanamke peke yake kama vile tunavyosikia tezi dume lipo kwa mwanaume, lakini kwa mwanamke halipo. 

Kwa hiyo, mtu namba moja ambaye yupo katika hatari ya kupata haya maradhi ni mwanamke. Na zaidi tunaangalia umri kuanzia miaka 30 na kuendelea yupo kwenye hatari zaidi. Ingawa kutokana na kadri unavyozidi kufanya kazi katika hii taaluma ya mambo ya saratani tumekuwa tukishuhudia kwamba hata mabinti wenye miaka 20 au chini ya hapo wanapata hili tatizo la saratani ya shingo ya kizazi. 

Lakini watu wanaoishi na maradhi, au niseme maambukizi ya virusi vya UKIMWI, wameonesha wapo kwenye hatari kubwa zaidi ukilinganisha na akina mama au watu ambao hawana haya maradhi. 

Na hii imefikia hatua mpaka wanaita saratani ya shingo ya kizazi imekuwa ni AIDs-defined cancer, yaani kwamba kwa kiasi kikubwa mtu mwenye saratani ya shingo ya kizazi, walio wengi, wanakuwa wameathirika pia na VVU. Kwa hiyo, utakuja kukuta hata tukiwa katika matibabu yetu, au tukiwa tunamhudumia mtu wa namna hii, ni lazima pia tumuulize hali yake ya VVU ikoje.

The Chanzo: Mwanamke anaweza kuepuka vipi?

Dk Johnson Katanga: Saratani ya shingo ya kizazi, naomba nikiri kwa sasa kwa Tanzania, na siyo Tanzania tu peke yake, karibia nchi nyingi zenye uwezo wa chini, au wanasema zenye uwezo wa chini na uwezo wa kati, au uchumi wa chini na uwezo wa kati wanapenda kuita, ni saratani ambayo ninaweza nikasema inaongoza kwa kuathiri kinamama sana tu. 

Lakini jambo zuri na la kupendeza na la kufurahisha ni kwamba saratani hii ni miongoni mwa saratani ambazo zina tibika kirahisi sana na zaidi ya hapo unaweza ukajikinga kirahisi sana kama hatua zitachukuliwa kwa wakati.

Cha kwanza kabisa katika kumkinga huyu mwanamama kuhusiana na hili suala la saratani ni pamoja na, kama tunavyofanya hapa tunavyozungumza kwa ajili ya kutoa uelewa, kwamba uelewa wa kila mtu, uelewa wa wababa, waweze kuwaelewesha wamama na uelewa wa mabinti wenyewe kuhusiana na hii saratani ya shingo ya kizazi. 

Uelewa wa ujumla na wenyewe ni wa muhimu sana, sana kuweza kuelewa kwa maana utajua unaambukizwaje, utajua unaweza kufanyaje ukajikinga. Kwa hiyo, watu wakiona vijarida tofauti tofauti, wakisikia habari zinatangazwa za saratani ya shingo ya kizazi, naomba waweze kusikia na ule ujumbe utakaotolewa pale waweze kuufanyia kazi.

Lakini pia kingine kuna ule uchunguzi wa afya kwa kina mama wa awali wa hiyo saratani ya mlango wa kizazi. Tunashukuru nchi yetu, au Serikali yetu, karibu vituo vingi sana vya afya hapa Tanzania wana hii huduma ya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi. 

Na lengo lake ni nini kufanya huo uchunguzi? Kwa sababu saratani haiji ghafla kama vile unavyoona maralia, kwamba umeumwa na mbu leo kesho tayari una nini, hapana. Huwa inakuja taratibu, na inachukua muda ili kuweza kutokea. 

Sasa hapa katikati kabla haijawa saratani kunakuwa kuna mabadiliko fulani yanakuwa yanatokea kwenye shingo ya kizazi, tunaita mabadiliko ya awali, kwamba zile chembechembe kabla hazijaenda kuwa katika zile chembe zinazoasi kuna mabadiliko ambazo zinakuwa zinapitia. 

Sasa ukienda kwenye uchunguzi wa, tunaita uchunguzi wa awali wa saratani, kazi yetu kubwa, au kazi yake kubwa ule uchunguzi, ni kuweza kubaini hivi viashiria vya awali, na vikibainika vinatibiwa. Kwa hiyo, ina maana vikitibiwa unakuwa tayari haupo kwenye ile hatari ya kuweza kupata haya maradhi ya saratani. 

Hii pia inasaidia hata kama kuna shida utaweza kuikuta katika hali ya mwanzo kabisa. Kwa hiyo, hilo suala zima la uchunguzi ni muhimu sana sana, naomba niwasisitize katika hilo ni la muhimu sana.

Na kingine pia tumesikia kuna njia mbalimbali zinafanywa ikiwemo juhudi za Serikali za kutoa chanjo ya ‘HPV’ ambayo HPV ni kirusi ambacho kwa asilimia kubwa kinahusika katika kusababisha zile chembechembe za kwenye shingo ya kizazi zibadilike na kuweza kuwa saratani. 

Kwa hiyo, ukipata na hii chanjo inakuwa umefanya namna moja ya kujikinga na hii saratani. Ila zaidi ya hapo ni kuishi vizuri kwa maana mfumo mzuri wa maisha, ikiwemo kufanya mazoezi, kula vizuri, na yenyewe ina nafasi yake pia katika kuzuia hii saratani ya shingo ya kizazi.

The Chanzo: Ni vitu gani vinaweza kusababisha ugonjwa huu?

Dk Johnson Katanga: Kwa kifupi, kama nilivyosema hapo mwanzo, kwamba saratani ya shingo ya kizazi inatokea pale chembechembe za shingo ya kizazi zinapobadilika na kuwa zikahasi. 

Sasa kuna vitu, au tunasema vihatarishi, au vile vitu ambavyo vikiwepo vinakuwa vinachochea ile hali ya zile chembechembe zibadilike na kuwa saratani. Kwa hiyo, tutakavyoviongelea hapa siyo kwamba chenyewe ni moja kwa moja kinaenda kusababisha, hapana, ila vyenyewe vinaenda kuchangia, au kuamsha, ile hali ya zile chembechembe kubadilika na kuwa saratani. 

Karibia asilimia 99 ya wamama wote wenye saratani ya shingo ya kizazi wameonekana pia wana maambukizi ya virusi vya ‘Papilloma’ ambapo kitaalamu tunaita ni ‘Human Papillomavirus.’ 

Hiki kirusi sifa yake kubwa kinaambukizwa kwa njia ya kujamiiana au kitaalamu tunasema ni ‘sexual-transmitted disease’ au ‘sexual-transmitted infection.’ Lakini naomba niwaeleze jambo moja kinamama ili kuwapunguzia hofu au kuwaondolea hofu. 

Wanawake wengi wanapata haya marazi au haya maambukizi ya HPV ila kwa bahati nzuri asilimia kubwa, 60 mpaka 80, wana uwezo wa kuyaondoa haya maradhi kupitia kinga zao za mwili ndani ya miezi sita mpaka mwaka, unakuta mtu kashaondoa hayo maambukizi. 

Kwa hiyo, ili upate haya maambukizi lazima kuwe na ‘persistent infection,’ yaani kwamba, mwili wako wewe mwanamama ushindwe kumuondoa, au kuondoa yale maambukizi. 

Kwa hiyo, unakufanya yale maambukizi yakae pale kwa muda mrefu. Na maambukizi yakikaa pale kwa muda mrefu ndiyo yanasababisha sasa zile chembechembe zako zianze kufanya yale mabadiliko na kuwa saratani.

Kwa hiyo, ni wanawake wengi wanapata hayo maambukizi lakini pia kama tunavyosema walio wengi pia wanaweza kuondoa ni wachache wanaoshindwa ndiyo maana wanapata hiyo hali ya kuweza kupata hiyo saratani kupata hiyo maambukizi endelevu kisha kupata hiyo saratani. 

Kwa hiyo, sasa hapo ndipo ule mchango wa chanjo ile ambayo imeletwa na Serikali, ya HPV, unapoingia. Kwamba ukipata ile chanjo mwili wako unaongezewa uwezo wa kuweza kupambana na hivi virusi ambavyo vimeonekana kwa asilimia kubwa ndivyo vinasababisha hili tatizo.

Kingine kuhusiana na hiki kirusi kama nilivyosema ni ‘sexual transmitted’ kwanza, kabla sijaenda huko kwa maana tumeona kwamba ili upate lazima uwe na hii ‘persistent infection,’ kwamba mwili wako ushindwe kuondoa hiki kirusi hapo pia ndipo linapokuja kuingia suala la wale wanaoishi na virusi vya HIV. 

Tunajua virusi vya HIV sana kwa wale ambao hawazingatii kumeza dawa vizuri kinga kidogo inakuwa imeshuka. Kwa hiyo, kinga kidogo inakuwa imeshuka, ikishuka ina maana unapunguza ule uwezo wa kuweza kukiondoa hichi kirusi. 

Huo uwezo ukipungua kile kirusi kinapata fursa ya kukaa pale kwa muda mrefu ndiyo tunaita ‘persistent infection,’ unakuwa unapata hiyo, unapata hayo mabadiliko ambayo yanaweza kuwa saratani ya shingo ya kizazi.

Kwa maana nyingine sasa hiki kirusi cha HPV kinaenezwa kwa njia ya kujamiiana, kwa hiyo zile tabia zote ambazo zinaendana na mambo ya kujamiiana ambayo siyo salama kiujumla wake pia ni vihatarishi vya saratani ya shingo ya kizazi. 

Kwa maana kuwa na wapenzi wengi, au ukipata maradhi ya ukeni ya mara kwa mara, ukipata HIV, yaani tabia zote ambazo zinahusiana na mambo ya kujamiiana ikiwa siyo salama inasababisha hiyo hatari ya kupata hii saratani. 

Vitu vingine ni pamoja na kurithi na hii kurithi siyo moja kwa moja unarithi saratani lakini kama wazazi wako wakiwa wamepata haya maradhi ina maana na wewe kuna uwezekano umerirhi chembechembe ambazo ni rahisi kubadilika kuwa saratani. 

Kwa hiyo, ukipata hivi vihatarishi ukikaa navyo kwa muda unaona chembechembe zako zinabadilika zinakuwa saratani, zinakuwa na uwezo wa kubadilika kirahisi zaidi ukilinganisha na yule ambaye wazazi wake hawana haya matatizo. 

Zaidi ni hivyo. Vingine ni mfumo wa maisha usiyo mzuri, yaani ule mfumo siyo wa kiafya kama nilivyozungumza hapo awali, namna ya kula, namna ya kuishi, kufanya mazoezi, vitu vya namna hiyo.

The Chanzo: Huu ugonjwa upo kwa kiasi gani hapa Tanzania?

Dk Johnson Katanga: Kiujumla, kwa Tanzania, wanasema karibia asilimia 25 ya saratani zote ni hizi za shingo ya kizazi, hiyo ni kutokana na takwimu za Global Khan. Global Khan huu ni mfumo wa WHO ambao unakuwa unatoa hizo saratani. 

Kwa hiyo, kwa Ocean Road, huu ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi ndiyo unaongoza, unachukua karibia nusu ya wagonjwa wote tunaowapata wanaolazwa na hata wale wanaokuja kliniki kwa ajili ya kujiangalizia kwa Ocean Road. Kwa hiyo, ni tatizo kubwa kwa kweli ni tatizo kubwa sana.

The Chanzo: Matibabu yake yakoje, na ni ghali kiasi gani?

Dk Johnson Katanga: Kiujumla kwa saratani ya shingo ya kizazi, au matibabu ya saratani kiujumla, yanaendana na hatua, inategemeana na huo ugonjwa upo hatua gani. Ingawa, kwa bahati mbaya zaidi, wagonjwa wengi tunaowapata unakuta tayari unakuwa umeshasogea zaidi, unakuwa ni hatua kubwa. 

Kwa hiyo, matibabu yake kwa mionzi tiba na tiba kemia ambayo tunaita ‘chemotherapy’ ukichukua tu gharama za hiyo peke yake zinafika karibia Shilingi milioni tano peke yake, mpaka kumaliza ule mzunguko wote. 

Lakini tunashukuru Mungu kuna kitu tunaita kugawana gharama ambapo kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikiweka hapo pesa zake. Kwa hiyo, wale wanaokuja wasiokuwa na uwezo kuna namna wanaingizwa katika utaratibu wa kugawana gharama. 

Kwa hiyo, gharama zinakuwa zinashuka zaidi. Lakini gharama halisi ndiyo hiyo, wale wanaokuja kwa binafsi, au kwa bima inafika huko kote. Ila kwa wale wanaokuja kwa maana ya ‘cost-sharing,’ Kiswahili chake sijui nisemaje, yaani wale wanaokuja kwa rufaa ndiyo tunaita watu wa namna hiyo.

Kwa rufaa ina maana pengine umetoka hospitali ya chini, au umetoka hospitali ya mkoa fulani, umepewa barua ya kwamba nenda Ocean Road kwa ajili ya matibabu, wale kidogo inakuwa nafuu. 

Lakini kwa wale wanaokuja kama kwa pesa taslimu, au kama kwa binafsi mwenyewe ameona ngoja niende moja kwa moja Ocean Road niweze kuwahi gharama zake, ndizo zinaweza kufika mpaka huko Shilingi milioni tano, sita na kuendelea kutokana na ugharama wa zile dawa zenyewe. 

Kwa hiyo, utakuja kuona kwamba matibabu yake ni ghali zaidi ukilinganisha na mtu akiweza kuamua kufanya uchunguzi ili tatizo liweze kugundulika mapema na kuweza kujikinga na hili tatizo la saratani ya shingo ya kizazi.

The Chanzo: Ni maeneo gani ugonjwa huu umeshamiri zaidi hapa nchini?

Dk Johnson Katanga: Kwa tathmini yetu ilikuwa ikionesha Nyanda za Juu Kusini, hii tunaita ‘Southern Highland Zones,’ huku Mbeya, Iringa, walikuwa wanakuja kwa wingi. Pia, Kanda ya Ziwa walikuwa wanakuja kwa wingi ukilinganisha na maeneo mengine. 

Ila kwa sasa tunashukuru Mungu kwa sababu huko pia vimeanzishwa vituo Kanda ya Ziwa Bugando ipo inafanya vizuri, hata huku tunaona Mbeya Rufaa na yenyewe inajitahidi kuweza kuwagundua wale watu mapema na kuwaleta, Kanda ya Kaskazini pia kuna hospitali ya KCMC. 

Kwa hiyo, kwa sasa hivi tunashukuru Mungu walio wengi wanakuwa wanatibiwa kule lakini licha ya kwamba huko bado kuna kanda hizo za matibabu lakini inabidi pia waje wapatiwe huku kwetu.

The Chanzo: Ni hatua gani zimekuwa zikichukuliwa katika kupambana na huu ugonjwa?

Dk Johnson Katanga: Kiujumla, hata Serikali imeliona hili tatizo la saratani kiujumla wake hasa hii saratani ya shingo ya kizazi. Kwa hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuanzisha huduma ya uchunguzi katika vituo vya afya. 

Kwa sasa hii huduma ya uchunguzi inapatikana katika vituo vingi sana vya afya hata ukienda kwenye zahanati huko chini mikoani, wilayani humo ndani zipo hizi huduma za uchunguzi pia. 

Zipo wanachunguza kuweza kugundua vile viashiria vya awali na vikigundulika wanawatibu kama wanahitaji msaada wanawapa rufaa kwa ajili ya kuja sehemu za juu zaidi.

Pia, Ocean Road hata sisi tukiwa kama taasisi ya Serikali tumekuwa mstari wa mbele katika kulisimamia hili, tumekuwa tukitoa mafunzo katika hospitali mbalimbali za mkoa, tumekuwa tukienda hospitali za mkoa tunawachukua wale watoa huduma mbalimbali wa ule mkoa husika, au wa wilaya husika, tunawaweka pamoja, tunawafanyia kama mafunzo elekezi ya namna nzuri ya kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti na hata pia saratani ya tezi dume, tumekuwa tukiwaeleza hivyo vitu. 

Ambapo mwaka jana [2022] tulizunguka mikoa karibuni yote na mwaka huu pia tunaendelea tumeshaenda Tanga, tumeshaenda Arusha, na pia tunatarajia kwenda mikoa mingine yote kwa kadri itakavyowezekana kuweza kuanza kuhuisha ule uelewa wa hii saratani. 

Pia, kuboresha huduma ya wale wanaotoa huduma ya uchunguzi ya saratani ili watu waweze kupata huduma iliyostahiki na kuweza kupata na watu kuweza kugundulika haya matatizo katika hatua za awali.

Hadija Said ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dar es Salaam. Unaweza kumpata kupitia hadijasaid826@gmail.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *