Mtwara. Hatua ya Serikali kumfutia kesi Peter Gasaya, Mkurugenzi wa JATU PLC, kampuni inayojihusisha na kilimo, bila shaka itapokelewa kwa hisia tofauti na mamia ya Watanzania ambao wanaendelea kuugulia maumivu kufuatia pesa walizowekeza kwenye kampuni hiyo kutoweka katika mazingira yaliyojaa utata.
Mnamo Jumanne, Aprili 11, 2023, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) aliitaarifu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba hana nia ya kuendelea na kesi hiyo ambayo Gasaya alikuwa akishukiwa kujipatia Shilingi bilioni 5.1 kwa njia ya udanganyifu.
Kwenye kesi hiyo, Gasaya alikuwa anadaiwa kujipatia fedha hizo kutoka katika Saccos ya JATU kwa madai kuwa fedha hizo anazipanda ili kuzalisha faida zaidi, wakati akijua kuwa ni uongo, akidaiwa kutenda kosa hilo kati ya Januari 1, 2020, na Desemba 31, 2021 katika jiji la Dar es Salaam.
Gasaya, 32, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hapo Disemba 29, 2022, kujibu mashtaka yake hayo, na kusomewa shtaka lake na wakili wa Serikali Tumaini Mafuru, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mary Mrio.
Habari za kuachiwa kwake, hata hivyo, itapokelewa kwa masikitiko makubwa na wanawake wanaofanya biashara mbalimbali kwenye soko kuu lililopo Manispaa ya Mtwara Mikindani ambao waliieleza The Chanzo hivi karibuni namna walivyoathirika baada ya kuwekeza pesa zaidi ya Shilingi milioni nane kwenye kampuni ya JATU PLC.
Wanawake hao, kupitia kikundi chao kiitwacho ‘Sauti ya Mwanamke Sokoni,’ chenye wanachama 16, walikuwa wakiwekeza pesa zao kwenye kampuni hiyo kwa makubaliano ya kuwalimia mashamba na kisha kupata mazao ambayo wangeyauza kwa faida.
Katibu wa kikundi hicho, Zainabu Numbi, aliiambia The Chanzo mnamo Januari 30, 2023, kwamba kitendo hicho kimewarudisha nyuma sana kibiashara kutokana na kupoteza pesa zao walizokuwa wakizitegemea kwa ajili wa kuwainua kwa kuongeza mitaji kwenye biashara wanazaofanya.
SOMA ZAIDI: Nini Kinawasukuma Watanzania Kujiunga na Biashara ya Upatu Haramu?
Numbi alilalama pia kwamba kitendo hicho pia kimepelekea uhai wa kikundi chao, ambacho kilikuwa kikijiendesha kwa kukopeshana wenyewe kwa wenyewe, umekuwa mashakani kutokana na wanachama kukosa pesa za kuendesha kikundi baada ya pesa nyingi kuzipeleka JATU na kutorudi.
Tumeumia kupita kiasi
“Tumeumia kupita kiasi,” Numbi alisema kabla ya uamuzi wa leo wa Mahakama. “Biashara zenyewe za kuungua moto [mama ntilie]. Tunasema tujiwekeze na wao [JATU] walituambia sisi hii biashara ni ya kujikwamua sisi kama wafanyabiashara wadogo wadogo ili tutoke hatua moja kwenda hatua nyingine kibiashara. Lakini ndiyo wamezidi kutudidimiza.”
Wanakikundi hao walidai kwamba mwaka 2020 walikubaliana na kampuni ya JATU kulima mahindi ambapo mara baada ya kulipia gharama zote kama walivyoelekezwa na kampuni walilima hekari tano.
Baada ya kufika hatua ya mavuno, kikundi kilipojaribu kuuliza namna ya kupata marejesho ya pesa walizowekeza, waliambiwa na kiongozi wa kampuni kuwa kikundi chao hakionekani miongoni mwa watu ama vikundi vilivyolima kwa mwaka huo.
Akina mama hao wakaambiwa itabidi warudishiwe pesa zao kwa kukodiwa shamba jingine badala ya kupewa pesa taslimu. Baada ya kujadiliana kwa mara nyingine kama kikundi waliridhia kukodi shamba jingine la maharage lenye ukubwa wa heka nane, ambalo hata hivyo hawakulipata.
SOMA ZAIDI: Simulizi ya Kijana wa Mjini Aliyetaka Kupata Utajiri wa Haraka Kupitia Kilimo
“Tukakodi heka nane za shamba la maharage kwa kila heka moja tulilipia Shilingi 150, 000,” Numbi aliiambia The Chanzo. “[JATU] wakatuambia tununue hisa na kila heka moja ilikuwa na hisa hamsini, tukazinunua zote. Kwa hiyo, mpaka dakika hii tunavyoongea hapa tunaambiwa fedha hazipo na mashamba hayajulikani kama yapo au la. Kwa hiyo, sisi tumechanganyikiwa tu.”
The Chanzo ilijaribu kuifikia kampuni ya JATU ili ijibu tuhuma hizi. Hata hivyo, hatukufanikiwa kwani simu za wahusika zilikuwa hazipokelewi.
Sofia Hassan Kombo, mwanachama wa ‘Sauti ya Mwanamke Sokoni,’ anayejihusisha na kuuza mboga mboga, alidai kuwa kutokana na hasara aliyopata kwa kutapoteza pesa aliyowekeza JATU imempelekea kushindwa kuwalipia gharama za masomo watoto wake wawili.
Nitasomeshaje wanangu?
“Mwanangu alikuwa anasoma Chuo cha Utumishi wa Umma lakini nimeshindwa kumlipia ada, nimeona bora akasome VETA,” Sofia, mama wa watoto watano, alilamika. “Hata huko VETA sina uhakika kama nitamudu gharama za kumlipia kutokana na hali niliyokuwanayo sasa.”
Swahiba Rajabu, mwanachama mwengine wa ‘Sauti ya Mwanamke Sokoni,’ anayeuza miguu ya kuku sokoni hapo, aliiomba Serikali kuwasaidia warejeshe pesa zao.
“Kwa kweli tumeumia kuhusu JATU,” Swahiba alisema. “Maana wengine sisi ndiyo kama hivyo tunauza miguu ya kuku. Utumbo unaukamua, tunapata fangasi. Tunakutana na minyoo. Tukasema tujiwekeze JATU. Matokeo yake leo hii hakuna kinachoeleweka na pesa zetu zimechukuliwa.”
“Tunakuomba Mheshimiwa Rais Mama Samia [Suluhu Hassan], Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Waziri [mwenye dhamana] pamoja na Mkuu wa Wilaya na viongozi wote kwa ujumla, tunaomba mtusaidie kuhusu JATU [ili] tupate pesa zetu,” Swahiba aliomba.
Akina mama wa ‘Sauti ya Mwanamke Sokoni,’ ni kati ya wananchi kadhaa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ambao kwa siku nyingi sasa wamekuwa wakilalamikia kudhulumiwa na kampuni hiyo ya JATU, wakiitaka Serikali iingilie kati kukomesha vitendo hivyo.
Hakuna kilimo cha WhatsApp
Malalamiko haya yalimuibua Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ambaye ofisi yake iliyafanyia uchunguzi malalamiko hayo na kuahidi, hapo Agosti 16, 2022, kukabidhi ripoti ya matokeo kwa vyombo vya dola kwa ajili ya hatua nyingine stahiki, huku Bashe akiwataka wakulima kuwa makini wanapowekeza fedha zao.
SOMA ZAIDI: Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania
“Nasisitiza wanaotaka kuwekeza kwenye kilimo [wa]jiridhishe kwanza,” Bashe aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
“Pesa zako unakabidhi kwenye taasisi gani? Je, hayo maeneo wanayokuambia watakulimia umeyaona? Umeyatembelea? Je, halmashauri husika, ama Wizara ya Kilimo, inatambua hicho kitu? Kumekua na watu wengi wakija wizarani baada ya kupata athari ya kupoteza pesa zao.”
Bashe, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (Chama cha Mapinduzi – CCM), aliwatahadharisha Watanzania kwa kuwaambia kwamba hakuna kilimo cha kwenye mitandao ya kijamii, akiwataka wananchi waende shambani wao wenyewe.
“Usikubali hizi habari [za] lete Shilingi milioni 10, nikakulimie, utapata Shilingi milioni 15,” Bashe alitahadharisha. “Nasisitiza, hakuna kilimo cha WhatsApp. Nenda shambani mwenyewe.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.