The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Kilimo na Umasikini, Malaysia na Tanzania

Tofauti kubwa za kifikra na kimaendeleo zinaweza kuelezea kwa nini Malaysia imeushinda umasikini kupitia kilimo huku Tanzania ikikwama.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Februari 2017, miaka sita sasa imepita, niliandika, kupitia ukurusa wangu wa Facebook, makala haya kuelekea kuadhimisha miaka 50 ya Azimio la Arusha. Niliamua kurudi kuisoma makala hii tena kutokana na sababu mbili haswa. 

Moja, nilipokuwa katika ziara ya chama chetu cha ACT-Wazalendo, chama ninachokiongoza, katika mikoa nane ya Tanzania Bara, ziara ambayo imekamilika hivi karibuni, nilikutana na umasikini wa kutisha wa Watanzania. 

Kama kawaida yangu, niliwaeleza wananchi kwamba umasikini wa Tanzania unatokana na Serikali kutojali sekta ya kilimo. 

Nilipokuwa Tabora, kwa mfano, nilieleza hili kwa kina, kwamba sura ya umasikini wa Tanzania ni wakulima; kwamba sekta ya kilimo ni tegemezi kwa theluthi mbili ya Watanzania lakini mchango wake kwenye Pato la Taifa ni theluthi moja tu. 

Kwa hiyo, kipato kidogo kinagawiwa kwa watu wengi sana. Kisha nikapendekeza suala la kisera kuwa, kama ilivyo kwenye sekta ya madini, au mafuta na gesi, Serikali itunge Sheria ya Maendeleo ya Kilimo itakayoweka mfumo mahususi wa kodi kwa sekta yetu ya kilimo tu. 

Mfumo ambao utakuwa imara kwa muda mrefu ili kuvutia uwekezaji kwenye kilimo na kuhakikisha kuwa mkulima anapata angalau asilimia 80 ya bei ya bidhaa yake katika Soko la Dunia, kwa mazao ya biashara.

Mbili, Serikali ilikuwa inazindua rasmi mpango wa kuwachochea vijana kushiriki kwenye kilimo uitwao BBT-YAI. Mpango huu, pamoja na mambo mengine, una shabaha ya kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya kilimo mpaka kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. 

Shabaha hii ikifikiwa, na ikawa endelevu kwa miaka mitano mfululizo, tutafuta ufukara kabisa nchini kwetu. 

SOMA ZAIDI: Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

Ni muhimu kukumbuka kwamba tafiti zilizowahi kufanyika nchini zinaonesha kwamba iwapo sekta ya kilimo Tanzania itakuwa na kasi ya ukuaji wa kati ya asilimia sita mpaka asilimia nane kwa miaka mitatu mfululizo, asilimia 50 ya Watanzania wataondoka kwenye dimbwi la umasikini. Hali itakuwaje kasi ya ukuaji ikifika asilimia 10? 

Ni dhahiri itakuwa ni mafanikio makubwa na kwa mara ya kwanza tutaweza kusimama kifua mbele na kusema kuwa umasikini sasa basi. Hata hivyo, mashaka ni mengi sana. Mzee Jakaya Kikwete, Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, alipata kusema wasiwasi, au mashaka, ndiyo akili!

Kumekuwa na mipango kama hii hapa nchini katika miaka ya uhai wetu kama taifa. Nilitafakari kama tunapozindua mpango huu wa BBT-YAI tulijifunza kutokana na makosa ya nyuma yaliyopelekea mipango kama hii kushindwa. Ndipo nikakumbuka makala haya ya kulinganisha Tanzania na Malaysia miaka ya 1970-1990.

Nimeyasoma makala haya tena na tena na, kwa hakika, siwezi kubadili hata nukta. Ni makala natamani kila mtunga sera ayasome. Kuna mafunzo makubwa kutoka nchi ya Malaysia. Karibu usome makala haya na pia kunipatia mrejesho wako:

Wakati Tanganyika inapata uhuru mwaka 1961, nchi ya Malaya ilikuwa tayari ina uhuru miaka minne kabla, ikipata uhuru wake mwaka 1957. Malaya ilijiunga na Singapore, Sabah na Sarawak mnamo Septemba 16, 1963, kuunda nchi ya Malaysia.

SOMA ZAIDI: Serikali, Wadau Waeleza Mikakati ya Kuboresha Kilimo cha Mwani Zanzibar

Tanganyika ilijiunga na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania miezi saba baadaye. Hata hivyo, Singapore ilifukuzwa kutoka katika Muungano wa Malaysia hapo Agosti 1965 kutokana na kutofautiana kisera kuhusu watu wa asili na namna ya kuwalinda kiuchumi.

Viongozi wa Kuala Lumpur walitaka kuweka sera za kusaidia wazawa kwa kuwapa upendeleo maalumu, wakati viongozi wa Singapore, chini ya Lee Kuan Yew, walitaka kuwepo na Malaysia moja kwa wote bila upendeleo maalumu kwa Bumiputera, watu wa asili wa taifa hilo. 

Singapore ina wakazi wengi zaidi wahamiaji kutoka China, hivyo ilipinga wazo hilo na ikajitoa kwenye muungano. Tanzania imeendelea kudumu na muungano licha ya changamoto kadhaa zinazoukabili! Tanzania na Malaysia zote zilitawaliwa na Mwingereza. 

Wakati Tanzania inaundwa mwaka 1964, pato la wastani la mtu mmoja lilikuwa Dola za Kimarekani 63, sawa na Sh130,000, wakati Malaysia ilikuwa na pato la Dola za Kimarekani 113, sawa na Sh250,000. 

Kimsingi, nchi hizi zilikuwa sawa kimaendeleo ingawa Tanzania ni kubwa kwa zaidi ya mara tatu ya Malaysia.

SOMA ZAIDI: Parachichi Inavyokimbiza Kilimo cha Kahawa Mbozi

Hivi sasa [Februari 2017], Malaysia kipato cha wastani cha mwananchi ni Dola za Kimarekani 10,000, sawa na Shilingi milioni 22, na Tanzania ni Dola za Kimarekani 600, swa na Shilingi milioni 1.3. 

Kwa Tanzania, pato la wastani limeongezeka mara kumi takribani na kwa Malaysia limeongezeka mara elfu moja! Nini tofauti ya mikakati ya maendeleo ya nchi hizi mbili?

Kilimo kilivyoivusha Malaysia

Leo tutaangalia eneo moja tu, la kilimo, na namna kilimo kilivyoweza kuivusha nchi ya Malaysia na kilimo hicho hicho bado hakijaweza kuivusha Tanzania.

Malaysia iliunda Shirika la Umma linaloitwa Federal Land Development Authority (FELDA), likiwa na wajibu mmoja mkubwa wa kuhakikisha wananchi maskini wanapata ardhi, wanalima kisasa, na kuongeza uzalishaji na hivyo kufuta umasikini.

Kila mwananchi maskini aligawiwa ardhi yenye ukubwa wa hekta 4.1, ardhi husika ikasafishwa na kuwekwa miundombinu yote muhimu ya kilimo, ikapandwa michikichi, na mwananchi akapata huduma za ugani ili kukuza michikichi hiyo.

Shughuli zote hizi zilifanywa kwa gharama za Serikali, na wananchi wale wakapewa kama mkopo ambao walikuwa wanaulipa kidogo kidogo kila wanapovuna na kuuza migazi/mawese kwa shirika hili la FELDA. 

Hivi sasa FELDA ni shirika kubwa sana, lina thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 3.5, sawa na takribani Shilingi trilioni 7.7, na kupitia ushirika wao, wananchi hawa waliopewa ardhi ya kulima michikichi, sasa wanamiliki asilimia 20 ya hisa za shirika hilo!

SOMA ZAIDI: Wakulima Mbozi Wagoma Kuuza Kahawa Yao Wakidai Bei Hairidhishi

Malaysia iliweza kuondoa umasikini kutoka asilimia 57 ya wananchi wanaoishi kwenye dimbwi la umaskini mwaka 1965 mpaka chini ya asilimia tatu mwaka 2012. FELDA sasa ni shirika la kimataifa, maana linaanza kuwekeza duniani kote. 

FELDA ilipouza hisa zake kwenye masoko ya mitaji, au IPO, ambayo ni mauzo ya hisa hadharani kwa mara ya kwanza, ilikuwa ni ya tatu kwa ukubwa baada ya makampuni ya Facebook na Japanese Airlines.

Shirika la umma linalomilikiwa na Serikali, wakulima na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (EPF) na linaloendeshwa kwa misingi ya utawala bora wa makampuni, FELDA limeweza kufuta umaskini kwa zao moja tu la michikichi. 

Malaysia leo inaongoza kwa kuuza mawese duniani. Michikichi hiyo ilitoka Kigoma, Tanzania, na kupelekwa Malaya na Waingereza kwenye miaka ya 1950!

Tunapokwama Watanzania

Tanzania nasi tulikuwa na shirika la umma kwa ajili ya kilimo, leo tuchukulie Shirika la Chakula na Kilimo (NAFCO). 

Kama FELDA, NAFCO walichukua ardhi kubwa maeneo kadhaa nchini. Tofauti na FELDA, hata hivyo, wao NAFCO walilima wenyewe mashamba haya na kuweka miundombinu ya kilimo. 

SOMA ZAIDI: ‘Sitegemei Kuvuna Kitu’: Wakulima Mtwara Walia na Ukosefu wa Mvua

Tuchukue mfano wa mashamba ya mpunga kule Kapunga, wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya. Mnamo mwaka 1985, NAFCO walikwenda kijijini Kapunga kuwaomba wananchi wawape ardhi ya kulima mpunga. 

Wananchi wakawapa hekta 3,000 hivi, kwa mujibu wa muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Kijiji niliooneshwa mwaka 2009 nilipokwenda kutembelea mashamba haya kufuatia mgogoro wa ubinafsishaji.

NAFCO wakapata msaada kutoka Serikali ya Japan na uwekezaji mkubwa ukafanyika, ikiwemo kuweka kinu cha kukoboa mpunga cha kisasa kabisa.

Hata hivyo, NAFCO ilijiendesha kwa hasara, kwa sababu ambazo sitazieleza kwenye makala haya, na ilipofika katikati ya miaka ya 1990 ikaamuriwa kubinafsishwa. NAFCO ikauza mashamba yale kupitia Mpango wa Ubinafsishaji kwa Kampuni Binafsi. 

Katika uuzaji huo, NAFCO waliuza hekta 3,500 badala ya 3,000 walizopewa na wananchi, maana yake ni kwamba kijiji cha Kapunga nacho pia kiliuzwa!

Tofauti za kifikra

Mifano hii miwili inaonesha tofauti kubwa za kifikra na kimaendeleo kati ya nchi hizi mbili. Moja iliwezesha wananchi kumiliki ardhi na imefanikiwa. 

SOMA ZAIDI: GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?

Nyingine iliamua kufanya kupitia shirika la umma, na baada ya kushindwa, badala ya kurejesha ardhi kwa wananchi na kuwawezesha kulima, ardhi ile ikauzwa kwa kampuni ya mtu mmoja!

Ujamaa wa Malaysia ulikuwa ni wa kumilikisha wananchi wao ardhi na kuwawezesha kuzalisha. Ujamaa wetu hapa Tanzania ulikuwa ni wa kumiliki kwa pamoja na faida ya mavuno kufaidisha wananchi wote. 

Njia iliyotumika Malaysia ilifanikiwa, njia yetu, kwa sababu ya ufisadi na kukosekana uwajibikaji, haikufanikiwa. 

Badala ya kuboresha kwa kujaribu njia ya kijamaa ya Malaysia tuliona ni bora kufuata njia ya kibepari ya kugawa ardhi hovyo kwa wakulima wakubwa na wachache, na kuwaacha wananchi wetu wakiwa mafukara kabisa!

Zitto Kabwe ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo. Unaweza kumpata Twitter kupitia @zittokabwe. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa maelezo zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Kuna baadhi ya Watu wanafikili huu umaskini tulio Nao Kama umetoka Kwa Mungu Kumbe Sio Kweli Baraka za Mungu zipo Ni Uhakika Kweli Kweli na Huu umaskini ambao upo kwa Watanzania Unasababishwa Na Watu wachache Ambao Wasipodhibitiwa Basi hautaisha Daima

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *