The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

GMO: Suluhisho la Usalama wa Chakula Afrika?

Kuna hofu kwamba matumizi ya mbegu za GMO yanaweza kuathiri uhuru wa mwanadamu kwenye upatikanaji wa chakula.

subscribe to our newsletter!

Hali ya usalama wa chakula barani Afrika kwa sasa imeendelea kuwa tete huku Ripoti ya Shirika la Biashara na Maendeleo Duniani (UNCTAD) ikieleza kuwa kati ya mwaka 2016 mpaka 2018, asilimia 85 ya matumizi yote ya chakula barani humo, yenye thamani sawa na Dola za Kimarekani bilioni 35, yalihusu uagizaji wa chakula kutoka mataifa ya nje ya bara hilo.

Inakadiriwa pia kwamba kufikia mwaka 2025, uingizaji wa chakula kutoka nje ya bara la Afrika utaongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani bilioni 110 kwa mwaka, kutokana na idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye maeneo ya uzalishaji wa chakula (hasa vijijini), kuhamia kwenye miji.

Ikumbukwe kwamba, uhalisia huu umekuja ikiwa mapema mwanzoni mwa karne 21 viongozi wa mataifa huru ya Afrika walikutana Maputo kujidhatiti kwenye sekta ya kilimo.

Katika Makubaliano ya Maputo, Serikali za Afrika zilikubaliana kutenga asilimia 10 ya bajeti ya Serikali kila mwaka kwa ajili ya kilimo.

Lakini hadi kufika mwaka 2020, ni nchi nne tu – Malawi, Lesotho, Ethiopia na Benin – ambazo zilizoweza kutekeleza makubaliano ya Maputo huku nchi nyingi nyingine zimekuwa  zikitenga kati ya 2-3% ya bajeti kwenda kwenye kilimo, hivyo kumeifanya sekta ya kilimo kuendelea kudumaa.

Sekta ya kilimo kwenye mataifa mengi barani Afrika kwa sasa imekuwa ikiachiwa zaidi sekta binafsi kwenye utekelezaji, hali ambayo imekuwa ikiathiri zaidi uzalishaji, hususan mazao ya chakula.

Sekta binafsi kwenye kilimo imekuwa ikijikita zaidi na mazao ya biashara, hususan kwenye tafiti, uzalishaji na usimamiaji.

Kwa kiasi mafanikio kwenye mazao ya biashara kumefanya pia wakulima wazalishaji wa mazao ya chakula kuhama na kujiwekeza zaidi kwenye kilimo cha biashara. Hali hii imepelekea kupungua kwa uzalishaji na mfumuko wa juu wa bei kwa bidhaa za chakula.

Ukiachilia mbali kiwango kidogo kinachotengwa kwenye bajeti ya kilimo kwenye nchi nyingi za Afrika, pia kumekuwa na sababu mbalimbali zinazopelekea uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kudorora.

Sababu kama matumizi duni ya teknolojia, mabadiliko ya tabia nchi yanayopeleka ukame, elimu ya mabadiliko ya uzalishaji wa mazao na kukosekana kwa mnyororo wa uthaminishaji wa mazao ya kilimo zimeifanya sekta ya kilimo kutokukua kwa kasi inayohitajika ili kuiwezesha Afrika kuwa na usalama wa chakula.

Suluhisho ni GMO? 

Mnamo Oktoba 3, 2022, Serikali ya Kenya iliondoa katazo la utafiti, uzalishaji na uingizaji wa chakula au mazao yanayotokana na mbegu za kiuandisi-jeni yaani kwa kimombo Genetically Modified Organism (GMO).

Katazo hili lililodumu kwa miaka 10 liliondolewa baada ya kutokea kwa ukame uliopelekea upungufu mkubwa wa chakula na maji nchini humo. Ikumbukwe kwamba kabla ya hapo ni nchi nane tu za Afrika ndiyo zilikuwa zimeruhusu matumizi ya GMO.

Kwa mujibu wa Serikali ya Kenya; matumizi ya mbegu za GMO yatapelekea ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula, hususan ikitazamiwa mbegu hizi kuwa na uwezo mkubwa wa kuhimili ukame na kupambana na wadudu.

Kuchelea kwa mataifa mengi barani Afrika kupokea teknolojia hii pamoja na changamoto zake za chakula imechagizwa na maswali mengi ambayo baadhi ya tafiti zilizofanywa zimeonesha mbegu hizi kutokuwa suluhisho la changamoto ya uzalishaji wa chakula pamoja, kuonekana kuwa na athari kwenye afya za binadamu na kuwa teknolojia yake imehodhiwa na makampuni machache yanayotaka kudhibiti uzalishaji wa chakula duniani.

Kwa upande wa Tanzania, Waziri wa Kilimo Hussein Bashe hivi karibuni amenukuliwa akilinganisha uzalishaji wa pamba itokanayo na mbegu za GMO kuwa zinaweza kuzalisha kilogramu 850 za pamba kwa ekari moja huku mbegu za kawaida zinazotumika sasa, yaani mbegu chotara na zile za asili, uzalishaji wake upo chini yaani tani 1.2 hadi tani 1.75 kwa ekari moja.

Mpishano wa uzalishaji huo umekuwa ukionekana pia kwenye mazao mengine, hivyo kuifanya GMO siyo jawabu kwenye suala la uzalishaji mdogo kwenye kilimo.

TAZAMA: Mbegu za GMO ni Hatari kwa Mfumo wa Taifa wa Chakula

Athari za GMO

Matumizi ya kemikali ya glyphosate ambayo hutumika kwenye utengenezaji wa mbolea itakayotumika kwenye mimea ya mbegu za GMO, yameonekana yataongeza athari kwenye viumbe ndani ya udongo.

Ili viumbe hivyo visipatwe na madhara hayo, itahitajika pia vibadilishiwe uhandisi wa maumbile yaani kwa kimombo genetic engineering ili viweze kupambana na mazingira hayo. Hivyo basi, matumizi ya GMO yatachangia kuharibu ikolojia asili ya wanyama na mimea.

Matumizi ya mbegu za GMO pia yameonekana kuathiri mazao yaliyokaribu, hasa ikizingatiwa kuwa mimea itokanayo na GMO ni mimea vamizi  na hivyo inapotokea uchavishaji (Cross Pollination), mimea mingine inakuwa kwenye hatari ya kuharibika.

Kwa hali hiyo, mbegu hizi zinaonekana kuweza kuathiri mimea na mazao mengine yasiyo na maumbile ya GMO.

Taasisi ya utafiti ya Afya yaThe Lancet ya nchini Uingereza ilifanya utafiti kuhusu vyakula vinavyotokana na mazao yaliyozalishwa na mbegu za GMO.

Jarida la Institute for Agriculture and Trade Policy lilitoa ripoti hiyo ya tafiti ikionesha kuwa matumizi ya kiazi kilichozalishwa kwa mbegu ya GMO ambacho kinawekewa kemikali ya Bacillus Thuringiensis inayotumika kukisaidia kiazi hicho kupambana na wadudu, kama mwanadamu atakitumia atakuwa yupo hatarini kuathiriwa kiafya hasa uwezo wake wa kupambana na magonjwa, ukuaji wa viungo pamoja na mfumo wake wa mmeng’enyo wa chakula.

Pia, kumekuwa na mkingano wa umiliki wa teknolojia hii ya uzalishaji wa mbegu, hasa ikizingatiwa kuwa utengenezaji wa mbegu hizi hufanywa na taasisi binafsi.

Hali hii imeonekana italazimisha mataifa mengi kukabidhi haki ya upatikanaji wa chakula wa wananchi wao kwa taasisi binafsi. Suala hili linatazamwa kuathiri uhuru wa mwanadamu kwenye upatikanaji wa chakula.

TAZAMA: ‘Sioni Uhususiano Kati ya Majaribio ya Mbegu za GMO na Tanzania Kuwa Tegemezi Kwenye Mbegu’

Nini Kifanyike?

Mataifa mengi barani Afrika yameonekana kutokuwa tayari kupokea teknolojia hii. Hali hii inapelekea mataifa yaliyoidhinisha matumizi ya teknolojia hii kutokuwa na uwezo wa kuuza bidhaa hizo nje ya mipaka yao.

Hatua hii itaathiri kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa mkataba wa eneo huru la biashara barani Afrika yaani African Continental Free Trade Area (AfCFTA), unaojumuisha jumla ya mataifa 43.

Kwa kuwa AfCFTA imelenga kuondoa ushuru wa forodha pamoja na kupunguza vizuizi visivyo na ushuru baina ya nchi washirika kwa bidhaa zaidi ya 60,000 zikiwemo bidhaa za kilimo.

Kwa maana hiyo basi, nchi za Afrika zinapaswa kwa pamoja kuwa na sera za kilimo zinazotilia mkazo uzalishaji wa mazao ya chakula na mnyororo mzima wa thamani wa bidhaa za kilimo.

Kwa mataifa yenye hatari ya kupata ukame mara kwa mara yanapaswa kuweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo yasiyo na ukame na kujikita zaidi kwenye kilimo cha mazao yanayohimili ukame mfano wa Mtama, Uwele, Ulezi ,viazi nakadhalika ambayo pia mazao hayo yanaweza kuzalishwa kwa ziada na yakauzwa katika mataifa mengine barani Afrika.

Pia, sheria za umiliki na mgawanyo wa ardhi  zinapaswa kutazamwa upya. Nchini Kenya kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu juu ya umiliki wa ardhi ambapo idadi ndogo ya watu imekuwa ikimiliki ardhi kubwa na yenye kuonekana kuwa na rutuba.

Wakenya wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ardhi hiyo zaidi hutumika kwenye kilimo cha biashara hasa maua, hivyo kuonekana kunufaisha watu wachache wenye kujihusisha na biashara hiyo.

Suluhisho kubwa zaidi ni Serikali za mataifa ya Afrika kurudi na kutekeleza Makubaliano ya Maputo kwani ustawi wa sekta ya kilimo unategemea sana kutengwa kwa bajeti ambayo itawezesha kufanyika kwa tafiti, usimamizi wa sera, uboreshaji wa miundombinu ya kilimo, utoaji wa elimu na ujuzi katika kilimo pamoja na utoaji ruzuku kwenye zana, mbolea na pembejeo.

Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Mwandishi kaelezea kwa mapana sana
    Ni kweli kuna haja ya kujitathmini kabla ya kuadopt new technology
    We need research fund for our agriculture sector

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *