Search
Close this search box.

Mabadiliko ya Tabianchi Yatajwa Kuathiri Kilimo cha Korosho Lindi, Mtwara

Uzalishaji wa korosho umetajwa kushuka ukilinganisha na misimu iliyopita hali ambayo wataalamu wameihusisha na athari za mabadiliko ya tabianchi.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuhusishwa na changamoto za maisha wanazokabiliana nazo Watanzania baada ya wadau mkoani hapa kulihusisha janga hilo la kidunia na kushuka kwa uzalishaji wa zao la korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Hilo lilidhihirika hapo Novemba 25, 2022, wakati wa kikao cha tathmini cha wadau wa tafiti za kilimo nchini kilichofanyika kwenye ofisi za Taasisi ya Utaifiti wa Kilimo (TARI – Naliendele) mkoani hapa.

Wataalamu hao walieleza kwamba kutokana na madadiliko ya tabianchi huenda mwaka huu wa 2022 uzalishaji wa zao hilo ukashuka ulinganisha na misimu iliyopita na hivyo kushindwa kufikia malengo ya uzalishaji yaliyowekwa hapo awali.

Ally Linjenje, mshauri wa kilimo mkoa wa Mtwara, akizungumza na The Chanzo mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho, alisema kwamba katika msimu huu hali ya hewa iliyokuwepo haikufaa kwa uzalishaji wa korosho.

“Kwa mfano, korosho zinasitawi zaidi kwenye joto la nyuzijoto ya 23 mpaka 24 na vilevile hali ya unyevu inatakiwa isizidi asilimia 70, lakini mwaka huu joto kwa kipindi kirefu lilikuwa chini ya nyuzijoto 20,” alisema Linjenje.

“Na kwa taarifa zilizotolewa na wenzetu wa hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa, zinaonesha kuwa hali ya unyevu kwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilikuwa ni zaidi ya asilimia 75. Kwa hiyo, unaweza kuona hapo,” aliongeza mtaalamu huyo.

SOMA ZAIDI: Wananchi Mkuranga Walia Na Athari Za Mabadiliko Tabia Nchi

The Chanzo inafahamu kwamba wakati minada ya korosho ikiendelea kufanyika kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara, hali ya ukasanyaji wa zao hilo la biashara bado siyo nzuri.

Korosho chache

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, korosho zilizokusanywa mpaka sasa ni chache ukilinganisha na malengo ambayo mikoa ya Lindi na Mtwara ilijiwekea ya uzalishaji wa zao la korosho kwa msimu wa mwaka 2022.

Kwa mfano, mkoa wa Mtwara ambao unatajwa kuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo kwa kuchangia asilimia 50 ya korosho yote inayozalishwa hapa nchini, uliweka malengo ya kuzalisha tani 248,000 za korosho.

Lakini mpaka sasa tayari minada mitano imefanyika na ni tani 48,000 tu ndizo zilizokusanywa, kiasi ambacho kinawafanya wadau wawe na mashaka kwamba malengo yaliyowekwa ya uzalishaji yanaweza yasitimie.

Pamoja na sababu nyengine, wataalamu waliokutana mkoani hapa wanakubaliana kwamba mabadiliko ya tabianchi yamechochea athari hii.

Wataalamu wanabainisha uwepo wa hali ya hewa tofauti na ile iliyozoeleka kuwepo hapo zamani, ikiwemo kuwepo kwa kipindi kirefu cha baridi.

Kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, kipindi cha baridi, yaani kipupwe, kwa kawaida huanza mwishoni mwa Mei mpaka katikati ya Agosti.

Kwa mwaka huu, kipindi cha kipupwe kimedumu mpaka Oktoba hali ambayo wataalamu wanasema imepelelea mikorosho kushambuliwa na magonjwa, kama vile ugonjwa aina ya bright ambao hukausha maua ya mikorosho.

SOMA ZAIDI: Ni Upi Mtazamo wa Wakulima Wadogo Juu ya Mabadiliko ya Tabia ya Nchi?

Hadija Bakiri ni mshauri wa kilimo mkoa wa Lindi ambaye ameiambia The Chanzo: “Kwa mkoa wa Lindi, mabadilko ya tabianchi yametuathiri sana kupitia zao la korosho. Kumejitokeza magonjwa mengi ya mikorosho ambayo imepelekea kukauka kwa maua ghafla.”

Mabadiliko ya mbegu

Mkurugenzi wa TARI-Naliendele Dk Fortanus Kapinga amesema kuwa kwa sasa tafiti zinaendelea kufanyika kuangalia ni mbegu gani ya korosho ambayo itafaa kutokana na madadiliko haya ya tabianchi kwa sababu mbegu zilizopo sasa hazihimili hali ya hewa ya unyevu unyevu na baridi.

Kapinga anasema hatua hii ni kama mpango wa muda mrefu katika kutatua changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa mikoa ya Lindi na Mtwara kwenye uzalishaji wa zao la korosho.

SOMA ZAIDI: Tozo, Pembejeo Zinavyowatesa Wakulima wa Korosho Mtwara

Mtaalamu huyo aliongeza kuwa kwa sasa wakulima wanatakiwa kupalilia mashamba ya mikorosho kisha kupanda mazao mengine ya muda mfupi, akitolea mfano wa mazao kama kunde kunde, karanga na njugu ili kutunza maji wakati wa mvua kwa kuwa mvua zimekuwa zikinyesha chini ya wastani kwenye mikoa hii ya kusini.

“Fikiria kama hali tu ya umande kwenye majani ya mikorosho inasababisha ugonjwa wa bright kutokea atapulizia viuwatilifu mara ngapi mkulima? Ndiyo maana sasa hivi tafiti zetu zinalenga kupambana na changamoto kama hiyo,” alisema Dk Kapinga kwenye mahojiano na The Chanzo.

“Hivi ninanavyoongea sasa hivi tupo kwenye hatua za mwisho kabisa, kusema sasa kuna mbegu ambayo tunataka kujiridhisha kwamba inaweza ikapandwa bila kutumia viuwatilifu vya kupambana na bright na mkulima akapata korosho,” aliongeza Dk Kapinga.

Mvua hafifu

Lakini athari hazitokani na kuwepo na kipindi kirefu cha baridi na unyevu unyevu katika mikoa ya kusini tu bali hata upatikanaji wa mvua ambao kwa mwaka 2022 mikoa hii ilipata mvua chini ya wastani, hali iliyopelekea mikorosho kushindwa kuzaa vizuri.

Kwa mujibu wa wataalamu, miti ya mikorosho huhitaji mvua vyingi kwa ajili ya kutunza maji ardhini yatakayotumika wakati mikorosho inapochipua tayari kwa kuzaa.

Omari Kahoki ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utabiri wa Hali ya Hewa cha TARI-Naliendele ambaye anakiri kwamba ukiacha sababu nyengine zinazoonekana kusababisha uzalishaji wa korosho kushuka, uchache wa mvua umekuwa ni sababu mojawapo zilizosababisha hali hiyo.

SOMA ZAIDI: Wakulima Wadogo Hawaridhishwi na Hali ya Ushirika Tanzania

Kahoki aliiambia The Chanzo:

“Mvua za jumla za msimu wa 2021/2022 ni mililita 691.5 ambazo ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na hali ya kawaida kwa sababu wastani wa mvua za maeneo ya mikoa ya Lindi na Mtwara ni mililita 950 mpaka mililita 1040.

“Kitendo cha kupata mvua chini hata ya nusu ya kiasi kile ambacho kinatarajiwa tayari kinakuja kuathiri kwa kiasi kikubwa mazao yanayohitaji maji kwa kipindi hicho.

“Kwa hiyo, utagundua kwamba watu wanalalamika anguko la uzalishaji wa korosho ni kweli kwa sababu mimea kama mikorosho haikushiba maji ya kutosha ambayo yangeweza kurutubisha mmea na kuupa nguvu ya kuzalisha maua yake.”

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *