The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wakulima Wadogo Hawaridhishwi na Hali ya Ushirika Tanzania 

Wakulima wanadai kwamba ushirika umeshindwa kuwasaidia kuondokana na changamoto zao za kila siku ikiwemo ukosefu wa masoko.

subscribe to our newsletter!

Morogoro. Wakulima wadogo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi wamelalamikiwa hali ya ushirika nchini, wengi wao wakibainisha kutoridhishwa na ushirika unavyoendeshwa hali wanayodai imesababisha changamoto zao nyingi zinazowakabili kushindwa kupata ufumbuzi wa kudumu.

Wakulima hao walitoa dukuduku hilo wakati wakiongea na The Chanzo pembezoni mwa Mkutano wa 26 wa Mtandao wa Wakulima Wadogo Tanzania (MVIWATA). Mkutano huo wa siku mbili ulifanyika mkoani Morogoro kati ya Disemba 6 na Disemba 7 na uliambatana na uwasilishwaji wa mada mbalimbali kuhusu kilimo na wakulima wadogo.

Madai hayo ya wakulima wadogo dhidi ya hali ya ushirika nchini yanakuja takriban miezi mitano baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuibua hoja hiyo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani Julai 3, 2021 yaliyozinduliwa Julai 29, 2021 viwanja vya Nanenane Mkoani Tabora, ambapo alibainisha kwamba ipo haja ya Serikali kuimarisha ushirika ili uweze kuwa na tija kwa wakulima wadogo.

“Kama mimi ni mkulima ambaye nalima alizeti na najitahidi kuilima alizeti  katika misingi inayoonesha kama naweza kuilima kisawa sawa lakini baadae soko linakuwa gumu,” Mohamed Haji, mkulima mdogo kutoka Mtwara, aliiambia The Chanzo. “Na katika hili, kusema kweli ushirika haujaweza kutusaidia.”

Kutokuwepo kwa ushirikishwaji

Pengine hakuna kitu kinawaumiza zaidi wakulima mdogo kama kutokushirikishwa katika hatua za maamuzi juu ya mambo kadhaa yanayohusu hatma na ustawi wa ushirika wao kama wakulima. Wakulima wadogo wengi wameieleza The Chanzo kwamba hili ni tatizo sugu na linachangia kwa kiasi kikubwa watu kukosa imani na vyama vyao vya ushirika.

“Kwa mfano, wanapokuja wanunuzi wa mazao, hasa zao la korosho, unaweza ukakuta siyo kwamba midahalo au vikao havifanyiki vya ununuaji wa mazao, vinafanyika,lakini wanao hudhuria ni wachache,” anasema Asha Maharola kutoka Mtwara. “Kwa hiyo, maamuzi yanakuwa ni ya watu wachache. Matokeo yake sasa linaporudishwa kwa mkulima utakuta wanakukata hili, wanakata  bei hii wakati wakulima walioshiriki pale ni wachache.”

Hili ni jambo moja lakini kuna na madai ya viongozi wa ushirika kuwapa kipaumbele wafanyabiashara kwa gharama ya wakulima, licha ya ukweli kwamba viongozi hao wa ushirika wanapaswa kulinda maslahi ya wanachama wa ushirika husika.

Hii ni hoja inayoibuliwa na Charles Kasamata, mkulima mdogo kutoka Rukwa, anayesema: “Tunapopewa fursa fulani au kununua mazao, kama viongozi hawathamini [wakulima] badala yake wanathamini wafanyabiashara. Hiyo ni changamoto kubwa kwenye vyama vyetu vya ushirika.”

Baadhi ya mada zilizowasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na Nafasi ya Ushirika katika Ustawi wa Wakulima Wadogo; Nafasi ya Wanawake katika Mapambano ya Wakulima Wadogo; na Mabadiliko ya Tabia ya Nchi na Haki ya Mazingira.

Akiwasilisha mada yake ya Nafasi ya Ushirika katika Ustawi wa Wakulima Wadogo, Mbunge wa Kuteuliwa na mdau wa siku nyingi wa MVIWATA Dk Bashiru Ally aligusia umuhimu wa uendeshaji wa ushirika nchini kubadilika na kuondokana na aina ya ushirika uliokuwepo miaka ya 1960 baada ya Tanganyika kupata uhuru.

Ushirika ubadilike

“Huwezi ukarekebisha upande mmoja ukaacha upande mwingine,” alisema Dk Ally ambaye alipata kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). “Kwa hiyo, tukibadilisha mfumo wa uzalishaji ndani ya kilimo na viwanda kwa pamoja kwa sababu vinategemeana. Vivyo hivyo, mabadiliko hayo yaende sambamba na mabadiliko ya mfumo wa ushirika.”

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Morogoro Keneth Shemdoe  anakiri kuwa kwenye ushirika kuna watu tofauti tofauti na wenye tabia tofauti tofauti, na ndio maana sheria zikawekwa ili kuhakikisha kwamba ili taasisi iweze kusimama ni lazima kuwepo na sheria ya udhibiti.

Anasema kumekuwa na ushirika wa aina nyingi na unaosikika sana ni ushirika wa mazao kwa sababu asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima.

“Na mazao yale yanayotajwa ni mazao ya kimkakati,” alisema Shemdoe. “Utasikia kahawa, korosho, [na] pamba. Mazao haya ya mbogamboga mara nyingi huwa hayatajwi sana. Lakini ushirika  wake upo. Lakini sasa humu kwenye ushirika kuna watu wanatabia tofauti tofauti kwa jinsi walivyo zaliwa kwao na nyingine za kurithi. Kwa hiyo, ndio maana unaweza ukakuta sehemu fulani imefanyika jambo inaharibu taswira nzima ya ushirika.”

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo, Mifugo na Maji  Dk Christine Ishengoma alisema kwamba Serikali inatambua changamoto za wakulima, hasa kwenye kuimarisha ushirika ili wapate sehemu ya kuuza bidhaa zao.

“Wakulima wengi hawana imani na vyama vya ushirika,” alikiri Mbunge huyo wa Viti Maalum (CCM). “Ushirika ni mzuri kama ukisimamiwa vizuri.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *