The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Watu 217 wapoteza maisha mahala pa kazi katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2021

Serikali yataka wafanyakazi wote sekta ya umma na binafsi kuhakikisha wanaandikishwa kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi .

subscribe to our newsletter!

Dodoma: Watu 217 wamepoteza maisha mahala pa kazi katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2019 hadi Juni 2021. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ambapo inaonesha pia ajali zilikuwa 4,993 huku magonjwa yakiwa ni 249.

Haya yamezungumzwa jana April 26,2023, na wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemevu Prof. Joyce ndalichako wakati akiongea na waandishi wa habari kuelekea katika siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi inayoadhimishwa Aprili 28 ya kila mwaka.

“Naamini watu wote mtakubaliana nami kwamba takwimu hizo ni kubwa sana [na} zinaathiri utendaji [kazi].”anasema Prof. Ndalichako.

“Zinasababisha upotevu wa maisha ya wafanyakazi na pia kuathiri shughuli wakati wafanyakazi walioumia wakiendelea kupata matibabu.”

Profesa Ndalichako anasema, suala la ajali na magonjwa yatokanayo na kazi ni jambo linalohitaji jitihada za makusudi katika kukabiliana nalo. Serikali inatambua na kuthamini nguvu kazi ya taifa, na inatambua umuhimu wa kulinda nguvu kazi ya taifa.

Kupitia Wakala wa Afya na Usalama Mahala pa Kazi, Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria namba tano ya Afya na Usalama Mahala pa kazi ya mwaka 2003.

Kwa takwimu za kidunia zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani [ILO] mwaka 2022 zinaonesha zaidi ya watu milioni mbili na laki tisa [2.9] hupoteza maisha kutokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Takwimu hizo pia zinaonesha kuwa zaidi ya wafanyakazi milioni mia nne na mbili [402,000,000] huumia wakiwa kazini na hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kipindi chote wanachopatiwa matibabu hadi hapo watakapopona.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi [OSHA] Khadija Mwenda anasema kutokana na utafiti walioufanya unaoenesha sekta ya uzalishaji ni miongoni mwa sekta zinazoongoza kwa ajali.

“Sekta ya uzalishaji ndiyo ambayo imeajiri watu wengi na inaajiri vijana wengi.” anasema Khadija.

“Na tunafahamu kwamba vijana wanakuwa na ile hali ya kutaka ajira. kwa hiyo mara nyingi wanakuwa wako tayari kuchukua kazi yoyote bila hata kutathmini vihatarishi ambavyo viko kwenye hiyo kazi.”

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (TUCTA) linatambua changamoto zinazojitokea kwa wafanyakazi mahala pa kazi. Rais wa Shirikisho hilo Tumaini Nyamhokya anasema maeneo ya kazi wakati mwingine yasiposimamiwa kikamilifu yanakuwa hatarishi.

“Tumeshuhudia viwandani huko unaweza kukuta mahala pa kazi mafuta yanamwagika lakini kuna mitambo mule ndani. Inakuwa rahisi kwa mfanyakazi kutekeleza na kwenda kwenye mashine akaliwa na mashine.” anasema Nyamhokya.

Kukabiliana na hilo, Nyamhokya anasema kama viongozi wanashirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania [ATE] kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama.

Kwa upande wa waajiri, Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba anasema kazi ya chama chao ni kuendelea kuwakumbusha waajiri kuhusiana na kufuata taratibu, Sheria na Kanuni zilizowekwa.

Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa kazi, 2003 inamtaka mwajiri kutoa mazingira yenye afya, usalama na ustawi kwa wafanyakazi wake wote na kuhakikisha kurudi kwa maisha ya kawaida kwa wafanyakazi walioathiriwa.Ni lazima mmiliki kutoa na kuendeleza kifaa na mifumo na utaratibu wa kazi ambao ni salama na bila hatari kwa afya ya wafanyakazi.

Mwajiri lazima ahakikishe usalama na kutokuwepo na hatari ya kiafya katika utumizi, shughuli, uwekaji na usafirishaji wa kikorokoro na mali.

Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani ILO Getrude Sima anasema jukumu lao kubwa ni kuendelea kutoa msaada kwa maana ya utalaam kwa nchi ili kuweza kutekeleza mikataba yote ya Shirika la Kazi Duniani inayohusu masuala ya afya, usalama

Waziri Profesa Ndalichako anaongeza kuwa, kiutaratibu wafanyakazi wote wanapaswa kuandikishwa kwenye Mfumo wa Fidia wa Wafanyakazi ili inapotokea ajali wawe na kinga ya kuwasaidia.

“ Nitoe msisitizo kwa wafanyakazi wote sekta ya umma na binafsi kuhakikisha kwamba mnaandikishwa kwenye Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi . Ni kinga yenu na imekuwa ni msaada mkubwa ili inapotokea ajali uwe na kinga ambayo itakuwezesha kuweza kunufaika.” anaongeza.

Kwa mwaka huu, maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi yanakwenda sambamba na kauli mbiu isemayo “ Mazingira Salama na Afya kazini ni Kanuni na Haki ya Msingi Mahali pa Kazi.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana mkoani Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *