Dodoma. Pamoja ongezeko la matumizi ya bima nchini,baadhi ya kampuni za bima zimeendelea kulalamikiwa kwa kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wananchi pindi wanapokumbwa na majanga kama vile ajali.
Haya yameibuka Aprili 27,2023 kwenye Mkutano wa Kupokea na Kusikiliza Malalamiko ya Bima ulioandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) uliofanyika jijini Dodoma.
Sehemu kubwa ya malalamiko mengi kwa kampuni za bima yamekuwa yakielekezwa hasa katika bima za kawaida (general insurance), bima zinazotumika zaidi nchini.
Akiwasilisha malalamiko yake kwenye mkutano huo Leila Banji mkazi wa Dar es salaam ambaye alipata ajali ya gari maeneo ya Kinyerezi mwezi Julai, 2022, baada ya kugongwa na Lori, amekuwa akihangaika kwa muda mrefu kupata haki yake tangu alipowasiisha taarifa na malalamiko yake kwenye moja ya kampuni aliyokata bima.
“Niliwasilisha vielelezo vyote [na] niliendelea kufuatilia . Naenda naambiwa njoo kesho, njoo wiki ijayo, mwezi ujao nakwenda .” anaeleza Banji .
“Yule mama wa pale [kwenye hiyo kampuni] alikuwa ananijibu hovyo kama anavyojua mwenyewe. [Hadi sasa] wamegoma kunilipa gari yangu na mpaka leo lipo kituo cha polisi Stakishari.”
Adelard Swai mkazi wa Dodoma anasema, gari yake ilipata ajali Mei 9,2022. Anadai kuwa pamoja na kupeleka nyaraka zote zinazostahili mpaka sasa hajalipwa fedha zake.
“Matokeo yake wananiletea barua wananiambia nieleze gari lilikuwa linatoka wapi, linaenda wapi, sababu za gari kusafiri na kwa nini imeanguka.” anasema Swai .
Changamoto ya elimu
Wakati wananchi wakilalamikia kampuni za bima kuwa hazitendi haki, moja ya changamoto inayoonekana wazi wazi ni ukosefu wa elimu ya bima.
Kutokana na kuwepo kwa historia ya ulaghai mwingi katika sekta ya bima, jambo ambalo limepungua kutokana na mifumo kuimarika, kampuni nyingi huhitaji nyaraka mbalimbali zinazothibitisha ajali au tatizo husika.
Sehemu ya nyaraka hizo kwa mfano katika ajali ya vyombo vya moto ni pamoja na mchoro wa ajali, fomu ya Polisi (PF90), fomu ya Polisi (PF115), kama kesi ikifika Mahakamani na pia nyaraka za Mahakama, kama kuna uhitaji wa kuthibitisha zaidi.
Hata hivyo wananchi na pia baadhi ya vyombo muhimu vimekuwa na ufahamu mdogo juu ya taratibu hizi, kama anavyoeleza Malilo Ramadhan ambaye ni Meneja kampuni wa bima ya ICEA LION kanda ya kati. Anasema, kampuni za bima zinalitegemea na kuliamini Jeshi la Polisi pindi wanapohitajika kufanya malipo ya madai mbalimbali.
“[Polisi] wanashindwa kuwapa maelekezo wateja wetu wanapokuwa wanafika kule kwao. Ombi langu kwa mamlaka [ni muhimu] kulitilia maanani kwenye hivi vyombo vyetu, kwa kuwapa elimu stahiki ya kufuatilia nyaraka muhimu ambazo tunahitaji watu wa bima.” Anaeleza Malilo.
Ili kutatua changamoto ya elimu kwa umma, Balozi wa Bima na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed Said anasisitiza juu ya kampuni za bima kuwa na huduma rafiki kwa wateja wao
“Hata tutoe matangazo ya aina gani nyinyi kampuni za bima kama wateja watalalamika kuhusu bima ni ngumu sekta kukua,”anasema Mhandisi Zena Said.
“Tuwatunze wateja wetu [na] tuwahudumie vizuri. Lugha [iwe nzuri ] kwa wateja siyo umjibu kwa jeuri mueleweshe wakati mwingine ni suala la elimu.”
Faida mbele ya huduma?
Mpaka kufikia Disemba 2021, kampuni za bima zilikua na mtaji Trilioni 1.279, huku kwa ujumla sekta ya fedha na bima zikichangia asilimia 3 ya pato la taifa.
Katika jitihada za kupata faida zaidi, sehemu ya mapato ya Kampuni za Bima hutumika katika uwekezaji wa amana za muda mfupi au mrefu katika mabenki ya biashara na pia kupitia kutoa mikopo kwa serikali.
Ripoti ya Benki Kuu inaonesha Mpaka Februari 2023 sekta ya bima imekopesha serikali takribani Trilioni 1.5 sawa na asilimia 5.5 ya mkopo wote wa ndani wa serikali. Huku ripoti ya TIRA ikionesha asilimia 53 wa mali za bima ziko katika mabenki.
Wakati ni jambo la kawaida kwa kampuni za bima kukuza ukwasi wao kupitia uwekezaji kuna uwezekano mkubwa katika nyakati mbalimbali kampuni kukosa fedha za kulipa madai ya wateja kama uwekezaji utafanyika kwa namna ambayo haina tija.
Pale ambapo kampuni ya bima inapokua na ukwasi mdogo (liquidity), iwe kwa fedha nyingi kufungwa katika uwekezaji au biashara kuwa mbaya uzoefu unaonesha huwa ni moja ya sababu ya danadana kwa wateja wenye madai.
Mamlaka ya Bima imekuwa ikichukua hatua katika vipindi tofauti tofauti pale kampuni inapozorota kifedha, mfano Mei 10,2022, Kampuni ya Resolution ilizuiwa kuendelea kupokea wateja kutokana na mwenendo mbaya wa kifedha.
Nafasi ya TIRA
Katika mdahalo huo Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dkt. Baghayo Saqware aliweza kueleza nafasi ya TIRA katika kutatua kero za wateja.
Saqware alisisitiza kuwa jambo la kwanza ambalo mteja anatakiwa kufanya akiwa na changamoto ni kupeleka malalamiko kwa kampuni husika kwa njia ya maandishi, na mteja apate majibu ya maandishi.
“Wakishakujibu na haujaridhika nayo na hawashughuliki, hatua inayofuata ni wewe kuja katika Mamlaka [TIRA] wala usiruke hizo hatua,” alifafanua zaidi Kamishna Saqware.
Saqware pia alishauri wateja juu ya kutokufanya haraka kwenda Mahakamani kabla ya kutumia njia za mwanzo za kutatua malalamiko.
“Ninawasihi sana wadau wa bima mtu yeyote kwenye kampuni ya bima akikushauri upeleke shauri mahakamani anakuingiza chaka.”
“Kwa sababu anajua wewe ni mwananchi wa kawaida mahakamani ataenda kuweka vipingamizi, atachelewesha muda [na] hauna hela ya kufuatilia.” Alifafanua zaidi.
Kamishna huyo anafafanua kuwa baada ya mteja kufika kwenye Mamlaka ya Bima, ndipo hapo wanaweza kumshauri kama aende Mahakamani au la.
Uzoefu wa kesi mbalimbali za bima unaonesha wateja wengi waliweza kupata ahueni walivyofikisha malalamiko yao kwa Mamlaka ya Bima.
Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anapatikana Dodoma unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com