The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tamu,Chungu Bajeti ya TAMISEMI 2023/24

Uchambuzi wa The Chanzo umebainisha kwamba wakati wizara hiyo inafanya vizuri kwenye baadhi ya maeneo, nguvu zaidi zinahitajika kuwekezwa kwenye kurekebisha mapungufu ya msingi.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Uchambuzi uliofanywa na The Chanzo juu ya bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, umebainisha kwamba wakati wizara hiyo inafanya vizuri kwenye baadhi ya maeneo, nguvu zaidi zinahitajika kuwekezwa kwenye kurekebisha mapungufu ya msingi.

Bajeti ya wizara hiyo inayochukua takriban asilimia 21 ya bajeti yote ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 iliwasilishwa bungeni hapo Aprili 14, 2023, ikisimama kwenye kiwango cha Shilingi trilioni 9.14, ambayo ni ongezeko la asilimia nne ukilinganisha na ile ya mwaka 2022/23.

Kwenye uchambuzi wake, The Chanzo imeangalia maeneo sita muhimu, ikiwemo afya, elimu, Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), lishe, ustawi wa jamii, usimamizi, na taasisi zingine zilizoko chini ya TAMISEMI.

mwendendo wa bajeti ya TAMISEMI ndani ya miaka mitatu
Mwenendo wa bajeti ya TAMISEMI ndani ya miaka mitatu

The Chanzo imetumia madaraja, A mpaka D kuonesha ufanisi wa eneo husika. A ikiwa  nzuri sana, B+ ikiwa nzuri, B wastani, C hairidhishi na D mbaya. Vigezo vya msingi vilivyotumika ikiwa ni utoaji wa fedha katika mwaka uliopita, bajeti iliyotengwa kwa vipaumbele muhimu vya sekta husika, na utatuaji wa mtatizo ya wananchi kwenye neo husika.

Afya – A

Katika afya, The Chanzo inaipa wizara alama A, ikitumia kigezo cha kuongezeka kwa bajeti ya miundombinu ya afya kutoka Shilingi bilioni 73 mpaka Shilingi bilioni 86.5. 

Kwa upande wa vifaa tiba pia, kuna ongezeko la kutoka Shilingi bilioni 69.95 mpaka Shilingi bilioni 116.9.

Katika mwaka wa bajeti uliopita kumekuwa na ujenzi wa miundo mbinu mingi ya afya, licha ya ukweli kwamba kumekuwa na changamoto kwenye suala zima la vifaa tiba na wataalamu, hali inayozifanya baadhi ya zahanati na vituo vipya vya afya visitumike kabisa. 

Kigezo kingine kilichoifanya The Chanzo iipe wizara alama A kwenye afya ni utolewaji wa fedha unaoridhisha. Uchambuzi unaonesha kwamba mpaka kufikia Februari 2023, asilimia 86 ya bajeti kwa mwaka unaomalizika iilitolewa.

Mwenendo wa bajeti eneo la afya (vifaa tiba na miundombinu)

Hata hivyo, kwenye uchambuzi wake, The Chanzo ilibaini kwamba katika taarifa ya bajeti, kuna baadhi ya matumizi wizara haikufanikiwa kuyaeleza vizuri. Moja kati ya matumizi haya ni yale ya Shilingi bilioni 44.8 ya Mradi wa Kuimarisha Huduma za Rufaa na Ubora wa Huduma za Afya ya Msingi. 

Fedha hizi zimeelezwa kuwa zitatumika  kwenye kutoa ajira ya mkataba kwa watumishi 300; utoaji wa huduma ya rufaa kwa mama na mtoto; na kufanya ufuatiliaji katika vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi.

Ili kuimarisha uwajibikaji, The Chanzo inaamini kwamba wizara itahitajika kutoa maelezo zaidi yakionesha maeneo husika yatakayonufaika.

Usimamizi – B

The Chanzo imeipa wizara alama B kwenye eneo la usimamizi. Ni ukweli usiopingika kwamba halmashauri nchini zimekuwa zikiimarika, hususan katika ukusanyaji wa mapato. Katika mwaka 2021/22, kwa mfano, halmashauri kwa ujumla zilivuka lengo la makusanyo na kufikia Shilingi bilioni 891 kutoka bajeti ya Shilingi bilioni 873.9.

Hata hivyo, kuna changamoto katika matumizi, ikiwemo kutokuwepo kwa sera ya uwekezaji ya halmashauri, matumizi yasiyo sahihi ya mashine za POS na upotevu wa mapato kama ilivyooneshwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Kwa mfano,  CAG anaonesha Dodoma iliwekeza kwenye mradi wa hoteli wa zaidi ya Shilingi bilioni 10 bila kuwa na upembuzi yakinifu wa kibiashara. Hata katika utekelezaji wake, mfumo unaotumiwa na Dodoma, ikiwemo bei iliyopangwa ya ukodishaji haioneshi upatikanaji endelevu wa faida katika mradi.

Katika usimamizi baadhi ya maeneo yanayotoa matumaini ni pamoja na mfumo mpya wa TAUSI, mfumo unaosimamia malipo mbalimbali ya halmashauri. 

Hata hivyo, mfumo huu bado upo katika hatua za awali, huku baadhi ya wananchi wakilalamikia uwepo wa usumbufu wa hapa na pale kama kutokupata namba ya malipo, au control number, na mfumo kutopatikana baadhi ya nyakati.

Elimu – B

Katika upande wa huduma za elimu, The Chanzo imeipa wizara alama B kwa sababu ya kushuka kwa bajeti ya miundombinu ya shule. 

Wakati mwaka 2021/22 bajeti ya miundombinu ya shule ilifikia takribani Shilingi bilioni 560 na kwa 2022/23 ikawa Shilingi bilioni 324, kwa mwaka 2023/24 wa fedha imeshuka mpaka Shilingi bilioni 104.5.

Fedha zilizotengwa kwa ajili ya miundombinu ya elimu

Pia, mwenendo wa bajeti unaonesha kwamba pamoja na kuwa hitaji la elimu na ongezeko la wanafunzi ni jambo linalojulikana, bado wizara inaonekana haijafanikiwa kuwa na mkakati wa kudumu wa kutatua changamoto za miundombinu, walimu na vifaa shuleni. 

Sehemu kubwa ya bajeti ya maendeleo katika elimu bado inategemea wadau wa maendeleo.

Maeneo ambayo wizara imeendelea kufanya vizuri kulingana na uchambuzi huo wa The Chanzo ni pamoja na usaili wa wanafunzi pamoja na utoaji wa fedha za ruzuku. 

Katika miundombinu pia, wizara imetenga Shilingi bilioni 37 kwa ajili ya kukarabati shule kongwe. Uchakavu wa shule nyingi za zamani ni moja ya kilio cha wananchi wengi, na hoja hizi pia ziliwasilishwa bungeni na baadhi ya wabunge.

Ongezeko la wanafunzi na fedh za ruzuku

Ustawi wa jamii, lishe – C

Katika eneo la lishe, The Chanzo imeipa wizara alama C. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kiasi kilichotengwa na wizara kwenye eneo hilo ni Shilingi millioni 158.48 ya programu ya kuboresha chakula na lishe kwa ajili ya kuboresha afya kwa watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi. 

Bajeti haijaonesha mipango mahsusi kwa mwaka 2023/24.

Kwenye ustawi wa jamii, wizara imepata alama C. Moja ya majukumu ya TAMISEMI ni kusimamia na kuratibu mambo yanayohusu ustawi wa jamii katika ngazi ya mikoa na halmashauri.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG (2021/22), moja ya jambo linalosababisha ongezeko la matukio ya ukatili ni uchache wa watumishi katika eneo la ustawi wa jamii. 

Kwa mfano, katika mikoa kunahitajika maafisa 62, ila wako maafisa 36 tu. Halmashauri zinahitaji maafisa 1,969 ila wako maafisa 467, huku katika ngazi za mtaa na vijiji kukiwa hamna maafisa kabisa.

CAG pia anaonesha uwiano usioridhisha wa upangaji wa bajeti kwa ajili ya ustawi wa jamii, huku baadhi ya maeneo yanye changamoto kubwa za ukatili yakiwa na bajeti kidogo. 

Katika bajeti 2023/24, wizara haijaelezea kuhusu mipango ya ustawi wa jamii.

TARURA – B

Kwenye tathmini yake hiyo, The Chanzo imeipa wizara alama B kwenye eneo la TARURA, kutokana na ukweli kwamba licha kuongezeka kwa bajeti, bado kuna sehemu ya fedha zimekuwa hazifiki TARURA kama mpango wa bajeti ulivyo, hali inayochangia utekelezaji usio kamili.

Moja ya eneo linalotegemewa katika bajeti hii ni kanuni ambayo TARURA wataiandaa itakayoeleza namna fedha za ujenzi wa barabara za wilaya zitakavyokuwa zinagawanywa. 

Kanuni hii inategemewa kupunguza malalamiko, hususan juu ya maeneo yasiyofikiwa mara kwa mara.

Bajeti ya TARURA ndani ya miaka minne

Usimamizi wa taasisi zingine – C

Eneo la mwisho ni usimamizi wa taasisi. Wizara ya TAMISEMI ina taasisi takribani saba zilizo chini yake, ikiwemo TARURA, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Chuo cha Serikali za Mitaa, Wakala ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART), Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa na Shirika la Masoko ya Kariakoo (KMC).

Katika eneo hili, The Chanzo imeipa wizara alama C kutokana na ukweli kwamba bado taasisi hizi zina changamoto kubwa, ikiwemo upotevu wa fedha na uwajibikaji hafifu wa watendaji.

Kwa mfano, DART imejikuta kwenye madeni ya Shilingi bilioni 8.45 katika mwaka wa fedha wa 2021/22, huku CAG akihusisha madeni hayo na usimamizi dhaifu. 

Kwa Shirika la Masoko ya Kariakoo, wizara iliripoti kuwa baadhi ya nyaraka muhimu zilidaiwa kuungua na watendaji wa shirika hilo. 

Hata hivyo, taarifa ya bajeti haijaweza kuelezea kama nyaraka zilipatikana na njia nyingine zitakazotumika kuongeza uwajibikaji na ulinzi wa fedha za umma katika taasisi hizi.

Ushirikishaji wananchi ni muhimu kujenga uwajibikaji

Ni ukweli usiopingika kuwa jitihada nyingi zimeendelea kufanyika kuhakikisha fedha za serikali zinatumika ipasavyo katika halmashauri,hata hivyo bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

Moja ya jambo linaloweza kuimarisha uwajibikaji hasa katika ngazi za chini za serikali ni kujengea wananchi uwezo wa kushiriki moja kwa moja katika usimamizi wa rasilimali na miradi mbalimbali ya serikali katika ngazi zao.

Hili linaweza kufanikiwa kwa kuendelea kutoa taarifa mara kwa mara, na kuhakikisha utendaji wa halmashauri unazingatia uwazi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *