The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ukosefu wa Vituo vya Upataji Nafuu Waacha Waraibu wa Dawa za Kulevya Njia Panda Mtwara

Wataka wafikishiwe huduma za nyumba za upataji nafuu na vituo vya methadone.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Ukosefu wa huduma za nyumba za upataji nafuu, au sober houses kama nyumba hizo zinavyojulikana kwa kimombo, na vituo vya methadone, kumetajwa kuathiri mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya mkoani hapa, hususan kwenye kuwasaidia waraibu wa madawa hayo kuachana na matumizi yake.

Uchunguzi uliofanywa na The Chanzo umebaini kwamba mkoa wa Mtwara, na kanda nzima ya kusini inayojumuisha mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma kuna ukosefu wa huduma hizi muhimu, hali inayoibua hofu miongoni mwa waraibu na mamlaka za Serikali juu ya kufanikiwa kwa jitihada za kukabiliana na madawa ya kulevya.

Baadhi ya waliokuwa waraibu wa madawa hayo ya kulevya wameiambia The Chanzo kwamba safari yao ya kuacha uraibu ilikuwa ngumu maradufu kutokana na ukosefu wa huduma hizo muhimu, wakisisitiza uwepo wao ili waathirika zaidi wa madawa hayo waweze kuacha kuyatumia.

George Mumanyi, mkazi wa Mtwara Mikindani, alifanikiwa kuacha matumizi ya madawa ya kulevya mnamo mwaka 2018 baada ya kuwa mraibu tangu mwaka 1990, akitumia madawa ya kulevya aina ya heroine, moja kati ya dawa za kulevya zinazoongoza kwa kusababisha uteja haraka.

Baba huyo wa watoto wawili anasema safari yake ya kuacha matumizi ya madawa hayo haikuwa rahisi hata kidogo, akibainisha kwamba alijaribu mara kadhaa kuacha lakini alishindwa, hali aliyoihusisha na ukosefu wa huduma hizo za nyumba za upataji nafuu na vituo vya methadone mkoani hapa.

Siyo rahisi

“Vijana wengi nia ya kuacha wanayo na wanajaribu [kuacha] lakini wanashindwa kutokana na siyo rahisi kwa hali ya kawaida,” Mumanyi, 51, alisema kwenye mahojiano maalum na The Chanzo.

“Kwa sababu zikishakuzoea, zile dawa kwa kweli kuacha kwake ni ngumu sana, na bila msaada kama huo wa nyumba za upataji nafuu na vituo vya methadone, kwa kweli inakuwa ngumu sana [kuacha],” aliongeza Mumanyi ambaye ni kondakta wa daladala zinazotoka Mtwara kwenda Mpapura.

Ripoti ya mwaka 2021 kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inaonesha kwamba mpaka kufikia Disemba mwaka huo, kulikuwa na nyumba za upataji nafuu 44 nchi nzima, huku nyingi ya nyumba hizo zikipatikana kwenye mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Tanga, na Kilimanjaro.

Nyumba hizo pia zinapatikana kwa kiwango kidogo kwenye mikoa ya Dodoma, Morogoro, Iringa, na Kagera, huku mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma ikiwa haionekani kabisa kwenye ripoti hiyo. Kwa waraibu wengi wa madawa ya kulevya mkoani hapa, hiki ni kikwazo kikubwa cha jitihada zao za kuacha matumizi ya dawa hizo.

Labda hatari kubwa ya kukosekana kwa huduma hizi muhimu ni ile ya waraibu walioacha kutaka kurudia kutumia madawa hayo, hali iliyowahi kumpata Mbembele Said, mwathirika wa madawa ya kulevya ambaye alimudu kuvuka vigingi na kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Kurudia uraibu

“Wapo vijana wengi wanaacha lakini wanajikuta tena baadaye wanarudi [kutumia dawa za kulevya] kwa sababu ya kwamba hapa kwetu Mtwara hakuna nyumba za upataji nafuu,” alisema baba huyo wa watoto wawili kwenye mahojiano maalum na The Chanzo.

Said, 54, ni moja kati ya watu wanaojutia sana matumizi ya madawa hayo kutokana na ulemavu wa mguu alioupata kutokana na matumizi ya madawa hayo yaliyopelekea kugongwa na treni alipokuwa akiishi huko nchini Uturuki.

“Hizi nyumba za upataji nafuu na vituo vya methadone ni muhimu sana kwenye kumsaidia mtu kuacha [matumizi ya] madawa,” Said, ambaye kwa sasa anatafuta kazi aweze kuishughulikia vizuri familia yake, alisema. “Hizi huduma zinasaidia kwenye masuala ya elimu na ushauri, ambazo ni muhimu kwenye mchakato mzima wa kuacha.”

Ni katika mazingira haya ambapo Mwajuma Hassan, aliyekuwa akitumia madawa ya kulevya lakini kwa sasa ameacha, ameziangukia mamlaka za nchi pamoja na wadau wengine kuona umuhimu wa kuanzisha huduma hizo mkoani Mtwara, akisema zitasaidia kuokoa maisha ya mamia ya vijana mkoani humo.

Madawa ya kulevya yalimfanya Mwajuma, 38, kuzaa watoto watatu na wanaume tofauti, hali ambayo anaijutia, akisema kwamba kama isingekuwa matumizi ya madawa ya kulevya, kitu hicho kisingetokea kwenye maisha yake.

“Sisi tunaomba zipatikane nyumba za upataji nafuu hapa Mtwara,” Mwajuma, ambaye anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, aliiambia The Chanzo. “[Hizi nyumba] zitasaidia sana wengine kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.”

Huduma muhimu

Kwa mujibu wa Mratibu wa Afya ya Akili Manispaa ya Mtwara Mikindani, Koreta Mnunduma, manispaa hiyo ina jumla ya waathirika wa madawa ya kulevya wapatao 88, wengi wao wakiwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 45, ambao wapo chini ya uangalizi wa kitabibu.

Mnunduma alisema kwamba kwa sasa waraibu wa madawa ya kulevya mkoani Mtwara hupata huduma kutoka hospitali mbalimbali zilizopo mkoani humo. Hata hivyo, Mnunduma anakiri kwamba kukosekana kwa huduma za nyumba za upataji nafuu na vituo vya methadone kunakwamisha jitihada za kuwasaidia vijana wanaotaka kuacha.

“Vijana hawa wanatamani sana kuacha lakini kutokana na kukosekana kwa hizi huduma katika halmashauri yetu ya Mtwara Mikindani, vijana huwa wanaacha na kurudi tena kwenda kutumia,” Mnunduma aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalum.

“Kwa hiyo, na mimi nasisitiza uwepo wa huduma za methadone katika mkoa wetu na halmashauri zetu, lakini pia hizi nyumba za upataji nafuu ziwepo kwenye mkoa wetu,” aliongeza mtaalamu huyo.

The Chanzo ilimuuliza Kaimu Kamishna Msaidizi wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kusini, Salome Mbonile, endapo kama huduma hizo zinaweza kutarajiwa mkoani humo muda wowote kutoka sasa.

Siyo kazi yetu

Kuhusu nyumba za upataji nafuu, Mbonile alisema kwamba uanzishwaji wa nyumba hizo siyo miongoni mwa majukumu ya DCEA, akisema kazi ya mamlaka hiyo ni kuratibu tu nyumba hizo ambazo zinapaswa zianzishwe na mashirika yasiyo ya Kiserikali au watu binafsi.

“Mashirika yasiyo ya Kiserikali ndiyo yanayoanzisha huduma hiyo ya nyumba za upataji nafuu,” Mbonile alisema kwenye mahojiano. “Toka tumefika huku Kusini [mwaka 2021] tunajitahidi kuhamasisha hapa Mtwara na nje ziweze kuanzishwa, lakini kwa bahati mbaya mpaka sasa hatujapata wadau wa kufanya hivyo.”

Nyumba za upataji nafuu ni nyumba ambazo waraibu wa dawa za kulevya hutunzwa na kupatiwa huduma kwa kupitia hatua 12 za upataji nafuu na huduma za unasihi bila kutumia dawa.

Ili nyumba ikidhi vigezo vya kuwa nyumba ya upataji nafuu ni lazima iwe na ua na iwe karibu na kituo cha afya. Pia, mtu ambaye atakuwa anaendesha hiyo nyumba ni lazima awe alikuwa anatumia dawa za kulevya na sasa ameacha.

“Kwa hiyo, natoa wito kwa mashirika ambayo yana uwezo wa kuanzisha nyumba hizo kuanzisha kwa sababu kweli kuna tatizo la dawa za kulevya na wapo vijana wengi tu ambao wana matatizo ya dawa za kulevya [mkoani Mtwara],” alisema Mbonile.

Kuhusu vituo vya methadone, Mbonile alisema DCEA kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali zina mpango wa kupeleka huduma hiyo kwenye mikoa ya Kanda ya Kusini, akisema kwa sasa kinachofanyika ni tathmini ya kugundua huduma hiyo inahitajika kwa kiwango gani maeneo hayo.

Tunafanya utafiti

“Tunataka kuanzisha kliniki za methadone lakini kwa sasa tupo kwenye kufanya utafiti wa kuangalia kiasi cha tatizo la matumizi ya dawa kulevya kwenye hii mikoa ya kusini,” alisema Mbonile.

“Kwa sababu methadone huwa inawalenga wale wanaojidunga, au tuseme watumiaji wa heroine. Kwa hiyo, tunataka tufanye utafiti ili tujue je, tuna ukubwa kiasi gani wa hili tatizo?” aliongeza.

Mikoa ya Kusini inatajwa kuwa sehemu mojawapo ya milango ya kuingiza dawa za kulevya nchini Tanzania, hali inayotokana na kupakana kwao na Bahari ya Hindi.

Hii ni moja wapo ya sababu ya DCEA kuanzisha ofisi ya kanda kwenye mikoa hiyo hapo mwaka 2021 ikiwa ni sehemu ya juhudi za kitaifa za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya nchini, ikiwemo kudhibiti uingizwaji wake.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *