The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Nini Hasa Chimbuko la Mapigano Yanayoendelea Sudan?

Mapigano nchini humo yanahatarisha kutokea kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe inayotishia kufifisha matumaini ya kurudishwa kwa Serikali ya kiraia katika kipindi cha hivi karibuni.

subscribe to our newsletter!

Ni takribani miezi miwili sasa tangu kuzuka kwa mapigano nchini Sudani kati ya vikosi vya Jeshi la Sudan (SAF) vinavyoongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, ambaye pia ni kiongozi wa Serikali ya Mpito wa taifa hilo dhidi, ya Vikosi Vya Dharura, au Rapid Support Forces (RSF), vinavyoongozwa na aliyekuwa makamu kiongozi wa Serikali hiyo, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo.

Zaidi ya watu 1,800 wanakadiriwa kufa na wengine takribani milioni moja na laki tano wamekimbia makazi yao tangu kuibuka kwa mapigano hayo, huku huduma muhimu kama vile umeme, maji, masoko na hata usafiri wa umma zikiwa hazipatikani kabisa katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Huu ni mgogoro ambao hivi karibuni umetawala vichwa vingi vya habari ukiachana na ule wa Ukraine. Kwa hapa Tanzania, mgogoro huu ulipata umaarufu kufuatia hatua ya Serikali kuwaondoa raia wake na baadhi ya raia wa kigeni nchini humo, hususan kwenye mji mkuu wake, Khartoum.

Kabla sijafafanua kwa kina chimbuko la mgogoro huo, ni muhimu kukumbuka kwamba kambi mbili zinazopigana zilikuwa ni washirika wa karibu walioiangusha Serikali ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo kwa miaka 30, Omar Al-Bashir, hapo Aprili 2019, baada ya maandamano ya wananchi.

Wadadisi wanahoji, hivi vikosi vya RSF, au ‘wanamgambo’ kama wengi wanavyowaita, vimepataje nguvu ya haraka ya kuweza kushindana na vikosi vya jeshi rasmi la nchi? Katikati ya mgogoro huu, hatma ya Sudani ni ipi? Upo uwezekano wa kupatikana kwa mshindi kati ya pande hizo mbili zinazopigana? Na je, ushindi huo utajenga Sudani mpya?

Kupata majibu ya maswali yote haya itatulazimu kuelewa siyo tu historia ya hawa majenerali wawili  na utawala uliopita wa Bashir,  bali pia kuifahamu historia ya maendeleo ya siasa na utaifa nchini Sudan.

Mapinduzi ya kijeshi

Sudani ina historia ndefu ya uhaini wa kijeshi, au mapinduzi ya kijeshi, tangu nchi hiyo ilipopata uhuru wake mwaka 1956 kutoka kwa utawala mseto wa kikoloni kati ya Waingereza na Mfalme wa Misri uliotawala tangu mwaka 1898.

Wakati huo, taifa hilo lilijumuisha eneo lote la nchi ya Sudan ya sasa na eneo la Sudan Kusini ambayo ilikuja kujitenga Julai 9, 2011, kufuatia mapigano ya muda mrefu kati ya Serikali ya Sudan iliyotawaliwa na watu wa kaskazini dhidi ya jamii za wa kusini  wa nchi hiyo. Hii ni hadithi nyingine ambayo kwa leo inafaa tuiachie hapa.

Eneo la kaskazini la Sudan linakaliwa na watu wengi ambao ni Waarabu na waumini wa dini ya Kiislamu ambao wanatambuana kwa makabila na koo ambazo zina historia ndefu sana katika eneo la nchi hiyo.

Makabila haya na koo hizi ni taasisi zenye nguvu katika historia ya Sudani hadi leo hii, hali iliyotokana na namna nchi hiyo ilivyotawaliwa na Waingereza katika mtindo ambao, kwa kiasi kikubwa, uliendelea kuwapa nguvu viongozi wa makabila na koo hizi.

Lakini kwenye utumishi serikalini na jeshini, moja ya taasisi imara hasa baada ya uhuru, makabila ya Kaskazini na pembezoni mwa kingo za mto Nile, husuani eneo la Khartoum, ndiyo walipewa nafasi zaidi, na jamii hizi zimeendelea kushika hatamu ya sehemu kubwa ya utumishi kwenye vyombo hivi.

Kundi hili la walionufaika zaidi na fursa hii ya utawala, hususan maofisa wa jeshi, waliweza kujijenga kibiashara na kujaribu kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, kama mawakala wa makampuni ya kimataifa na hivyo kujijenga kitabaka ambalo ndilo limekuwa ni sehemu ya udhibiti wa uchumi wa Sudani.

Japo sehemu kubwa ya wananchi walitegemea kilimo na ufugaji katika kuendesha maisha yao, kundi hili halikuwahi kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa ukilinganisha na kundi la wafanyabiashara na wafanyakazi waliokuwa maeneo ya miji walioweza, kwa nyakati kadhaa, kuwa na ushawishi  wa kuhamasisha umma kisiasa.

Matokeo yake, jamii nyingi za wakulima na wafugaji, ambazo ziliunda takribani asilimia 80 ya wananchi, zilijikuta mateka wa misukumo ya siasa za kikabila, dini, na siasa za mabwanyenye waliojinasibisha na uzalendo, au utaifa.

Ndiyo maana miaka miwili tu baada ya uhuru, jeshi, likiongozwa na Jenerali Abboud mwaka 1958, lilifanya mapinduzi na kuchukua Serikali iliyokuwa ikiongozwa kiraia bila ukinzani wowote kutokana na hali ya misuguano ya kisiasa iliyokuwa ikiendelea baina ya vyama vya kisiasa washirika waliounda Serikali, pamoja na hali ya utengano iliyotokana na mahusiano ya kijamii  yaliyokuwepo wakati huo.

Jeshi lilijinasibu kuwa limechukua Serikali ili kuleta utulivu katika nchi, lakini lilishindwa kufanya hivyo, hali iliyopelekea mwaka 1964 kurudisha madaraka kwa Serikali ya kiraia tena.

Ilipofika mwaka 1969, Kanali Jaafar Nimeiry, chini ya kikundi kilichojiita Maofisa Huru wa Jeshi la Sudan, walifanya uhaini na kuiondoa madarakani Serikali ya kiraia ya Ismail Al-Azhari aliyeingia madarakani mwaka 1964.

Pamoja na ukweli kwamba Kanali Nimeiry alipoingia madarakani alichukua hatua za kimaendeleo na za kizalendo za ujenzi wa nchi hiyo tofauti na watangulizi wake wa kijeshi, mwisho wa siku aliandamwa na wimbi la migongano ya kitabaka na utengano uliokuwa umekita mizizi nchini humo.

Kipindi hiki, tofauti na nyakati zingine zozote zile nchini Sudani, kilishuhudia vuguvugu kubwa la siasa za mrengo wa kushoto, yaani ukomunisti, likiongozwa na vyama vya wafanyakazi waliojaribu mara kadhaa kuangusha utawala Nimeiry ili kufanikisha kile walichokiita kujenga jamii mpya ya Sudani iliyo huru dhidi ya minyororo ya kikabila, matabaka, na ubeberu, dhima ambayo haikufanikiwa!

Hatimaye, Nimeiry alipinduliwa mwaka 1985 na Jenerali Abdel Al-Dahab, aliyekuwa kiongozi wa jeshi kipindi ambacho Sudan ikipitia kwenye hali ngumu ya kiuchumi na mapigano na Sudani Kusini.

Jenerali Abdel Al-Dahab hakutaka kung’ang’ania madaraka kama watangulizi wake wa kijeshi, kwani mwaka 1986 alikabidhi Serikali kwa kiongozi wa kiraia, Sadiq al-Mahdi, kufuatia uchaguzi uliofanyika nchini humo.

Kupanda, kuanguka kwa Bashir

Serikali ya kiraia chini ya Waziri Mkuu Sadiq al-Mahdi, hata hivyo, haikudumu muda mrefu kwani alipinduliwa na Omary Al-Bashir aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Sudan wakati huo, hapo Juni 30, 1989.

Baada ya kuingia madarakani, Bashir alipiga marufuku vyama vya siasa na kudhibiti upinzani wowote ule wa kiraia.  Ili kuhakikisha anapata uungwaji mkono zaidi kutoka upande wa dini aliweka mkazo wa mfumo wa sheria za Kiislamu nchi nzima.

Kitu kimoja ambacho unaweza kusema kama Bashir alikielewa vizuri sana, basi ni namna historia ya Sudani ilivyojengeka kabla na baada ya uhuru. Labda ndiyo maana alitawala kwa kipindi kirefu sana ukilinganisha na viongozi wengine wote.

Kwa mfano, Bashir alitambua nguvu ya dini, ndiyo maana kwa kiasi kikubwa aliweza kujinasibisha na vikundi na mavuguvugu ya kidini yenye nguvu nchini Sudani kama vile National Islamic Front, kundi ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa nchini humo tangu mwishoni mwa miaka 1979.

Bashir pia alitambua nguvu waliyonayo viongozi wa makabila na koo mbalimbali nchini Sudani, hivyo akaamua kuwatambua kwa kuwapa nafasi katika Serikali na akawaongezea nguvu viongozi hao katika maeneo yao ya kiutawala, kitendo ambacho kilimpa uungwaji mkono mkubwa sana.

Bashir alitambua nafasi ya jeshi kama taasisi yenye nguvu kushinda kitu kingine chochote nchini humo, na hivyo aliona ni muhimu kuanzisha mfumo utakaoweza kuliangalia na kulidhibiti jeshi lisiweze kuiangusha Serikali yake kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Katika kuhakikisha hilo, Bashir, kupitia  Idara ya Usalama ya Sudani (NISS), aliunda vikundi vidogovidogo vya kijeshi, au unaweza kuita wanamgambo, kutoka makabila na koo zilizounga mkono Serikali kwa ajili ya kujenga nguvu nyingine ya kidola nje ya jeshi rasmi la nchi.

Vikundi hivi viliundwa na watu kutoka maeneo ya vijijini waliofundishwa kupigana tu pasipo kuwa na taaluma kamili ya kijeshi, na ndivyo vilivyotumika kupambana na wapinzani wa Serikali ya Sudani katika eneo la Darfur, wakifahamika kama Janjaweed, tangu mwaka 2003, na kupelekea uhalifu mkubwa wa kibinadamu katika eneo hilo.

Mnamo mwaka 2013, vikundi hivi vya wanamgambo takribani 100,000 viliweza kusukwa upwa kimuundo na kuongezewa uwezo na hivyo kutambulika kama Vikosi Vya Dharura, au Rapid Support Forces (RSF), chini ya Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo ambaye aliongoza vikosi hivyo kwa muda mrefu eneo la Darfur.

Vikundi hivi, chini ya Jenerali Dagalo, au kama Bashir mwenye alivyopenda kumuita ‘Hemedti,’ viliendelea kupata uzoefu mkubwa wa kimapigano baada ya kupeleka wapiganaji zaidi ya 40,000 nchini Yemen kuungana na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kupambana na waasi wa Houthi.

Mapigano haya yanatajwa kuvipatia vikosi hivyo uzoefu mkubwa lakini pia yamemsaidia Dagalo kutengeneza mtandao mkubwa kimataifa, hususani katika nchi za Mashariki ya Kati.

Lakini kwa upande wa majeshi ndani ya Sudani, tofauti na maofisa wengine wengi wa Jeshi la Sudani, Dagalo yeye hakuwa mtu wa asili wa makabila ya Khartoum na kaskazini yaliyotawala Sudani kwa miaka mingi. Dagalo ametokea katika jamii za pembezoni za kiarabu za Baggara ambazo ni sehemu ya makabila yaliyotengwa kwa muda mrefu.

Inasemekana hili jambo liliwakera maofisa wengi wa Jeshi la Sudani kuona kwamba mtu waliyemuona siyo msomi, kutoka katika makabila ya pembezoni ya ‘watu wa hovyo,’ anapewa madaraka na jukumu kubwa ndani ya vikosi hivyo vya wanamgambo wa RSF na Bashir.

Jukumu kubwa la vikosi vya RSF ndani ya Sudani lilikuwa siyo tu kupambana na vikundi vya waasi vilivyokuwa vikijitokeza, lakini pia kuleta uwiano na Jeshi la Sudani kwa lengo la kulidhibiti lisiasi, ikizingatiwa kwamba tangu mwaka 2011 baada ya kuisha kwa vita na Sudani Kusini ilihofiwa jeshi lingepindua Serikali kwa kuwa lilikuwa na muda zaidi katika kujihusisha na mambo ya ndani.

Ili kuwapa nguvu RSF, Bashir alimwezesha Dagalo kumiliki shughuli nyingi za kiuchumi, ikiwemo uchimbaji wa dhahabu, ili aweze kuviendesha vikosi hivyo. Mbaya zaidi, vyanzo hivyo vya fedha viliwekwa chini ya familia ya Dagalo na ndugu zake wa damu, na siyo chini ya taasisi hiyo ya kijeshi.

Lakini kutokana na joto la kisiasa na wimbi kubwa la kudai mabadiliko liloongozwa na raia, majenerali wawili hawa, Al-Burhan wa SAF, na Dagalo wa RSF, badala ya kudhibitiana, waliweza kuungana na kuiangusha Serikali ya Al-Bashir hapo Aprili 2019 kufuatia maandamano makubwa ya wananchi.

Matumaini, hofu Sudani

Uhaini huu wa kijeshi ulitoa matumaini kwa baadhi ya wananchi, japo wengi waliyoielewa historia ya nchi yao waliendelea kushinikiza jeshi kujiondoa kabisa kwenye Serikali na kupisha utawala wa kiraia.

Kutuliza wingu hilo la wananchi wenye msimamo mkali, iliundwa Serikali ya Mpito, ambapo Burhan, aliyekuwa Brigedia Jenerali wa Jeshi la Sudan, alifanywa Mwenyekiti wa Serikali na Dagalo, aliyekuwa mkuu wa vikosi vya RSF, aliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.

Baraza hili la Serikali ya Mpito liliwajumuisha raia kutoka asasi za kiraia zilizoongoza mapambano dhidi ya Serikali ya Bashir, kwa makubaliano kwamba Serikali ya Mpito itakoma baada ya miaka mitatu, na Serikali ya kiraia itachukua hatamu baada ya uchaguzi huru.

Hata hivyo, haya hayakuwezekana kwani miezi takribani 22 baada ya kuundwa kwa Serikali ya Mpito, majenerali hawa walifanya mapinduzi mengine ya kijeshi kwa kuwaondoa viongozi wote wa kiraia kwenye Serikali hiyo hapo Oktoba 2021.

Viongozi hawa wa kijeshi waliyafanya haya, kimkakati sana, kwani kimataifa walijaribu kurudisha uhusiano na karibia nchi mahasimu wote, ikiwemo Marekani. Pengine lengo lao lilikuwa ni kupunguza kelele kutoka jumuiya za kimataifa endapo watachukua hatua kinyume na makubaliano na makundi ya kiraia.

Fahari wawili … 

Hali ya kutokuaminiana kati ya majenerali wawili hao inatajwa kuanza tangu mwaka 2022 baada ya kusemekana kiongozi wa nchi hiyo, Al-Burhan, kuanza kuwarejesha kwenye madaraka baadhi ya waliokuwa watu wa karibu wa utawala uliopita wa Bashir.

Lakini kuibuka kwa mapigano yanayoendelea hivi sasa nchini humo, kwa kiasi kikubwa, kumechagizwa na pendekezo la kurudisha raia katika Serikali ya mpito, huku vikosi vya SRF vikitakiwa vijiunge na SAF, hatua ambayo ingemuondolea nguvu Dagalo ambaye tayari ameanza kuonja utamu wa kuwa kiongozi wa kitaifa.

Wapiganaji wa SRF wenye uzoefu wa kupigana vita vya jangwani na msituni walijikusanya jijini Khartoum  kwa kasi mapema mwezi Aprili kupambana na vikosi vya SAF kujaribu kuchukua udhibiti wa maeneo muhimu ya Serikali, wakipata upinzani mkubwa kutoka kwa SAF yenye mafunzo na uzoefu mkubwa wa kulinda maeneo muhimu ya nchi.

Pamoja na ukweli kwamba SAF ina rasilimali na uwezo mkubwa wa kuendelea kudhibiti maeneo muhimu ya Serikali, hata kama watafanikiwa kuwaondoa kabisa SRF maeneo ya mijini, bado hawataweza kuwadhibiti SRF ambao wana uzoefu mkubwa wa vita vya jangwani na msituni.

Hali hii inaweza kupelekea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudani kudumu kwa muda mrefu na hivyo kushindwa kutoa nafasi ya kurudishwa kwa Serikali ya kiraia katika kipindi cha karibuni.

Pia, hata kama SRF itawashinda SAF katika mapigano haya, ni ngumu sana kutabiri nini hasa kitafuata nchini Sudani ikizingatiwa wanamgambo hawa kisiasa hawana mtazamo wowote unaoelezea ‘mradi wao wa kijamii’ hasa ni nini, na una malengo gani kwa watu wa Sudan.

Wengi wa wapiganaji hawa ni kutoka jamii zilizotengwa za Sudani zilizotumika kwenye mapigano huko Darfur, lakini wengi wao wakiwa hawana elimu rasmi na uzoefu wa kiutawala kama wenzao wa SAF.

Huu ni mtanzuko mkubwa wa kisiasa kwa watu wa Sudan, hususani makundi ya wafanyakazi, wakulima na wavujajasho wote wa Sudan ambao walianza kupata matumani ya mabadiliko kufuatia kuanguka kwa Serikali ya Bashir mwaka 2019.

Joel Ntile ni mwanamajumui wa Afrika na mchambuzi wa masuala ya kijamii-uchumi. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia barua pepe yake ntilejoel@protonmail.com au kupitia Twitter @NtileJoel. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi msimamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts