Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (Mstaafu) wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad, amehusisha kushamiri kwa vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma na aina nyingine za ufisadi serikalini, akisema hali hiyo inatokana na watu wanaothibitika kufanya vitendo hivyo kutokuchukuliwa hatua za kisheria.
Profesa Assad, ambaye kwa sasa anahudumu kama Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Kiislamu Morogoro (MUM), alitoa tathmini yake hiyo wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika nyumbani kwake, Dar es Salaam, hapo Mei 14, 2023.
“Kila mtu anamuona mtu ambaye aliiba pesa anaendelea na maisha yake, na ameonekana amefanikiwa, na ndiyo maisha,” Assad alisema kwenye mahojiano hayo. “Kwa hiyo, kila mtu anaiga namna hiyo, kwamba kuiba pesa, ukashinda kesi mahakamani, ni rahisi [kushinda kesi], kwa hiyo, wanaendelea watu kufanya mambo ambayo siyo vizuri kuyafanya.”
“Kwa hiyo, adhabu ni jambo la muhimu sana kuhakikisha kwamba watu wote, kwa lazima au kwa hiari, wanafuata mtazamo ambao unaendana na maadili ya nchi yetu,” aliongeza Profesa Assad ambaye Mahakama ilitamka hapo Disemba 5, 2023, kwamba kuondoshwa kwake ofisini, mnamo Novemba 3, 2029, kulifanyika kinyume na Katiba.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo, na hapa Profesa Assad anaeleza kwa nini alikubali kufanya mahojiano na The Chanzo:
Mussa Assad: Asante sana. Mimi naiichukua hili kama mkazi yangu. Ni jukumu letu sisi [viongozi wastaafu], kama tuna cha kuchangia katika jamii, tuchangie kwa jamii. Kwa hiyo, kwa namna hiyo, hili ni jambo ambalo na mimi mwenyewe nalifurahia vilevile.
The Chanzo: Kwa kiasi kikubwa, Watanzania kusema kweli, wanakuchukulia wewe kama mtu muadilifu sana, na kusema kweli nikijaribu kukumbuka mchakato huu ulivyoanza, mpaka tunakaa hapa, nadhani nashawishika kuamini hili pia, profesa.
Mussa Assad: Kwa kweli hiyo ni maoni ya watu, na sisi kama Waislamu haitoshi kuwasikiliza watu, unatakiwa ujipime wewe kwa kumtazama Mwenyezi Mungu peke yake.
Kwa hiyo, kila siku unajipima na kujitathimini kwamba je, leo hujafanya chochote ambacho Mwenyezi Mungu hakiridhii ili uhakikishe kwamba kila unachokifanya Mwenyezi Mungu anakiridhia, na kwa kweli huo ndiyo mtazamo wangu wa maisha.
Kila mara naangalia jambo hili linafaa au halifai. Najitahidi sana kufanya lile ambalo linafaa na ikitokea nimefanya ambalo halifai, najitahidi sana kurekebisha na kufanya lile ambalo linafaa. Kwa namna hiyo, nafikiri ndiyo maana watu wanaona kwamba huenda huyu bwana ana uadilifu fulani na kwa kweli tunashukuru kwa mtazamo huo.
The Chanzo: Kwa sababu tumeanza haya mahojiano kidogo na masuala binafsi, kama utaniruhusu, naweza nikaendelea hapo kidogo?
Mussa Assad: Hakuna tatizo.
The Chanzo: Tukirudi kwenye mitazamo ya watu pia, wakiangalia kile ambacho kilitokea mpaka wewe kuondoshwa kwenye nafasi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, maoni ya baadhi ya wananchi wanahisi kwamba wewe hukutendewa haki, na wewe pia ni muumini wa hilo, kwamba unahisi hukutendewa haki kwenye mchakato mzima ulivyotokea na tukumbuke pia kuwa Mahakama pia ilikuja ikatoa uamuzi kwamba ulitolewa kwenye nafasi ya CAG bila kufuata Katiba [ya nchi]. Unadhani pia na wewe una hizo hisia kwamba ulitendewa ndivyo sivyo?
Mussa Assad: Kwangu mimi sina wasiwasi [kwamba sikutendewa haki]. Kwa hiyo, si jambo la hisia. Kuanzia siku ya mwanzo kabisa, na hata kabla uamuzi haujafanyika, nilikuwa nahisi huenda jambo hili litatokea na kwa kweli nilishauriana na wanasheria wengi sana na kila niliyeshauriana naye aliniambia hili jambo haliwezekani kufanywa.
Lakini lilifanywa. Kwa hiyo, mimi tafsiri yangu ile ilikuwa ni dhuruma kwangu mimi na kwa chombo kile cha Taasisi ya Ukaguzi ya Tanzania. Kwa hiyo, si kwamba-, kwangu mimi si jambo la haki tu. Mimi ninaamini dhuluma ilifanyika.
The Chanzo: Asante sana, Profesa, na ni kwa kipindi hiki hiki, Watanzania, kwa mamia yao, walionekana kusimama na wewe na angalau-, hakukuwa na maandamano mtaani, lakini katika ulimwengu ambao ni wa mitandao, hili lilikuwa linaonekana na nataka kufahamu ulikuwa unaiona hii, unauona huu mshikamano ambao watu walikuwa wanauelezea juu yako kulingana na ile hali ambayo ulikuwa unaipitia wewe kama mwananchi?
Mussa Assad: Kwa kweli, mimi huu ni mwaka wa nne sasa, na kwa mtazamo wangu, kila ninapotembea, na mimi ni mtembezi sana mjini humu na nje ya Dar es Salaam, nimekutana na watu wengi sana ambao kweli, naweza kusema, ni watu wanaoniunga mkono na ni marafiki zangu kwa kweli, na ni kwa sababu tu waliona kwamba msimamo wangu ulikuwa ni msimamo sahihi na si kwamba ni hisia tu katika mitandao ya kijamii, lakini nakutana na waendesha pikipiki [maarufu kama] bodaboda.
Nakutana na watu misikitini. Nakutana na watu barabarani. Nakutana na watu katika nyanja nyingi za maisha na wote, kwa ujumla, yaani kwa kweli sijawahi kutana na hata na mtu mmoja ambaye kwa kweli anasema ulichofanya siyo sawasawa. Kwa hiyo, kwa kweli nafikiri na mimi watu wengi walikuwa wakiniunga mkono na kwa hilo kwa kweli nashukuru sana na kuna watu nakutana nao wanakufanyia dua na hilo, kwa kweli, ni jambo ambalo kwa kweli lilinifanya nikapata moyo mkubwa wa kuvumilia vitu vingi sana.
The Chanzo: Lakini kile kilichotokea, ilikuwa ni kitu ulichokuwa umekitarajia labda, pengine ulipopewa ile wadhifa au ile dhima?
Mussa Assad: Ni kweli kwamba, unajua ukisoma Katiba inasema kabisa, kama ilivyosema Mahakama, kwamba umri wa kustaafu ni miaka 60 au umri wowote ambao utatajwa na sheria, na sheria imetaja umri wa miaka 65. Kwa hiyo, mimi nilikaa katika nafasi ile nikijua nitakaa mpaka nitakapofikisha miaka 65.
Na, kwa kweli, mimi katika nafasi ambazo nilizikubali moja kwa moja likuwa ni hiyo. Kabla ya hapo, nakumbuka niliwahi kutajwa katika nafasi nyingine na nilizikataa na niliwaambia watu sitaki kwenda serikalini kwa sababu sina uhakika wa ajira yangu serikalini, nafurahi sana kukaa hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na nilikuwa na nia ya kukaa Chuo Kikuu cha Dar es salaam miaka yangu yote mpaka nitakapo staafu.
Lakini nilivyoitwa nakumbuka wakati ule na Balozi [Ombeni] Sefue, alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, kuniambia jambo hili, nilimwambia kwa nafasi hii, kwa sababu ya nafasi ya kikatiba, mimi nitaichukua kwa sababu ina ulinzi wa kikatiba katika kuondoshwa katika nafasi hii.
Kwa hiyo, nitaichukua na baada ya kuachana nayo alitangaza nafasi ile na kweli niliichukua kwa mtazamo huo kwamba nafasi hiyo nitaichukua mpaka nitakapotimiza umri wa miaka 65. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema, lile lililotokea si jambo la kawaida na, kwa kweli, kama Mahakama ilivyosema, lilikuwa ni kinyume na Katiba.
The Chanzo: Na ilikushangaza kidogo, [au] kukushitua?
Mussa Assad: Haikunishangaza kwa sababu nilipewa taarifa, siyo za moja kwa moja, lakini ulikuwa unajua. Kwa mfano, siku moja kabla, kuna mtu alinipigia simu akaniambia kesho saa nne kuna tangazo litatolewa na linakuhusu wewe, na nilikuwa niko Mwanza mjini na kama saa moja kabla ya tangazo lenyewe akanipigia mtu mwingine, akaniambia katika saa moja lijalo tangazo litatoka na wewe utatolewa katika nafasi yako, atateuliwa mtu mwingine.
Kwa hiyo, haikunishangaza kwa kweli. Ni jambo ambalo nililitegemea kwa sababu ya fujo zilizokuwepo wakati ule na, kwa kweli, lilitokea, na baada ya pale, kama walivyoona watu wengi, tulimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu yeye ndiye anayepanga mipango yote.
The Chanzo: Swadakta!
Mussa Assad: Kupata mimi kazi, kukosa kazi, kufanya chochote kinachoweza kufanyika, si mambo yangu mwenyewe. Ni mambo ambayo Mwenyezi Mungu anayapanga na tulishukuru kwa namna hiyo, na tangu siku ile tumekuwa tukifanya dua na, kwa kweli, Mwenyezi Mungu anazijibu dua za watu.
The Chanzo: Profesa nakushukuru sana, nilikuwa na hamu ya kutaka kupata [huo ufafanuzi]. Labda tuzungumzie hii taasisi sasa ya CAG. Nilikuwa nataka kufahamu labda kama inawezekana, ilikuwaje kuwaje, kwa mfano, mpaka Tanzania ikawa na ofisi ya CAG na pengine kuanzishwa kwake kulilenga kufanikisha kitu gani?
Mussa Assad: Kwa kweli, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ilianzishwa tangu enzi za ukoloni, na baada ya uhuru alikuwepo Mwingereza mmoja ambaye nafikiri alikaa miaka miwili, 1962 mpaka 1964. Halafu akawekwa Mtanzania ambaye alikaa mpaka mwaka 1996, nafikiri, mzee [Mohamed] Abood.
Halafu akaja bwana marehemu [Thomas] Kiama, halafu wakaja na wengine na wengine. Kwa hiyo, siyo ofisi iliyowekwa baada ya uhuru. Ilikuwa ni ofisi iliyokuwepo kabla ya uhuru na kazi yake kubwa ni ile ya kudhibiti matumizi ya Serikali lakini, vilevile, kufanya ukaguzi ili kuweza kupendekeza maeneo ambayo, kama kuna udhaifu, yafanyiwe kazi ili kazi za Serikali katika mapato na matumizi ziwe na manufaa makubwa kwa taifa.
Kwa hiyo, hizo ndiyo kazi muhimu za Taasisi za Ukaguzi wa Tanzania, na tangu wakati huo mpaka leo, kazi ni hizo hizo: kufanya udhibiti baada ya bajeti ya Serikali kupitishwa, yale mafungu, kuhakikisha kwamba kila zinavyotumika, au pesa inavyotoka, Mdhibiti na Mkaguzi anaweka sahihi yake pale.
Lakini, vilevile, kufanya ukaguzi wa Serikali za Mitaa. Kufanya ukaguzi wa mafungu yote [ya kibajeti] ya Serikali Kuu, na kufanya ukaguzi wa mashirika ya umma vilevile. Kwa hiyo, hizo ndiyo kazi za msingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Tanzania.
Na [kazi hizi] zilikuwepo tangu Katiba ya mwanzo ya mwaka 1977, na mpaka marekebisho ya Katiba, na nafikiri itaendelea kuwepo kwa namna hiyo hiyo.
The Chanzo: Na si taasisi ya kiupekee, kwamba ni Tanzania tu.
Mussa Assad: Katika nchi zote za dunia hii, sifahamu kama kuna nchi ambayo haina mtu wa nafasi hiyo. Uingereza ana nafasi kama hii anaitwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu, na Canada nafasi ni hiyo hiyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu.
Marekani wana taasisi hii lakini kwa jina tofauti kidogo na nchi zingine wana majina tofauti. Lakini kazi ni hizo hizo: kudhibiti na kukagua hesabu za Serikali na vyombo vyote ambavyo vipo chini ya Serikali.
Kwa hiyo, ni taasisi ambayo ipo katika nchi zote. Katika Afrika hii, kwa mfano, nchi zote zina nafasi hii na mpaka kuna Umoja wa Afrika Wa Wadhibiti na Wakaguzi Wakuu wa Hesabu za Serikali.
Isipokuwa kuna nchi ambazo zimeondoa ile nafasi ya mdhibiti kutoka katika ukaguzi na kuna mtu anaitwa Mdhibiti wa Bajeti, tofauti na Mkaguzi Mkuu, na hilo naamini lipo Kenya. Uganda bado wana Mkaguzi Mkuu, hawana Mdhibiti, wana Mkaguzi Mkuu.
Na kuna Mdhibiti wa Bajeti vilevile, na nchi nyingi zinafanya namna hiyo. Tanzania, nafikiri, hatujakubali kufanya hivyo. Kwa hiyo, bado tuna Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [ambayo], kama nilivyosema mwanzo, ni taasisi ambayo inaishi katika nchi zote za Afrika hii. Sikumbuki hata nchi moja ambayo haina nafasi hiyo.
The Chanzo: Na labda kiutaratibu, kumekuwa na hoja nyingi, au majadiliano, miongoni mwa wadau wa matumizi sahihi ya fedha za umma, kwamba kiutaratibu CAG, ambaye ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, aripoti bungeni, asiwe anaripoti kwa Rais, wakisema kwamba pengine huo ni utaratibu uliopo kwenye Jumuiya ya Madola.
Nilikuwa nataka kufahamu ndivyo hivyo, kwamba sisi utaratibu tumeugeuza kidogo kwa sababu sisi CAG anawasilisha ripoti yake kwa Rais kwanza halafu ndiyo anawasilisha bungeni? Wapo watu wanasema kwamba inatakiwa ripoti ipelekwe bungeni kama kutakuwa na uwajibishwaji vifanyike kule. Nilikuwa nataka kufahamu hiyo imekaaje kiutaratibu?
Mussa Assad: Kiutaratibu sioni kama kuna tofauti mimi kwa sababu anapopokea ripoti ile yule Rais, Katiba inamtaka siku hiyo hiyo, kabla ya kikao kinachofuata cha Bunge, ahakikishe imewasilishwa bungeni, na inasema Katiba kwamba asipofanya kazi hiyo, yule Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu mwenyewe anaweza kuiwasilisha bungeni.
Kwa hiyo, sioni kama kuna tatizo hapo. Kuripoti kwa Rais haimanishi kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anafanya kazi chini ya Rais. Kuna masharti katika Katiba na kama akifanya kazi yake sawasawa pale hana tatizo kwamba anaripoti kwa nani.
Lakini kawaida, katika nchi zingine, zile ambazo, kwa mfano, uteuzi wa nafasi hii lazima upitishwe na Bunge, basi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu anaripoti, anakuwa ni Afisa wa Bunge, na utaratibu huo upo katika nchi nyingi tu, lakini hapa kwetu tumeamua kwamba Rais ndiye anayeteua, na kwa kweli, Rais ndiye anayepokea ripoti na Rais ana jukumu la kupeleka ripoti bungeni na Bunge linafanya kazi yake kama kawaida.
Kwa hiyo, sioni kama kuna tatizo kubwa ingawaje unahisi kwamba huenda Bunge lingependa sana Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu aripoti kule. Kwa sababu nakumbuka kuna wakati yule bwana Spika [mstaafu, Job Ndugai], alisema huyu ni mfanyakazi wa Bunge, wakati haikuwa hivo.
Mimi kwa nafasi ile [ya CAG] sikuwa mtumishi wa mtu yeyote na Katiba inasema kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali hatapokea maagizo, au maelekezo, kutoka kwa afisa yeyote au idara yeyote ya Serikali.
Kwa hiyo, kwa namna hiyo, ni mtu ambaye ni mtu huru kabisa. Anafanya kazi yake mwenyewe na kufanya kama avyotaka, isipokuwa tu asiende kinyume na maadili, na zile sababu zingine ambazo zimetajwa katika Katiba kama ni sababu ambazo zinaweza kumtoa katika madaraka yake.
The Chanzo: Profesa, wewe ulikuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ulipata nafasi ambayo Watanzania wengi hatuna, ya kukagua hizi ofisi, kutembelea, kuhoji watu na nini. Na nilikuwa nataka kufahamu, bila shaka ni kwa sababu ya baadhi yetu tunaamini hivyo, unadhani wewe kama CAG mstaafu unadhani kuna nia ya dhati ndani ya Serikali ya kuweza kuzuia matukio kama haya ya ubadhirifu kutokujitokeza?
Mussa Assad: Mimi nafikiri kwamba hilo swali unaweza kulijibu kwa kutazama hizi awamu tofauti tofauti. Kwa hiyo, kuna awamu fulani ulikuwa unaona kwamba kuna msukumo wa kuwachukulia hatua watu na kuna wengine unaona kwamba huenda labda ule msukumo umepungua kidogo.
Kwa hiyo, kwa namna hiyo unaweza kusema kuna tofauti kidogo katika uchukuaji wa hatua. Lakini mimi naamini kwamba hatua zichukuliwe pale ambapo ukaguzi umeonyesha wazi kwamba kuna ubadhirifu katika maeneo kadhaa kadhaa. Lakini pale ukaguzi unapotoa maoni ya jumla, kunakuwa na tatizo kidogo, nafikiri.
The Chanzo: Tatizo la?
Mussa Assad: Nakumbuka mimi kesi moja ambayo ilitokea na huyu Mkurugenzi Mkuu alikuwa mwanafunzi wangu, akawa Mkurugenzi Mkuu wa shirika, halafu ripoti yetu ilisema kwamba alikiuka Sheria ya Manunuzi [ya Umma], ambayo ilikuwa ni kweli, alikuwa amekiuka Sheria ya Manunuzi.
Kwa hiyo, ripoti ikasema namna hiyo, halafu akaja ofsini kwangu akaniambia, Profesa hili jambo halikuwekwa sawasawa, kwa sababu mimi nilikiuka lakini sababu ni kwamba nilichukua uamuzi ambao ulikuwa unaokoa fedha. Kwa hiyo, sikufuata sheria lakini niliokoa fedha.
Nikamwambia niletee ushahidi, akaniletea ushahidi, na nikawaambia watu wangu [kwamba] siku zote jamani siku zote kama mnafanya ukaguzi lazima utoe muktadha sahihi. Uelezee tatizo, lakini kuna na faida zimepatikana, pia uelezee kulikuwa na faida ambayo imepatikana ili mtu aweze kufanya uamuzi akitazama ramani yote ya jambo lilivyokuwa.
Kwa hiyo, huo ndiyo ushauri wangu vilevile, kwamba sasa hivi katika ukaguzi wetu tujibu haya maswali ya kitu gani kimtokea? Kimetokea wapi? Kimetokea kwa namna gani? Kwa nini kimetokea? Ukishajibu haya, kimetokea kwa namna gani, na kwa nini kimetokea, baada ya hapo una uwezo wa kusema sasa, utatuzi wa tatizo hili ni kadhaa, kadhaa, kadhaa.
Ukishakua umejibu maswali mawili ya mwanzo, [yaani] kimetokea wapi [na] lini? Haitoshi hiyo. Sasa wasiwasi wangu ni kwamba sisi vitu vingi tunavyoviona ni kimetokea wapi [na] lini. Kimetokea kwa namna gani na kwa nini kimetokea, haya maswali mawili hatuyajibu vizuri.
Kwa hiyo, unaona kwamba kunakuwa na wasiwasi wa mapendekezo yenyewe. Kwa hiyo, tatizo unaliona ni hapo, kwamba kimetokeaje na kwa nini kimetokea? Haya maswali tuyajibu vilevile ili kuwapa wasomaji taswira nzima ya tatizo lenyewe ili waweze kuona kwamba mapendekezo ya mkaguzi yanaelekea kutatua tatizo lenyewe.
Hilo, nafikiri, ndiyo jambo ambalo, kwa mtazamo wangu, ni jambo ambalo hatulifanyi sawasawa na tunatakiwa kulifanya sawasawa.
The Chanzo: Vipi kuhusu uwajibikaji?
Mussa Assad: Uwajibikaji, kwa kweli, ni jambo ambalo mimi binafsi naliona ni tofauti ukitazama eneo la Serikali na eneo la sekta binafsi, [yaani] sekta binafsi na sekta ya umma.
Kwa sababu baada ya kutoka katika nafasi yangu, nimekuwa natazama sana kwa kweli maisha na kila ukipita unaona kwamba katika sekta ya umma kuna tatizo la kuoanisha ufanyaji kazi na mshahara.
Nilikuwa natoa mfano wa soko fulani hivi liko nje ya Dar es Salaam kidogo, soko la samaki, na mimi huwa napita sana pale kununua nunua samaki, hata leo nimepita pele kununua samaki, na kama mara nne zilizopita kila nikiingia pale kuna kijana anakata tiketi za kuweka gari mule ndani.
Kila ukitoka pale [nje ya soko], unaambiwa yule kijana hayupo, msubiri kidogo, kwamba kaenda mahala mpaka aje pale, akija tena aanze kuwarekodi, atoe tiketi yako, umpe Shilingi 1,000, anachukua [Shilingi] 1,000, anendelea.
Sasa mara ya kwanza nilimwambia wewe kijana hiki unachokifanya siyo sawasawa. Hujui kwamba mshahara wako unatokana na mapato haya tunayoyakusanya hapa? Ukikusanya mapato hapa ndiyo mshahara wako unalipwa. Kaa hapa hapa getini ukusanye pesa ili upate mapato makubwa zaidi.
Mara ya pili nikakuta jambo hilo hilo, haji. Mara ya tatu, haji. Mara ya nne, vilevile hakuja. Leo nimemkuta pale getini. Kwa hiyo, unaona angalau kuna marekebisho yamefanyika. Lakini [ni] tatizo kubwa sana katika sekta ya umma. Watu hawaoanishi kazi anayoifanya na mshahara wake, yaani huduma kwa mteja, yule mteja kumuhudumia kwamba lile ndilo jambo ambalo linampa yeye mshahara, halipo, na utaliona sehemu nyingi sana kwa kweli.
Toka hapa leo nenda shirika lolote la umma ambalo linatoa huduma. Simama pale uone, hakuna atakaye kufuata. Halafu toka nenda shirika la simu la binafsi, ukiingia tu utakaribishwa, [na kuulizwa], “tukusaidie nini?” Ukitaja jambo unalolitaka, watakwambia nenda kwa fulani pale, utapata mtu atakusaidia.
Kwa hiyo, tulichokuwa tunakisema ni kwamba sekta binafsi kuna mtazamo ambao unamfanya mfanyakazi aone kwamba huduma anayoitoa kwa mteja ndiyo jambo ambalo linalompa mshahara yeye. Sekta ya umma huo mtazamo ni tofauti kidogo, haupo.
The Chanzo: Labda mtu anaweza akijiuliza, hiyo sasa iinachochea vipi vitendo vya ubadharifu kwenye taasisi za umma?
Mussa Assad: Mimi, [kwa] tafsiri yangu, huo wenyewe ni ubadhirifu. Yaani kukaa ofsini usifanye kazi inayostahiki na kupata mshahara, huo kwangu pekee yake ni ubadhilifu, acha mambo mengine. Kupata mshahara ambao huustahili, kwa tafsiri yangu, huo ni ubadhirifu. Kwa hiyo, tuanzie hapo kwanza.
Kila mtu anatakiwa atoe jasho na alipwe kutokana na jasho lake. Kama mtu hafanyi kazi inayotakiwa, kwa kweli, anatakiwa asipate mshahara ambao analipwa. Kwa mfano, hata ofsi kufungua tu, unaweza kwenda mahala sekta binafsi saa 8:30 ofisi imefunguliwa. Sekta ya umma unaweza ukakuta mpaka saa nne mtu hajafika bado, au amefika lakini amekwenda kunywa chai kwanza kabla ya kufanya kazi.
Yaani ukifika sekta ya umma unaweza ukakuta mkuu asubuhi analetewa supu, chapati na chai, anakunywa kabla ya kuanza kazi, na kwa gharama za Serikali. Sasa unajiuliza, mtu huyu huko nyumbani kwake hakunywa chai, kwa nini anakuja ofisini na kunywa michuzi katika ofisi?
Lakini imekuwa sasa hivi inakubalika kwamba ni jambo la kawaida. Wakati mimi naamini si sawa. Huo kwangu vilevile ni ubadhirifu, inatakiwa mtu anywe chai nyumbani kwake, apige gari moto, aende ofisini, akifika ofsini afanye kazi.
Kwa hiyo, sisi, nafikiri, ninavyosema, mtazamo wetu katika sekta ya umma ni tofauti sana na matazamo katika sekta binafsi. Sekta binafsi unalipwa kwa jasho lako. Sekta ya umma unaweza kulipwa bila kufanya kazi kabisa, au ukafanya kazi nusu na bado utalipwa mwisho wa mwezi.
Na kitu kingine ambacho nafikiri ni tatizo kubwa ni namna ya kumtoa mfanyakazi [kwenye utumishi]. Sekta binafsi, ukiharibu kazi, siku hiyo hiyo unapewa cheki yako ya mwisho na malipo yako, unaondoka, mnapeana mikono, kesi imeisha. Sekta ya umma kumfukuza mtu kazi ni kitu kizito mno, yaani ni jambo ambalo, kwa kweli, mimi nafikiri haliwezekani. Inawezekana lakini kwa kufuata utaratibu ambao ni mgumu sana kufanya.
Nakumbuka rafiki yangu mmoja mimi alikuwa akifanya kazi katika shirika la mafuta na alikuwa na kampuni yake binafsi ya mafuta. Ikagundulika kwamba katika kampuni ile wanajua kwamba ana kampuni yake ya mafuta na anachukua wateja kuwapeleka katika kampuni yake binafsi na siku hiyo hiyo mkurugenzi wake alipogundua jambo hilo saa hiyo hiyo alimfukuza kazi, na tangu siku hakuwa na kazi na mpaka leo, anaendelea na biashara zake.
Lakini unaona mtazamo wa sekta binafsi, kwamba ukiwa na mgongano wa masilahi, saa hiyo hiyo kazi inaondoka. Sekta ya umma unaweza ukawa na mgongano wa masilahi na bado utaendelea kufanya kazi, inakuwa vigumu sana kumfukuza mtu kazi.
Kwa hiyo, hayo mambo mawili yanachangia sana ubadhirifu, nafikiri. Lakini vilevile naamini kwamba ubadhirifu unaendana na mwenyewe amejengeka vipi kimaadili na maadili mimi naamini yanajengwa tangu utotoni kabisa, yanajengwa hasa kwa kuiga wazazi wako, kwa kuiga kaka zako na kwa kuambiwa na wazee wako kitu gani kinafaa na kitu gani haifai.
Vilevile maadili yanajengwa na dini, kama ni mtu ambaye dini kwako ni umuhimu, utaona kwamba kuna vitu vinakataza na kuna vitu havikatazwi. Vile vinavyokatazwa utaviacha, vile ambavyo ni halali kuvifanya, unavifanya. Sasa ukiwa mtu ambaye mlengo wako wa kimaadili uko namna hiyo, utaona katika maisha yako hupati shida sana ya kufuata vitu ambavyo taifa linavitaka.
Ukiwa umejengwa katika mlengo ambao unaendana kinyume na maadili ya dini na ya wazazi wako, kama wazazi wako walikuwa sawasawa, utaona pia katika maisha yako vilevile utakuwa ni mtu ambaye una shida shida kidogo kufuata maadili.
Tunaona watu ambao tumesoma nao, ambao walikuwa wakorofi korofi, wameendelea kuwa wakorofi mpaka mwisho, na wengi kati yao wameenda mpaka jela kabisa kwa sababu maadili yao hayakuwa sawa sawa.
Na wale ambao walikuwa wazuri wamekuwa wazuri, wengine wamekuwa Mapadri, wamekuwa Mashehe, wamekuwa viongozi wetu mpaka leo hii. Kwa hiyo, hayo mambo matatu muhimu, yaani lile la utotoni umefundishwa vipi? Kujali kazi yako na uwajibikaji. Yote haya ni mambo yakuchangia katika maadili.
Lakini vilevile jambo la nne ni adhabu. Kwa sababu adhabu pia inarekebisha. Nakumbuka mimi kama miaka 20 iliyopita, Iran ukibaka, una uwawa, na kuuwawa kwako ni kwamba unapelekwa katika mlima, na utasukumwa, utaanguka mpaka chini. Ukipiga kichwa, [au] ukipiga kiuno, umevunjika vunjika, na diyo kifo chako, na watu wote wataletwa pale kuona jinsi unavyouwawa.
Sasa kama umekuzwa katika namna ambayo unafikiri, unahisi, unaweza kubaka, likishakuja wazo la kubaka tu, ile picha ya kutupwa katika mlima itakuja, na lile litakuzuia. Kwa hiyo, naamini adhabu inaweza kabisa kuzuia namna fulani ya utovu wa maadili.
Sasa kama adhabu hakuna, tunafika hapa tulipofika sisi sasa hivi, kwamba kila mtu anamuona mtu ambaye aliiba pesa anaendelea na maisha yake, na ameonekana amefanikiwa, na ndiyo maisha. Kwa hiyo, kila mtu anaiga namna hiyo, kwamba kuiba pesa, ukashinda kesi mahakamani, ni rahisi [kushinda kesi], kwa hiyo, wanaendelea watu kufanya mambo ambayo siyo vizuri kuyafanya.
Kwa hiyo, adhabu ni jambo la muhimu sana kuhakikisha kwamba watu wote, kwa lazima au kwa hiari, wanafuata mtazamo ambao unaendana na maadili ya nchi yetu.
The Chanzo: Sasa, kwa mfano, watu ambao wanathibitika kuwa wabadhirifu, ni adhabu gani ambazo [wanapaswa kupatiwa]?
Mussa Assad: Sheria [za nchi] zimepanga adhabu za watu wote ambao wamethibitika kwamba ni wabadhirifu. Hilo sheria imeainisha. Kwa hiyo, kuna adhabu ambazo zipo katika sheria na hizo zinatakiwa zitolewe.
Tatizo ninaloliona ni kwamba huko kuthibitisha hakufanyiki kwa sababu taasisi zetu, ama hazifanyi uchunguzi unaotakiwa, au haziwasilishi ushahidi unaotakiwa [mahakamani], au Mahakama zenyewe hazitoi adhabu zinazostahili kwa wahusika.
Kwa hiyo, vitu vitatu vikitokea hivyo: ushahidi haukupatikana, haukuwasilishwa mahakamani, au umepatikana, umewasilishwa, lakini mahakimu wetu hawakufanya kazi zao sawasawa. Zikipatikana sababu tatu hizo, adhabu [kwa mbadhirifu] haiwezi kupatikana.
The Chanzo: Kwa hiyo, Profesa, mtu anaweza akajiuliza, sasa hii hali itaendelea mpaka lini?
Mussa Assad: Itaendelea kwa muda mrefu sana mpaka itakavyotokea hali ya kutostahimili kabisa mambo haya. Kama alivyosema yule mtu wa Singapore, Lee Kwan Yew, [Waziri Mkuu mstaafu], yule waziri mdogo ambaye alikwenda mapumziko kwa kulipiwa na tajiri aliporudi akafungwa.
Sasa ule unakuwa [ni] mfano, hatokei mwingine yeyote akafanya jambo la namna hiyo kwa sababu anajua kwamba hili ni tatizo. Lakini sasa hiyo, kinachotakiwa ni kwamba hata yule kiongozi wenu naye awe anafuata mfano huo huo, yaani anaishi kimaadili, yaani watu wote wako sawasawa.
Kwa hiyo, ukimtazama yule wa juu yuko sawasawa na yule wa chini. Tatizo letu sisi ni kwamba anaweza akatokea kiongozi ambaye tuseme si mwadilifu sana, na wametokeaa watu hao, anasema hiki halafu anafanya kitu kingine.
Sasa yule anakuwa hapati ushirikiano na wenzake kwa sababu anachofanya sicho kile ambacho anatakiwa akifanye, ingawaje anasema mimi nasimamia wanyonge, nafanya kitu hiki, lakini huku pembeni anachukua vitu kwa manufaa yake binafsi.
Umenikumbusha ile-. Zamani kulikuwa na hadithi ya babu paka. Babu paka alikuwa ana tasbih yake ya vichwa vya samaki, akizungusha hivi, mpaka panya wakamuamini kwamba paka sasa hivi hivi vichwa vya samaki havili, wakawa panya wanazunguka pale.
Sasa baada ya muda ikawa panya wanapotea pale mmoja mmoja. Baada ya muda wakagundua kwamba babu paka ile tasbih ni uongo mtupu huo, nia yake bado ni kula panya. Sasa viongozi wetu wana tasibih za vichwa vya samaki, tunaona kwamba hawawezi kula vichwa vya samaki, lakini huku wakipata nafasi wanakula vitu ambavyo si mali yao.
Sasa akitokea kiongozi wa namna hiyo, hamuwezi kuwa na maadili kabisa kwa sababu watu wa chini wanaona, na wataiga vilevile.
The Chanzo: Labda kuna mifano ya kimataifa ambazo Tanzania tunaweza tukazifuata, au kuziiga, kuhakikisha kwamba tunafuata.
Mussa Assad: Zipo. Kama utakumbuka kwamba kuna kesi ya rada ile. Kesi ya rada ilijulikana kwa sababu ya mtu mmoja wa Uingereza aliipata kutokana na miamala ambayo ilifanyika Tanzania, na alivyiona tu akasema hili ni tatizo kubwa na akawakabili watu waliofanya jambo lile, na moja kwa moja wakasema kweli hili ni tatizo na kisheria unatakiwa uende mahakamani, utangaze kwamba kulikuwa na tatizo la rushwa hapa na uitoe ile rushwa, na upewe adhabu.
Kwa hiyo, kuna mitazamo na makubaliano ya kimataifa katika nchi fulani fulani kwamba rushwa haitakiwi popote pale. Sasa hata tukifuata mifano ile tunaweza kwenda vizuri vilevile.
Kwa hiyo, ni kwamba kama ikionekana kwamba kuna dalili za rushwa mahali, basi taasisi za kiuchunguzi zinakwenda chini, na si jambo gumu sana kupata, au kujua kwamba fulani alichukua rushwa. Kwa mfano, kama ni fedha-. Tatizo la kwetu hapa ni kwamba vitu vingi tunafanya kwa fedha taslimu.
Tungekuwa tunahakikisha kwamba vitu havifanyiki kwa fedha taslimu, [kwamba] lazima vipite kupitia mifumo ya kibenki au mifumo ya kidijitali, vingekuwa vitu vinaonekana. Kwa hiyo, mtu ananunua nyumba sasa hivi, ananunua nyumba kwa fedha taslimu. Inatakiwa nyumba isinunuliwe kwa fedha taslimu, kama unanua nyumba peleka hela benki ili irekodiwe, ulipe kodi za watu, na kila kitu. Lakini hakuna anayefuatilia. Sasa hivi unaweza ukanunua nyumba ukalipa fedha taslimu na usipate shida yoyote ile. Kwa hiyo, hilo ni muhimu: kuhakikisha kwamba mifumo yetu inarekodi kila kitu kinachotakiwa kurekodiwa na pia ufuatiliaji unakuwa rahisi zaidi.
The Chanzo: Profesa kama itakuwa nakuelewa, ni kwamba, tangu mwanzo kule ulipozungumza, ni kwamba tatizo letu kama nchi, kwenye suala hili la kukabiliana na ufisadi, au ubadhirifu, ni la kihulka na kitabia na kiutamaduni zaidi kuliko kuwa ni tatizo la kuwa na mifumo, sheria, na taasisi dhaifu, kama nitakuwa nakuelewa.
Mussa Assad: Kuna bwana mmoja anaitwa Peter Ekeh. Peter Ekeh ni mwandishi wa Nigeria, aliandika andiko lake moja na kuchapishwa mwaka 1975, na yule bwana anasema hivi, kwamba kuna tofauti kati ya mtu katika Afrika na Serikali ya Mitaa, yaani Serikali ya nyumbani kwao, na mfanyakazi yule yule na Serikali Kuu.
Serikali ya Mitaa ni jambo lake binafsi kwa sababu yeye anatoka maeneo yale kwa namna hiyo akiwa mfanyakazi wa Serikali ya Mtaa hawezi kuiibia Serikali ya Mtaa kwa sababu anawaibia ndugu zake. Lakini Serikali Kuu ni kitu kingine kabisa.
Kwa hiyo, yule Mnaigeria nasema uhusiano wa Mwafrika na Serikali Kuu ni kwamba Serikali Kuu inaweza kuibiwa ili usaidie jamii yako, na kule kwao ni jambo la kawaida kabisa, na mimi nafikiri kwamba hiyo mtazamo wa kule Nigeria umekuja mpaka huku kwetu kabisa.
Lakini sisi tumezidi kiasi ambacho sasa hata hapa kwetu wizi wa Serikali ya Mtaa unakubalika, wakati inatakiwa kwamba kama unaiibia, kwa mfano, mfanyakazi wa Kilimanjaro Native Cooperative Union, yuko pale hawezi kuiibia taasisi hiyo kwa sababu ni taasisi yake mwenyewe, akiibia watawfuata wazazi wake, bwana mtoto wenu amefanya kadhaa, kadhaa, kadhaa.
Anafuatwa mtoto, anarudisha pesa, mambo yanaisha. Kwa hiyo, hiyo dhana nadhani inaendelea mpaka huku kwetu sisi. Mfanyakazi na Serikali Kuu tunahisia kwamba unaweza ukaiibia hata Serikali Kuu bila tatizo lolote, kwa manufaa yako binafsi, au kwa manufaa ya watu wa kijijini kwako, na hilo, kwa kweli, limekuwa likiendelea kwa muda mrefu sana, ambalo naamini ni tatizo kubwa sana. Sasa, nafikiri, ulichokisema kama nimeelezea vizuri.
The Chanzo: Sasa hiyo inakwambia nini?
Mussa Assad: Inakwambia kwamba, kwa kweli, mtu wetu wa nchi hii anatakiwa afanyiwe kazi, si kizazi hiki, kwa kizazi kinachokuja. Tuwatazame watoto wetu. Tuwatengeneze katika namna ambayo watakuwa watendaji wazuri serikalini.
The Chanzo: Unadhani mwananchi wa kawaida Tanzania ana nafasi yeyote ya kuhakikisha kwamba hivi vitendo vya ubadhirifu havitokei serikalini, mwananchi moja mmoja, unadhani ana nafasi.
Mussa Assad: Mwananchi mmoja mmoja, kama nitasema ukweli, hana nafasi yoyote kwa sababu hana uwezo wa kufuatilia chochote. Wananchi, kwa ujumla wao, wangeweza kufanya kitu na kitu chenyewe kingeweza kufanyika kama tu kuna uwazi katika utendaji wa Serikali.
Sasa, tatizo ni kwamba, mambo mengi ya Serikali tunaambiwa ni siri. Sasa ukishakuwa na usiri katika utendaji wa Serikali, mwananchi wa kawaida hana namna ya kujua kitu gani kinaendelea. Kwa mfano, inatangazwa zabuni ya kusambaza vitu kupeleka vitu, kwa mfano, shirika la reli, limetangaza zabuni.
Wote tumeona lile tangazo la zabuni. Siku ile ya kupeleka zabuni, wote tunaona kwamba fulani na fulani wameingiza zabuni zao, huyu kasema shilingi fulani, huyu kasema shilingi fulani, huyu kasema shilingi fulani. Baada ya kuingiza zile zabuni zinapitishwa kwenye taratibu fulani.
Taratibu ya kwanza ni kuyaifanyia tathimini yale mawasilisho. Sasa likifanya hilo jambo, sisi wananchi wa kawaida hatuoni na hatujui. Inatengenezwa orodha ya watu wanne au watatu ambao wanaonekana wanaweza kupewa kazi hii, sisi wananchi wa kawaida hatujui kitu gani kimefanyiwa tathimini ili wakapatikana wale watatu.
Tunakuja kujua mwisho fulani ndiyo amechaguliwa na atafanya hiyo kazi. Sasa haya mambo yote yangekuwa yapo wazi, na kwa nchi zingine yako wazi kabisa, yaani vikao vya tathimini viko wazi na vinarekodiwa na watu wa kawaida wanaweza kuona. Sasa kukishakuwa kuna uwazi, mwananchi wa kawaida ataona, hapa kuna tatizo, huyu fulani na huyu aliyeleta zabuni wana uhusiano, huyu mkwewe huyu na amekaa katika kikao kile, huyu alitakiwa asikae.
Tungeweza kupiga kelele lakini watu wanamgongano wa masilahi na wanakaa na wanafanya vitu vyao na hakuna namna ya kufanya. Kwa hiyo, mimi nafikiri, wananchi, kwa sasa hivi, hawana uwezo lakini ingekuwa kuna uwazi kati ya utendaji wa Serikali, mwananchi wa kawaida angeweza kuwa na uwezo.
Nakumbuka mimi kama miaka sita iliyopita wakati niko ofisini [kama CAG], niliwahi kutembelewa na mama mmoja kutoka Norway, wakati ule zabuni ya gesi kule Mtwara inatangazwa tangazwa, akaniuliza vipi hii zabuni, tunaweza kuona vitalu gani vinakuwepo hapa?
Nikamwambia bwana kwa kweli hilo jambo lipo serikalini na sisi watu wa ujumla hatujui. [Akauliza], na nani ameshaomba zabuni? Nikamwambia hata aliyetuma maombi mimi sijui. Akaniambia angalia simu yangu. Norway, kwenye simu yake, anaweza kujua vitalu gani, nani inatangazwa na nani anawasilisha na hatua zilizofikia, kwenye simu yake. Kwa hiyo, kuna uwazi mkubwa sana kwa wenzetu ambao sisi hatunao na hilo ni tatizo kubwa sana.
Mfano wa pili, wakati niko ofisini mimi kuliwahi kuwa na shida kidogo na ile shida ilinifanya mimi niwe na ulazima wa kuwasiliana na [CAG] mwezangu wa Sweden kwa kutumia barua pepe. Maana walikuja kwetu, wakagundua kwamba kulikuwa na tatizo la uwasilishaji wa stakabadhi ambazo zilikuwa zimefanyiwa udanganyifu, yaani badala ya milioni tatu ikaandikwa milioni thelathini, na wakanambia mimi kwamba bwana kuna ubadhirifu umefanyika hapa.
Kwa hiyo, nitamtafuta mtaalamu akafanye uchunguzi, tukapata ushahidi, nikamwambia bwana ushahidi umepatikana, hawa watu kwa kweli mimi nitawafukuza kazi, na tukawafukuza kazi wale watu. Sasa hayo yote yakawa yanafanyika na ripoti nikawa nawapelekea wale [wa Sweden] kwa kutumia barua pepe.
Siku moja [yule CAG wa Sweden] akanipigia simu, akanambia bwana kesho kuna gazeti hapa Sweden litaandika hiyo habari ya Tanzania, kwamba ofisi yako kumetokea wizi wa namna kadhaa kadhaa. Nikamwambia bwana imefikaje hiyo habari huko kwenu?
Wakanambia bwana hapa kwetu ukiandika kitu chochote katika barua pepe ya Serikali ni jambo ambalo mtu yeyote ndani ya Sweden hii anaweza kuona. Umeona uwazi wa namna hiyo?
Kwamba mimi naandika barua pepe hapa kumuandikia mwenzangu wa Sweden, ile barua pepe mwandishi wa habari wa Sweden anaweza kuiona na ameiona na anaweza kuingiza katika gazeti lake. Sasa uwazi huo sisi hatuna hapa kabisa.
The Chanzo: Siyo kwamba wananchi tunaweza kuudai?
Mussa Assad: Unaweza kuudai lakini huwezi kuudai katika mfumo huu ambao tunao sasa hivi, ni jambo ambalo lazima liingizwe katika sheria, ikiwezekana katika Katiba, katika sheria, kwamba mawasiliano ya Serikali hayatakuwa siri tena, kila mtu aweze kuona. Lakini nina uhakika itakuwa shida kubwa sana [kwa Serikali] kukubaliana na jambo hilo.
The Chanzo: Kwa sababu gani?
Mussa Assad: Kwa sababu watu wengi katika Serikali wamekuwa wakiishi katika namna ambayo kuna usiri mkubwa katika mambo yao na hakuna anayetaka mambo yawe wazi kabisa.
Nitakwambia jambo moja tu hata, unajua kuna taasisi za binafsi ambazo gari ikitoka getini, mlinzi anasoma umbali, na anaingiza kwenye kompyuta yake pale pale getini, na dereva ataandika amekwenda wapi, kufanya nini [na] kwa kilomita ngapi. Kila siku, na mwisho wa mwezi ripoti ya getini na ripoti ya dereva zinaainishwa vinaonekana pamoja, kwenye sekta binafsi.
Serikalini hilo huwezi kulifanya kabisa. Haliwezekani. Haliwezekani kwa sababu watu miaka yote wamekuwa wakitumia magari kama magari yao binafsi, na uwazi wa namna hiyo hauwezekani katika gari. Je, utawezekana katika vitu ambavyo ni nyeti zaidi? Itakuwa tatizo kubwa zaidi.
The Chanzo: Lakini Profesa, inabidi nikwambie, tangu mwanzo, vile unavyozungumza ni kwamba unaonekana kukata tamaa kabisa, yaani ni kama vile huna matumaini.
Mussa Assad: Kwa kweli matumaini siyo makubwa sana. Siyo makubwa sana kwa sababu ukitazama utaona kwamba katika nchi hii utumishi wa umma umevurugwa sana, na tumepata sasa hivi watu ambao siwaoni kama ni watu ambao wanaweza kutufanyia mabadiliko makubwa. Ndiyo maana naamini kwamba tujitayarishe katika kizazi kijacho, ili wao ndiyo watufanyie kazi hiyo ipasayo. Kwa sababu sisi wenyewe hatuwezi kufanya hiyo.
The Chanzo: Hiyo kazi tunaweza tukaifanyaje?
Mussa Assad: Kwa mfano, mimi nilikuwa Dodoma juzi na jana kwa ajili ya kuangalia mitaala mipya. Kuna kozi mpya inashauriwa iingizwe sasa hivi, kozi ya Maadili, tuwafundishe watoto wetu, tangu wakiwa wadogo, namna ya kuishi sawasawa, nje ya Serikali na ndani ya Serikali, binafsi na katika umma vilevile.
Sasa watoto wale kama tutawakuza sawasawa, wakifikia miaka 18 [au] 20, wakasoma vizuri, wakafika miaka 25 [au] 30 wakafanya shahada zao, huenda wakawa vijana wazuri, watatufanyia kazi hiyo huko tunakokwenda, inshaallah. Lakini kwa sasa hivi, kwa kweli, kwa watu tulionao, itakuwa kazi kubwa sana kufanya mabadiliko.
The Chanzo: Lakini tuna Bunge. Wanachi wanaenda kupiga kura, wanachagua wabunge, wanamchangua Rais. Unadhani mifumo iliyopo ya kidemokrasia, kwa mfano, kama wananchi kupiga kura kila baada ya miaka mitano, haiwezi [kubadilisha hali ya mambo?] Kwa sababu unachokizungunmza ni kwa mradi wa muda mrefu.
Mussa Assad: Ni kweli kabisa.
The Chanzo: Kwa mradi wa muda mfupi, hudhani kwamba angalau wananchi kuwakataa labda wawakilishi wao kwenye sanduku la kura, inaweza ikachochoea mabadiliko kidogo?
Mussa Assad: Hilo kwa kweli silioni kama linaweza kutokea, wananchi kuwakataa [wawakilishi wao] kwa namna gani? Umeona wewe jinsi kura zinavyopatikana nchi hii. [Kuanzia kwenye] kampeni, na zipo mpaka picha watu wanapewa pesa ili wampigie kura mtu fulani, na kuna wakati fulani rafu inafanyika kabisa, fulani ambaye anastahili kupewa hapewi, asiyestahili kupewa, anapewa. Tumeliona [hili] katika chaguzi za chama. Tumeliona katika chaguzi za ubunge.
Kwa hiyo, kwa kweli, kama navyosema kwa watu tulionao sasa hivi sina tamaa kubwa. Lakini inaweza kutokea. Labda nitakuwa kidogo sina mawazo ya wengi, mimi nafikiri inaweza kutokea kama kutatokea kitu kinachoitwa radical change.
The Chanzo: Mapinduzi?
Mussa Assad: Radical change ni kitu kama mapinduzi hivi. Itokee, aje mtu mwamba hapa na nini. Lakini mtu mwenye dhamira nzuri na nchi hii. Maana anaweza kutokea mwamba ikawa shida kubwa kabisa
The Chanzo: Ndiyo nilitaka kusema kwa sababu tulikuwa na [mwamba hapa].
Mussa Assad: Naona atokee mtu mwenye dhamira nzuri, akasimamia kwa miaka 20 ijayo, kila kitu kikakaa sawasawa, inawezekana kufanyika. Lakini itakuwa mpango wa muda mfupi, miaka 10 [au] 15 ijayo. Lakini kwa mtazamo wangu, hilo jambo pia ni ngumu sana kufanyika sasa hivi.
The Chanzo: Na Katiba Mpya?
Mussa Assad: Katiba Mpya ni nzuri. Mimi nafikiri tatizo wala si Katiba Mpya. Tatizo ni usimamizi wa Katiba. Mimi nimewaambia watu hata hii Katiba tuliyonayo sasa hivi si Katiba mbaya sana, ni Katiba ambayo tumeshindwa kuisimamia ipasavyo. Tungeweza kuisimamia ipasavyo tungeweza kwenda vizuri sana.
Kwa hiyo, Katiba Mpya ni vizuri kuwa nayo lakini sioni kama itatupa mafanikio makubwa sana Katiba Mpya. Katiba Mpya itatusaidia tu pale tutakapoweza kuisimamia Katiba hiyo sawasawa.
Na muhimu kweli, kwa mimi ninavyoona, ni kuwa na taasisi ya Mahakama ambayo inajitegemea, ina uwezo wa kifedha, na ina uwezo wa kufanya maamuzi magumu, hata pale ambapo maamuzi hayo ni dhidi ya Serikali. Kama hatutafika hapo, tutakuwa na shida kubwa, hata kama tutakuwa na Katiba Mpya.
The Chanzo: Profesa, mimi nakushukuru sana kusema ukweli, lakini nikiri sikutegemea kwamba naweza kukukuta katika hali hii ya kukata tamaa kabisa, kwa sababu ni kitu ambacho kimenigusa kusema ukweli.
Mussa Assad: Unajua, labda hujaona vizuri, lakini mimi katika maisha ya kawaida si mtu wa kukata tamaa, kwa sababu, kama ninavyokwambia, mimi siwezi kukata tamaa, huwezi kukata tamaa, maana yake umekata tamaa na maisha na mimi siwezi kukata tamaa ya maisha.
The Chanzo: Nini kinakupa matumaini?
Mussa Assad: Kinachonipa matumaini ni kwamba, kwa mfano, sasa hivi kuna uongozi, unaona kabisa Rais [Samia Suluhu Hassan] ametoa nafasi kwa watu kuweza kupumua. Kwa watu kuendelea kununua mali zao na kuzimiliki na kuziendesha mali zao.
The chanzo: Unataka kuniambia kwamba utendaji kazi wa Rais Samia unakupa matumaini ya mabadiliko yanayokuja?
Mussa Assad: Ni kweli, ni kweli, unanipa matumaini makubwa sana, na tuseme kwamba ni utendaji kazi jumuishi, yaani anathamini michango ya watu wengine badala ya kuamini kwamba yeye tu ndiye ana uwezo wa kufanya kila kitu.
Sasa ukishakuwa na uungwana wa namna hiyo, kwa kweli, watu wanapata matumaini na wanakusaidia, na naamini sisi sote tuna matumaini hayo, kwamba Mwenyezi Mungu akimjaalia, kati ya miaka hii mitano au kumi ijayo, tutakwenda mbali kidogo, inshaallah.
The chanzo: Lakini unadhani anaweza kufanya zaidi ya hapa, hususan kwenye eneo la uwajibikaji?
Mussa Assad: Anaweza, pale ambapo wenzake watampa ushirikiano, anaweza akafanya. Anahitaji kuwa na taasisi zinazomsaidia kuona sehemu mbalimbali, zimsaidie. Zimsaidie kufanya uchunguzi. Zimsaidie kukusanya ushahidi, na zimsaidie kupeleka kesi mahakamani ili Mahakama zifanye kazi zake vizuri na kufanya uamuzi na mambo hayo yakianza kufanyika tu, nina hakika mambo yatakwenda vizuri zaidi.
The Chanzo: Na huo ndiyo ushauri, bila shaka, [ambao] kama ungepata nafasi ya kumwambia, ungemwambia?
Mussa Assad: Ningemwambia kwamba zile taasisi zetu za utazamaji, [yaani] watchdog institutions, maana yake ni CAG, maana yake ni TAKUKURU, maana yake ni Financial Intelligence Unit [FIU], maana yake ni Sekretarieti ya Maadili, nataka kuitoa [Mahakama] kidogo kwa sababu Mahakama itakuwa ya juu zaidi.
Hizi zikifanya kazi sawasawa, zinaweza kukusanya ushahidi unaotosheleza, ukapelekwa mahakamani, Mahakama zikatoa uamuzi, uamuzi ukatekelezwa, na watu wakapata haki zao, basi mambo yatakuwa yanaenda vizuri.
Kwa hiyo, nafikiri hizo taasisi zikimsaidia [Rais], nina uhakika Mwenyezi Mungu akijaalia Rais wetu anaweza kwenda vizuri zaidi, na tutapata matokeo tunayotarajia katika miaka mitano au kumi ijayo, inshaallah!
The Chanzo: Kwa sababu tulianza na maswali binafsi, nilikuwa nataka kumalizia pengine swali la mwisho: wewe unapenda kufanya nini kwenye muda wako wa ziada, kwenye muda ambao hupo kazini?
Mussa Assad: Mimi ni msomaji mzuri sana wa vitabu. Kwa hiyo, kwa kweli, mara nyingi, kama sina kitu cha kufanya, nitasoma kitabu, na siku hizi, mara nyingi, jioni, kama sina kazi, naingia kwenye kompyuta, natafuta [vitu] na kusoma, nasoma kwa kutazama kompyuta. Kwa hiyo, kwa kweli, usomaji ni jambo la muhimu sana kwangu mimi, na naendelea sana kusoma. Na siku hizi nimekuwa msomaji wa autobiographies.
The Chanzo: Kitabu chako cha sasa hivi ni kitabu gani?
Mussa Assad: Nasoma kitabu kinachoitwa Don’t Disturb.
The Chanzo: Cha Michelle Wrong?
Mussa Assad: Ameandika Michelle Wrong, ndiyo, hicho ndicho kitabu ninachosoma sasa hivi, na namalizia sura yangu ya mwisho. Kwa hiyo, nafikiri kesho nakwenda Nairobi, [Kenya], ndani ya siku mbili nitakuwa nimemaliza, nitachukua kitabu kingine Nairobi nitakuja kusoma nikirudi [Tanzania].
The Chanzo: Mashallah!
Mussa Assad: Kwa hiyo, usomaji ndiyo kazi kubwa tunayoifanya na, bila shaka, kukaa na mabinti zangu hapa, na kuongea nao, ni katika vitu ambavyo tunavipenda vilevile, na kuwaona watoto wanakuwa watu wazima kabisa, na wanaweza kubishana na wewe, kitu ambacho ni faraja.
Kwa hiyo, nakushukuru sana ndugu yangu kwa kuja vilevile, kama nilivyosema mwanzo, hii kwangu ni kazi, ni wajibu, kusaidia jamii, na kwa kweli, kama ikipatikana fursa nyingine, tutakuwa tayari kuzungumza vilevile.
The Chanzo: Sawasawa, nakushukuru sana, Profesa!
Mahojiano haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda maneno na mwandishi wa The Chanzo, Asifiwe Mbembela. Stephen Gimbi amesimamia mahojiano haya. Kwa maoni, tuandikie: editor@thechanzo.com.