Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (Chama cha Mapinduzi – CCM), Profesa Kitila Mkumbo, amewataka watu wanaopinga hoja ya uraia pacha waweke mezani hoja zenye mantiki badala ya kujificha kwenye kivuli cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Profesa Mkumbo, ambaye amewahi kuhudumu kama waziri na kushikilia nyadhifa nyingine kubwa Serikalini, alitoa wito huo wakati wa mahojiano maalum aliyofanya na The Chanzo nyumbani kwake jijini hapa hivi karibuni.
“Ni lazima niwe mkweli, nimesikiliza hoja zote [kwenye mjadala wa uraia pacha], lakini kwa wenzetu wanaopinga uraia pacha, kwa kweli hoja zao sijaziona,” Mkumbo alisema kwenye mahojiano hayo.
“Kwa mfano, juzi nimeona watu wamemrejea Mwalimu [Julius] Nyerere [kupinga uraia pacha], yaani unajua watu wakikosa hoja wanaenda kutafuta kitabu cha Mwalimu Nyerere,” aliongeza Mkumbo. “Lakini Mwalimu Nyerere hakuwa dogmatic, alikuwa progresive.”
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo na hapa Profesa Kitila Mkumbo anaanza kwa kueleza kwa nini chama chake, CCM, kinauogopa uraia pacha:
Kitila Mkumbo: Sidhani kama CCM, kama chama, kwa sababu hata ndani ya Chama cha Mapinduzi hatuwezi kusema kwamba ni msimamo mmoja [kupinga uraia pacha]. Kwanza, halipo katika ilani ya Chama cha Mapinduzi, ni jambo ambalo linazungumzika ndani ya chama, ndiyo maana unaona kuna mjadala.
Ukiona limeingia pale bungeni, na wabunge wanalizungumza kwa maoni tofauti tofauti, ujue hilo jambo halijawa na masimamo mmoja wa chama. Kama kuna msimamo mmoja wa chama basi utaona wabunge wanakuja katika mrengo ambao unafanana.
Kwa hiyo, haya ni maoni ambayo tunayatoa, na Serikali imekuja na maoni yake na msimamo wake, sisi wabunge tunatoa maoni kwa ajili ya kuboresha. Kwa hiyo, [hiyo] ndiyo hali halisi.
The Chanzo: Bungeni ulisema, na ningependa ufafanue, kama nitakumbuka vizuri, kwamba wewe, kwa mtazamo wako, unadhani Serikali, ulitoa mfano, nimeondoka hapa nimeenda Afrika Kusini, nimefanya kazi kule baadaye napoteza uraia wangu, kwa mfano nikiamua kuchukuwa uraia wa kule. Na wewe ukasema kwamba hiyo ni sawa na kumpokonya mtu haki yake aliyopewa na Mungu ya kuwa Mtanzania. Lakini ukazungumza pia kwamba tunachoweza kuzuia ni kuhakikisha pengine watu wengine hawachukui uraia wa Tanzania, hebu fafanua kidogo.
Kitila Mkumbo: Hoja yangu ya msingi ni kwamba kuna haki mbili za msingi ambazo mtu anapewa, ambazo zile hazitoi Serikali. Haki ya kwanza ni haki ya uhai. Wewe kuzaliwa hukuchagua uzaliwe. Kwa hiyo, umezaliwa. Ukishazaliwa, Serikali haina haki ya kuondoa uhai wako isipokuwa ina haki ya kuulinda. Mimi naita ni haki ya Kimungu.
Haki ya pili ni haki ya kuwa raia wa nchi fulani. Mimi kuwa Mtanzania sikuchagua kuwa Mtanzania. Nimejikuta nimezaliwa Tanzania. Kwa hiyo, Serikali haiwezi kuninyang’anya Utanzania wangu. Isipokuwa ina wajibu wa kuulinda Utanzania wangu.
Sheria yoyote ambayo itatungwa [na] inaondoa uhai wa mtu [au] inaondoa haki ya mtu kuwa Mtanzania, hiyo sheria haifai. Na kimsingi inaenda kinyume na Katiba na inaenda kinyume [na] misingi ya uasili na ndiyo hoja yangu ya msingi.
[Kwa] bahati mbaya, sheria yetu ya uraia unakuwa raia kwa nja tatu. Kuna uraia wa kuzaliwa na pili wa kuomba, nakadhalika. Sasa huu uraia wa kuzaliwa, wa asili, tumeweka kwenye sheria yetu kwamba ukishachukua uraia wa nchi nyingine [ni] lazima uukane uraia wa Tanzania.
Mimi, kwa maoni yangu, [naona hilo] ni kosa kubwa kwa sababu linaenda kinyume na uasili wa binadamu. Kwa hiyo, wanaoamini katika dini [wanaweza kusema] inaenda kinyume na uhaki wa Kimungu. Hizi ni God-given rights ambazo Serikali haipaswi kucheza nazo.
Pili, kwa maoni yangu, sheria hii inakinzana na sera za msingi za kiuchumi za Tanzania. Kwa sababu sasa hivi Rais Samia [Suluhu Hassan], moja ya sifa ambazo tunampa, ambazo ni sahihi kabisa, ni kuwa amekuwa mzuri sana kwenye diplomasia ya uchumi. Tunatumia neno maarufu ‘kuifungua nchi.’
Kuifungua nchi maana yake ni kukaribisha wawekezaji lakini pia unawafanya Watanzania waende kuwekeza huko nje.
Kwa hiyo, unawasukuma Watanzania waende nje kuwekeza, lakini ukienda kuwekeza labda Marekani wanasema uwekezaji wako ni mzuri lakini uwekezaji wako hautakuwa salama kama wewe siyo raia wa nchi hii, kwa hiyo tukupe uraia wa Marekani ili uwe salama na uwekezaji wako.
Kwa kitendo hicho unasema sawa. Kwa kulinda mali zako Marekani, unakana wewe siyo raia wa Tanzania. Kwa hiyo, hiyo inaenda kinyume na diplomasia ya uchumi. Ni sheria ambayo inakanyaga sera ya msingi ya Serikali na sera ya msingi ya Rais Samia.
Kwa hiyo, nikajenga hizo hoja za msingi kwamba, kwa kweli, hiyo sheria lazima tuibadilishe ili kwamba Mtanzania asipoteze uraia wake kwa sababu yoyote ile, uraia wake lazima ulindwe.
Sasa hii ni tofauti na mambo ya uraia pacha. Kwa sababu uraia pacha maana yake ni kwamba tutakupa uraia wa Sweden na wewe utapata wa kwetu, siyo lazima. Sisi tutalinda uraia wetu.
Sasa yeye [Mtanzania] akienda kule, Mswideni akija kuomba huku siyo lazima tumpe, sisi hapa Tanzania hatutoi uraia pacha. Vigezo vipo, ukitaka kuwa raia wa Tanzania, [lazima ukidhi vigezo] moja, mbili, tatu. Siyo kwa sababu umempa uraia raia wetu na sisi tumpe wa kwako. Hapana. Haina mfanano ila tunazungumzia kulinda uraia wa watu wetu.
Hoja ya tatu ambayo inayokuja [kwenye kupinga uraia pacha] ni kwamba hawa watu [waishio nje ya nchi] wamepoteza uazalendo, kuna mambo ya usalama, nakadhalika, nakadhalika. Hiyo ya uzalendo ni hoja dhaifu sana kwa sababu hapa Tanzania kuna watu ambao wametuibia sisi hata ndege hawajawahi kupanda.
Yaani ni Mtanzania milele hapa hajawahi kupanda hata ndege wametuibia tena kwa ukubwa, tena kashfa za karibuni, kuna Richmond, ESCROW, EPA. Si waliiba Watanzania ambao wapo hapa hapa Tanzania, siku zote, hawana uraia pacha, lakini wameiba? Kwa hiyo, suala la uzalendo halina uhusiano.
Mimi nimekaa nje [ya nchi] nikiwa nasoma. Ukiwa nje, unakuwa na uchungu na nchi yako kuliko hata ukiwa hapa. Yaani, kuna Watanzania wanaishi huko nje wana uzalendo kuliko sisi tuliopo hapa. Kwa hiyo, hoja ya uzalendo haina maana yoyote na wala siyo suala la kufikiria.
Lakini suala la usalama, au kufanya kazi gani, tunaweza tukazungumza. Tukasema sawa, kwa kuwa umechukua uraia wa nchi nyingine bwana, sasa sisi kuna haki fulani utazikosa, ambazo ni za upendeleo, wala siyo haki, kuna upendeleo ambao utaukosa.
Kwa mfano, kuwa kiongozi ni upendeleo, siyo haki. Kuwa mbunge [au] kuwa Rais ni upendeleo. Huo upendeleo hatutokupa, tutakunyang’anya. Upendeleo wa kufanya kazi kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, hatutokupa kwa sababu siyo haki ni upendeleo [na] siyo lazima ufanye kazi kule.
Kwa hiyo, kuna mambo fulani tunaweza tukayawekea vizuizi ambayo tunadhani kwamba tunaogopa, tutawazuia kufanya kazi huko, ni sawa. Lakini suala la msingi, hili la uraia, [ni] lazima tulilinde.
The Chanzo: Najua wewe siyo mwakilishi wa Serikali, pengine hili ni swali ambalo alitakiwa alijibu Dk [Stergomena] Tax mwenyewe. Lakini unadhani hofu kubwa ya Tanzania, kama nchi, kuruhusu, kwa mfano, hicho ambacho unakipendekeza, ambacho, kusema ukweli, ndiyo kilio kikubwa cha Watanzania wanaoishi nje ya nchi, hofu kubwa ni ipi, yaani inatokana na nini?
Kitila Mkumbo: Ukweli ni historia tu. Ukisikiliza hoja za wanaopinga uraia pacha, huzipati. Hamna Hoja. Huioni. Kwa mfano, juzi nimeona watu wamemrejea Mwalimu [Julius] Nyerere, yaani unajua watu wakikosa hoja wanaenda kutafuta kitabu cha Mwalimu Nyerere.
Lakini Mwalimu Nyerere hakuwa dogmatic, alikuwa progresive. Ni Mwalimu [ndiye] aliyetuingiza kwenye mfumo wa vyama vingi, watu waelewe. Mwalimu Nyerere ilibidi aende Mwanza akazungumze na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi.
Tena aliona aanze na vijana kuliko kuanza na wazee wenzake. Kwa hiyo, mwalimu hakuwa dogmatic, alikuwa progresive, na mimi naamini angekuwepo leo, jambo hilo angelizungumza kwa mtazamo tofauti.
Mwalimu alikuwa mjamaa ambaye alikuwa anaamini kwamba Serikali [ni lazima] imiliki njia [kuu] za uchumi, Serikali tu, mpaka ilikuwa inauza bia, Serikali.
Lakini [Mwalimu] aliruhusu mabadiliko, ndiyo maana akaona mimi siwezi kuyafanya haya, ngoja nimpishe afanye mtu mwingine. Kwa hiyo, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mtu wa mabadiliko.
Na watu ambao wanapinga vitu hivi wasimtumie Mwalimu Nyerere vibaya. Hayupo sasa hivi lakini tunaamini, kwa jinsi alivyokuwa, yeye mwenyewe ameandika kitabu Tujisahihishe.
Kwa hiyo, kuna mambo ambayo-. Yeye [Mwalimu] alitoa hotuba mwaka 1962 [kuhusu uraia pacha] wakati huo ilikuwa inaeleweka kwa sababu ndiyo tulikuwa tumetoka kwenye uhuru. Kulikuwa na matabaka makubwa. Waingereza wanaondoka hapa, hawaamini wabaki hapa au waondoke.
Ndiyo Mwalimu akawaambia inabidi uchague uraia kama utakuwa Mtanzania au Mwingereza. Ni katika mazingira hayo ya uhuru lakini, siyo leo, na mtu anasema hatujawa tayari [kuwa na uraia pacha]. Miaka 60 baada ya uhuru hujawa tayari, utakuwa tayari lini sasa?
Kwa hiyo, ni lazima niwe mkweli. Nimesikiliza hoja zote [kwenye mjadala wa uraia pacha], lakini kwa wenzetu wanaopinga uraia pacha, kwa kweli hoja zao sijaziona.
Na mimi naheshimu uelekeo wa Serikali wa kutaka kutoa hadhi maalumu, lakini ukisikiliza naona kama ni Green Card fulani. Sasa Green Card huwezi ukampa raia wako. Leo hii huwezi kwenda Marekani [ukakuta raia wao] anapewa Green Card. Hiyo ni kwa ajili ya wageni.
Mimi naelewa hadhi maalumu [maana yake] amekuja mtu tajiri, amekuja amewekeza hapa, kwa kumuheshimu mnasema kwamba wewe bwana tunakupa hadhi maalumu, inafanana na Utanzania, siyo Mtanzania, lakini inafanana. Mimi nadhani siyo sahihi sana kumpa Mtanzania huo uhadhi maalumu.
The Chanzo: Na hatujafahamu hiyo hadhi maalumu inajumuisha nini na nini haswa.
Kitila Mkumbo: Hatuna taarifa, labda zikija tutaziona. Lakini, nadhani, bado naamini kwamba Watanzania walioko nje, wanaofanya kazi, Watanzania wetu wasinyang’anywe haki yao ya msingi [ya kuwa Watanzania].
The Chanzo: Hapo umezungumzia kwamba hoja za wanaopinga uraia pacha, kwa kiasi kikubwa, ni za kihistoria, ni historia gani?
Kitila Mkumbo: Ndiyo hiyo kwamba Mwalimu Nyerere alikataa, kwamba mwaka 1962-. Msomi mwenzangu, Profesa [Palamagamba] Kabudi akatoa hotuba yake pale [bungeni], lakini haswa ukimuuliza achana na hiyo [historia], hoja ipi nyingine? Hana mantiki, huoini.
Mimi nimetoa mantiki mbili hapa. Nimesema haki hiyo ya asili, na suala la diplomasia ya uchumi ambao ni sera kubwa ya Serikali, ambayo, kwa maoni yangu mimi, hii tunayoifanya inaua lengo zima la Serikali.
Hebu na wao watupe hoja za kimantiki au za kitafiti, ndiyo huwa tunajenga hoja kwa njia mbili hizo, hatujaziona. Kuna za kihistoria ambazo kwa kweli mimi sijazielewa.
The Chanzo: Kuna hii hoja ya kuhusu Uzanzibari, kwamba labda pengine tukiruhusu uraia pacha wale waliopinduliwa wanaweza wakarudi na nini.
Kitila Mkumbo: Warudi kwenda wapi? Ndiyo maana tupo kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
The Chanzo: Unadhani na yenyewe inaweza kuwa inachangia kusukuma [hoja za kupinga uraia pacha]?
Kitila Mkumbo: Na yenyewe ni historia, lakini siyo sayansi. Tunavyozungumza hivi sasa kuna Wazanzibari wengi wanakaa Oman na kuna Wa-Oman wengi wanakuja Zanzibar, wanakuja Tanzania kwa ujumla.
Na huo uoga wote ndiyo maana tuna Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, muungano wetu, pamoja na sababu zingine za msingi, ni hiyo ya ulinzi na usalama wa nchi.
Kwa hiyo, dhana ya kuogopa Wa-Omani, Waarabu sidhani, kwa sababu hata leo moja ya wawekezaji wakubwa ambao tunawavutia ni [kutoka] Oman, Saudi Arabia, UAE, tunawavutia waje kuwekeza Tanzania. Unaogopa kitu gani?
Kwa hiyo, sioni, sioni [hoja] kabisa. Lakini pia kama tunawaogopa sana, tutaweka masharti kwamba uraia pacha sisi hatutokubali hizi [nchi] zifuatazo, moja, mbili, tatu, hizi nchi hapana.
Kwa hiyo, tunaweza tukaweka, tukasema, Oman tunawatoa kuwapa uraia pacha. Hatuwezi tukawapa Oman uraia wa Zanzibar kwa sababu uraia ni wa jamhuri, siyo wa Zanzibar, ni uraia wa Tanzania, kama tunaogopa hatutowapa kwani tatizo liko wapi?
The Chanzo: Profesa Palamagamba Kabudi, mbunge wa Kilosa kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi, alisema kwenye ile ile hotuba ambayo wewe pia umechangia kwamba, ameliita suala la mjadala wa uraia pacha kwamba ni suala la kihisia. Wewe unadhani hivyo pia?
Kitila Mkumbo: Kila kitu ni cha kihisia, mimi ni mwanasaikolojia [naelewa]. Hata hilo la kuzuia ni la kihisia. Kila kitu kinahusisha hisia. Uhai ni hisia. Hakuna kitu ambacho si cha kihisia.
Na huwezi kuacha kufanya maamuzi eti kwa sababu ni kitu cha kihisia. Hiyo hoja siioni kwa sababu sisi ni binadamu wenye hisia. Yaani, sisi ni binadamu, lakini pia ni binadamu wenye hisia, zipo kimwili na kiroho.
Kwa hiyo, kila kitu katika maamuzi kinakuwa na dhana ya kiroho na kihisia. Kwa hiyo, sasa kama Serikali huwezi kuacha kufanya maamuzi kwa sababu ya kuogoapa mwitiko wa kihisia. Muhimu ni kwamba maamuzi yako yawe ya kisayansi na yana hoja za msingi.
Hata kusema kwamba ni asilimia 49 ya nchi duniani ndiyo zinaruhusu uraia pacha [kama alivyosema Kabudi], hiyo yenyewe ni karibu nusu ya nchi duniani, [kwa hiyo, siyo hoja].
Lakini hata kama ingekuwa haipo hata moja, hiyo siyo hoja pia, kwani nyie mkiwa wa kwanza kuna tatizo gani? Mnaweza mkawa nyie ndiyo wa kwanza.
The Chanzo: Unadhani huu utaratibu ambao Serikali inataka kuja nao wa hadhi maalumu utafunga huu mjadala?
Kitila Mkumbo: Huo mjadala hauwezi kufungwa kwa sababu hadhi maaalum itatatua hoja moja ya diplomasia ya uchumi. Kwamba wewe unayetaka kuja kuwekeza Serikali inaweza kukutengenezea mazingira mazuri.
Lakini najaribu kuangalia kwa sababu sheria zetu za msingi, kwa mfano ya ardhi, huwezi kumiliki ardhi hapa kama siyo raia. Sasa najaribu kuangalia kuwa na hadhi maalumu siyo raia, kwa hiyo bado huwezi kumiliki ardhi.
Ndiyo maana nasema ngoja tusubiri hizi taarifa za hadhi maalumu tuzione. Lakini inaweza kutatua diplomasia ya uchumi, hiyo ya kuwekeza haiwezi kutatua tatizo la kwanza ambalo nimelizungumza la haki za mtu, kama Mtanzania, kwa kuninyang’anya mimi [haki ya msingi].
Huyu binti yangu hapa [mtoto wangu], nikiamua kwenda kumsomesha Canada, akafika Canada kule akaolewa, au akapata kazi Canada, akaamua kuuchukuwa uraia wa Canada ili apate fursa za kule, ndiyo aache kuwa Mtanzania?
Hiyo haiwezi kukubalika, utakuwa unaninyang’anya haki ya msingi kabisa. Unajua uraia wa nchi ni kama ubaba. Huyu mtoto hakuna namna atakuja kuacha kuwa mtoto wangu.
Kwa hiyo, mimi kama Kitila Mkumbo hakuna namna nitakuja kuacha kuwa mtoto wa Tanzania kwa sababu uraia ni makaratasi tu, lakini mimi ni Mtanzania.
Yaani hii siyo kwa bahati mbaya na hakuna mtu aliyeamua, ni Mungu mwenyewe kaamua. Sasa huwezi kuninyang’anya haki za Kimungu.
The Chanzo: Umezungumzia kuhusu suala la umiliki wa ardhi, na kwa mujibu wa utafiti wa jumuiya ya Watanzania wanaoishi ughaibuni walioufanya miongoni mwao, suala la umiliki wa ardhi ni mahitaji yao ya juu, kwamba tunataka na sisi tunaoishi nje ya nchi tuwe na haki hii ya kumiliki ardhi. Unadhani hii hadhi maalumu inaweza ikawapa hilo?
Kitila Mkumbo: Nadhani Serikali ikiamua inaweza ikabadili sheria ikawapa kwa sababu siyo Katiba [inayozuia wasiyo raia kumiliki ardhi], ni sheria tu. Kwa hiyo, Serikali ikiamua italeta muswada bungeni tutabadilisha, ili waweze kumiliki ardhi.
Hiyo wanaweza wakapewa kama itawasidia, lakini bado hii haitatatua tatizo langu la kwanza ambalo ni msingi, suala la uchumi ni la pili.
The Chanzo: Labda pengine ushauri wako?
Kitila Mkumbo: Ushauri wangu ni kwamba sisi, kwa upande wa Chama cha Mapinduzi na kwa upande wa Serikali, nilikuwa nadhani tuondoe hofu kuhusu hili jambo, na pili, Mwalimu Nyerere tumtumie [kupinga] kwa sababu alitengeneza misingi ya nchi hii, kwa hiyo hatuwezi kuacha.
Lakini Nyerere hakuwa dogmatic, Nyerere alikuwa progresive. Kwa hiyo, kudhani kwamba Nyerere wa 1962 angekuwa ni Nyerere wa 2023 ni kumuonea tu. Nyerere hakuwa vile, alikuwa ni mtu wa kubadilika, kwa hiyo hili kimsingi halina hoja.
Isipokuwa tukubaliane kwamba kama tunadhani, na mimi siyo mtaalamu wa usalama, kama kutakuwa kuna mambo ya kiusalama, tutawanyima upendeleo fulani.
Tutawanyima upendeleo wa kugombea, tutawanyima upendeleo wa kushika nafasi katika vyombo vyetu vya usalama. Tunaweza tukaweka baadhi ya mipaka, lakini mambo ya msingi ya kinchi, kiraia, na kiasili, wapewe!
Mazungumzo haya yamebadilishwa kutoka kwenye sauti kwenda kwenye maneno na Rahma Salumu na kuhaririwa na Lukelo Francis. Stephen Gimbi amesimamia uzalishaji wa mazunguzmo haya. Kwa maoni, tuandikie: editor@thechanzo.com.