The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Baada ya Serikali Kutakiwa Kulipa Mabilioni ya Fidia Tena, Bado Tunahitaji Mikataba ya Uwekezaji Baina Ya Nchi Mbili (BITs)?

Msingi wa madai ya kampuni ya Indiana ni Mkataba wa Uwekezaji Baina ya Nchi Mbili (BIT) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Uingereza (UK)

subscribe to our newsletter!

Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) Julai 14, 2023 kilitoa uamuzi wa kuitaka Serikali ya Tanzania kuilipa kampuni ya Indiana Resources Ltd ya nchini Australia takribani shilingi bilioni 250 baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika Mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.

Kiasi hiko ambacho Tanzania inatakiwa kulipa kinajumuisha fidia ya hasara, gharama za uendeshaji shauri na ada za kituo (ICSID), pamoja na riba. Uwepo wa riba unamaanisha kuwa jumla ya malipo ambayo Tanzania inapaswa kuilipa itazidi kuongezeka kadiri fedha hiyo itakavyochelewa kulipwa.

Kampuni ya Indiana Resources ilifikia hatua ya kuishitaki Serikali ya Tanzania kufuatia kufutwa kwa leseni hodhi, na kutwaa eneo la mradi wa Nikeli huko Nachingwea baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2017 na tangazo la Kanuni za Haki za Madini za Mwaka 2018, kitendo ambacho walikitafsiri  kama utaifishaji.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo Tanzania ilikiuka Mkataba wa Uwekezaji Baina ya Nchi Mbili (BIT) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Uingereza (UK) ambao moja ya vifungu vyake ni kulinda uwekezaji baina ya nchi hizo mbili dhidi ya vitendo vya utaifishaji.

Chanzo cha mgogoro  kati ya Serikali Tanzania na Indiana Resources Ltd

Kampuni ya Indiana Resources kupitia  kampuni ya Ntaka Holdings Ltd na Nachingewa UK Ltd zote za Uingereza inazozimiliki kwa asilimia 62.4 ya hisa  na Nachingewa Nickel Ltd ya Tanzania  ilikuwa ikimiliki na kusimamia mradi wa madini ya Nikeli unaoitwa ‘Ntaka Hill Nickel Project’ wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Kampuni hii ilipewa leseni ya hodhi ardhi na Serikali ya Tanzania April 21, 2015 ili kuhodhi haki ya kuchimba madini bila ya kufanya uchimbaji wenyewe chini ya vifungu vya 37 na 38 vya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, kabla ya marekebisho ya mwaka 2017.

Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, ilikuwa ikiruhusu wawekezaji katika madini, waliofanya utafiti wa madini, na wenye lengo la kuchimba madini, lakini kwa sababu kadhaa za muda mfupi, kama masuala ya kitalaamu na hali ya soko kwa muda huo, yanawalazimisha kuchelea uzalishaji madini kwa muda, hadi pale masuala hayo yatakapokuwa sawa, kuomba leseni hodhi.

Leseni hodhi zilitolewa kwa waombaji wenye vigezo hivyo, na zilidumu kwa miaka mitano, na baada ya kuisha muda wake, waliokuwa wamiliki wa leseni hodhi, walipaswa kuomba leseni za uchimbaji mkubwa wa madini (Special Mining License).

Ili kuongeza wigo wa manufaa ya rasilimali madini kwa taifa, mwaka 2017, Tanzania ilifanya marekebisho makubwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Marekebisho hayo, yaliyofanywa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Namba 7) ya Mwaka 2017. Marekebisho hayo, pamoja na mambo mengine, yalifuta msingi wa kisheria wa leseni hodhi kwa kuvifuta vifungu vya 37 na 38 vya sheria ya madini pasi na mbadala.

Kwa kufuta vifungu vya 37 na 38 vya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, marekebisho hayo ya Julai 2017 yaliathiri wamiliki wenye leseni za utafiti wa madini (Prospecting License) waliotarajia kuomba leseni hodhi badala ya leseni za uchimbaji wa madini. Kwani kwa mabadiliko hayo, maombi ya leseni hodhi yasingewezekana tena kwa sababu msingi wake kisheria ulikwishafutwa, Hatahivyo, leseni hodhi zilizokuwa zimekwishatolewa, na muda wake bado haujaisha, ziliendelewa kuwa halali hadi hapo muda wake utakapofika ukomo.

Katika hali ambayo pengine haikutarajiwa na wengi, mnamo Januari 10, 2018, Serikali ya Tanzania, kupitia Tangazo la Serikali (Government Notice) Namba 01 la mwaka 2018, ilitangaza Kanuni za Haki za Madini za Mwaka 2018, ambazo pamoja na mambo mengine, chini ya kanuni ya 21(1) zilifuta leseni hodhi zilizokwisha tolewa kisheria.

Aidha, Kanuni za Haki za Madini za Mwaka 2018 zilienda mbele zaidi, chini ya kanuni ya 21(2) kwa kueleza kuwa haki zote za madini zilizokuwa zikihodhiwa na wamiliki wa leseni hodhi kwenye maeneo yote yaliyokuwa chini ya leseni hodhi, zitakuwa haki za Serikali ya Tanzania.

Kwa lugha rahisi, Serikali ilianza kwa kufuta vifungu vya sheria ili kusitisha maombi ya leseni hodhi, miezi saba baadae ikafuta leseni hodhi zilizotolewa kwa mujibu wa Sheria, na kisha ikatwaa haki zote za madini juu ya maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa kwa leseni hodhi. Kwa kufanya hivyo serikali iliathiri maslahi ya makampuni yaliyokuwa yakimiliki leseni hodhi.

Makampuni hayo ni pamoja na kampuni ya Nachingwea Nickel Ltd ya Tanzania, ambayo ni matokeo ya ubia kati ya kampuni ya Ntaka Holdings Ltd, na kampuni ya Nachingewa UK Ltd. Ubia kati ya makampuni hayo katika kuendesha mradi wa ‘Ntaka Hilii Nickel Project’ ulikuwa ukisimamiwa na kampuni yenye umiliki wa makampuni hayo, yaani kampuni ya Indiana Resources Ltd.

Shauri la madai kupelekwa ICSID

Msingi wa madai ya kampuni ya Indiana ni Mkataba wa Uwekezaji Baina ya Nchi Mbili (BIT) kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ufalme wa Uingereza (UK). Mkataba huo, pamoja na mambo mengine unalenga kulinda uwekezaji kwa kudhibiti vitendo vya utaifishaji isipokuwa utaifishaji uliofanyika kwa maslahi ya Umma. Na iwapo utaifishaji utafanyika kwa maslahi ya Umma, mkataba huo unaweka masharti ya fidia.

Kitendo cha Serikali ya Tanzania kufuta leseni hodhi, na kutwaa eneo la mradi wa Nikeli huko Nachingwea kwa mujibu wa Indiana Resources Ltd ilikuwa ni sawa na utaifishaji na kinyume na makubaliano na Sheria kwani haukuambatana na fidia kwa kampuni hiyo.

Hivyo basi Indiana Resources Ltd iliwasilisha malalamiko ICSID na kuambatanisha madai ya fidia ya hasara kwa uwekezaji uliofanyika na pia gharama za kuendesha shauri, ada za kufungua shauri pamoja na riba ikokotolewayo tokea siku ya hasara iliposababishwa mpaka siku malipo ya fidia yatakapofanyika.

Kwa upande wa Serikali ya Tanzania iliwasilisha utetezi wake dhidi ya madai ya mlalamikaji,  hata hivyo baada ya kupitia madai na utetezi, ICSID wakatoa maamuzi ambayo hayakuwa upande wa Serikali ya Tanzania.

Kwa sababu Mkataba wa kuunda ICSID ulioasiniwa na Mataifa 154 duniani ikiwemo Tanzania u nataka maamuzi ya kituo hicho yanapaswa kutekelezwa kama hukumu za mahakama ya nchi mwanachama. Hii ina maana mali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama vile ndege za shirika la ndege la ATCL zinaweza kushikiliwa iwapo zitakutwa ndani ya mipaka ya nchi mwanachama wa mkataba wa ICSID, na zinaweza kuuzwa ili kulipa kulipa fidia kwa kampuni ya Indiana Resources Ltd kama sehemu ya utekelezaji wa hukumu hii.

Maamuzi haya ya ICSID yanaashiria nini?

Kwa upande mmoja maamuzi haya yanatuma ujumbe kwa wawekezaji kuwa uwekezaji wao upo salama Tanzania na iwapo usalama huo utaathiriwa bado wanazo njia za kulinda maslahi yao kutokea nje ya mipaka ya Tanzania.

Lakini kwa upande wa Watanzania wenyewe, hii ina maanisha kwamba usalama wa wawekezaji upo kwa gharama ya pesa ya Watanzania yaani walipakodi ambao wengi wao ni masikini. Kwa maana kwamba  deni la madai ya fidia litalipwa na Serikali kupitia kodi za wananchi hawa.

Sasa amri ya kuilipa kampunia ya Indiana Resources Ltd ni moja, je, kuna amri zingine kama hizo ngapi zinakuja siku za usoni? Kama amri hiyo imetokana na kufanya marekebisho ya Sheria ambayo jumuiya ya wawekezaji, pamoja na ICSID, wameyatafsiri kama utaifishaji, je ni wawekezaji wangapi waligadhibika na uamuzi wa kufuta leseni hodhi na kutwaa haki za wawekezaji chini ya leseni hodhi na kuzipeleka kwa serikali ya Tanzania?

Mfano dhahiri wa wawekezaji wa aina hiyo ni kampuni ya Winshear Gold Corporation ambayo awali iliitwa Helio Resources Corporation iliyomiliki kampuni tanzu iliyoitwa Bafex Tanzania Ltd iliyokuwa na leseni za utafiti wa madini na leseni hodhi kwenye mradi wake wa madini ya dhahabu ulioitwa Saza Mining Project (SMP) uliokuwepo wilayani Chunya mkoani Mbeya.

Shauri la madai la Winshear Gold Corporation dhidi ya Serikali ya Tanzania lilishafunguliwa ICSID. Kama ambavyo si busara kujadili shauri ambalo bado halijaamuliwa na chombo chenye dhamana ya kufanya maamuzi kwa sababu kwa kufanya hivyo ni sawa na kuingilia uhuru wa chombo hicho, vivyohivyo si busara kuwa na matumaini kuwa maamuzi ya chombo hicho yatakuwa tofauti na yale ambayo weledi wa kawaida kabisa unakutuma kuamini.

Msingi wa matarajio ya aina hiyo ni kuwa chombo chenye dhamana ya kufanya maamuzi kinatarajiwa kufanya maamuzi yanayofanana iwapo muktadha wa shauri la awali unafanana na muktadha wa shauri lilipo mbele yake kwa wakati huo. Kinyume na hapo chombo hicho kinaweza kutizamwa kama kina upendeleo ama uonevu. Upendeleo na uonevu sio sifa ya vyombo vyenye kutafsiri sheria na kuamua haki.

Mazungumzo yatapunguza kulipishwa fidia

Ni vema Serikali ione namna ya kuoa kila senti moja ya Watanzania inayoweza kuokolewa kwa kupunguza mzigo wa malipo ya fidia ambayo kwa namna yoyote ile, iwapo itaendelea  kuamriwa hivyo ni mzigo kwa Watazania.

Hivyo basi, kwa njia ya mazungumzo Serikali inaweza kuafikiana na walalamikaji, na kufikia makubaliano ya malipo pungufu na yale ambayo yangeamriwa na ICSID ama taasisi zingine za aina hiyo.

Aidha, Ni vema sasa serikali ipitie mianya yote inayopelekea mashauri nje ya nchi na malipo ya fidia kubwa za pesa kwa wawekezaji ambao pengine hawajafanya uzalishaji na hawajaliingiza taifa mapato yoyote ya maana.

BITs mwiba kwa nchi masikini

Ni muhimu kwa serikali kuwahakikishia ulinzi wawekezaji, lakini siyo kwa kusaini mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili (BITs) bali kwa kuziishi kanuni za utawala bora ikiwemo demokrasia hai, utawala wa sheria na uhuru wa mahakama.

Hili linawezekana kwani kadiri siku zinavyozidi kwenda, mataifa yasiyo na mikataba ya BITs yanazidi kuvutia uwekezaji mkubwa kutoka nje. Hivyo haipo haja ya kuwa na wingi wa BIT ambazo mara zote zinaongozwa na dhanio batili.

Dhanio la BITs ni kuwa nchi inayoendelea kama Tanzania na nchi iliyoendelea kama Uingereza zina uwezo sawa kiuchumi na kiteknolojia hivyo watu ama makampuni kutoka Uingereza yanaweza kuwekeza Tanzania na kutoka Tanzania wanaweza kuwekeza Uingereza, kitu ambacho, katika uhalisia wake, si kweli.

Na unaweza kulithibitisha hilo kwa kutazama idadi ya makampuni kutoka nchi zilizoendelea kama Tanzania yaliyowahi kuzishitaki nchi zilizoendelea kama vile Uingereza kwa madai ya kukiuka masharti ya BIT hivyo kuyasababishia makampuni hayo hasara, na kisha ukafananisha idadi hiyo  dhidi ya idadi ya makampuni kutoka nchi zilizoendelea, kama vile Canada yaliyozishitaki nchi zinazoendelea kama Tanzania kwa kukiuka mikataba ya uwekezaji baina ya nchi mbili.

Katika BITs kinacholindwa sio uwekezaji wa nchi mbili bali uwekezaji wa makampuni ya nchi moja tajiri kwenye nchi nyingine masikini. Hii ni sawa na mechi ya mpira wa miguu inayoanza angali timu moja inaongoza kwa tofauti ya magoli saba kwa sifuri.

Mikitaba ya Uwekezaji Baiana ya Nchi Mbili inaweza kuwa jawabu iwapo nchi hizo zinawiana ama zinakaribiana uwezo. Ffano, BIT kati ya Misri na Afrika Kusini ni njema kama itakavyokuwa kati ya Tanzania na Ghana.

Mwisho, uamuzi wa ICSID dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukawe chachu kwa Watanzania kudai uwazi kwenye mikataba ya uwekezaji. Watanzania, ambao mmoja wao ni mimi, wanataka kunufaika na uwekezaji na wanaitegemea sana Serikali yao iwasaidie kupata manufaa hayo kwa ajili ya ustawi wao na wa vizazi  vya sasa na vijavyo. Mungu ibariki Tanzania.

Clay Mwaifwani ni  Mwanasheria na mdau wa usimamizi dumivu wa rasilimali za maliasili anapatikana kupitia : +255 (0) 758 850 023 au kwa barua pepe claymwaifwani09@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo.Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

3 Responses

  1. Mawazo binafsi ya mwandishi yakikutana na mawazo yangu binafsi basi yangu yanabustiwa.

  2. Jamaa Yuko makini saana huyu. Je ni mwanasheria wa Serikali? Kuna spelling mistake moja tu lakini kila alicho andika ni logical. Saafi saana. Ajumuishwe sio Yule wa sijui Viwanja vya Ndege.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *