Mapigano makali yamezuka kuanzia Aprili 15, 2023, nchini Sudan baina ya makundi mawili ya kijeshi kufuatia mvutano wa kugombania madaraka baina ya makamanda wawili. Ugomvi wao ulianza tangu kupinduliwa kwa Rais Omar al Bashir mwaka 2019 baada ya kutawala kwa muda wa miaka 30.
Makundi haya yanaongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na Jenerali Mohamed Hamdan ‘Hemedti’ Dagalo, ambaye ni kamanda wa kikosi cha wanamgambo, au Rapid Support Forces – RSF, kama kikosi hicho kinavyojulikana kwa kimombo.
Wasuluhishi wa kimataifa walipendekeza mpango wa kuunda Serikali ya Kiraia. Kikosi cha Dagalo, yaani RSF, kilitakiwa kijiunge na jeshi rasmi la Burhan. Dagalo angekuwa makamo wa Burhan bila ya RSF. Ndipo tofauti zao zikalipuka na vita vikaanza.
Ujumbe kutoka Umoja wa Afrika na kutoka Saudi Arabia uliwasili Sudan ili kusuluhisha. Pande mbili zikakubali kusitisha mapigano ili angalau misaada ya kiraia isambazwe na majeruhi waokolewe. Hata hivyo, haikuchukua muda mapigano yakaanza tena.
SOMA ZAIDI: Nini Hasa Chimbuko la Mapigano Yanayoendelea Sudan?
Vita hivi, kwa hivyo, ni baina ya Dagalo na Burhan; watu wawili ambao wanagombania utawala wa nchi. Wakati huo huo, tangu kupinduliwa kwa Bashir, wananchi wamekuwa wakidai demokrasia na uhuru wa kuchagua Serikali yao. Badala yake sasa wanaona nchi imekumbwa na vita vya mafahali hawa wawili.
Mafahali wawili
Ni vizuri tukawaelewa mafahali hawa. Kimsingi, Burhan na Dagalo waliteuliwa na Bashir. Rais huyo aliwatuma kwenda kushirikiana na Ufaransa na Marekani katika kumpindua na kumuua Muammar Gaddafi, aliyekuwa kiongozi wa Libya. Pia, Bashir aliwatuma kwenda kupigana nchi za Chad na Yemen.
Wananchi wakaukataa utawala wa Bashir. Hali ikazidi kuchafuka na mwaka 2019 majeshi yake, yakiongozwa na Burhan na Dagalo, yakampindua.
Baada ya hapo, wananchi wakadai utawala wa kiraia ukiongozwa na muungano wa vyama vya siasa na asasi za kiraia. Ikaundwa Serikali ya Mpito. Hili halikuwapendeza Burhan na Dagalo. Wakaipindua Serikali hiyo mnamo Oktoba 2021.
Majenerali hawa wakashirikiana kukandamiza maandamano ya raia waliokuwa wakidai utawala wa kidemokrasia na uchaguzi ulio wazi na wa haki. Wengi wakauawa huku majeshi ya RSF yakidiriki hata kuwabaka wanawake waliokuwa wakiandamana
Wakati huohuo, makamanda hawa wawili wakaanza kugombania utawala wa nchi.
Dagalo akakataa kuwa makamo wa Burhan. Ukweli ni kuwa wamekuwa wakigombania utajiri wa nchi, kwani tangu enzi za Bashir, makamanda wamekuwa wakidhibiti uchumi wa nchi, pamoja na madini na mabenki.
SOMA ZAIDI: Juhudi za Dhati Zinahitajika Kuifikia Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo
Kwa njia hii, makamanda wametajirika na kuwa mamilionea. Kuja kwa utawala wa kidemokrasia, kwa hiyo, ni tishio kwao ndipo wakatumia silaha kuzuia mageuzi.
Jeshi la Sudan linaloongozwa na Burhan lina wanajeshi takriban 205,000 pamoja na ndege na vifaru. Hata hivyo, Burhan hadi sasa ameshindwa kumdhibiti Dagalo ingawa anasaidiwa na Marekani kupitia Misri, Saudi Arabia, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Mara kwa mara, Burhan amekuwa akitembelea nchi hizi kwa ajili ya maagizo na misaada. Dagalo naye anasemekana kupata msaada kutoka Urusi kupitia kikosi cha Wagner, kikundi binafsi cha wapiganaji wa kimamluki.
Mwaka 2022, asasi za kiraia zikiongozwa na jumuiya yao ya Forces for Freedom and Change, yaani vuguvugu la uhuru na mageuzi, zilipendekeza kuwepo kwa utawala wa kiraia utakaopangwa kufanyika kwa uchaguzi katika muda wa miaka miwili.
Burhan akaja juu na kuwaambia wanajeshi wake: “Msisikilize upuuzi huu wa wanasiasa, hatutakubali kuyaweka majeshi yetu chini ya utawala wa kiraia. Hakuna atakayethubutu kuyaingilia majeshi yetu.”
Akataa kumezwa
Wakati huohuo, Burhan anataka majeshi 100,000 ya RSF yamezwe na majeshi yake katika muda wa miaka miwili. Dagalo naye anakataa “kumezwa” na majeshi ya Burhan. Badala yake, anapendekeza muda huo ucheleweshwe hadi miaka kumi. Ndipo mapigano kati yao yanaendelea na wananchi wanateseka.
Dagalo ameupata ujenerali bila ya kuhudhuria mafunzo yoyote ya kijeshi au hata ya kiraia. Ndiyo maana Bashir alimtumia katika kuongoza askari mamluki takriban 100,000 walioshambulia jimbo la Darfur. Wakijulikana kama Janjaweed, askari hao waliendesha mauaji ya watu takriban 300,000, huku milioni 2.5 wengine wakiyakimbia makazi yao.
Mwaka 2004, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) lilipitisha azimio namba 1556 likiwalaani Janjaweed kwa mauaji ya halaiki jimboni Darfur. Kwa hilo, Dagalo anaweza akafikishwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ingawa Burhan naye alishiriki akiwa Mkuu wa Majeshi. Bosi wao, Bashir, tayari amefunguliwa mashtaka na anatakiwa afikishwe ICC.
SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika
Kazi nyingine aliyokuwa akiifanya Dagalo huko Darfur ni kupora dhahabu na kuitorosha nje ya nchi. Mkuu huyo wa RSF akadhibiti madini, mifugo na miundombinu. Akawaingiza na ndugu zake katika uporaji huo. RSF ikawa kama kampuni binafsi.
Kwa mujibu wa jarida la Global Witness, Dagalo alijilimbikizia zaidi ya dola bilioni moja za Kimarekani katika Benki ya Sudan. Hatujui ni ngapi ameficha nje ya nchi. Ndiyo maana Dagalo alitamba hadharani kuwa yeye hatumii vijisilaha vidogo vidogo, bali huwa ananunua silaha za kisasa tena za babu kubwa!
Wananchi walipompindua Bashir, Dagalo alijaribu kumlinda. Hata hivyo, baada ya maandamano kupamba moto, Dagalo akaamua kumgeuka bosi na mlezi wake na kusaidia kumg’oa madarakani. Dagalo akajinyakulia madaraka na kuanza utawala mpya wa kijeshi akishirikiana na Burhan.
Katika vita vyake dhidi ya Burhan, inadaiwa kuwa Dagalo anawaajiri askari mamluki kutoka nchi jirani kama Chad, Niger na Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuwalipa kutokana na biashara zake haramu.
Wakati huohuo, Dagalo ameingia mkataba na kampuni za kigeni ili kumpigia debe katika nchi za Magharibi. Mwaka 2019, kwa mfano, kamanda huyo alisaini mkataba wa dola milioni sita za Kimarekani na kampuni ya Canada ya Dickens and Madson iliyoanzishwa na Ari Ben-Menashe aliyekuwa jasusi wa Israel.
Mpaka sasa katika vita hivi, inasemekana watu kati ya 3,000 hadi 5,000 wamepoteza maisha yao, takriban 8,000 wamejeruhiwa na zaidi ya milioni tatu wameyakimbia makazi yao. Wengine 740,000 wamelazimika kukimbilia nchi za jirani.
Tayari ICC imetangaza kuwa inachunguza uhalifu wa kivita nchini Sudan, huku ushahidi mmoja uliopatikana ukiwa ni kaburi la halaiki ambamo miili 87 ilifukiwa katika jimbo la Darfur. ICC, hata hivyo, imesema uchunguzi zaidi bado unaendelea.
Nizar Visram ni mchambuzi wa siku nyingi wa siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia au nizar1941@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.