The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Juhudi za Dhati Zinahitajika Kuifikia Ajenda 2063 ya Afrika Tuitakayo

Mwendelezo wa mipango na uwezeshaji wa mipango hiyo bado imekuwa ni doa kubwa kwa AU na wanachama wake.

subscribe to our newsletter!

Mnamo Mei 26, 2013, katika mkutano wa kawaida wa Umoja wa Afrika (AU), ilisomwa barua kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dk Nkosazana Dlaminin Zuma, iliyokuja kujulikana kama email from the future.

Kilichokuwemo ndani ya barua hiyo ni maono ya miaka 50 ya baadaye ya Afrika katika nyanja za uchumi, tekonolojia, amani na usalama, demokrasia, mazingira, miundombinu, usawa wa kijinsia, ajira, kilimo, pamoja na afya. Maono haya yalikuja kupewa jina la Ajenda 2063: Afrika Tuitakayo.

Katika utekelezaji na ufuatiliaji wa maono haya, hujitathmini kila baada ya kipindi fulani chini ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika, pamoja na Wasimamizi wa Maendeleo wa Umoja wa Afrika (AUDA-NEPAD). Kwa mfano, tathmini ya awali, au preliminary kwa kimombo, ilifanywa mwaka 2020 na tathmini nyingine imefanywa kupitia mataifa 38 kati ya 55 yote barani Afrika.

AU iliweka vipengele saba kama vipimo vya malengo kusudiwa ambavyo ni: maendeleo ya uchumi jumuishi; mashirikiano ya ki-bara chini ya mwamvuli wa umajumui wa Kiafrika; demokrasia na utawala wa sheria; amani; utamaduni; maendeleo yatokanayo na watu; na ukuaji wa ushawishi wa bara la Afrika katika maamuzi ya kidunia.

Ni tathmini ya AU kwenye maeneo mawili makubwa – lile la afya na lile la usalama kwenye bara la Afrika – ndiyo iliyonipelekea kuandika makala haya na kutoa tafakuri yangu fupi.

Afya duni

Kwenye  afya, ripoti imeeleza kuwa Afrika imefikia asilimia 77 ya mpango wake wa afya kwa wananchi wake, huku ikieleza kuwa asilimia chache zilizobaki zimesababishwa na uwepo wa ugonjwa wa UVIKO-19. Huduma za afya ya uzazi pamoja na kudhibiti vifo vya watoto wachanga ndiyo imeelezwa kama sababu kuu za ufaulu wa asilimia kubwa hiyo katika lengo hili.

Ni maoni yangu kwamba wakuu wetu katika AU wamejipa asilimia hizi kujifurahisha tu. Nasema hivi kwa sababu bara la Afrika limekuwa likiagiza zaidi ya asilimia 70 ya vifaa tiba na dawa zote zinazotumiwa na wananchi wake kutoka mataifa ya nje. Hali hii imekuwa ikisababisha uingizwaji wa dawa chache sambamba na dawa hizo kuuzwa kwa gharama kubwa.

Utafiti wa Center for Global Developmment unaeleza kwa kina kuwa mataifa yenye uchumi wa chini hulipa mara 20 mpaka 30 ziada ya gharama za dawa ukilinganisha na mataifa yenye uchumi wa juu.

SOMA ZAIDI: Tanzania Inaenda Kumuuzia Nani Kahawa Ndani ya AfCFTA?

Mwaka 2019, AU ilianzisha taasisi iliyoitwa African Medicines Agency (AMA) ambayo lengo lake ni kusimamia huduma za afya barani humo. Moja ya jukumu iliopewa AMA ni uboreshaji na uendelezaji wa maabara za uzalishaji wa dawa na vifaa tiba ijapokuwa ni mataifa 22 tu barani Afrika yaliridhia ushiriki wao katika taasisi hii.

Kwa kuwa AMA inategemea michango ya mataifa washirika, taasisi hii imekuwa ikifanya shughuli zake kwa kusuasua kiasi ya kupelekea kuomba msaada wa kuchangiwa Euro milioni 100 kutoka taasisi ya Bill & Melinda Gate Foundation pamoja na Umoja wa Ulaya ili iweze kutekeleza majukumu yake.

Ifahamike kuwa mafanikio katika sekta ya afya kupitia huduma za afya ya uzazi yaliyotajwa kwenye ripoti hiyo ya AU bado ni msaada pia kutoka mataifa ya nje hasa Marekani kupitia mpango waka wa AMPLIFY-PF na PEPFAR barani Afrika.

Vita visivyokwisha

Tuje kwenye lengo la kuhakikisha amani na usalama kwenye bara la Afrika. Tathmini ya AU imechambua eneo moja tu la vifo vitokanavyo na mashambulizi ya kigaidi hasa katika nchi za Burkina Faso na Chad.

Nadhani uchambuzi haukupaswa kuishia hapa na kwenda mbali zaidi hasa kwenye kutazama masuala kama vita visivyoisha katika nchi ya Libya ambayo kwa kiasi kikubwa AU imeisusa na kuziachia nchi za Uturuki, Marekani, Urusi, Saudi Arabia na Umoja wa Ulaya katika upatanishi na kuimaliza vita hivyo.

Afrika imekuwa watazamaji tu ndani ya vita katika ardhi yake. Ni wazi vita hivyo vimeendelea kuchochea janga lingine la kiusalama barani Afrika la uuzaji wa binadamu kwenye makontena unaofanywa eneo la pwani mwa Libya.

SOMA ZAIDI: Urusi Inavyotumia Karata ya Ulinzi, Usalama Kukita Mizizi Afrika

Inakadiriwa kila mwaka takribani watu 150,000 hujaribu kuvuka Bahari ya Meditteranian na Kwenda Ulaya. Mpaka kufikia mwaka 2019, inakadiriwa takribani watu 19,000 walikufa maji wakijaribu kuvuka, na ripoti hii ni vifo vya ndani ya miaka sita tu.

Wakati madhila haya yakiendelea kwa Waafrika, nchi ya Rwanda imechukua jambo hili kama fursa ya kiuchumi na kuhitaji kulipwa fedha na Serikali ya Uingereza ili “izisaidie” nchi za Ulaya kuwatunza Waafrika hao wengi kutoka nchi za Nigeria, Ghana, Gambia na Elitrea waliokuwa wakijaribu kuvuka kwenda mataifa hayo ya Ulaya.

Si jambo la ajabu pia kukuta mataifa mengine ndani ya Afrika yanaionea wivu Rwanda kwa kuwahi “dili” hilo. Bado Afrika haikamatiki katika baa la njaa na usalama wa chakula.

Kwa mfano, nchini Somalia, Sudan na Kenya changamoto ya ukame imeendelea kutishia uwepo wa binadamu katika maeneo hayo achilia mbali vita visivyokwisha Sudan, Mali, Congo DR, Msumbiji, nakadhalika.

Jitihada za dhati

Kwa hiyo, maoni yangu ni kwamba katika mchakato mzima wa kuielekea Afrika Tuitakayo jitihada nyingi na za dhati zinapaswa kuchukuliwa. Mwendelezo wa mipango na uwezeshaji wa mipango hiyo bado imekuwa ni doa kubwa kwa AU na wanachama wake.

Mara kadhaa kumeripotiwa Jeshi la Akiba la Umoja wa Afrika (AU Standdby Force) kushindwa kutekeleza shughuli zake kutokana na kiasi kidogo cha michango ya fedha kutoka kwa nchi washirika.

Hali hii inapelekea kuwepo na vita zisizokwisha ambazo nchi zinazoathirika hupelekea kuomba msaada kwa vikundi na mataifa ya nje, hatua ambayo hutishia uhuru wa mataifa hayo ya Afrika.

SOMA ZAIDI: Fursa Tanzania Inaweza Kuvuna Kwenye Uzalishaji wa Mbolea

Mnamo mwaka 2022, AU ilipitisha azimio la kuanzisha African Pharmaceutical Technology Foundation (APTF) kama mpango wa kuhakikisha Afrika inaweza kuzalisha chanjo, dawa na vifaa tiba.

Mpango huu kiutekelezaji hauna tofauti na AMA, ijapokuwa mfadhili wa APTF ni Benki ya Maendeleo ya Afrika. Kama mpango huu utafanikiwa Afrika itakuwa imepiga hatua kubwa kwenye sekta ya afya na uhuru wa mataifa yake.

Ni vyema kusubiri, ila kama waaminivyo Waafrika wengi basi “tusiache kuombea” hata jambo hili moja tu lifanikiwe!

Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *