The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Fursa Tanzania Inaweza Kuvuna Kwenye Uzalishaji wa Mbolea

Uzalishaji huu utapunguza gharama za uingizaji wa mbolea kutoka mataifa ya nje, hivyo kumfanya mkulima kupata unafuu wa bei

subscribe to our newsletter!

Kwa mwaka 2022, mahitaji ya matumizi ya mbolea nchini Tanzania yalikuwa ni tani 698,260, huku kati ya hizo, tani 274,973 zilinunuliwa kutoka nchi za nje; tani 117,900 zilikuwa ni bakaa na tani 43,579, sawa na asilimia sita, ndizo zilizozalishwa nchini.

Mbolea aina ya UREA na DAP ndizo zinazotumika zaidi hapa nchini. Kwa mfano, mwaka 2022, mahitaji ya DAP yalikuwa ni tani 166,310 huku UREA ikiwa ni tani 210,769, na kwa mwaka huo hakukuwa na uzalishaji wa mbolea hizo nchini.

DAP hutumika kama mbolea ya kupandia na UREA hutumika kukuzia mazao.

Mbolea aina ya minjingu, inayozalishwa mkoani Manyara, imekuwa ikitumika sana nchini kama mbolea ya kupandia. 

Hata hivyo, matumizi ya mbolea hii yamekuwa ni ya kiwango cha chini kutokana na uzalishaji wake, ikikadiriwa kuzalishwa chini ya tani 100,000, huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya tani 500,000 kwa mwaka. Kwa msimu wa kilimo wa 2021/22, uzalishaji ulikuwa tani 25,732 tu. 

Upungufu huu umechagiza manunuzi ya mbolea kutoka nje ya nchi ambapo, pamoja na jitihada za Serikali kuziwekea ruzuku, bado gharama zao zimekuwa kubwa kwa wakulima wengi.

SOMA ZAIDI: Serikali Yatenga Bilioni 150 kwa Ajili ya Ruzuku ya Mbolea

Hivi karibuni, Tanzania imefanikiwa kupata mwekezaji kutoka Burundi, kiwanda cha Itracom Fertilizer Limited, ambacho kinategemewa kuzalisha mbolea ya kupandia aina ya Fomi-Otesha kwa wastani wa uzalishaji wa tani 200,000 kwa mwaka. 

Uzalishaji huu, bila shaka, utapunguza uhaba wa mbolea na gharama kutokuwa kubwa ukilinganisha na mbolea ya kuagizwa kutoka nje ya nchi.

Mwaka 2016 pia, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) lilianzisha kampuni ya uzalishaji wa mbolea nchini iliyofahamika kama Tanzania Mbolea and Petrochemical Company (TMPC) yenye lengo la kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbolea, hususan mbolea aina ya DAP na UREA.

Uwekezaji huu wenye thamani ya Shilingi trilioni 6.8 umehusisha pia wawekezaji tofauti, wakiwemo Fauji Fertilizer CO. LTD (Pakistan), Haldor Topsoe AS (Denmark) na Ferostaal Industrial Projects (Ujerumani) ambapo kila mwekezaji atakuwa na umiliki wa hisa asilimia 25.

Kukamilika kwa kiwanda hiki kutaifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa mbolea katika eneo la kusini mwa Jangwa la Sahara. Hatua hii ilifikiwa siyo tu kwa sababu Tanzania ilikuwa na uhitaji mkubwa wa mbolea bali pia uwepo wa uchimbaji wa gesi asilia katika mwambao wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

SOMA ZAIDI: Wakulima: Bei za Mbolea Zahatarisha Uzalishaji wa Chakula Nchini

Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati Medard Kalemani aliwahi kunukuliwa akisema kuwa katika uchimbaji wa gesi asili hiyo, jumla ya mita za ujazo (M3) bilioni 121 za gesi zingetumika katika uzalishaji wa mbolea ambao bidhaa ya kwanza itatoka kiwandani mwaka 2027, huku mbolea aina ya UREA kwa asilimia 64 na DAP kwa asilimia 36 zikitarajiwa kuzalishwa.

Mtikisiko soko la dunia

Nchi ya Urusi imekuwa muuzaji mkubwa wa mbolea kwenye mataifa mengi duniani. Baada ya vikwazo vya uchumi ilivyowekewa na mataifa ya Ulaya kufuatia uvamizi wake nchini Ukraine, hali ya upatikanaji wa mbolea duniani imepungua. Mataifa mengi yameathirika, hususan yale ya Afrika. 

Ifahamike kuwa asilimia 80 ya mbolea yote barani Afrika imekuwa ikiagizwa kutoka mataifa ya nje, huku ukanda wa Afrika Magharibi ukichangia asilimia 40 na mataifa ya Kusini na Mashariki yakichangia asilimia 60 ya matumizi yote ya mbolea katika ukanda wa Sahara. 

Nchi ya Nigeria kwa sasa imekuwa si tegemezi tena wa mbolea kutoka mataifa ya Ulaya baada ya kukamilisha kiwanda chake cha Indorama Fertilizer CO.LTD ambacho kinakadiriwa kuzalisha takribani tani milioni tatu za mbolea kwa mwaka.

Kutokana na changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa sasa, mataifa mengi zalishaji barani Afrika, hasa Morocco, Nigeria, na Algeria yamejikuta zaidi yakifanya biashara na mataifa nje ya Afrika kwa kulenga faida zaidi, hivyo kuacha uhitaji na ongezeko la mbolea barani Afrika likiendelea kukua.

Kwa mfano, nchi ya Brazil imekuwa ikiagiza moja ya tano ya mbolea yake yote kutoka Urusi, hali ya vikwazo imepelekea kutengeneza mashirikiano zaidi ya kibishara kwa sasa na Morocco.

SOMA ZAIDI: Wakulima Mbozi Wagoma Kuuza Kahawa Yao Wakidai Bei Hairidhishi

Kasi hii ya mahitaji ya mbolea nje ya Afrika imekuwa ikionekana pia ikizinufaisha nchi kama Nigeria na Algeria.

Kwa Upande wa Afrika, hali hii imeendelea kuathiri na inategemewa athari zake zitaendelea kukua endapo mgogoro baina ya nchi ya Urusi na mataifa ya Ulaya pamoja na Ukraine hayatofika muafaka.

Inachoweza kuvuna Tanzania

Soko la Tanzania kwa sasa linapaswa kulenga hasa kwenye kutimiza hitaji la uzalishaji na usambazaji wa mbolea kwa wakulima wa ndani ya nchi. Uzalishaji huu utapunguza gharama za uingizaji wa mbolea kutoka mataifa ya nje, hivyo kumfanya mkulima kupata unafuu wa bei. 

Kupitia mpango wa ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP), Serikali inaweza kuchangia zaidi kwenye kuongeza na kuboresha uzalishaji kwenye viwanda viwili vikubwa vinavyojihusisha na uzalishaji wa mbolea kwa sasa, kiwanda cha Minjingu na kile cha Itracom. 

Ubia huu utachagiza uzalishaji kuwa wa kasi na mkubwa, hivyo kuweza kuhimili soko la ndani lakini pia kuweza kupanua soko katika nchi za jirani ambazo zimekuwa njia panda katika upatikanaji wa mbolea na hasa ukizingatia nafasi ya mashirikiano ya kibiashara kupitia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfcFTA).

Katika Ukanda wa SADC, ni Tanzania na Msumbiji pekee ndiyo zenye rasilimali muhimu za uzalishaji wa mbolea, hali inayoifanya Tanzania kuwa na upekee wa kuzifikia nchi nyingi katika ukanda huu achilia mbali urahisi wa usafirishaji kupitia bandari na reli.

Tanzania inapaswa, kwa haraka, kuangalia namna inavyoweza kujiingiza kwenye uzalishaji na usimamizi wa biashara hii kama ilivyofanya Nigeria kupitia Benki Kuu ya nchi hiyo katika ushirikiano wa ujenzi na uzalishaji katika kiwanda cha Dangote Fertilizer Plant.

SOMA ZAIDI: Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri

Ripoti ya tathmini ya matumizi ya mbolea nchini Kenya imeeleza kwa kina namna mbolea ya Minjingu ilivyosaidia wakulima nchini humo, hususan katika zao la mahindi. 

Pia, nchini humo, kilimo cha mazao ya mapambo, kama vile maua, ni kikubwa na mbolea inayotumika kwa wingi ni Urea-formadehyde ambayo huzalishwa nchini Tanzania.

Wakati ujenzi wa kiwanda cha TMPC ukiendelea, ni vyema Serikali ikaona fursa iliyopo katika kipindi hiki na kuitumia kutengeneza soko na kujiingiza kwenye biashara ya mbolea mapema, hasa ikizingatiwa mahitaji ya bidhaa hiyo ni makubwa barani Afrika kuliko uzalishaji. 

Tanzania ina vyanzo vya uzalishaji wa bidhaa hii katika maeneo mengi kuanzia Manyara, Lindi, Mtwara, na Dodoma. Hivyo, Serikali inapaswa kujiwekeza zaidi kwa kushirikiana na wawekezaji wazalishaji wa sasa ili bidhaa hii iwe na manufaa katika kipindi hiki.

Ni muda muafaka sasa kwa Mifuko ya Hifadhi za Jamii, Benki Kuu, Benki ya Kilimo na mashirika mengine ya umma kushirikiana na viwanda hivi viwili ili kuongeza mitaji ya uzalishaji, teknolojia, na wataalam wa masoko ili Tanzania iweze kunufaika na fursa iliyopo kwenye uzalishaji wa mbolea.

Ezra Nnko ni mchambuzi wa uchumi na siasa za kimataifa. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ezra.nnko@gmail.com au +255 765 571917/+255 784 527018. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *