The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rais Samia, Tunaomba Utuachie Kitabu Chenye Hadithi Nzuri

Falsafa yako ya kisiasa imeeleweka, lakini naamini unaweza kuacha urithi zaidi katika uchumi na maendeleo ya Watanzania.

subscribe to our newsletter!

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan,

Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, aliwahi kusema kwamba kila zama na kitabu chake. Na Machi 19, 2021, ulipoapa rasmi kuitumikia Tanzania kama Mkuu wa Nchi na Kiongozi Mkuu wa Serikali, ulianza rasmi kuandika kitabu cha zama zako. 

Imetimia miaka miwili sasa, na kwa hakika, wabobezi na wanagenzi wa uchambuzi wa siasa-uchumi, wamekupa alama nzuri katika tathmini zao. 

Pamoja na kuendeleza miradi ya kielelezo na huduma kwa jamii kama mtangulizi wako, Watanzania wanatambua kuwa umeliongoza taifa kutoka katika taharuki za watu wasiojulikana, UVIKO-19, na sura mbaya tuliyoijenga katika medani za kidiplomasia. 

Kwa hakika, unakula sahani moja na Baba wa Taifa kwa kuwa na falsafa ya uongozi inayotambua maridhiono, ustahimilivu, mabadiliko, na kujenga upya (ukiita Falsafa ya R4). 

Lakini pia, umegoma kuwaogopa wapinzani, na kuamua kutekeleza matakwa ya sheria kwa kuruhusu mikutano ya siasa ili mpambane kwa hoja. Lakini pia, umesisitiza upo tayari kushauriwa! 

Kwa hakika umesheheni sifa za kiongozi bora na haya ni mambo ya kupongezwa! Lakini si lengo la waraka huu kupongeza tu, bali kuainisha changamoto za wakati wetu na matarajio yetu kutoka kwako.

Msukumo wa kukuandika waraka huu unatokana na ukweli kuwa, mnamo Machi 16, 2023, nilialikwa kwenye kipindi cha Malumbano ya Hoja kinachorushwa na kituo cha ITV, na niwasifu sana ITV kwa kuitisha mjadala huo, na hasa kwa mtangazaji ndugu Juma Kapalatu, kwa kuvumilia hoja za kusifu na ukosoaji wenye tija zilizotolewa. 

Mheshimiwa Rais, umeyaruhusu maoni ya wadau kwa kuwa unaamini yataleta tija katika uongozi wako. Lakini katika mambo ambayo nilisema, na kwa bahati mbaya sikupata fursa ya kufafanua zaidi, ni kuwa tathmini zilizofanywa na taasisi zenye mamlaka zinasema hatukuwahi kuingia kwenye uchumi wa kati wa chini kama tulivyotangaziwa Julai 1, 2020.

Sikusema hilo kwa mara ya kwanza, kwani nimewahi kuandika makala ya uchokozi na tuliwahi kuwa na mjadala kuhusu jambo hilo kupitia kituo cha runinga cha UTV. Kauli hii ilipelekwa JamiiForums. 

Nilitegemea JamiiForums, kwa jinsi ilivyokuwa na watu makini, waendeleze mjadala. La hasha! Nikaishia kusoma matusi tu. Japo mimi ni mtetezi wa uhuru wa maoni, lakini nilitegemea maoni tofauti kwenye jamvi hili wa kiuanazauoni tofauti na Twitter au Instagram.

Lakini kuhusu ukweli kama tupo uchumi wa kati au la, hoja ya msingi inabaki palepale, na haya si maneno yangu, kwa sababu anayefanya tathmini na kupendekeza nchi kuhitimu kutoka kwenye uchumi wa chini kabisa siyo Benki ya Dunia, bali ni Commitee for Development Policy, iliyopo chini ya Department of Economic and Social Affairs iliyopo chini ya United Nations Economic and Social Council (ECOSOC).

Hawa wanatumia vigezo vitatu: Ukisoma ripoti ya kamati hii iliyoandikwa na wabobezi huru, utagundua kuwa hatujafikia kiwango cha kuhitimu katika vigezo vyote vitatu. Na kinachonisikitisha zaidi ni kwamba, katika nchi zinazoongelewa kuhitimu katika mwaka wa tathmini 2024 ni Cambodia, Comoro, Djibouti, Senegal, and Zambia, lakini Tanzania haimo. 

Tukumbuke kuwa Benki ya Dunia hufanya tathmini kwa malengo yake ya kibiashara ili wajue nani wanaweza kumpa mikopo ya kibiashara au mikopo ya masharti nafuu, lakini wanaangalia kigezo kimoja tu cha kipato, yaani GNI per capita, na hawaangalii Human Assets Index wala Economic and Environmental Vulnerability Index. Kwa hiyo, hatupwaswi kuchukua ripoti ya Benki ya Dunia kama ndiyo tamko la mwisho. 

Labda nisisitize tu hapa, kukiri kuwa hatukuvuka si dhambi hata kidogo, bali ni ukomavu wa kisiasa na itatusaidia kuongeza bidii zaidi ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea ifikapo 2025. 

Huenda 2024 tathmini itakapofanyika ni jirani mno, lakini kwa nionavyo kasi ya uwekezaji katika elimu, afya, miundombinu, na uzalishaji mali tunayoenda nayo awamu ya sita, huenda tutakuwa tumevuka wakati wa tathmini ya mwaka 2027. 

Naam! Tuna changamoto nyingi katika jamii, lakini kama nilivyotanabahisha hapo awali, Chifu Hangaya umeonyesha uwezo na mbinu za kipekee za kiuongozi kuweza kutuvusha. Serikali unayoingoza ina mipango mingi kuliko hata tunavyoweza kuigharamia! 

Lakini hii haiondoi uhalali wa sisi kuendelea kukujazia mipango, ilihali tukufanyie tathmini utakapoondoka madarakani. Nikukumbushe tu kuwa, wewe ni Rais si kwa bahati mbaya, ila kwetu sisi tunaoamini katika Mungu, ni kwa makusudi maalum. 

Na hivyo basi, vita vyako viwe ni namna gani utawaachia Watanzania urithi mzuri ili usemwe kwa mema katika ndimi zao, na si namna gani utaendelea kubaki madarakani kwa kupambana na kila wanayekuambia anataka kukuangusha usichaguliwe 2025. Ili uwe wa pekee, itakupasa uwe juu ya siasa uchwara.

Mheshimiwa Rais unalindwa na Ibara ya 37-(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kupokea ushauri. Lakini hatuna budi kuendelea kutoa ushauri. Na mimi nitaangazia katika maeneo machache tu ninayoyaona kuwa ni ya kimkakati.

Sekta ya kilimo

Mara baada ya kuibuka kwa vita vya Urusi na Ukraine, naikumbuka siku ambayo mawaziri wako watatu – Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Kilimo na Waziri wa Uwekezaji – walilazimika kutoa ufafanuzi kwa mapungufu yaliyotukumba kutokana na vita hiyo katika mafuta ya kula na unga wa ngano. 

Lakini pia kwa nyakati tofauti tumekuwa na tatizo la sukari hapa nchini. Chief Hangaya, Ukraine ni theluthi mbili tu ya ukubwa wa nchi yetu. Wana takribani hekta milioni 32 za ardhi inayofaa kwa kilimo wakati ardhi yetu ya kilimo ni hekta milioni 44. 

Kwa nini tuwategemee Ukraine watutimizie mahitaji yetu? Nimemsikia Waziri wa Kilimo Hussein Bashe akiongelea kupeleka wataalam kupima ardhi ya Njombe ili ngano zilimwe kama zao la kimkakati eneo hilo, hizi ni habari njema. 

Lakini nakumbuka enzi za Mwalimu Nyerere NAFCO ilikuwa na mashamba ya ngano (mfano – Wilaya ya Hanang), yalifia wapi? Tuna uwezo mkubwa wa kuzalisha alizeti na mawese, kwa nini tusijitosholeze kwenye mafuta ya kula? 

Tuna uwezo mkubwa pia wa kuzalisha miwa na kutengeneza sukari, tunakwama wapi? Ningetamani Serikali yako iweke mikakati katika uzalishaji wa mazao haya ya kimkakati ili kukidhi mahitaji ya ndani na mauzo ya nje.

Mheshimiwa Rais, sekta ya kilimo kamwe haitafanya vizuri bila kufungamanisha sekta hiyo na viwanda. Ukisoma Kifungu cha 46 (c) cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020-2025) ahadi hii ipo wazi. Mwendelezo wa uzalishaji wa mazao yanayotoa mafuta ya kula, sukari na ngao unalazimu tuwe na viwanda vya kuchakata mazao haya. 

Tukishahimiza uzalishaji, Serikali hainabudi kuhimiza uwekezaji katika viwanda husika kama sekta binafsi haipo tayari. Ningependekeza tufuate modeli ya ubepari wa dola (state developmentalism), iliyofanya vizuri Japana na nchi zinazofahamika kama East Asian Tigers kama vile China, Korea Kusini, Singapore nakadhalika.

Modeli hii inahimiza dola kufanya uwekezaji wa moja kwa moja katika miradi ya kimkakati badala ya kusubiri wawekezaji binafsi. 

Lakini pia Mheshimiwa Rais, tunapaswa kuwekeza katika sekta ya viwanda vinavyosaidia maendeleo ya kilimo. Tukianza na mbolea, Tanzania ina malighafi zote zinazohitajika katika kuanzisha viwanda vya mbolea. 

Ni habari njema kwa kiwanda kikubwa kinachoanzishwa Dodoma, Intracome Fertilizers, na kile cha Minjungu, lakini tunapaswa kufanya tathmini ili tuzalishe mbolea ya kutosha nchini na kuuza nje ya nchi. Tunatumia pesa nyingi kuagiza mbolea ambayo tungeweza kuzalisha hapa nchini.

Tunahitaji pia viwanda vinavyozalisha zana za kilimo za kisasa. Tofauti na Zana za Kilimo – Mbeya, tunahitaji zana zinazotumia mota, rahisi kutumia na bei yake ni nafuu. Tafiti zinaonyesha kuwa China na Vietnam zimepiga hatua kubwa kwa kuwa na zana za namna hiyo, na naamini tunaweza kujifunza kutoka kwao. 

Ni aibu kwa nchi katika karne ya 21 kuwaacha wakulima wetu wategemee jembe la mkono na wateseke kwa kutumia nguvu na muda mwingi katika mnyororo wa uzalishaji. 

Niliwahi kufanya tathmini ya mradi mmoja wa asasi za kiraia ambao ulilenga kuhamasisha ubunifu hapa nchini, na walengwa walikuwa na uwezo wa kuunda zana zenye mota zinazoweza kulima, kupanda, kumwagilia, kuvuna, kupukuchua, na kuchakata mazao mbalimbali. 

Tunahitaji teknolojia hiyo, na tunaweza kuzikaribisha nchi za Asia Mashariki zenye uzoefu nayo watufundishe.

Lakini katika kuongeza tija na kulima kisasa, Mheshimiwa Rais tunahitaji kuviwezesha vituo vyetu vya utafiti. Sijui tunavijali vipi kwa sasa, lakini nilipata kuvitembelea vituo hivi mwaka 2014 – Ilonga, Ukirigulu, Uyole, Dakawa, na vinginevyo – vilikuwa katika hali mbaya. 

Watafiti wetu wanapaswa kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu mbegu, udongo, mbolea nakadhalika. Nimefurahishwa na mradi wa kuhuisha kazi za wagani, lakini wagani wanapaswa kuwa waenezi wazuri wa matokeo ya tafiti zinazofanywa na taasisi zetu za kilimo.

Mwisho katika kilimo ni kuwa na soko rafiki kwa wakulima. Tusidanganyane, mkulima aliyezalisha msimu huu kwa wingi na akakosa soko hatazalisha tena msimu ujao. Na akizalisha kwa wingi, atakuwa anafanya biashara kichaa. 

Natambua kuwa Wizara ya Kilimo ina kitengo kinachoitwa Market Intelligence Unit, lakini pia katika ngazi ya kitaifa kuna Tanzania Mercantile Exchanges (TMX), taasisi ya PPP inayoshughulika na biashara zingine mbali na kilimo. Lakini kulikuwa na wazo la Market Intelligence Unit (MIU) kuwa kitengo kinachojitegemea. 

Hili ni wazo zuri na lenye msaada kwa sekta ya kilimo, na napendekeza tuwe na Taanzania Agricultural Commodity Exchange (TACE) badala ya MIU na ifanye kazi kama taasisi inayojitegemea lakini chini ya Wizara ya Kilimo. 

Taasisi hii itakuwa na uwezo wa kusaka taarifa za mazao yenayohitajika kwa wingi na bei za mazao na kuzisambaza kwa wakulima kwa mifumo rafiki. TACE inaweza kushirikiana na TMX katika biashara kwa ujumla, lakini ni muhimu kuwa na chombo mahsusi kwa ajili ya sekta ya kilimo.

Sekta ya Utalii

Mheshimiwa Rais, Tanzania: The Royal Tour imetutangaza kwa dhati kabisa, lakini tunahitaji kufanya zaidi. Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha miji inayotembelewa zaidi duniani ni Paris na Dubai. 

Wengi tunavutiwa kutembea huko, lakini hakuna maajabu ya vivutio kama ambavyo Tanzania tunavyo, kwa kuwa tumejaaliwa vivutio vya asili. Lakini kwa bahati mbaya, hatufahamiki. 

Mwaka 2022, nilikuwa Dubai nikakutana na watalii wa Kijerumani, wakaniuliza natoka wapi nikawajibu Tanzania, lakini wakanishangaza eti hawaijui Tanzania. Hata hawa waliotutawala bado hawatujui kweli? Tuongeze kujitangaza. 

Sijui Rais Paul Kagame wa Rwanda alilipa pesa ngapi kuwa katika jezi ya Arsenal, lakini nimesikia mara kadhaa tukisema UAE ni marafiki zetu. Sijui, ila kama UAE ni marafiki zetu, basi watubebe kwenye kututangaza kama walivyopandisha ile bendera yetu kwenye jengo refu la Burj Khalifa. 

Naamini utalii ni life style na mara baada ya kufika sehemu ungependa kujua mwaka kesho utaenda wapi na si kurudi kulekule. Kama Dubai wakiwa marafiki wazuri watatutangaza kwa watalii wanaomwagika nchi hiyo mwaka hata mwaka ili watembee Tanzania pia. 

Lakini jambo la maana zaidi ni kuwa, tuweke mikakati ya kuutangaza zaidi utalii wetu.

Mheshimiwa Rais, ulizungumzia kuhusu medical tourism hapa kwetu. Kwa hakika tuna utangamano wa kisiasa kiasi cha kumfanya mtu yeyote ajisikie amani kuwa Tanzania. 

Naunga mkono utalii wa afya, lakini natamani tuwekeze kwenye huduma za juu kabisa za afya. Viongozi wa Afrika mara nyingi wanakimbilia India kwa utalii wa afya, japo pia kuna hospitali maarufu zaidi duniani. 

Kwa nini na sisi tusiwe na hospitali maalum ya kutoa huduma za afya kwa viongozi wa Afrika na kada zingine maalum? Tuna maeneo mazuri yenye mandhari kama Ulaya tu. 

Arusha, au hata Lushoto, inaweza kuwa kituo cha utalii wa afya chenye huduma zote tunazofuata India, Israel, Ulaya na kwingineko na tukahudumia maelfu ya watalii wa afaya kwa faida ya uchumi wetu.

Utalii wa michezo, kukuza vipaji

Kwenye utalii pia ningependekeza tuandae mazingira ya utalii wa michezo. Sisi tunaopenda michezo tunasikia kila siku Arsenal au Manchester United, Manchester City, Barcelona, Real Madrid nakadhalika wameenda kuweka kambi Dubai au Afrika Kusini. Tungetamani wawe pia wanakuja Tanzania. 

Kwa nini tusitengeneze mazingira ya vituo vya michezo vyenye hotel nzuri za nyota tano na viwanja bora japo vinne tu kule Arusha ili kuvutia watalii wa michezo? Lakini uwekezaji huu unapaswa kuendana na ujenzi wa viwanja vyenye hadhi ya kimataifa. 

Sijui ule uwanja wa Dodoma aliotuahidi Mfalme wa Morocco umeishia wapi, na nakumbuka pia ahadi yako ya kukarabati viwanja vya michezo. Ningematani katika kipindi chako cha uongozi utuachie japo viwanja viwili vyenye hadhi kama kile cha Hayati Ben Mkapa. Si pesa n yingi, na ukiamua utaweza.

Katika suala la michezo ningependa kuhitimisha na ombi nyeti kabisa lenye lengo la kukuza vipaji nchini. Tanzania vipaji vya michezo mbalimbali vipo lakini hatujawahi kufanya jitihada za makududi kuviendeleza. Vipaji ni ajira na kama tukipata watakaowakilisha nchi nje ya nchi ni chanzo cha mapato kwa nchi. 

Tukitaka kuviendeleza vipaji hivi tunapaswa kuwa na mkakati. Nashauri tujenge vituo vya michezo (Sports Academy) japo katika kanda tano za nchi hii Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, na Arusha. Vituo hivi vitusaidie kulea vipaji katika michezo ya mpira wa miguu, mpira wa kikapu, kuogelea, riadha, na tenisi. 

Hatuwezi kuwaachia kulea vipaji TFF peke yao kwani tutakosa kuendeleza vipaji vya michezo mingine. Tunaweza kujenga vituo hivi karibu na shule za sekondari za umma ili wanamichezo wapate fursa ya kusoma masomo mengine. Shule hizi zitakuwa maalum kwa vipaji vya michezo japo zinaweza kuwa na wanafunzi wengine ambao si wanamichezo.

Kutengeneza mabilionea

Hayati John Pombe Joseph Magufuli wakati akifungua Bunge la 12 nilialikwa TBC kufanya tathmini ya yaliyojiri. Nilisikiliza hotuba kwa umakini kabisa, na kati ya mambo yaliyonivutia ni hoja yake ya kutengeneza mabilionea. 

Kwa bahati mbaya hakuishi kuyatimiza hayo, ila hii ni moja ya hoja ya msingi inayogusa umiliki wetu wa uchumi. Ni sawa kuvutia wawekezaji, lakini nchi zilizopiga hatua muhimu kama za Asia ya Mashariki zilihakikisha zinakuwa na kada ya wawekezaji wa ndani wanaoshikilia uchumi wa nchi. 

Hatuwezi sote tukawa wawekezaji lakini ni muhimu kada hii ikawepo. Kwa namna yeyote ile, dhana ya kutengeneza mabilonea siyo dhana inayouzika sana kwa umma na watu wengine wanaweza kuiona hoja tata. 

Lakini taarifa zinaonyesha kuwa nchi kama China zimefanya vizuri mno katika eneo hili. Napenda kutoa mapendekezo machache ya namna ya kutekeleza hili.

Mosi, kusaidia Watanzania kuanzisha makampuni yatakayokuwa na uwezo wa kutekeleza miradi ya nchi ya ndani na hata kupata uzoefu wa kupata miradi ya maendeleo nje ya nchi. 

Makampuni haya yanapaswa kujengewa uwezo, kuaminiwa, na kusimamiwa kwa karibu zaidi katika kazi zao kitu ambacho kitawapa uzoefu zaidi. Ni wazi kwamba nchi kama China, wakikupa mkopo wa kujenga miundombinu, kwenye masharti ni lazima wakupe kampuni ya kichina kutekeleza mradi. 

Lakini walianza na kuyakuza makampuni haya nchini kwao, na yanaitwa flagship companies kwa kuwa yanapeperusha bendera ya China. 

Pili, taifa linapaswa kuwahamasisha na kutoa mchango kwa wawekezaji wa ndani wanaotaka kujenga viwanda vya uzalishaji kwa kutumia bidhaa za ndani. Si muda wote wawekezaji wa nje watavutiwa na uwekezaji hapa nchini. 

Kuna maeneo ya kimkakati ambapo nchi inataka uwekezaji ufanyike, ni lazima tuwe na mikakati ya kisera. Nchi hutumia mbinu nyingi katika eneo hili la kutengeneza mabilionea, lakini njia ambayo haitazua maswali ni pamoja na Serikali na Wizara ya Uwekezaji kupokea maombi mahsusi ya watu wanaotaka kuwekeza katika viwanda. 

Wizara inaweza kuainisha fursa zilizopo na kuitisha wadau wawasilishe miradi ya uwekezaji. Wakapewa masharti ya mtaji wa uwekezaji, watoe tathmini ya uwezo wa kuajiri wa viwanda wanaokusudia kuvijenga na mchango wao katika mtaji wa kuanzisha kiwanda. 

Kwenye miradi bora kabisa, Serikali inaweza kuongezea mtaji na ikawa na hisa katika viwanda husika. Mpango huu ukisimamiwa vizuri utatusaidia kuwa na viwanda vya kimkakati na vikaendeshwa kwa tija kubwa.

Miundombinu ya kimkakati

Mheshimiwa Rais, tunahitaji kuwa na picha pana katika eneo hili. Kwa kuanzia, wazo la Bandari ya Bagamoyo linahitaji kauli yako thabiti kuwa ‘tutawekeza.’ Kumekuwa na kauli za uoga katika mradi huu, lakini tumefanya mijadala mingi ya kiuanazuoni na hitimisho linaonyesha kuwa ni mradi wenye tija kubwa kwa taifa. 

Tunapaswa kuangalia ni namna gani tutahimiza uwekezaji wenye masilahi mapana kwa taifa letu. Najaribu kufikiri kwa kina muunganiko ya mambo yafuatayo: Mosi, hamasa yetu ya kukuza uchumi kupitia modeli ya Export-led Growth, kazi ambayo inaendelea kwenye Export Processing Zones (EPZ); nawaza fursa tuliyonanayo ya kuzalisha zaidi na kuuza nje bidhaa za viwanda zinazotokana na kilimo; fursa yetu ya kuwa kitovu cha kibiashara (commercial hub) katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kupokea bidhaa zinazotoka nje na kuzisambaza kwenye ukanda;- utagundua kuwa tuna baraka kubwa mno ya kijiografia. 

Pamoja na kukusihi uwe na kauli imara kuhusu Bandari ya Bagamoyo, lakini nashauri pia tuwekeze zaidi katika ujenzi wa reli ya kisasa ili kupata muunganiko. Nasoma Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-25, nahamasika na mikakati iliyowekwa kwenye Sekta ya Uchukuzi Ukurasa wa 86. 

Mheshimiwa Rais, sidhani kama kuna uwekezaji katika miundombinu utakaotulipa kama reli ya kisasa (SGR). Tunajenga barabara mara kwa mara na bado zinachakaa mno kwa kuwa tunazitegemea sana. Hata ajali nyingi zinazotokea si bahati mbaya tu, ni kwa sababu tunategemea sana usafiri wa barabara kusafirisha watu na mizigo.  

Hivyo basi, ukiachilia mbali kazi inayoendelea katika ujenzi wa reli, ningetamani katika kipindi cha utawala wako ijengwe reli ya Mtwara- Mbambabay ili bandari yetu ya Mtwara iwahudumie ndugu zetu wa Malawi ambao wanakaribia milioni 20. 

Watu miloni 20 (theluthi moja ya idadi yetu) ni soko kubwa sana, hatuwezi kujuta kulihudumia, na huu utakuwa uwekezaji wenye tija kubwa kiuchumi. Lakini pia reli ya kisasa ya Dar es Salaam – Tanga; halafu Tanga- Moshi- Arusha hadi Musoma itahamasisha sana utalii wa Kanda ya Kaskazini na usafirishaji wa watu (watalii) na bidhaa.  

Naomba pia utawala wako ufikirie kuiboresha reli ya TAZARA ili iwe ya kisasa (SGR) kwa ajili ya kuwahudumia ndugu zetu wa Zambia. Zambia inatajwa kuingia katika uchumi wa kati ifikapo 2024 na pia ina idadi ya watu takribani milioni 20. 

Hii ni fursa kubwa mno kwetu. Kwa hakika reli ya TAZARA ilijengwa kwa ushirikiano, na naamini Zambia watashawishika kuipandisha hadhi reli hii. 

Mheshimiwa Rais, wachambuzi wa siasa-uchumi huwa wanatuita a sleeping giant kwa sababu uwezo wetu wa kuwa regional power ni mkubwa mno. Kwa mfano, wanatushangaa gesi tunayo ya kutosha lakini tunazubaa kuhamasisha matumizi yake kwenye magari na majumbani. 

Wakati tunapambana na kupanda kwa bei ya nishati na hasa mafuta, inashangaza kuona watu wanapanga foleni masaa matatu ili kujaza gesi kwenye magari na huduma hii inapatikana Dar es Salaam tu! Kwa nini tushindwe kutumia rasilimali zetu za ndani kwa ufanisi? 

Lakini kwa maoni yangu tunaweza kuamka usingizini na kuwa ‘Kaka Mkuu’ wa Ukanda (regional power) kwa kuwekeza kwenye hii miundombinu ya kimkakati, yaani Bandari ya Bagamoyo na reli ya kisasa kama CCM ilivyofafanua kwenye Ilani yake. 

Hata hivyo, hii ni ilani ambayo Serikali inapaswa kuitekeleza. Natambua kuwa huu ni uwekezaji mkubwa na tunapaswa tujidhatiti. Mara nyingi nimefuatilia mjadala wa mikopo na Deni la Taifa ikiwemo Deni la Serikali. 

Watu wengi wamekuwa hasi kwa mwenendo wetu wa kukopa na jinsi Deni la Taifa linavyoongezeka. Lakini katika uwekezaji wenye tija kukopa ni kawaida. Kama lengo letu la kukopa ni kwa ajili ya uwekezaji utakaobadili uchumi wa nchi yetu katika miundombinu hii, hatuna budi kukopa zaidi. Isipokuwa tu yafaa tukope kwa masharti nafuu na deni letu liendelee kuwa himilivu.

Hitimisho

Hizi ni zama za kitabu cha Chifu Hangaya, na sisi wachambuzi tutakifanyia uchambuzi kitabu hiki mara Awamu ya Sita itakapokamilika. Nikukumbushe tu Mheshimiwa Rais kuwa kipindi hicho tutakuwa huru, kuandika kwa uzuri au kwa ubaya. 

Maisha ya binadamu yeyote ni kama hadithi, lakini maisha ya kiongozi ni hadithi inayovutia hisia za wengi. Tungeomba utuachie kitabu chenye hadithi nzuri. Falsafa yako ya kisiasa imeeleweka, lakini naamini unaweza kuacha urithi zaidi katika uchumi na maendeleo ya Watanzania. 

Naiona kesho iliyo njema, na kwa hakika tupo kwenye hatua ya kugeuka katika mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu. Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais, akupe ujasiri wa kuanzisha mserereko huu wa kimaendeleo. 

Mungu Ibariki Tanzania!

Dk Richard Mbunda ni Mhadhari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya siasa-uchumi. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia rmbunda@gmail.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Nimesoma kwa makini Uchambuzi wa Dr Richard Mbunda na kuona umekaa vizuri kisomi na kitaaluma ya Uchumi. Wasomi wetu waondokane na wimbi la kusifia nao kuwa Chawa badala yake wachukue mstari kama huu wa Dr Mbunda kuchambua na kushauri kwa ufasaha. Uchambuzi huu ungekuwa mzuri na more informed zaidi iwapo kwa kila pendekezo lake angebainisha – best approach, source of costs, faida na hasara ya kutokufanya yapendekezwayo. Nimefurahi kama msomi kuizugumzia Bandari ya Bagamoyo na kutilia chapuo unapaswa kuendelezwa lakini walinyamaza wakati ulipokuwa ukikanyagwa huku katika Miradi ambayo ilikuwa ikijadiliwa na Baraza la Mawaziri, Kamati ya Makatibu wa Kuu na Wataalamu huu ulikuwa Mmoja wapo na huku Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi chini ya Waziri aliekuja kuwa Rais ikiwa Dereva au Rubani Mkuu. Wenzetu Kenya wakachukua hesitance yetu wakaendeleza Bandari ya Lamu na hivyo kuongeza Ushindani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *