Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemfikisha Wakili Boniface Mwabukusi mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili kwa kile kilichodaiwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Katika shauri hilo Mwanasheria Mkuu analalamika juu ya kauli alizozitoa Mabukusi akiongea na vyombo vya habari. Moja ya kauli iliyotajwa katika malalamiko hayo ni maneno ya Mwabukusi kwamba, “Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawajui walichopitisha Bungeni kwamba hata Chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua ni Mkataba.”
Mwanasheria Mkuu anaelezea kuwa Wakili Mwabukusi alitoa kauli ambazo ni za kichochezi, zisizo na staha na zisizozingatia taaluma ya uwakili.
Katika siku za hivi karibuni Wakili Mwabukusi ameibuka kuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa Mkataba kati ya Tanzania na Dubai, mkataba unaoipa kampuni ya DP World ya Dubai kuendesha, kuboresha na kuendeleza bandari za Tanzania. Mwabukusi amekuwa akitumia majukwaa mbalimbali ikiwemo mikutano ya hadhara kukosoa mkataba huo.
“Mbarawa na Katibu Mkuu wake waondoke katika ile nafasi wanahatarisha mali za Tanganyika,” kauli nyingine aliyoitoa Mwabukusi ambayo Mwanasheria Mkuu anaitaja katika lalamiko lake hilo kama moja ya kauli za kichochezi, zisizo na staha.
Nipo Tayari Kulipa Gharama
Mwabukusi ni wakili anayesimamia kesi ya kupinga vipengele vya mkataba wa bandari kati ya Dubai na Tanzania, kesi iliyofunguliwa na wananchi wanne ambao ni Wanasheria, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus. Kesi hii inategemewa kutolewa uamuzi Agosti 7,2023, katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.
Akiongea katika majukwaa mbalimbali Mwabukusi ameelezea kuwa msimamo wake katika sakata la bandari ni kama wito, “sito ondoa mguu wangu katika hili [Sakata la Bandari], kwa sababu najua Mungu ameniweka kwa wakati huu, kama itabidi kufa ni vizuri hivyo” alieleza Mwabukusi Julai 12 akizungumza na waandishi wa habari.
Mwabukusi ameendelea kusisistiza kuwa haikua bahati mbaya yeye kuamua kupinga mkataba huo kama mwanaharakati na wakili, “Nilipiga hesabu nikajua gharama ya hiki ninachokifanya niko tayari kulipa gharama,” anaelezea Mwabukusi katika sehemu ya mawasilisho yake alipozungumza na vyombo vya habari.
Julai 14, Mwabukusi aliitikia wito wa Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya waliomtaka kufika kituoni kufuatia kauli zake mbalimbali alizozitoa. Hata hivyo baada ya mahojiano aliweza kuachiwa huru huku akisisitiza msimamo wake katika sakata la bandari umeendelea kuimarishwa.
Mwabukusi anatakiwa kupeleka utetezi wake katika Kamati ya Maadili ya Mawakili ndani ya siku ishirini na moja. Kama utetezi wake hautakubalika moja ya adhabu inayotegemewa katika shauri hili ni kuvuliwa uwakili kwa kuondolewa katika orodha ya mawakili Tanzania.
Wakosoaji wa Mkataba wa Bandari Matatani?
Wito kwa Mwabukusi unakuja takribani wiki mbili toka mkosoaji mwingine wa mkataba huu, Wakili Peter Madeleka awekwe mahabusu kufuatia kutolewa kwa uamuzi wa rufaa aliyokata katika makubaliano yake na Mwendesha Mashitaka katika kesi ya zamani iliyokuwa ikiunguruma Mahakamani Kuu Kanda ya Arusha. Toka Julai 17,2023, Madeleka ameendelea kusota mahabusu.
Mkosoaji mwingine wa Mkataba huu ambaye pia alikuwa Rais wa Chama Cha Mawakili Tanzania bara, Rugemeleza Nshala naye alilalamika kutishia kudhuriwa kwa sababu ya ukosoaji wake juu ya mkataba huu. Nshala aliitwa kwa mahojiano kituo cha Polisi sambamba na kusachiwa ofisini kwake.
Mkosoaji mwingine wa Mkataba huu Askofu Maxmilian Machumu, maarufu kama Mwanamapinduzi analalamika kuwa baada ya kushikiri mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CHADEMA na Sauti za Wananchi Julai 23,2023, alifuatiliwa na watu wasiojulikana, nyumbani kwake na pia katika ofisi yake iliyopo ndani ya kanisa analoliongoza. Machumu anaeleza kuwa alifuatiliwa na watu waliovaa mavazi rasmi ya vyombo vya ulinzi.
Mkosoaji mwingine wa Mkataba huu Deusdedith Soka ameendelea kulalamika kuwa toka akamatwe baada ya kuitisha maandamano ya kupinga mkataba wa DP World, Juni 19, ameendelea kupitia usumbufu mkubwa ikiwemo kushikilia vitu vyake kama funguo za nyumba pamoja na simu yake. Mkosoaji mwingine Mdude Nyangali alikamatwa na polisi Julai 17 na kukaa mahabusu kwa takribani siku tatu kwa sababu ya matamshi yake.