The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Wakuu wa Mikoa, Wilaya Wasiwe na Mamlaka ya Kukamata Watu, Tume Yashauri

Tume yataka iwapo mwathirika wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa au Wilaya atafungua shauri Mahakamani, basi huyo kiongozi awajibike yeye mwenyewe badala ya Serikali.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Vyombo vilivyo na mamlaka ya kukamata Tanzania vimelaumiwa kwa kutumia vibaya mamlaka yake ya ukamataji kwa ajili ya kuzuia na kupambana na uhalifu, hali inayotajwa kusababisha bughudha na kero nyingi kwa wananchi.

Lawama hizo zimeibuliwa na Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai Tanzania iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Janauri 31, 2023, na kukabidhi ripoti yake kwa Mkuu huyo wa Nchi hapo Julai 15, 2023.

Kwenye ripoti yake, tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, imebainisha uwepo wa mazoea miongoni mwa vyombo vya ukamataji Tanzania kukamata watu bila sababu na kukamata watu kwa makosa ya madai. 

Tume imegusia kesi ya mwanasiasa maarufu nchini Tanzania, Mchungaji Christopher Mtikila, aliyemshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwekwa mahabusu bila sababu za msingi, ambapo alishinda kwenye kesi hiyo. 

Tume pia imerejea shauri la Mary Peter Otaru dhidi ya Onesmo Buswelo na Wenzake, ambapo mlalamikaji aliwekwa mahabusu kwa siku tano na Mkuu wa Wilaya ya Siha kutokana na shauri la madai. 

Kwa kuwa Mkuu wa Wilaya hakuzingatia sheria katika kutoa amri ya kumweka mahabusu mlalamikaji, Mahakama Kuu iliagiza Serikali kumlipa mlalamikaji fidia ya Shillingi milioni tisini, tume hiyo imebainisha kwenye ripoti yake.

“Tume imebaini kuwa imejengeka desturi ya baadhi ya Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutumia Sheria ya Tawala za Mkoa, Sura ya 97 na Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61 kuminya haki za wananchi kwa masuala mbalimbali bila kuzingatia masharti yaliyowekwa na sheria,” inaeleza tume hiyo. 

“Aidha, tume imebaini kuwa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamekuwa wakiambatana na Wajumbe wa Kamati za Usalama katika ziara mbalimbali hata zile zisizostahili uwepo wa vyombo hivi,” inaongeza.

SOMA ZAIDI: Tume Yataka Mkakati wa Kitaifa Kubaini, Kuzuia Uhalifu Tanzania

Tathmini ya tume hiyo imebaini kuwa, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hujitambulisha kama Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, kitu ambacho imesema ni kinyume na Sheria ya Baraza la Usalama la Taifa, Sura ya 61 inayowatambua kama Wenyeviti wa Kamati za Usalama za Mikoa au Kamati za Usalama za Wilaya. 

“Vilevile, desturi ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuambatana na Kamati za Usalama katika ziara zao inaweza kusababisha hofu kwa wananchi na kuwafanya washindwe kufikisha mawazo na kero zao kwa viongozi hao,” tume imebainisha. 

Pia, tume imesema kwamba kwa viongozi hao kuambatana na Kamati za Usalama kunasimamisha baadhi ya majukumu yanayotakiwa kutekelezwa na Wajumbe wa Kamati za Usalama kwa nafasi zao. 

“Mathalan, wakuu wa vyombo vinavyohusika wanakosa muda wa kutosha wa kutekeleza majukumu yao ya msingi na mara nyingi hutumia vyombo vya usafiri vinavyohitajika katika utekelezaji wa majukumu mengine ya chombo kinachohusika,” tume imeeleza. “Aidha, desturi hii inaiongezea Serikali gharama kubwa ya matumizi ya fedha za umma.”

Kufuatia kubainika kwa masuala hayo, tume imependekeza yafuatayo:

  • Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura ya 97 irekebishwe ili kuondoa mamlaka ya ukamataji waliyonayo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na viongozi wengine kwa nafasi zao na badala yake viongozi hao wafuate utaratibu uliopo katika Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura 20 ambao unaruhusu mtu yeyote kumkamata mtu anayefanya kosa mbele yake.
  • Endapo ni muhimu kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuendelea kuwa na mamlaka ya ukamataji, viongozi hao waelekezwe kuwa wanapotekeleza mamlaka hayo kupitia vifungu vya 7 na 15 vya Sheria ya Tawala za Mikao, Sura ya 97 mtawalia, wazingatie masharti yote yaliyoelekezwa kupitia vifungu tajwa.
  • Baadhi ya masharti hayo ni: kosa liwe linatendeka mbele yake, liwe kosa la jinai ambalo mtu anaweza kushtakiwa, kosa litakalokuwa limetendwa liwe limesababisha kuvunjika kwa amani na utulivu na hakuna namna ya kulizuia kutendeka, ni lazima Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya, mara baada ya mtuhumiwa kukamatwa, amwandikie hakimu kueleza sababu zilizosababisha mtuhumiwa kukamatwa.
  • Mara baada ya maelekezo hayo ya kuzingatia matakwa ya sheria kutolewa, kiongozi yeyote atakayeyakiuka itabidi achukuliwe hatua kali, na iwapo mwathirika wa maagizo yake atafungua shauri Mahakamani, basi huyo kiongozi awajibike yeye mwenyewe na Serikali isiwe sehemu ya shauri hilo.
  • Serikali itoe maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusitisha utaratibu wa kuambatana na Wajumbe wa Kamati za Usalama pasipo kuwa na ulazima na pia waache kujitambulisha kama wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama.
  • Askari polisi au watendaji wengine wa vyombo vyenye mamlaka ya ukamataji wanaotumia vibaya mamlaka hayo wachukuliwe hatua za kinidhamu.
  • Wananchi wapewe elimu ili waweze kutambua haki zao ndani ya Mfumo wa Haki Jinai.
Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts