Jeshi la Polisi limethibitisha kumkamata Wakili Boniface Mwabukusi pamoja na Mpaluka Nyangali maarufu kama Mdude kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi.
Taarifa ya Jeshi la Polisi inakuja siku moja toka Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camilius Wambura kusema watachukua hatua za kisheria juu ya watu wanaofanya uchochezi, akiwataja wakosoaji wa mkataba kati ya Tanzania na Dubai juu ya uendeshaji bandari.
Akizungumza jana Agosti 11,2023, na waandishi wa habari IGP Wambura alielezea kuwa kumekuwa kukisambaa taarifa za kuandaa maandamano dhidi ya mkataba wa bandari.
“Taarifa hii inahusu kundi la watu ambao wanaeleza kuwa wanaandaa maandamano ya nchi nzima, ili kuiangusha ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya awamu ya sita kabla ya mwaka 2025,” alieleza Wambura.
“Lakini wakati wanaongelea taarifa hii na kutoa taarifa za ajabu hizo wanahusisha maandamano haya wanayofikiria kuyapanga na kushawishi jumuiya ya Watanzania kuwaunga mkono na hoja zinazoendelea za Bandari,” alifafanua zaidi Wambura.
Taaria ya IGP ilienda mbali zaidi na kuhusisha wakosoaji hao wa mkataba wa bandari na vitendo vya kupanga uhaini, “Tuliamini hoja za bandari hujibiwa kwa hoja na vile vile tukaamini kwasababu baadhi ya watu hawa walikwenda Mahakamani basi wangeheshimu maaumuzi ya Mahakama.”
“Badala yake wametoka sasa na kuanza kutafuta ushawishi na kuchochea kuwataka Watanzania waingie kwenye maandamano ya nchi nzima.
“Lakini mmoja amekwenda mbali zaidi na kusema watahakikisha wanaangusha serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya mwaka 2025, huu ni uhaini,” aliendelea kufafanua IGP Wambura.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, Mwabukusi na Mdude wamekamatwa majira ya saa nane usiku, maeneo ya Mikumi Morogoro.
Kukamatwa kwa Mwabukusi ni takribani siku mbili toka Mahakama Kuu Mbeya itoe hukumu juu ya kesi iliyofunguliwa kupinga mkataba unaoipa kampuni ya DP World ya Dubai haki za kuendesha, kuendeleza na kuboresha bandari za Tanzania.
SOMA:Mwanasheria Mkuu Ampeleka Mwabukusi Kamati Ya Maadili
Akizungumza nje ya Mahakama baada ya hukumu hiyo, Mwabukusi alieleza kuwa wanapanga kukata rufaa juu ya uamuzi huo na pia akaeleza kuwa wataitisha maandamano. Hata hivyo hakukua na mahali popote alipozungumza juu ya kuiangusha serikali.
“Tutatoa taarifa ya maandamano ambayo hayatakuwa na ukomo kama mkataba huu usivyokuwa na ukomo,” alieleza Mwabukusi Alhamisi ya Agosti 10,2023.
“Kulinda rasilimali ya taifa sio uhaini..tutatoa taarifa kama sheria inavyotaka kwa wahusika, na tutawataarifu Watanganyika kwamba ni wakati sasa wa kuzilinda rasilimali zetu kwa kutumia utashi wetu huru wa kikatiba wa kueleza hisia zetu kupitia ‘civil movemement’; maandamano na mikutano ya hadhara.”
Wakati taarifa za Mwabukusi kukamatwa zikisambaa majira ya asubuhi, moja ya walalamikaji katika kesi ya kupinga mkataba wa bandari, Alphonce Lusako, alieleza kuwa wakili huyo alikuwa akitoka Mbeya kuja Dar es Salaam kufanya taratibu za kukata rufaa katika kesi hiyo.
Hii ni mara ya pili kwa Mwabukusi kujikuta uso kwa uso na Polisi katika kipindi cha mwezi mmoja, mara ya kwanza alihojiwa Julai 17 na kuachiliwa. Mwabukusi pia anakabiliwa na madai katika kamati ya nidhamu ya mawakili, ambapo Mwanasheria Mkuu wa serikali amemshitaki, kwa kuvuja maadili ya uwakili katika matamshi yake juu ya mkataba wa bandari. katika kamati hii Mwabukusi anaweza kufutwa uwakili.