The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Ma-MC na Wengine Wanaotumia Taarifa Binafsi Bila Ridhaa Wanaweza Kudaiwa Fidia Kwa Sheria Hii Mpya

Kwa mujibu wa sheria hiyo taarifa binafsi ni taarifa kuhusu mtu anayetambulika ambazo zimetunzwa kwa namna yoyote

subscribe to our newsletter!

Wadau wanaotumia taarifa binafsi za watu bila ridhaa yao na wakati mwingine kuchepusha madhumuni ya matumizi yaliyokubalika wameaswa kuacha tabia hiyo kwani inaweza kuwaingiza mtatani kwa kujikuta wakilipa fidia kwa walalamikaji.

Hii ni kutokana na sheria mpya ya  Ulinzi Wa Taarifa Binafsi, 2022, sheria inayotoa ulinzi juu ya taarifa binafsi na faragha za watu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo taarifa binafsi ni taarifa kuhusu mtu anayetambulika ambazo zimetunzwa kwa namna yoyote. Sheria hiyo pia imeonesha kuwa pia kuwa kuna taarifa nyeti ambazo zinajumuisha  taarifa ya vinasaba, biometri, taarifa inayohusu watoto, taarifa inayohusu makosa, miamala ya kifedha, taarifa za kiafya au mahusiano ya kingono na mengineyo.

Sheria hii imeweka vigezo ambapo taarifa binafsi zinaweza kukusanywa kihalali, kwanza mkusanyaji wa taarifa lazima ahakikishe mhusika anatambua madhumuni ya ukusanyaji huo wa taarifa binafsi, na ajulishwe  wapokeaji wa taarifa hiyo ni nani na aridhie taarifa yake kutumika. Hii ni kwa taarifa binafsi ambazo hazijawekwa wazi.

Akizungumzia juu ya sheria hiyo mwanasheria Raymond Kanegene, mtaalamu wa sheria toka Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu, alitoa mfano juu ya namna Ma-MC wa sherehe mablimbali au kumbi za burudani wamekua na tabia ya kurusha picha na video za wateja wao katika mitandao bila kuwajulisha au kukubaliana nao.

“Hili ni kosa na wanaweza kulipishwa fidia kama waathirika wakilalamika,” alielezea Kanegene katika warsha ya masuala ya kidigitali iliyoandaliwa na taasisi ya isiyo ya kiserikali  ya Mulika, Agosti 17,2023, hapa jijini Dar es Salaam.

Mtalamu huyo aliendelea kueleza kuwa kwa watu waliokumbwa na kadhia hizo hatua ya kwanza ya kufanya ni kuchukua ushahidi kamili, kuwaandikia wahusika juu ya hali hiyo ambayo hujaridhika nayo na pia kupeleka malalamiko katika Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

Pia alishauri kwa Ma-MC, kumbi za buruduni na wengine ambao hukusanya taarifa za watu na kutuma mtandaoni ni vyema wakiwa kwenye kumbi husika kutoa tangazo juu ya taarifa zinazokusanywa, zinapelekwa wapi na pia kutoa fursa kama kuna mtu hataki taarifa zake zisitumike aweze kuwa na nafasi ya kuwajulisha.

Kwa taarifa nyeti kama afya, mahusiano ya kingono, taarifa ya vinasaba, miamala ya kifedha, idhini inayohitajika kwa ajili ya matumizi mbalimbali toka kwa mhusika lazima iwe ya maandishi. Sheria pia imezuia kwa wakusanyaji na wachakataji wa taarifa kutumia taarifa kwa madhumuni mengine yasiyohusika bila idhini ya mhusika wa taarifa ikiwemo matangazo ya kibiashara.

Iwapo taarifa binafsi imetumika kwa namna ambayo ni kinyume na madhumuni ya ukusanyaji, mhusika wa taarifa atakayepata madhara kwa sababu za ukiukwaji wa sheria ana haki ya kulipwa fidia. Tume ya Ulinzi wa Data ndiyo itakayosimamia taratibu za ulipwaji fidia.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *