Serikali kupitia msemaji wake Gerson Msigwa imeeleza kuwa tarehe ya mwisho kwa taasisi za umma kutumia mfumo wa manunuzi unaotumika sasa TANEPs ni Septemba 30,2023.
“Serikali imekuja na mfumo mpya unaitwa National e-Procurement System of Tanzania yaani NeST, alieleza jana Msigwa katika mkutano wake na waandishi wa habari. “Huu mfumo umejengwa na wataalamu Watanzania, wazalendo na umeeanza kutumika tangu Julai 01,2023.”
Mfumo wa TANEPS ambao unaondolewa ulianza kutumika nchini mwaka 2018, tofauti na mfumo wa sasa ulioundwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao(e-GA), TANEPS iliundwa na kampuni ya European Dynamics.
Baadhi ya changamoto zilizolalamikiwa juu ya mfumo huo unaoondolewa ni pamoja na ugumu wake wa kutumika, na mpaka mwaka 2023 bado kuna taasisi zilishindwa kuutumia kwa ukamilifu. Mfumo huo pia haukua una urahisi wa kutoa takwimu mbalimbali zinazoweza kusaidia Mamlaka kufanya maamuzi mbalimbali.
Wataalamu wa masuala ya manunuzi pia walikuwa wakikosoa namna mfumo huo ulivyofanya kazi, huku hatua za mwanzo za manunuzi kama mpango wa manunuzi, na tenda ndizo zilizokuwa zinaonekana kwa wadau wote, hatua zingine zikiwemo tathmini, mkataba na uendeshaji wa mkataba hazikuwa wazi. Jambo hili lilikuwa linatajwa kutokuendana na nadhari ya kuongeza uwazi serikalini.
Mfumo wa NeST unategemewa kuongeza uwazi zaidi hasa katika hatua zote za manunuzi, huku teknologia ya mfumo ikihakikisha taratibu zote za manunuzi zinaweza kufanyika ndani ya mfumo.
Msigwa ameeleza kuwa tayari Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha alikwisha kutoa waraka, Julai 27,2023, waraka ulionesha mwisho wa kutumia TANEPs ni Septemba 30.
“Hivyo basi kuanzia tarehe 01 mwezi wa kumi 2023 michakato yote ya zabuni za serikali, zabuni za umma zitafanyika kupitia mfumo wa NeST na hakuna taasisi yeyote itakayoruhusiwa kuchakata zabuni nje ya mfumo wa NeST,” alifafanua zaidi Msigwa katika mkutano wake huo wa waandishi wa habari.
Jambo lingine aliloeleze Msigwa ni kuwa tayari mfumo huo umeanza kuungwanishwa na mifumo mingine, ambapo mpaka Agost 26, tayari ulikuwa umeunganishwa na mifumo 19 ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na Mamlaka ya Mapato (TRA).
Hii inamaanisha kuwa kupitia Nest itakuwa rahisi zaidi kupata takwimu mbalimbali, na kuhakikisha baadhi ya fursa kama ile ya kuhakikisha asilimia 30 ya manunuzi ya umma, yanaenda kutekelezwa na kampuni za makundi maalum, zinaweza kufanikiwa kwa ukamilifu.