Dar es Salaam. Serikali imeyaondoa mapendekezo yaliyopelekwa Bungeni ya kufanya marekebisho ya sheria ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Maliasili ya nchi ya mwaka 2017 kuwa zisitumike katika miradi ya bandari.
Sheria hizo zilikuwa ni miongoni mwa sheria zilizojumuishwa katika Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 wa Mwaka 2023, uliokusudia kurekebisha, pamoja na sheria nyingine, sheria hizo mbili ili zisitumike katika uendeshaji wa miradi ya uendeshaji, uendelezaji na bandari.
Taarifa ya kuondolewa kwa marekebisho hayo ilitolewa leo Jumanne, Agosti 29, 2023, na Spika wa Bunge Tulia Ackson.
“Sehemu ya nne inafutwa ambayo inahusu mabadiliko kwenye sheria yetu ile ya marekebisho ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili ya mwaka 2017, mapendekezo yaliyokuwa yameletwa yanafutwa yote,” alitamka Dk Ackson.
“Sehemu ya tano inahusu marekebisho ya Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi Katika Maliasili ya nchi ya mwaka 2017 nayo inafutwa kwa maana ya kwamba Bunge halijaafiki,” aliongeza kiongozi huyo.
Hatua hii ya Bunge inakuja siku tano tangu The Chanzo iongee na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Masuala ya Kisheria, Joseph Mhagama, ambaye alieleza kuwa Kamati yake ilisitisha kupokea maoni juu ya mabadiliko haya yaliyopendekezwa na Serikali kwa sababu ilihitaji maelezo zaidi juu ya maudhui ya mapendekezo hayo.
“Muswada huo una sehemu sita, kamati iliona ifanyie kazi vipengele vinne tu, na kuviacha vingine viwili ili kutengeneza njia ya mashauriano na Serikali kwa lengo la kupata ufafanuzi wa maudhui ya sheria hizo mbili,” alieleza , Mhagama, ambaye ni mbunge wa Madaba (Chama cha Mapinduzi – CCM).
Sheria hizi mbili, pamoja na mambo mengine, ndiyo zinaipa nguvu Bunge kuweza kuipitia mikataba mbalimbali inayohusiana na maliasili na hata kuazimia kutaka Serikali ifanye mabadiliko. Sheria hizi zilipitishwa ili kuzuia mikataba mibovu na pia kuhakikisha Watanzania wananufaika na maliasili zao.
Wakati akifunga kikao cha Bunge cha Jumanne, Spika Ackson alitolea ufafanuzi wa sheria hizo mbili, akisema kwamba mhimili huo wa utungaji sheria haukuyakubali mapendekezo hayo ya Serikali, akisema: “Kwa hivyo, hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika katika sheria.”
One Response
Kwa hili Bunge nalipongeza kwa 100%. Naomba pia Bunge liachane au lifanye marekebisho makubwa kwenye Mkataba wa Dpw, hususan ukomo, bandari zote, uwepo wa haja ya kuijulisha Dpw kuhusu fursa zingine, Material breach, Usuluhishi wa Afrika Kusini.