The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

UN Women Yataka Ushiriki Zaidi wa Wanawake Kwenye Siasa, Uchumi

Kupitia mradi wake mpya, shirika hilo la UN lataka kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na wanawake kumiliki ardhi kwa njia rasmi.

subscribe to our newsletter!

Mtwara. Taifa likiwa linajiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa hapo mwaka 2024, na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025, wadau wamezidi kuonesha muamko wa kuchukua hatua zitakazoongeza ushiriki mkubwa zaidi wa wanawake kwenye michakato hiyo ya kidemokrasia ambayo imekuwa ikionekana kutokuwa rafiki kwa wanawake kutokana na mila na desturi potofu katika jamii.

Mdau wa hivi karibuni kabisa kujiunga na jitihada hizo ni UN Women, shirika la kimataifa linalofanya kazi kuchochea usawa wa kijinsia ulimwenguni, ambalo kwa sasa linatekeleza mradi kwenye mikoa sita ya Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Singida, Pwani na Singida, kushajihisha ushiriki mpana zaidi wa wanawake kwenye uongozi, hususan ule wa chini kabisa katika jamii zao.

Mradi huo unatokana na utafiti uliofanywa na shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwenye mikoa tajwa ambapo ilibainika kwamba ushiriki hafifu wa wanawake kwenye michakato ya kidemokrasia, ikiwemo kushiriki kwenye chaguzi, inatokana na mila na desturi potofu zilizokita mizizi kwenye jamii na kuwapunguzia nguvu wanawake kujitokeza kwenye michakato hiyo.

Hodan Addou ni Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania ambaye alisema kwenye hafla iliyowakutanisha wadau hapo Agosti 25, 2023, mjini hapa kwamba utafiti huo uliofanyika mwaka 2022 ulionesha mila na desturi hizo huwanyima wanawake nafasi ya kuzungumzia masuala yanayowagusa na kushindwa kuendana na mipango na bajeti zinazowekwa katika ngazi za Serikali za Mitaa.

“Kwa upande wa haki za kiuchumi kwa wananwake, utafiti huo unaonesha kwamba wanawake wachache humiliki vitega uchumi ukilinganisha na wanaume,” Addou alisema. 

“Wanawake wameendelea kukabiliwa na vizuizi katika haki ya kurithi mali na hutumia muda mchache kwa ajili kufanya shughuli za uzalishaji wa kipato ikilinganishwa na wanaume kutokana na kuwa na kazi kubwa sizizolipa zinahusu malezi na uangalizi wa familia wanazaofanya kila siku,” aliongeza Addou.

Kwenye mradi wao huo ambao utekelezaji wake ulianza rasmi Julai 2022, UN Women wanashirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote za wilaya, manispaa, kata na vijiji. Wadau wengine kwenye mradi huo unaotegemewa kutekelezwa katika kipindi cha miaka minne ni asasi za kiraia, taasisi za kielimu, viongozi wa kijamii, vilabu shuleni, watu maarufu na vyombo vya habari.

SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Mikakati Imara Kuongeza Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Kwa Mtwara, mradi huu umeanza kutekelezwa kwenye halmashauri za wilaya ya Mtwara na Manispaa ya Mtwara Mikindani, huku kwa halmsauri ya wilaya ya Mtwara ukitekelezwa kata za Naumbu na Msanga Mkuu ambazo kwa pamoja zikiwa na vikundi vya wanawake 43 wanaofikiwa na mradi huo. 

Kwa upande wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, mradi unatekelezwa katika kata ya Chuno na Mikindani ambapo umeweza kuwafikia wanawake zaidi ya zaidi ya 1,055 kutoka katika mitaa ambapo mradi huo unatekelezwa.

Ukombozi wa kiuchumi

Mbali na kulenga kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi, mradi huo pia unalenga kufanikisha ukombozi wa kiuchumi wa wanawake, huku ushajihishaji wa wanawake kuwa na hati za ardhi wanazomiliki ukitajwa kama sehemu muhimu ya mchakato huo.

Kwa mujibu wa maafisa maendeleo wa halmashauri ambazo mradi huu unatekelezwa, wanawake kwenye maeneo hayo wanadaiwa kutokuwa na uelewa juu ya kumiliki ardhi, huku wanaume wakitajwa kama ndiyo wenye mamlaka ya kumiliki ardhi kupitia hati miliki zinazotolewa na Serikali.

Vilevile, ndoa nyingi zinazofungwa kiholela zimeripotiwa kushamiri kwenye maeneo hayo, huku watu wakidaiwa kufunga ndoa bila kuwa na mtu sahihi wa kuwafungisha ndoa, badala yake huangalia tu watu ambao wanauelewa wa kusoma Quran ama maandiko matakatifu bila kujali utambulisho wao kwa mamlaka za kidini na Serikali. 

SOMA ZAIDI: TGNP Yataka Wanahabari Kuchochea Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Hali hiyo imedaiwa kuwaathiri wanawake kwa kuwa mara nyingi ndoa hizo zinapovunjika mwanamke huondoka bila kupata stahiki zake kama kugawana mali zilozozalishwa wakati wa ndoa, hali ambayo inapelekea wanawake wanaoishi kwenye maeneo haya kudidimizwa kuichumi.

Juliana Manyama, Afisa Maendeleo ya Jamii, Manispaa ya Mtwara Mikindani, alisema kwenye kikao hicho cha wadau kwamba kwa kipindi kifupi ambacho mradi umekuwa ukitekelezwa, wanawake wengi wameonekana kuwa na mwamko wa kufuatilia hati miliki za ardhi wanazomiliki.

“Katika mradi huu, tumebaini wanawake takribani 425 ambao wanamiliki vipande vya ardhi katika mitaa yote ambayo inapitiwa na mradi,” alisema Manyama. “Japokuwa vipande hivyo vya ardhi wanawake hao hawavimiliki kisheria, yaani bado hawana hati miliki ya hivyo vipande vyao vya ardhi.”

Naye Athmini Mapalilo, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, alisema kuwa mradi huo umeendelea kuonesha matumaini kwa wanawake kutambua haki zao za kiuchumi.

Shirika la UN Women lilifanya ziara ya kutembelea vijiji na mitaa inayotekeleza mradi wake ambapo katika vijiji hivyo wanawake wananufaika na mradi walielezea uzoefu wao na namna mradi huo unavyosaidia jitihada zao za kujitambua zaidi na kujikomboa kisiasa, kijamii, na kiuchumi.

Tulikandamizwa

“Akina mama sisi leo tunajua haki zetu za kumiliki ardhi na tunajua haki za kugombea uongozi,” alisema Mwanahamisi Libubulu, 50, mkazi wa mtaa wa Lwelu, Manispaa ya Mtwara Mikindani. 

“Sisi zamani tulikandamizwa,” aliongeza. “Ukienda kuolewa yaani unakuwa kama mtumwa. Unalima, unamaliza, mazao yakiwa tayari kwa mavuno, unaachwa, anakuja mwanamke mwingine anakuja kufaidika. Lakini sasa hivi kupitia elimu hii akina baba majumbani sasa hawatatufanyia tena matendo hayo.”

SOMA ZAIDI: ‘Sipendi Lakini Inanilazimu’: Simulizi za Wanawake Wanaolea Watoto Masokoni

Naye Salma Hamis, mkazi wa kijiji cha Mkungu, kata ya Nakumbuka, alieleza namna elimu iliyotolewa kupitia mradi huo imemsaidia siyo tu kujua thamani yake kama binadamu bali pia haki zake za msingi kama mwanamke na raia pia.

“Nimegundua kwamba kama nitakuwa na kile cheti cha ndoa, nitatumia kwenda mahakamani kupeleka maelezo yangu pale nitakapoachwa na kuwepo kwa dalili za kunyang’anywa mali zangu,” Salma, 27, alisema. “Kwa hiyo, utapata haki yako bila kizuizi chochote.”

Ipo hofu miongoni mwa wanaume, na hata miongoni mwa wanawake, kwamba endapo kama wanawake watawezeshwa kujua haki na thamani yao, na namna wanavyoweza kuzilinda na kuzipigania, hali hiyo itapelekea kukandamizwa kwa wanaume, hofu ambayo 

Lilian Liundi, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) amesema haina msingi wowote.

Imani potofu

“Imani kwamba mwanamke akiwezeshwa, na akaweza, ni chanzo cha kuvunjika kwa mahusiano, au ndoa, siyo kweli kwa sababu mwanamke anapoweza, na mwanaume anapoweza, ndipo wanaposhirikiana kwa pamoja na kwenda mbele kwa haraka zaidi,” Liundi alisema. 

“Na hicho ndicho tunachosema,” aliongeza mwanaharakati huyo, “kwamba ushirikiano kati ya wanawake na wanaume ni muhimu ili kusonga mbele zaidi kwa jamii yetu, kwa familia, na kwa taifa letu kwa ujumla.”

SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?

Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Wizara ya TAMISEMI, Adolf Ndunguru, ambaye aliambatana na wawakilishi wa shirika la UN Women kwenye ziara hiyo, aliuita mradi huo kama mradi wa kimsingi, unaolenga kuisaidia Serikali kwenye kufanikisha malengo na mipango yake.

“Mradi kama huu tunataka uongezwe kiasi ili uweze kutekelezwa kwenye nchi nzima ili Watanzania wanawake wajijue kwamba wana jukumu kubwa sana la kushiriki katika maendeleo ya taifa,” alisema Ndunguru.

Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts