The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Cheo cha Naibu Waziri Mkuu, Gharama Kuendesha Serikali Zazua Gumzo Mabadiliko Baraza la Mawaziri. Uchaguzi Mkuu 2025 Watajwa

Kwenye mabadiliko hayo, Jerry Slaa anakuwa mjumbe mpya kabisa kwenye Baraza la Mawaziri, huku Angeline Mabula akitupwa nje.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan leo Jumatano, Agosti 30, 2023, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, ambapo, pamoja na mambo mengine, ameanzisha cheo kipya cha Naibu Waziri Mkuu, na kumteua Dotto Biteko kuhudumu kwenye nafasi hiyo.

Kwenye mabadiliko hayo, Rais Samia pia ameivunja Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kutengeneza wizara mbili tofauti. Mbali na Naibu Waziri Mkuu, Samia pia ameteua mawaziri wanne, naibu waziri watano, Makatibu Wakuu watatu na Naibu Katibu Wakuu watatu pia.

Katika panga pangua hiyo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Angelina Mabula, ameachwa nje ya uteuzi, nafasi ambayo kwa sasa inashikiliwa na Jerry Slaa, Mbunge wa Ukonga (Chama cha Mapinduzi – CCM).

Silaa, ambaye hivi karibuni amekuwa akizunguka nchi nzima kama sehemu ya ujumbe wa CCM kufafanua juu ya mkataba wa bandari, ni ingizo jipya katika Baraza la Mawaziri. Silaa pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji.

Mbali na kumteua Biteko kama Naibu Waziri Mkuu, Samia pia amemteua Mbunge huyo wa Bukombe kuwa Waziri wa Nishati. Taarifa ya uteuzi imesema kwamba Biteko, aliyekuwa Waziri wa Madini, atakuwa anashughulikia uratibu wa shughuli za Serikali.

Anthony Peter Mavunde ameteuliwa kuwa Waziri wa Madini, huku Innocent Bashungwa, aliyekuwa Wizara ya Ulinzi, amepelekwa kwenye Wizara mpya ya Ujenzi.

Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchukuzi. Wakati tangazo la uteuzi likitolewa, Profesa Mbarawa alikuwa Bungeni akiongea na Wabunge juu ya mkataba wa masuala ya anga kimataifa.

Teuzi mpya nyingine ni zile za Manaibu Waziri, ambapo Alexander Mnyeti, Mbunge wa Misungwi ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo; David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini amekuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi; Judith Salvio Kapinga, Mbunge wa Viti Maalum (Ruvuma) amekuwa Naibu Waziri wa Nishati; na Dunstan Luka Kitandula, Mbunge wa Jimbo la Mkinga aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.

Naibu Waziri Mkuu

Kufuatia mabadiliko hayo kwenye Baraza la Mawaziri, mjadala mpana umeibuka kwenye majukwaa mbalimbali, ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii, kuhusiana na hatua hiyo, huku baadhi wakijiuliza yanalenga kufanikisha nini na endapo kama Uchaguzi Mkuu wa 2025 unaweza kuwa unahusika kwa namna moja au nyingine.

Moja kati ya masuala yaliyozua mjadala mpana, hata hivyo, ni uamuzi wa Rais Samia kutengeneza cheo kipya cha Naibu Waziri Mkuu, wengi wakijadili wadhifa atakaokuwa nao kiongozi huyo katika wakati ambapo kuna Waziri Mkuu, ambaye ni Kassim Majaliwa.

Hii, hata hivyo, siyo mara ya kwanza kwa cheo hiki kuwepo serikalini kwani Hayati Augustine Mrema alishawahi kuhudumu katika cheo kama hicho mwaka 1993 chini ya Serikali ya Alli Hassan Mwinyi. Mrema alitumikia cheo hicho huku akihudumu pia kama Waziri wa Mambo ya Ndani.

Mtu mwingine pia ambaye amewahi kuhudumu katika nafasi hiyo ni Salim Ahmed Salim aliyeshika nafasi hiyo huku akihudumu pia kama Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Baadhi ya watu waliochangia kwenye uamuzi huo walidai kwamba cheo hicho hakipo kikatiba, hoja ambayo hata hivyo mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kikatiba nchini, Deus Kibamba, siyo ya msingi, akisema kwamba hata kama cheo hicho hakipo kikatiba, Rais hazuiwi kumteua mtu kwenye cheo hicho.

“Ibara ya 36(1) ya Katiba inampa Rais mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya umma,” Kibamba aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Hivyo, katika hilo, [Rais] anayo madaraka.”

Kibamba amehusisha uwezo huo wa kimamlaka wa Rais na kile alichokiita mapungufu ya Kikatiba ambapo mkuu huyo wa nchi anakuwa na madaraka makubwa kupita kiasi.

“Rais  anaweza siyo tu kupangua mawaziri na kila mtu bali pia anaweza kupanga au kupangua muundo wa Serikali,” alisema Kibamba. “Katiba ya nchi nyingine zimekataza kubomoa muundo. Sisi yetu imeruhusu; [Rais] ana ruhusa ya kuunda na kubomoa muundo wa Serikali.”

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Israel Ilunde, ameiambia The Chanzo: “Labda kuna majukumu [Rais] anataka kuongeza kwenye ofisi ya Waziri Mkuu. Lakini lingine inaweza kuwa ni muhimu pengine kwa Waziri Mkuu kujitafakari kwa nini aongezewe mtu.”

Kibamba pia anaamini kwamba mabadiliko haya kwenye Baraza la Mawaziri yanaweza yakawa yamechochewa na sakata la bandari linaloendelea nchini, akisema kwamba Rais Samia atakuwa amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kuona yakuona kinachotokea kwenye sakata hilo.

“Vurugu iliyotokea, na makaso yaliyofanyika yalivyo makubwa, imembidi [Rais Samia] afanye jambo,” alisema gwiji huyo wa sheria.

Namna nyingine ambayo wadau wameyaangalia mabadiliko hayo kwenye Baraza la Mawaziri ni ile inayoutafsiri uamuzi huo kama sehemu ya mkakati wa Rais Samia kuimarisha Serikali yake, hususani katika kipindi hiki ambacho nchi inajiandaa na Uchaguzi Mkuu hapo mwaka 2025.

Baadhi ya wadadisi wameyaelezea mabadiliko hayo kama sehemu ya mpango wa Rais Samia kuwaweka karibu watu wanaonekana kuwa waaminifu kwake kwake kama Kiongozi wa Nchi.

Hata hivyo, baadi ya wadau wameiangalia hatua ya Rais Samia kwa jicho la kuongezeka ukubwa wa Serikali, wakitaja uundwaji wa Wizara mpya kama vichocheo vya kuongezeka kwa mzigo kwa walipa kodi wa Tanzania, hoja ambayo Thobias Messanga kutoka Jukwaa la Katiba (JUKATA) ameonesha kuinga mkono.

“Tunazidi kuongeza ukubwa wa Serikali,” Messanga, ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema. “Anayebebeshwa hapa mzigo ni mlipa kodi wa nchi hii. “Tunachohitaji ni uwajibikaji wa Serikali siyo kutanua ukubwa wa Serikali.”

Uteuzi wa Dotto na Mnyeti, wote kutoka Kanda ya Ziwa, umetafsiriwa kama mkakati wa makusudi wa kuendelea kujiimarisha kisiasa kwa Rais Samia kwenye eneo hilo linaloonekana kuwa ngome ya chama cha upinzani CHADEMA ambayo inaonekana kuelekeza nguvu zaidi tangu katazo la mikutano ya hadhara liondolewe.

Kwenye mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yaliyotangazwa Jumatano, inaonekana pia Rais Samia alishawishiwa na uwezo ambao baadhi ya wale walioteuliwa kuwa Manaibu Waziri ambao wamekuwa wakiuonesha mara kwa mara kwenye michango yao bungeni.

Moja kati ya watu hao Judith Kapinga ambaye amekua akitumia elimu yake ya uwakili kuchangia mambo mengi Bungeni, Dunstun Kitandula ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati Bungeni, na David Mwakiposa Kihenzile, ambaye pia ni alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara.

Mabadiliko mengine

Watu walioachwa kama Manaibu Waziri kwenye uteuzi huo wa Jumatano ni Freddy Atupele Mwakibete aliyekuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Marry Masanja aliyekuwa Naibu Waziri wa Mali Asili na Utali. Manaibu hawa wote wawili tangazo likitolewa walikuwa wakiendelea na shughuhuli zao Bungeni ikiwemo kujibu maswali na kutoa fafanuzi mbambali kuhusu Wizara zao.

Mawaziri waliohamishwa Wizara ni pamoja na January Makamba aliyehamishwa kutoka Wizara ya Nishati na kupelekwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato amehamishwa pia na kupelekwa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje kama naibu.

Uongozi wa Wizara ya Nishati unabadilishwa katika kipindi ambacho kumekuwa na changamato kubwa ya upatikanaji wa dola, hali iliyopelekea waingizaji mafuta kulalamika kwamba wanapitia mkwamo mkubwa, pamoja na bei ya mafuta kuongezeka mtaani.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wanaamini kwamba hatua ya Rais Samia kuwapeleka Makamba na Byabato katika Wizara ya Mambo ya Nje inaonesha bado Rais Samia ana imani na wateule wake hao, ukizingatia namna ambavyo Samia amekuwa akiingalia kwa karibu wizara hiyo.

Pia kwenye mabadiliko hayo, Stergomena Lawrence Tax amerudishwa kwenye Wizara ya Ulinzi, wizara aliyoitumikia kabla ya kuwa Waziri wa Mambo ya Nje.

Mohamed Mchengerwa amepelekwa kwenye Wizara ya TAMISEMI, huku Angela Kairuki akipelekwa kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa upande wake, Damas Daniel Ndumbaro amehamishwa kwenda kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Dk Pindi Chana, aliyekuwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, amepelekwa kuchukua nafasi ya Dk Ndumbaro katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Posts