Wahenga walituasa kwamba kila zama huja na mambo yake. Sisi wazazi wa leo, swali letu kubwa ni televisheni na mtandao wa intaneti. Tunalea watoto katika dunia ‘halisi’ na ile ya mtandaoni.
Kuna tofauti kubwa kati ya malezi ya zamani na malezi katika ulimwengu huu wa sasa. Wajibu wetu ni kuwafunda watoto wetu kuishi dunia zote mbili kwa weledi na mafanikio, kinyume na hapo, tutawanyima fursa za kuwa washindani katika dunia yao, wakati sisi tukiwa wazee sana ama tumelala mauti na hatupo tena duniani.
Sasa, ili kufanikiwa katika zoezi hili, tunapendekeza kwako utambue kwamba, wewe ni mfano wa kwanza kwa mtoto wako. Vitu vingi unavyofanya mtoto wako anaona na atajaribu kufanya kama wewe.
Kwa mfano, unapoingia Instagram, unatazama nini? Mipasho na maisha ya watu wa ‘mjini?’ Je, unafuatilia siasa za kitaifa na kimataifa? Au unatafuta kujifunza jambo au biashara, nakadhalika? Hakuna namna nyingine ya kujua kijana ama binti yako atakuwa mtu wa aina gani. Yeye ni matokeo ya wewe wa leo.
Je, wewe unayo maisha nje ya mtandao? Ni muhimu kuhakikisha kwamba mtoto anapata wakati wa kutosha nje ya mtandao na televisheni. Mtoto wako ajue kwamba kuna muda wa kutazama vipindi anavyopenda kwenye runinga, kwenye mitandao ya kijamii, na kuna muda wa kufanya vitu vingine.
SOMA ZAIDI: Je, Wazazi Tunajua Watoto Wetu Wanashinda, Kucheza Wapi?
Tenga muda wa kusoma vitabu au gazeti, hata kama ni la michezo. Tenga muda hata mara moja kwa wiki wa kusaidia kazi ndogondogo za nyumbani. Nenda shambani kalime hata kama ni bustani ya maua au mbogamboga.
Mtoto apate muda kucheza na wenzake, hii ni muhimu kwa mahusiano na koneksheni za ukubwani. Hii itampa nafasi ya kufurahia mazingira yanayomzunguka kwa kupata nafasi ya kujifunza vitu mbalimbali kutoka kwa wengine na kujumuika na wenzake.
Weka mipaka iliyo wazi kuhusu matumizi ya vifaa vya teknolojia na muda wa kuvitumia. Ukiweka kanuni za wazi kuhusu muda wa kuangalia runinga au kutumia simu na kompyuta itasaidia kumjengea mtoto nidhamu ya kufata ratiba yake pamoja na kutengenza uwiano mzuri kati ya ulimwengu wa kidijitali na maisha yake ya kawaida.
Ratiba na mipaka hii siyo kwa ajili ya mtoto pekee, hapana. Mipaka na ratiba hizi, ingawa ni kwa ajili ya mtoto wenu, zinawahusu zaidi nyie wazazi. Bora msiweke mipaka hii kama hamtaiheshimu.
Vipi kuhusu mtoto anayelilia simu na ukimpa tu simu hiyo ananyamaza? Kwa kweli, jibu sahihi kwa swali hili ni kutompa simu anapoililia. Fanya hivi mara zote anapolilia simu na kwa hakika utamsaidia kujifunza kwamba vilio na machozi siyo njia nzuri ya kuomba kitu au vitu.
SOMA ZAIDI: Fahamu Namna Unavyoweza Kusuluhisha Ugomvi Baina ya Watoto Wako
Zoezi hili linawahusu watoto wote bila kujali umri wao. Unamfundisha nidhamu adhimu: ukitaka kitu, au jambo, omba lakini usililie kama njia ya kushurutisha ombi.
Mwisho, inawezekana kabisa mtoto wako kutotumia simu yako ya mkononi. Mweleze simu ni kifaa cha mawasiliano na mahususi kwa ajili ya kazi, biashara, nakadhalika.
Mweleweshe kwa nini hawezi kuwa na simu kwa sasa na kwamba kutumia simu ya mtu mwingine ni kuingilia faragha ya mtu huyo, ikiwa ni pamoja na wewe mzazi wake.
Umewaona watoto wanaoparamia simu za wageni na kuomba nywila ili waingie kucheza gemu za simu? Unaipenda tabia hiyo? Basi mwambie mtoto wako muda wake wa kutumia simu utakuja.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.