Mtwara. Zuhairah Rajabu aligundilika kuwa na ugonjwa wa kisukari akiwa na umri wa miaka 17 tu. Sasa akiwa na umri wa miaka 22, mkazi huyu wa Manispaa ya Mtwara anakiri kwamba haijawahi kuwa rahisi kwake kukabiliana na ugonjwa huo, akitaja gharama kubwa za matibabu kama moja ya changamoto kubwa zinazomkabili.
Lakini kama ilivyo kwa wenzake wengi wenye umri kati ya 0 na 25 mkoani hapa, Zuhairah ana kila sababu ya kuwa na tumaini jipya baada ya kuanzishwa kwa kliniki ya kisukari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, maarufu kama Ligula, ambapo huduma hizo muhimu zimekuwa zikitolewa bure kwa wagonjwa wa kisukari walio na umri chini ya miaka 25.
Kliniki hiyo iliyoanza kufanya kazi Mei mwaka huu wa 2023 imeanzishwa kwa msaada wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA), shirika lisilo la kiserikali ambalo, pamoja na mambo mengine, husaidia watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari nchini Tanzania, ambapo inakadiriwa kuwa ni asilimia tisa ya Watanzania wote.
Mnamo Agosti 19, 2023, The Chanzo ilifika kwenye kliniki hiyo ikiwa ni siku mojawapo ya watoto wenye kisukari kuhudhuria, ambapo ilioni baadhi ya watoto, pamoja na wazazi waliowasindikiza, wakiwa wamekaa kwenye madawati wakiendelea kupatiwa huduma mbalimbali, ikiwemo elimu za namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Unafuu
Miongoni mwa waliofika hapa kliniki kupata huduma hiyo ni Zuhairah, ambaye alieleza ni namna gani uwepo wa kliniki hiyo unavyomsaidia yeye na wagonjwa wenzake katika kukabiliana na ugonjwa huo sugu.
“Kwa mfano kama dawa, nilikuwa natumia chupa mbili; kwa hiyo, ilikuwa inanigharimu sana,” alisema Zuhairah. “Natumia chupa mbili na chupa moja inauzwa Shilingi 20,000, chupa mbili ina maana inakuwa ni Shilingi 40,000.”
SOMA ZAIDI: Soma Hapa, Unaweza Kuwa na Uraibu wa ‘Energy Drinks’
“Kuna bomba [za sindano], na unakuta inabidi utumie bomba sitini [kwa mwezi mmoja], ina maana unatumia Shilingi 18,000, maana bomba moja linagharimu Shilingi 300. Kwa hiyo, hapo inakuwa kama Shilingi 58,000. Hizo ni gharama tu za dawa,” alieleza Zuhairah.
“Na unapoenda kliniki, unakuta lazima ukate cheti, na vile mimi sina bima, lazima ukate cheti kwa Shilingi 5,000 ndiyo unaenda kumuona daktari, na nauli bado hujatumia,” aliendelea kueleza. “Hii kliniki imekuwa msaada mkubwa kwa sababu sasa hivi unakuta unakwenda tu kila mwezi [na] unagharamia tu nauli.”
Ugonjwa sugu
Ugonjwa wa kisukari ni moja kati ya magonjwa sugu yanayoisumbua Tanzania, huku takwimu zikionesha kwamba watu wapatao 436,232 waliripotiwa kutafuta matibabu ya ugonjwa huo nchi nzima kati ya Julai 2022 na Machi 2023.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa ajili ya mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni, jijini Dodoma hapo Mei 12, 2023.
Kisukari, ambacho kinahusiana na uwepo wa sukari nyingi kwenye damu kuliko inavyotakiwa, ni moja kati ya magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanahofiwa kusababisha asilimia 33 ya vifo vyote vinavyotokea nchini Tanzania kila mwaka.
SOMA ZAIDI: Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?
Mbali na kisukari, magonjwa mengine yaliyopo kwenye kundi la magonjwa yasiyoambukiza ni kama vile pumu, shinikizo la juu la damu, kifua sugu, saratani, na uzito uliopindukia, pamoja na magonjwa mengine menig.
Wataalam wanataja mtindo wa maisha, ikiwemo ulaji usiyofaa, matumizi ya chumvi, msongo wa mawazo, na matumizi ya wanga kwa wingi kama baadhi ya sababu zinazopelekea kuongezeka kwa maradhi haya duniani.
Magonjwa yasiyoambukiza yanakadiriwa kuuwa watu wapatao milioni 41 kila mwaka duniani kote, sawa na kusababisha vifo saba kati ya kila vifo 10 vinavyotokea ulimwenguni kote.
Kila mwaka, watu milioni 17 huuwawa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza kabla ya kufika umri wa miaka 70, huku asilimia 86 ya vifo hivi vikiripotiwa kutokea kwenye nchi zenye uchumi wa chini na wa kati kama vile Tanzania.
Kwa hapa mkoani Mtwara, The Chanzo ilishindwa kupata takwimu sahihi za ukubwa wa ugonjwa huo baada ya kukosa majibu kutoka kwa mamlaka husika. Hata hivyo, ilipotembelea kliniki hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, The Chanzo ilishuhudia watoto kadhaa wakisubiri huduma za ugonjwa huo.
Mbali na Zuhairah, The Chanzo pia ilizungumza na Pendo Rashid ambaye alisema kwamba aligundulika kuwa na ugonjwa huo akiwa na umri wa miaka 15.
Sasa akiwa na umri wa miaka 20, Pendo anasema kwamba alikuwa anapatwa na uchovu wa mara kwa mara, kujisaidia haja ndogo mara kwa mara pamoja na kunywa maji mengi kabla ya kupimwa na kugundulika na ugonjwa huo.
SOMA ZAIDI: Wazazi wa Watoto Njiti Bahi Wafurahia Kufikiwa na Huduma za Watoto Wao
Kama wagonjwa wengine waliokuwepo katika kliniki hiyo, Pendo alishukuru uwepo wake, akisema itakuwa na msaada mkubwa kwa watu kama yeye ambao hapo mwanzo walilazimika kutumia gharama kubwa kukabiliana na ugonjwa huo unaowasumbua.
Dk Shukuru Shukuru ni Afisa Matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara ambaye aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano maalumu kwamba uwepo wa kliniki hiyo umesaidia kwa kiwango kikubwa kuhakikisha kwamba watoto wenye kisukari mkoani humo wanapata huduma stahiki.
Dk Shukuru alifafanua kwamba kabla ya uwepo wa kliniki hiyo, dawa zilikuwa zinanunuliwa na kutokana na gharama, wakati mwingine wazazi walikuwa wanashindwa kuhimili na hivyo kutowapeleka watoto kliniki kwa ajili ya matibabu.
“Kwa hiyo, wengine walikuwa wanajijua wana huo ugonjwa lakini walikuwa hawapati dawa kutokana na gharama,” Dk Shukuru aliiambia The Chanzo. “Kwa hiyo, uwepo wa hii kliniki umetatua hiyo changamoto.”
Zoezi endelevu
Happy Nchimbi ni Meneja wa Miradi kutoka TDA, shirika lililoanzisha kliniki hiyo ya kisukari mkoani Mtwara, aliiambia The Chanzo kwamba kliniki hiyo ni kati ya kliniki 38 ambazo shirika hilo limeanzisha kwenye maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara kusaida watoto wenye kisukari.
“Hili zoezi ni endelevu ambalo linahakikisha watoto wanakuwa na usaidizi katika kuzimudu hali walizonazo,” alisema Nchimbi kwenye mahojiano hayo. “Kwa hiyo, tunawasaidia [watoto] kuhakikisha kwamba wanapata insulin na huduma zingine zote wanazotakiwa kupata.”
Tiba ya sindano za insulin hutumiwa na wenye aina ya kwanza ya kisukari.
SOMA ZAIDI: Hii Ndiyo Njia Bora Ya Kukabiliana Na Magonjwa Yasiyombukiza
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara imeiteua Jumamosi kama siku ambayo wazazi wanaweza kuwapeleka watoto wao wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kisukari, huku Afisa Muuguzi Msaidizi hospitalini hapo, Mwanaisha Waziri, akisema siku hiyo imetengwa kwa makusudi ili kuwapata watoto hao kwa urahisi.
Waziri alisema kwamba siku ya Jumamosi watoto hupata muda wa kutosha tofauti na siku nyingine za wiki ambazo watoto, kwa kiwango kikubwa, huzitumia wakiwa shuleni.
“Mtoto anapofika kliniki tunapata muda wa kuongea naye, tukimuuliza changamoto alizopata kwenye matumizi ya dawa, muendelezo mzima wa sukari yake kwa ule muda wa mwezi mzima ambao hatujaonana naye,” alisema Waziri.
“Kama mtoto ana changamoto yoyote, atatuelezea, kama kuna ushauri, tutamshauri kwa wakati huo,” aliongeza mtaalamu huyo. “Lakini kwanza hapo ni kwa mtoto mmoja mmoja.”
Omari Mikoma ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Mtwara. Anapatikana kupitia omarmikoma@gmail.com.