The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Je, Unafahamu Kwamba Hata Mtoto Anaweza Kupata Kifua Kikuu?

Kati ya maambukizi mapya na ya kujirudia ya TB 86,653 yaliyoripotiwa nchini mwaka 2021, wagonjwa wapatao 14,033 walikuwa ni watoto chini ya miaka 15.

subscribe to our newsletter!

Alipofika akasema nimemleta mtoto anaumwa. Nesi akamuuliza mama mtu yuko wapi mtoto mwenyewe sasa, mbona umekuja peke yako? Kumbe vile vitenge alivyokuwa ameshika kwenye mkono mmoja ndani alikuwepo mtoto wa miezi kadhaa.

Mtoto alikuwa amedhoofu, amelegea!

Nesi aliita mwenzake haraka na kumuita daktari wampime, huku akimuuliza mama wa mtoto, “We mama, huyu mtoto kaanza kuumwa lini? Jamani nyie wamama nyie.” Mtoto alipimwa vipimo vya dharura na kuwekwa katika kitanda cha uangalizi wa karibu, huku akiwa ametundikiwa dripu.

Mtoto sukari yake ilikuwa chini, ameishiwa na maji na anahema kwa shida. Baada ya huduma ya kwanza, mama aliketi na daktari kumueleza historia ya mwanae huku machozi yakitiririka.

“Mwanangu alikuwa na afya njema tu,” alianza mama huyo, “hadi nilipoenda kumuuguza kwa mama, tukakaa kule muda mrefu sana. Bahati mbaya mama alifariki. Mama alikuwa anakohoa sana na homa haishuki.

“Tuliporudi kutoka kumuuguza mama, baada ya muda mwanangu akashikwa na kifua, jioni anatokwa na jasho sana na anapata homa. Nikampeleka akatibiwa nimonia, akapata ahueni kidogo tukarudi nyumbani.

“Lakini hali ikaendelea. Mama mkubwa akasema mtoto amerogwa, basi akamchukua tukaenda kwa mtaalamu. Tukakaa huko mwezi mzima akiogeshwa dawa lakini hali ikazidi kuzorota. Hivi nimetoroka tu kumleta hapa ambapo ndiyo tumaini langu la mwisho.”

Daktari akaandika, akatoa damu kwa ajili ya vipimo na kuagiza kufanyiwa kipimo cha makohozi kesho asubuhi kabla hajala kitu na kisha Xray ya kifua. Matibabu yakaanza, mama akaenda kwa watu wa ustawi wa jamii kwa ajili ya msamaha. Majibu yalivyorudi, ikagundulika mtoto alikuwa anaumwa kifua kikuu.

SOMA ZAIDI: Tuseme Ukweli, Mama wa Nyumbani Siyo ‘Golikipa’

Inawezekana kabisa bibi mtu naye alikuwa anaumwa kifua kikuu na ndipo mtoto alipopata maambukizi. Mama huyu na mtoto wake walikaa wodini mwezi mmoja na siku kadhaa, huku mtoto akiendelea kutibiwa kwani alikuwa na kifua kikuu, utapiamlo na upungufu wa damu.

Siku aliyokuwa anaruhusiwa, usingeamini ni yule aliyekuja amelegea. Mtoto alikuwa anacheka, vishavu vimetoka na uso wake ulikuwa ang’avu!

Siyo kila kikohozi ni nimonia

Tunapoelekea kuadhimisha siku ya Kifua Kikuu (TB) duniani hapo Machi 24, 2023, ni vyema tukafahamu kwamba hata watoto hupata TB. Siyo kila kikohozi ni nimonia na siyo kila homa ni malaria!

Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kifua Kikuu Tanzania (NTLP) unaonyesha kuwa mwaka 2021, kati ya maambukizi mapya na ya kujirudia ya TB 86,653 yaliyoripotiwa nchini, wagonjwa wapatao 14,033 walikuwa ni watoto chini ya miaka 15, ambayo ni sawa na asilimia 16 ya maambukizi.

Kati ya watoto hao, watoto 7,956 walikuwa watoto chini ya miaka mitano. Hii ni zaidi ya nusu ya watoto wote waliokuwa na maambukizi ya TB nchini.

SOMA ZAIDI: Huduma za Afya ya Akili Ziingizwe Kwenye Huduma za Mama na Mtoto

Mwaka 2020, kati ya watoto 13,592 walioripotiwa kuwa na TB, watoto 202 walifariki, na watoto 13,245 matibabu yalifanikiwa.

Kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya TB duniani inasema, Ndiyo, Tunaweza Kutokomeza TB. Ili kutimiza lengo hili, hata hivyo, hatuna budi kujikita katika watoto pia wenye maambukizi ya TB.

Tanzania ni kati ya nchi zenye maambukizi makubwa ya TB na ili kufikia lengo la 2030 la kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 80 na vifo kwa asilimia 90 hatuna budi kuifahamu vyema TB na kuwahi kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kupata huduma.

Je, unafahamu kwamba unaweza kutambua TB kupitia simu yako ya mkononi bure kabisa? Ndiyo, piga namba *152*05# kisha fuata maelekezo yanayokuja. TB bado ni tishio na tunaweza kuishinda.

Serikali ikishirikiana na wadau wengine wa afya kitaifa na kimataifa waameanzisha afua mbalimbali, ikiwemo hii ya Tambua TB; lakini pia kliniki ya TB inayotembea (mobile TB clinic) kuwafikia wananchi popote walipo ili wapime ugonjwa huo.

Kuduishe Kisowile ni daktari na mchambuzi wa masuala ya afya ya umma. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia kuduzekudu@gmail.com au kupitia Twitter kama @Kudu_ze_Kudu. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *