Michezo ina umuhimu mkubwa sana katika ukuaji, ustawi, na maisha ya mtoto kwa ujumla. Wataalamu wa malezi wanatuambia kwamba michezo inamsaidia mtoto kupanua wigo wa kufikiri, kushirikiana na wenzake, kujenga misuli na kuijua dunia inayomzunguka.
Michezo husaidia kukuza akili za watoto na hivyo kuwafanya wawe wepesi wa kujifunza. Hii ni kwa sababu michezo huaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kujenga ubongo wa mtoto na kuimarisha uwezo wake wa kufikiri na kuchanganua mambo kwa upeo mkubwa tofauti na umri alionao.
Kwa mfano, pale watoto wanapocheza michezo ya kujipikisha inaweza kuonekana kama vile wanajifurahisha lakini ukweli ni kuwa wanajenga uwezo wa kufuata hatua za mapishi.
Kupitia michezo hii watoto, hujenga udadisi na uchunguzi wa mambo, mara nyingi kwa kuuliza maswali ambayo huhitaji ufafanuzi kutoka kwa mzazi, mlezi, mwalimu, na yoyote aliyemzidi umri.
Michezo pia hukuza tabia ya upendo na ushirikiano baina ya watoto, hali inayowaandaa kujiamini waendapo shuleni na kukutana na watoto wenzao.
SOMA ZAIDI: Je, Watoto Wako Wanamheshimu Dada wa Kazi?
Watoto wanapocheza michezo mbalimbali pamoja huhisi kama wote ni familia, kwani kila mmoja huwa na umuhimu katika michezo wanayocheza na kutokuwepo kwa mmoja huenda kukasababisha pengo.
Kwa mfano, pale watoto wanapocheza mchezo wa kujificha, ni lazima wengine wajifiche mmoja awatafute.
Michezo ni sehemu ya burudani na furaha kwa watoto kwani mara nyingi michezo ya watoto hutawaliwa na vicheko na tabasamu. Watoto wanapocheza husahau yote waliyoyapitia na huhisi furaha.
Ndiyo maana muda wa kucheza unapofika watoto hawapendi kupoteza hata sekunde moja kwa jambo jingine kwani michezo kwao ni chanzo kikubwa cha furaha.
Kiafya pia, mazoezi husaidia kudhibiti uzito wa mwili. Kwa watoto walio na uzito uliozidi, mazoezi yanaweza kusaidia kupunguza uzito, wakati kwa wale walio na uzito wa kawaida, yanaweza kusaidia kudumisha hali hiyo.
SOMA ZAIDI: Je, Unamshirikisha Mtoto Wako Katika Kufanya Maamuzi ya Kifamilia?
Pia, mazoezi hulinda afya ya moyo kwa kuboresha mzunguko wa damu na kuimarisha moyo. Hii inaweza kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo katika maisha ya mtoto hapo baadaye.
Tusisahau kwamba, mazoezi siyo ya viungo tu, hivyo basi mzazi, au mlezi, hakikisha unampa mwanao vitu mbalimbali vya kuchezea kama vile midoli, michezo yenye mafumbo kama chess, au mpira, huku ukimsisitizia acheze michezo tofauti tofauti.
Pia, unapokua na muda wa ziada hakikisha unacheza na mtoto wako ili naye aone umuhimu wa michezo.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, Twitter: @SemaTanzania, na kupitia barua pepe yao www.sematanzania.org.
One Response
Your so good on your pages