Umri unaweza kutumika kama kigezo cha ubaguzi kwenye jamii, kama ulivyo ubaguzi mwingine wowote ule mwingineo, uwe wa rangi au kabila, na kuweza kuumiza kundi lolote katika jamii hiyo.
Hapa Tanzania, tunaweza kusema, upo ubaguzi wa kiumri, na makundi yanayoumizwa zaidi na ubaguzi huu huenda ikawa ni kundi la vijana na lile la wazee. Wazee wana changamoto zao lukuki, lakini mimi naomba nijikite na vijana kwa sababu nafanya kazi na vijana.
Pengine hakuna eneo ambapo madhara ya ubaguzi huu yanajidhihirisha waziwazi kama kwenye eneo la kugombea nafasi za uongozi wa kisiasa katika ngazi mbalimbali, iwe ni udiwani, ubunge, au hata urais.
Katiba yetu inaeleza sifa za mbunge, ambapo, pamoja na sifa nyingine, sifa ya umri imewekwa kuwa ni miaka 21. Hili ni takwa lisilo sahihi, linalochochea ubaguzi huu kwenye nchi yetu; ni takwa linalopaswa kufutwa na kuruhusu mtu anayeweza kupiga kura, agombee. Niruhusu nifafanue kwa nini naamini hivyo.
Mabadiliko ya mfumo wa elimu wa Tanzania yanayoendelea hivi sasa nchini mwetu yanapendekeza mtoto kuanza kusoma Darasa la Kwanza akiwa na wastani wa umri wa miaka sita na kumaliza Kidato cha Nne akiwa na wastani wa miaka 16.
SOMA ZAIDI: Vijana wa Siku Hizi ni Zao la Wazee wa Siku Hizi. Tuwe na Akiba ya Maneno Tunapowasimanga
Tuelewe kwamba baada ya miaka minne ya elimu ya sekondari, wanafunzi wengi wanaweza kuwa wamefikisha umri wa miaka 18, wakiwa tayari kisheria kama watu wazima. Si wote wataendelea na ngazi za juu za elimu kwani baadhi wanaweza kuingia kwenye maisha ya kujitegemea.
Ikiwa mapendekezo haya ya mfumo wa elimu yatatekelezwa, hii itamaanisha kijana mwenye umri wa miaka 16 atatakiwa kuanza maisha ya kujitegemea ikiwa hataendelea na ngazi nyingine ya masomo.
Bahati nzuri ni kwamba katika ngazi mbalimbali mpaka kufikia umri wa miaka 18, kijana anakuwa ameshashiriki katika nafasi mbalimbali za maamuzi na kuongoza, au angalau inapaswa kuwa hivyo. Shule zetu, kwa mfano, zina mifumo ya uongozi wa Serikali za Wanafunzi.
Kijana wa Kitanzania, kwa muktadha huu, mpaka anafikia umri wa miaka 18, anakuwa tayari ameshapata uzoefu wa kiuongozi, hususan katika kuendesha maisha yake binafsi, kusimamia maslahi ya wanafunzi wenzake na jamii inayomzunguka.
Ieleweke wazi kuwa kijana mwenye umri wa miaka 18 nchini Tanzania anaaminiwa tayari kuingia mikataba mbalimbali pamoja na kuingia katika ajira rasmi na kujiunga na jeshi na hata kutumia pombe na kucheza michezo ya kubahatisha.
SOMA ZAIDI: Je, Ni Kweli Ushirikishwaji wa Vijana Kwenye Uongozi Tanzania Ni Hafifu?
Mifano
Ipo mifano, hapa ndani ya nchi na kwengineko duniani, inayoonesha kwamba siyo lazima mtu atimize umri wa miaka 21 ndiyo astahili kuwa kiongozi wa kisiasa katika jamii yake. Sote tunahitaji kufikiria historia ya Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim, kutambua ukweli huu.
Akianza na majukumu mazito ya kiuongozi akiwa na umri chini ya miaka 21, Salim anakumbukwa nchini na duniani kote kwa uongozi wake thabiti unaoendelea kutambuliwa na kusifiwa na watu mbalimbali katika sehemu mbalimbali za dunia.
Hapo nchini Uganda, hadithi ya Hellen Auma Wandera, mwanasiasa anayeiwakilisha wilaya ya Busia kwenye Bunge la 11 la taifa hilo la Afrika Mashariki, inatufundisha somo muhimu kuhusiana na umri na uongozi.
Wandera, aliyeingia Bungeni akiwa na umri wa miaka 19 tu hapo mwaka 2021, aliwashinda wapinzani wake wengi waliokuwa na umri mkubwa kuliko yeye. Mpaka wakati naandika makala haya, sijasikia ripoti yoyote kuhusu kushindwa kwake kutekeleza majukumu yake ya kiuongozi kwa sababu ya umri wake!
Nyanja nyingine
Lakini tutakuwa tunafanya kosa kubwa sana kudhani kwamba uongozi unapatikana kwenye uwanda wa kisiasa tu. Hapa Tanzania, vijana wengi chini ya umri wa miaka 21 wamekuwa wakionesha uongozi uliotukuka kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo sanaa, biashara, ubunifu, na sayansi na teknolojia.
SOMA ZAIDI: Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe
Fikiria kijana kama Aslay aliyejipatia umaarufu mkubwa kwenye tasnia ya muziki nchini akiwa na umri wa miaka 16 tu. Au Abby Chams, binti anayelitikisa soko la muziki la Tanzania hivi sasa akiwa na umri wa miaka 20 tu, akitambulika kwenye dunia ya muziki tangu akiwa na miaka 18.
Au tumtazame kijana Baraka Mafole, kijana anayechochea mapinduzi ya kiteknolojia hapa nchini kwetu, akizindua kampuni yake ya Bongo Byte akiwa na umri wa miaka 17 tu, na mpaka kufika miaka 21 alikuwa tayari amekwishaandika kitabu chake juu matumizi ya majukwaa ya kiteknolojia katika kujitafutia kipato.
Mifano kama hii ipo mingi kiasi kwamba siwezi kuiorodhesha hapa yote. Itoshe kusema tu kwamba vijana walio chini ya umri wa miaka 21 wanaweza sana kuwa viongozi na punde Tanzania ikitambua ukweli huo itakuwa vizuri zaidi ili tuweze kunufaika na watu wetu.
Sasa, zipo hoja kutoka kwa watu wengi, wakiwemo wazee wetu, kwamba vijana chini ya umri wa miaka 21 hawawezi kuwa viongozi. Hii ni kauli inayosikitisha, hususan ikitoka kwa mzazi ambaye amempatia malezi sahihi kijana au binti yake kwa kipindi cha miaka 18.
Niseme hivi: kama wewe ni mzazi na unashawishika kwamba kijana wako aliyetimiza umri wa miaka 18 hawezi kuwa kiongozi, yaani hawezi kujisimamia mwenyewe na kusimamia wengine, basi unapaswa kujitazama upya na kutafakari kama kweli umetimiza wajibu sawasawa kama mzazi.
SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa
Nihitimishe safu hii kwa kutoa wito ambao wadau wengi wameendelea kuutoa, haja ya kuzifanyia marekebisho Katiba pamoja na sheria na kanuni za uchaguzi ili zitoe nafasi kwa kila mwenye sifa ya kupiga kura aweze kugombea nafasi ya uongozi wa kisiasa.
Tukumbuke kwamba Katiba yetu, sehemu ya tatu, inayosisitiza haki na wajibu, inataka isiwepo sheria yeyote Tanzania itakayombagua Mtanzania yeyote kwa kigoezo chochote kile.
Utaratibu wa sasa unaoweka sharti kwamba ili uweze kugombea nafasi ya uongozi wa kisiasa ni lazima uwe na umri wa miaka 21, unakiuka takwa hili muhimu la Kikatiba. Swali ni je, tutaendelea na ukiukwaji huu wa Katiba mpaka lini?
Ocheck Msuva ni Mkurugenzi Mtendaji wa Bridge For Change, shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa vijana. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ocheck.msuva@bridge4change.co. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.