The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Vijana Wachachamaa Wakitaka Umri wa Kugombea Upunguzwe

Wanataka umri wa kugombea ubunge, udiwani na uenyekiti wa Serikali ya Mtaa upunguzwe kutoka wa sasa 21 mpaka 18.

subscribe to our newsletter!

Dar es Salaam. Vuguvugu la vijana kushinikiza mamlaka za nchi kupunguza umri wa kugombea nafasi za uongozi wa umma katika ngazi mbalimbali limekuwa likishika kasi kwa siku za hivi karibuni, huku wawakilishi wa kundi hilo muhimu la kitaifa wakitaka mabadiliko hayo kufanyika kabla nchi haijaenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Vijana kutoka kwenye vyama vya siasa, asasi za kiraia na kwenye makundi mingine wanataka umri wa kugombea upunguzwe kutoka miaka 21 ya sasa mpaka miaka 18, wakisema kwamba hawaoni mantiki ya kwa nini mtu aweze kupewa leseni ya udereva akiwa na miaka 18 lakini bado aonekane hawezi kuwa kiongozi kwenye jamii yake.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 67(1), ili mtu aweze kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa mbunge ni lazima awe na umri wa miaka 21. Nayo Sheria ya Serikali za Mitaa, kifungu 39(2), inabainisha kwamba ili mtu aweze kuchaguliwa kwenye Serikali za Mitaa inambidi awe na umri wa kuanzia miaka 21.

Lakini vijana wamelalamika kwamba kwa kuweka kizingiti hiki, Katiba na Sheria ya Serikali za Mitaa zinawabagua maelfu ya vijana kwenye haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa kwa msingi wa kiumri, hali ambayo wamesema haikubaliki kulingana na ukubwa wa kundi lenyewe nchini Tanzania.

Taifa la vijana

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 34.5 ya Watanzania milioni 61.7 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35, huku watu milioni 3.7 wakiwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 20, ambayo ni sawa na asilimia sita ya Watanzania wote.

Ni katika msingi huu ndipo vijana wanaibua hoja yao ya kutaka umri wa mtu kugombea uongozi, ikiwemo ubunge, udiwani, na uenyekiti wa Serikali za Mtaa, upunguzwe ili kuruhusu vijana wengi kuomba ridhaa ya wananchi ili waweze kuzitumikia jamii zao husika.

SOMA ZAIDI: ‘Samaki Mkunje Angali Mbichi’: Shule Zinavyoandaa Vijana Dhidi ya Vitendo vya Rushwa

Mnamo Julai 2023 mwanasheria na mwanaharakati kijana Alponce Lusako alifungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Mahakama Kuu, akiitaka Mahakama iamuru kwamba vifungu hivyo vinakinzana na matakwa ya kikatiba yanayohusu haki na uhuru wa mtu kupiga na kupigiwa kura.

Hata hivyo, kesi hiyo ilishindwa kuendelea baada ya Serikali kuweka pingamizi, lakini Lusako aliiambia The Chanzo hapo Septemba 2, 2023, kwamba wanarudi tena mahakamani kuhakikisha kwamba mhimili huo wa utoaji haki nchini unaingilia kati kwenye kile alichokitafsiri kama ukiukwaji wa wazi wa haki za maelfu ya vijana.

Hakuna uwakilishi

“Vijana wana matatizo mengi kuhusu ajira,” Lusako alisema. “Inawezekana matatizo hayo yanatokana na kukosa uwakilishi wa vijana wenyewe kwenye vyombo vya umma. Kwa hiyo, tunachotamani sisi ni kuona vijana wenyewe wanaingia kwenye nafasi za maamuzi ili watetee ajenda zao, ikiwemo masuala ya ajira.”

Ikiwa ni sehemu ya vuguvugu hilo la kutaka uwakilishi zaidi kwenye nafasi za uongozi wa umma, vijana kutoka makundi na taasisi mbalimbali walikutana jijini Dar es Salaam hapo Septemba 2, 2023, chini ya mwavuli wa shirika lisilo la kiserikali la Policy and Legal Assistance Organisation (PLAO) kujadili mikakati itakayowezesha mabadiliko kwenye vifungu hivyo vya kikatiba na kisheria vinavyolalamikiwa.

Akizungumza na The Chanzo pembezoni mwa kongamano hilo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Abdul Nondo, alisema kwamba vifungu hivyo vinaenda kinyume na mantiki, akisema ni muda muafaka sasa wa Serikali kuvirekebisha kulingana na maoni ya vijana ili kuongeza ushiriki wa vijana kwenye uongozi wa umma. 

“Ukisikiliza hoja za watu ambao wanapinga, wanasema huyu kijana [mwenye umri wa miaka 18] bado hajapevuka kiakili,” alisema Nondo ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga matakwa hayo ya kikatiba na kisheria. “Lakini ni nani aliyesema kijana wa zaidi ya miaka 20, 21, 22, 23 kwamba ndiyo amepevuka?” 

SOMA ZAIDI: Barua ya Wazi kwa Wanasiasa Vijana wa CCM Kuhusu Rais Magufuli

“Ni kigezo gani mnakitumia kusema huyu kijana amepevuka sasa hivi kwa hiyo, akifikisha miaka 21 ndiyo agombee?” aliendelea kuhoji Nondo ambaye kitaaluma ni mwanasayansi ya siasa. “Kuna watu wana zaidi ya miaka 21, 22, 23, 24 lakini hawana uwezo kwenye uongozi. [Lakini] kuna mtu akishafikisha miaka 18 anaweza kuwa kiongozi.”

Mkanganyiko

John Pambalu ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) ambaye ameungana na Nondo kuonesha mapungufu kwenye matakwa hayo ya kikatiba na kisheria, akiungana na vijana wengine katika kushinikiza marekebisho juu yao.

“Kimsingi umri wa mtu mzima kwenye taifa letu la Tanzania unaanzia miaka 18,” Pambalu aliiambia The Chanzo kwenye mahojiano. “Na mtu akishafikisha umri wa miaka 18 kuna mambo, kwa mujibu wa sheria na Katiba zetu, unaruhusiwa kufanya. Kama kumiliki leseni ya biashara. Kumiliki leseni za vyombo vya moto [na] kuoa.” 

“Sasa kama mtu anaweza akafikia maamuzi makubwa kama maamuzi ya kuoa akiwa ana umri wa miaka 18, tunaamini umri huo unatosha kabisa kuwa kiongozi kuanzia Serikali za mitaa, udiwani na ubunge pia,” aliongeza Pambalu. “Kwa hiyo, sisi tunaona kwamba ipo haja ya kufanya marekebisho ya kikatiba pamoja na marekebisho ya kisheria yampe haki mtu atakapofikisha umri wa miaka 18 aweze kuchaguliwa.”

Janeth John ni mwanaharakati wa masuala ya vijana na jinsia ambaye anaamini kwamba ipo faida kubwa kwa vijana kushiriki kwenye michakato ya kiuchaguzi, akisema kwamba hata kama kijana huyo wa miaka 18 hatashinda, ushiriki wake utampa mafunzo muhimu yanayoweza kumjenga kwa baadaye.

“Kuna watu wanakaa miaka 10 wanaingia kwenye kampeni tu, miaka 10 mpaka 20, hajawahi kupata uongozi,” anabainisha Janeth. “Kwa nini kijana wa miaka 18 asiruhusiwe kugombea? Hata kama hatapata [ushindi] lakini atapata uzoefu ndani ya ile miaka yote; atakomaa kisiasa na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kushinda huko siku za usoni.”

Siyo nchi ya kwanza

Endapo kama vifungu hivyo vya kikatiba na sheria vitabadilishwa, Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kuruhusu vijana walio na umri wa miaka 18 kugombea nafasi za uongozi wa nchi, kwani tayari nchi kadhaa ulimwenguni zinaruhusu jambo hilo kwa vijana wao.

SOMA ZAIDI: Sababu za Mwamko Mkubwa wa Vijana Kugombea Nafasi za Uongozi Zatajwa

Nchi hizi ni pamoja na Australia, Denmark, Finland, Goergia, Germany, Kosovo, New Zealand, pamoja na nchi nyingine nyingi ulimwenguni. Mnamo mwaka 2021, kwa mfano, Maren Grøthe, raia wa Norway, alichaguliwa kama mwakilishi kwenye bunge la juu la nchi hiyo, Storting, akiwa na umri wa miaka 20 tu. 

Mnamo mwaka 2015 pia, wapiga kura katika jimbo la Paisley na Renfrewshire Kusini huko Scotland walimchagua Mhairi Black, binti aliyekuwa na umri wa miaka 20 tu, kuwawakilisha katika bunge la chini la Uingereza la House of Commons, akimuangusha mwanasiasa mwandamizi kutoka chama cha Labour, Douglas Alexander.

Ni mifano kama hii ndiyo vijana wa Tanzania huionesha kwenye harakati zao za kudai umri wa kugombea kupunguzwa, wakijenga hoja kwamba siyo lazima kijana atimize miaka 21 ndiyo awe na uwezo wa kuwawakilisha watu wa jamii zao.

Mnamo Agosti 12, 2023, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Vijana, miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na Jumuiya ya Vijana ya Chama cha Wananchi – CUF kuboresha ustawi wa vijana nchini ilikuwa ni pendekezo la umri wa kugombea kupunguzwa, huku Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo, Idd Mkanza, akitaka mabadiliko hayo yaharakishwe ili yaweza kutumika kwenye chaguzi za 2024 na 2025.

“Tunapendekeza kwamba badala ya Serikali kupeleka Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi na ile ya Vyama vya Siasa bungeni, yafanyike kwanza marekebisho ya haraka madogo ya Katiba ya mwaka 1977, ili kurekebisha vifungu vinavyotaja sifa za umri wa kugombea udiwani na ubunge uwe miaka 18 badala ya miaka 21 iliyopo kwenye Katiba na umri wa kugombea nafasi ya urais uwe miaka 35 badala ya miaka 40,” alisema Mkanza. 

“Umri wa kupiga kura uanzie miaka 15 badala ya miaka 18,” aliongeza mwanasiasa huyo kijana. “Tunafahamu tumeridhia mikataba, kama nilivyoeleza, na Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Tanzania ya 2007 inaeleza kijana miaka yake inaanza 15 mpaka 35. Kwa nini kijana alazimishwe kupiga kura mpaka kuanzia miaka 18?”

Lukelo Francis ni mwandishi wa The Chanzo kutoka Dar es Salaam. Anapatikana kupitia lukelo@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Mimi nataka niwape vijana changamoto ya kwanza kujijenga vizuri kifikra na kimmadili ili wawe viongozi wazuri. Hata wale ambao ni watu wazima na viongozi sasa ambao wanaminya uhuru wa wananchi kufanya maamuzi yao, waliwahi kuwa vijana. Na pengine walivyo leo kama watawala ni taswila ya jinsi walivyokuwa vijana. Vijana wasilalame bali waanzishe harakati za kuleta mabadiliko.Na wapambane kuleta mabadiliko ya kweli ya kimfumo ambayo yataishi hata baada ya wao nao kuwa wazee na hatimaye kufariki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *