The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Samaki Mkunje Angali Mbichi’: Shule Zinavyoandaa Vijana Dhidi ya Vitendo vya Rushwa

TAKUKURU inaamini kwamba elimu juu ya rushwa kwa watoto wadogo itasaidia kujenga taifa la wachukia rushwa.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Mamlaka nchini Tanzania zinaamini kwamba endapo elimu na mafunzo dhidi ya vitendo vya rushwa yataanza kuwafikia Watanzania wakiwa bado kwenye umri mdogo, vita dhidi ya vitendo hivyo vilivyopewa jina la adui wa haki inaweza kuzaa matunda yaliyokusudiwa.

Ni kutokana na imani hii ndipo Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) inawekeza katika kuendesha klabu za wapinga rushwa katika shule na vyuo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza usemi wa Kiswahili usemao samaki mkunje angali mbichi.

Kwenye mahojiano iliyofanya na wanafunzi kutoka shule mbalimbali ambao ni wanachama wa klabu za wapinga rushwa kwenye shule zao, The Chanzo iliona namna vijana hao wanavyolizungumzia suala la rushwa nchini, wakibainisha mchango wao katika kutokomeza vitendo hivyo.

Goodluck Samwel ni mwafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Bihawana ambaye aliiambia The Chanzo kwamba klabu za wapinga rushwa zimemsaidia kumuandaa na kumpa msingi imara unaomsaidia kufahamu athari za rushwa.

Zinasaidia

“Zinasaidia mahali pakubwa sana,” Samwel, 22, alisema kwenye mahojiano hayo. “Zinatuandaa kutoka chini.”

“Kwa hiyo, huko mbeleni, endapo siku moja nimekuwa kiongozi katika sekta fulani, watu watakuwa wanajua huyu mtu msingi wake toka chini alikuwa anapambania kitu fulani,” aliongeza. “Kwa hiyo, inatuandaa kuwa walimu bora na watu ambao ni washauri bora katika jamii.”

Gradson Kisambo ni mwanafunzi wa Biwahana Seminari anayesoma kidato cha tatu ambaye anaamini kwamba kupitia klabu hizo za wapinga rushwa, msingi imara unawekwa kwa ajili yake kuja kuwa kiongozi mzuri huko mbeleni. 

SOMA ZAIDI: Serikali za Mitaa, Halmashauri Zaongoza Kulalamikiwa kwa Rushwa Dodoma 2022

“Tutatokomeza kabisa rushwa kama Hayati Mwalimu Julius Nyerere alivyojitoa kukemea vitendo vya rushwa,” Kisambo, 17, alisema kwenye mahojiano hayo.

Naye Paulina Sekyusi, mwanafuzi wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Kizota, alisema sasa anajua namna ya kuepukana na vitendo vya rushwa wakiwa shuleni, akitolea mfano wa rushwa ya ngono.  

“Klabu inatusaidia sana katika kupinga vitendo vya rushwa ambazo zinaweza zikajitokeza shuleni,” Sekyusi, 17, alisema kwenye mahojiano na The Chanzo. “Kwa mfano, rushwa ya ngono kwa mwanafunzi na mwalimu au hata viranja wa shule inatusaidia kuziepuka.”

Rachael Mgude, mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Mnadani, anaamini kwamba klabu imemfanya kuwa balozi hata kwa jamii yake iliyo mzunguka kwa kukemea rushwa inapotokea.  

“Sisi kama vijana inatusaidia kupinga na kutokomeza rushwa inayofanyika majumbani mwetu au maeneo tofauti tofauti,” Mgude, 18, aliiambia The Chanzo. “Vitendo vya rushwa vinapotokea ni muhimu kutoa taarifa, kuwasilisha katika vitengo husika ili hatua ziweze kuchukuliwa.”

SOMA ZAIDI: Rushwa ya Ngono Kwenye Vyombo vya Habari Yawakera Wanahabari

Ikitajwa kama kikwazo kikubwa cha kuondokana na maisha duni ya Watanzania walio wengi, vita dhidi ya rushwa na aina zingine za ufisadi ni vita ya muda mrefu, ikitajwa kama kipaumbele cha kila Rais aliyewahi kuja kuongoza Tanzania.

Wakati hatua zimekuwa zikichukuliwa dhidi ya watu wanaothibitika kujihusisha na vitendo vya rushwa, wadau wamekuwa wakibainisha kwamba mapambano dhidi ya vitendo hivyo yanapaswa kwenda mbali zaidi ya hatua za kisheria na kujumuisha juhudi za kubadilisha tabia na utamaduni wa Watanzania kwa ujumla.

Shule na taasisi zingine za elimu zimekuwa zikitajwa kama sehemu sahihi za kutekeleza hilo kwani ni maeneo ambayo watoto wanakwenda wakiwa wadogo na hivyo wanaweza kujengewa msingi utakaowasaidia kutoa mchango sahihi dhidi ya kukomesha vitendo vya rushwa nchini.

Sheria kali

Hilary Boniface ni mwalimu mlezi wa klabu za wapinga rushwa kutoka Shule ya Kizota Sekondari aliyeiambia The Chanzo kwamba klabu zinatoa mchango wa kutengeneza taifa la baadaye kama wananchi wenyewe wanavyotaka kuliona.

“Tunagengeneza kizazi ambacho kitakuja kupambana na rushwa,” Boniface alisema. “Ninaona jamii inavyoenda kubadilika kwa kiasi kikubwa. Nguvu kubwa iongozeke. Tunatakiwa tusilegeze nguvu.”

SOMA ZAIDI: Je, Ubadhirifu Serikalini Unaweza Kudhibitiwa? Wataalamu Wanaamini Hivyo

Hoja hii inaungwa mkono na Mwalimu Baraka Emanuel wa Shule ya Sekondari Mnadani ambaye anaamini kwamba kizazi cha sasa kimebarikiwa, akibainisha kwamba zamani haikuwa rahisi kwa watoto kufahamu elimu ya rushwa mapema kama ilivyo sasa.  

Wakati akiamini kwamba juhudi za kuwalenga watoto katika mazingira ya shule zinaweza kuchangia katika kujenga jamii ya wachukia rushwa, Emanuel anaaminini pia sheria za nchi zilizopo za kukabiliana na wala rushwa ziongezewe makali zaidi.

“Sheria zetu zinapaswa ziwe kali zaidi,” alisema. “Tunazo sheria lakini wakati mwingine hazitekelezwi vile inavyotakiwa. Kwa mfano, wale ambao wanakuwa wanalisimamia zoezi hili kuna wakati mwingine hao hao wanakuwa chanzo cha kupokea na kutoa rushwa.”

Maadili kwa watoto

Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Dodoma Asha Kwariko aliiambia The Chanzo hapo Mei 11, 2023, kwamba ni muhimu sana kwa taasisi hiyo kuanza kuwajengea uelewa watoto kuhusu vitendo vya rushwa wakiwa wadogo, akisema hiyo ni hatua muhimu ya mapambano dhidi ya rushwa nchini. 

“Tuna imani kwamba ukimjenga mtoto kimaadili tayari atakuwa anafahamu apambane vipi na rushwa,” alisema Kwariko kwenye mahojiano hayo. 

“Vilevile, tukasema tutakuwa tumeisaidia jamii kwa sababu mwanafunzi anatoka kwenye jamii, wanao wazazi na jamii inayowazunguka,” aliongeza afisa huyo. “Kwa maana hiyo, tutakuwa tumepeleka ujumbe kwa hao wanaowazunguka wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla.”

Kwariko alisema klabu ambazo wamezianzisha zitakuwa endelevu, huku mipango ikisukwa kuanzisha klabu za wapinga rushwa kwa shule za msingi ili na wao waweze kufahamu madhara ya rushwa.

​​”Kila mtu kwa nafasi yake huko alipo ashiriki kwenye haya mapambano dhidi ya rushwa,” alisema Kwariko. 

“Lakini pale ambapo yanafanyika makosa ya rushwa, ukitusaidia ukaleta taarifa, maana yake itakuwa umesaidia,” aliongeza Kwariko. “Kwa maana hiyo, tunahitaji tuelimishe wananchi wote kwa ujumla. Tuanzie kwenye ngazi ya familia. Ndiyo maana tumeanza na watoto.”

Samaki mkunje …

Naye Mkuu wa Wilaya Dodoma Jabir Shekimweri, akiongea na The Chanzo hapo Mei 10, 2023, alizipongeza jitihada hizo za TAKUKURU kupeleka mapambano dhidi ya rushwa shuleni, akisema Waswahili hawakukosea waliposema samaki mkunje angali mbichi.

“Tunayo nafasi ya kuwaepusha tangu wakiwa mazingiara ya shule,” Shekimweri alisema. “Hata kwenye mazingira yao ya shule matendo hayo ya rushwa yapo. Mtu anataka kufaulu [unakuta anatoa] rushwa ya fedha au rushwa ngono.”

Shekimweri anaamini kwamba ili vita dhidi ya rushwa iweze kufanikiwa ni lazima vita hiyo iwe ni ya kila mtu, akibainisha kwamba kila mtu akikataa rushwa na kuikemea, Tanzania inaweza kupiga hatua za kimaendeleo.

“Jingine ni kwamba rushwa inapotokea mtu asikae kimya, atoe taarifa,” alishauri Shekimweri. “Mtu yuko tayari alalamike kwenye mikuktano ya hadhara lakini kutoa taarifa, au ushahidi, hataki kwa kuogopa kuonekana mbaya. Inabidi hilo libadilike.”

Jackine Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *