The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Rushwa ya Ngono Kwenye Vyombo vya Habari Yawakera Wanahabari

Waandishi wa habari wanasema rushwa ya ngono si tu inawaathiri wahanga kisaikolojia bali pia inaua taaluma yenyewe ya uandishi wa habari nchini Tanzania.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Waandishi wa habari wanawake kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wameonesha kusikitishwa kwao na kitendo cha vyombo vya habari kutokuyapa kipaumbele mapambano dhidi ya rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari ambayo wanasema hupelekea wao kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Waandishi hao walibainisha hayo hivi karibuni wakati wa mafunzo  juu ya ukatili wa jinsia yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) yaliyofanyika mkoani Morogoro, kati ya  Novemba 18 na Novemba 19, chini ya udhamini wa UNESCO.

Rushwa ya ngono katika vyombo vya habari ni tatizo kubwa nchini Tanzania huku utafiti wa hivi karibuni uliofanywa jijini Dar es Salaam na TAMWA ukibaini kwamba kati ya waliohojiwa kwa ajili ya utafiti huo, asilimia 48 walisema wamewahi kukumbwa na kadhia ya rushwa ya ngono.

Juhudi za kukomesha tabia hii zimekuwa zikiathiriwa na mambo mengi, ikiwemo kukosekana kwa utayari kwa baadhi ya waathirika na waandishi wengine wa habari wanawake kwa ujumla wa kuzungumzia uzoefu wao kuhusiana na kadhia hiyo. Utafiti wa TAMWA, kwa mfano, ulibaini kwamba asilimia 52 ya waliohojiwa hawakutaka kabisa kuzungumza chochote juu ya suala hilo.

“[Waandishi wa habari] tunazungumza kuhusu [shida za] mtu fulani kuliko kujizungumzia sisi wenyewe na shida zetu,” anasema Moza Saleh Ally kutoka Hit Radio iliyoko Zanzibar. Moza ana uzoefu wa miaka 15 wa kufanya kazi kwenye vyombo vya habari. “[Rushwa ya ngono] inadhoofisha kiutendaji na hata kuvunja moyo. Lazima ipigwe vita.”

Mazingira ya rushwa

Akizungumzia mazingira ambayo rushwa ya ngono hujitokeza kwenye vyombo vya habari, mwandishi wa habari anayefanyakazi na kituo cha redio chaa Sauti ya Injili kutoka Moshi, Kilimanjaro Hellen Madege anasema kwamba kitendo hicho ambacho ni jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania hujitokeza zaidi pale kunapotokea fursa ya mafunzo au fursa yoyote inayoweza kumpatia mwandishi husika kipato au hata kupata habari yako itoke redioni.

“Rushwa ya ngono inadumaza taaluma,” anasema Hellen mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 20 wa kufanya kazi kama mwandishi wa habari na ambaye ameshawahi kukumbana na kesi ya kuombwa rushwa ya ngono na kukataa. “Lakini [rushwa ya ngono] haitokei ndani tu [ya vyombo vya habari]. Inatokea pia nje unapoenda kutafuta habari mbalimbali ambapo [vyanzo vya habari] ndo wanakuwa wahusika wa kuchochea jinai hiyo.”

Njia moja inayoweza kutumika kukomesha hali hii ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanawake kuwa na uwezo wa kusema hapana na kutoa taarifa kuhusiana na matukio haya tangu kipindi wakiwa vyuoni wakijipatia mafunzo ya uandishi wa habari.

Tupokigwe Ambwene, mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka sita ya kufanya kazi na kituo cha runinga cha Star TV anashauri kwamba ikiwa hilo litafanyika, wanawake watakuwa na uwezo mkubwa wa kujitambua na kuchukua hatua stahiki pale wanapokabiliwa na tatizo hilo.

“[Waandishi wa habari wanawake] wajengewe uwezo wa kujua kwamba wafanye nini wakikutana na changamoto kama hii,” anasema Tupokigwe pembezoni mwa mafunzo hayo. “Tunapaswa kusema mara kwa mara hii itamfanya yule bosi hata kama ana nia hiyo ataacha.”

Uwajibishwaji

Ahmed Macha ni Maneja wa kituo cha redio SACHITA kilichopo mkoani Mara ambaye anakiri kupokea malalamiko ya rushwa ya ngono kutoka kwa wafanyakazi wake wanawake. Kwa mujibu wa Ahmed, hatua ambazo amekuwa akizichukua baada ya kupokea taarifa hizo ni kumuhamisha mlalamikiwa kwenda eneo jengine la kazi.

“Labda ni mhariri [au] mzalishaji wa kipindi. Lazima nimhamishe eneo hilo alilokuwa la sivyo lazima niwaite wote wawili hususan nimuite kijana kwa maana ya kwamba ya kumkanya na kumueleza nini anapaswa kufanya bila ya kutaja jina muhusika aliyeniambia,” Ahmed ameieleza The Chanzo.

Mtafiti wa masuala ya habari na mdau wa harakati za kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono kwenye vyombo vya habari Dk Joyce Bazira, ambaye alikuwa muwezeshaji katika mafunzo hayo, anasema kwenye harakati zake hizo amebaini kwamba kwenye vyumba vya habari unyanyasaji wa kingono ambao umekuwa ukiendelea ni mkubwa sana.

“Kila chombo cha habari ni muhimu kikawa na sera ya kupinga unyanyasaji wa jinsia,” Dk Bazira alisema, akipendekeza namna ya kutatua kero hiyo. “[Sera] hizo zikiwepo ziorodheshe mambo yote ambayo mtu akiwa anadhalilishwa, afanye hiyo ikitendeka ni hatua ya kwanza. Ya pili, ni kuhakikisha sera hizo wafanyakazi wote wameziona kwa sababu kuna wengine wanazo na wafanyakazi hawafahamu. Watu wazisome, wajue zinasema nini.”

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Dodoma. Unaweza kumfikia kupitia jackline@thechanzo.com. Kama una maoni yoyote kuhusiana na habari hii pia unaweza kuwasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com

 

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *