The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Serikali za Mitaa, Halmashauri Zaongoza Kulalamikiwa kwa Rushwa Dodoma 2022

TAKUKURU yasema kwa kiasi kikubwa malalamiko hayo huhusiana na matumizi mabaya ya madaraka.

subscribe to our newsletter!

Dodoma. Maafisa kutoka  Serikali za Mitaa na Halmashauri wameongoza kulalamikiwa kwa vitendo vya rushwa mkoani hapa kwa mwaka 2022, huku Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dodoma Sosthenes Kibwengo akihusisha hali hiyo na matumizi mabaya ya mamlaka.

Kibwengo alitoa tathmini hiyo hivi karibuni wakati wa mahojiano maalum na The Chanzo yaliyofanyika katika ofisi zake zilizopo mkoani hapa.

Lengo la mahojiano hayo lilikuwa ni kupata mtazamo wa afisa huyo mwandamizi wa TAKUKURU kuhusiana na juhudi zao za kupambana na rushwa kwa mwaka 2022 na mipango yao kwa mwaka 2023.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano hayo:

The Chanzo: Tangu Januari 2022, mpaka Novemba mwaka huu, TAKUKURU ilipokea taarifa ngapi za vitendo vya rushwa hapa kwenye makao makuu ya nchi?

Sosthenes Kibwengo: Kwa kipindi hicho, TAKUKURU mkoa wa Dodoma tulipokea jumla ya taarifa 436 ambazo tumezipata katika ofisi zetu zote zilizopo mkoani na zilizopo wilayani kupitia njia mbalimbali.

Lakini katika taarifa hizo 436, taarifa za vitendo vya rushwa zilikuwa 250 na makosa ambayo siyo ya rushwa yalikuwa 186.

The Chanzo: Ni sekta zipi ambazo ziliongoza kulalamikiwa kutokana na vitendo vya rushwa?

Sosthenes Kibwengo: Sekta ambayo ililalamikiwa katika yale makosa 250 ya vitendo vya rushwa ni sekta ya TAMISEMI ambapo hapa walilalamikiwa mara 88.

Hapa inamaanisha ni viongozi wote wa Serikali za Mitaa kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, mitaa, kata na halmashauri.

Kwa hiyo, TAMISEMI ndiyo ambayo iliongoza, ikifuatiwa na sekta ya elimu ambayo ililamikiwa mara 32, afya mara 22, na polisi mara 18.

The Chanzo: Ni sababu zipi ambazo zilisababisha sekta hizo kulalamikiwa?

Sosthenes Kibwengo: Mara nyingi makosa haya, au malalamiko haya, yanahusiana na vitendo vya matumizi mabaya ya mamlaka.

Hawa wenzetu ambao wanalalamikiwa ni watu ambao wamepata mamlaka fulani ili waweze kuwatumikia wananchi kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu za nchi.

Kwa hiyo, mara kadhaa hawa watu wanakuja kulalamikiwa kwa sababu ya matumizi mabaya ya mamlaka, au kutaka hongo, ili hao watu wafanye au wasifanye jambo fulani. Hiyo ni katika sekta zaidi eneo la TAMISEMI.

Ukienda katika elimu na afya ni katika mambo mbalimbali kuhusiana na utoaji wa huduma au suala la miradi.

Kwa sababu, unakuta haya ni maeneo ambayo yana fedha nyingi sana za miradi. Kwa hiyo, ni maeneo ambayo yalionekana kulalamikiwa.

Na ukija katika eneo la polisi ni katika haki za wananchi. Labda katika uchunguzi, au mtu anataka suala lake lichunguzwe, au mtu anatuhumiwa kwa ajili ya jambo fulani, au lingine wanapaswa au wanatakiwa watoe rushwa ili waweze kupata haki.

Wakati mwingine hiyo haki wanastahili au wakati mwingine hiyo haki hawastahili.

Aidha, katika sekta ambazo zilionekana kulalamikiwa sana lakini siyo vitendo vya rushwa ni sekta ya ardhi.

Katika malalamiko 186, kulikuwa na malalamiko 54 ambayo ni ya ardhi ambayo hayahusiani na vitendo vya rushwa.

Ukiangalia katika malalamiko 250 ambayo ni ya rushwa, ardhi imetokea mara saba tu. Lakini katika eneo ambalo siyo la rushwa limetokea mara 54.

Na hii inaonesha kwamba hakuna mahusiano mazuri, au mawasiliano mazuri, kati ya watu waliopo katika sekta ya ardhi na wananchi.

Au wananchi wakienda katika mamlaka zinazohusiana na masuala ya ardhi hawapati majibu kulingana na ambavyo walipaswa kupewa majibu.

Katika eneo hilo, kwa kweli, pamoja na kwamba ilikuwa haihusiani na rushwa, lakini tulijitahidi kufanya uchambuzi wa mfumo katika utoaji wa huduma za ardhi.

Na tukakaa na mamlaka zinazohusiana na sekta hii ya ardhi, tukakubaliana kwamba waboreshe mambo kadhaa katika eneo lao, hususan eneo la kutoa mrejesho kwa wananchi.

Eneo la kuwasikiliza wananchi kwa wakati, eneo la kuhakikisha kwamba malalamiko ya wananchi kuwe na siku maalumu ya kuwasikiliza wananchi.

Malalamikio yafikie mwisho ili wananchi waweze kufahamu.

The Chanzo: Ni watu wangapi waliokamatwa kutokana na makosa ya rushwa ambao wamefikishwa mahakamani mwaka huu?

Sosthenes Kibwengo: Kutoka mwezi Januari mpaka mwishoni mwa mwezi wa Novemba tumefungua kesi mpya zinazohusiana na rushwa katika Mahakama zetu mbalimbali hapa mkoani Dodoma 25.

Na maana yake ni kwamba, watu ambao tumewafikisha mahakamani katika kipindi hicho ni watu wengi.

Kwa sababu kesi nyingine unakuta imefunguliwa ina watu watatu, ina watu wanne, ina watu wawili na chache zina mtu mmoja mmoja.

Katika kipindi tajwa, tumefungua mashauri mapya 25, na hiyo ni katika Mahakama mbalimbali za mkoa wa Dodoma.

Kwa hayo mashauri 25 ya kijinai yanayohusiana na rushwa ambayo yamefunguliwa mahakamani ni kwa wale ambao juhudi za kuhakikisha kwamba tunazuia rushwa wao walizipuuza na wakaendelea kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Na sasa tunasubiri Mahakama ambayo kikatiba ina mamlaka ya kutenda haki ifanye maamuzi yake.

The Chanzo: Tukiwa tunaelekea kuingia 2023, ni mikakati gani TAKUKURU inayo katika kukabiliana na vitendo vya rushwa hapa kwenye makao makuu ya nchi?

Sosthenes Kibwengo: Tumeanzisha mikakati ya elimu ya kuhamasisha watu wa Dodoma watambue kwamba hawapaswi kuwa watazamaji bali washiriki kwa vitendo katika kuzuia rushwa.

Katika eneo hilo, pamoja na kwamba tunawaelimisha watu kupitia njia mbalimbali, ikiwemo katika mikusanyiko mbalimbali ya wananchi, tumeweka nguvu katika eneo la kuelimisha vijana.

Kwa sababu, vijana ndiyo chachu ya mabadiliko katika jamii. Vijana ndiyo taifa la leo, ndiyo taifa la kesho.

Vijana tunataka wakue katika hali ambayo wanakua na uadilifu, wanakuwa wazalendo, wanakuwa wanafahamu nini maana ya uwajibikaji.

Wanafahamu na wanatumbua na wanathamini utu wa mwenzake. Kwa sababu, unapothamini utu wa mwenzako huwezi kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Hawa vijana tunataka wao sasa waweze kuibadilisha jamii, na tunatumia mbinu mbalimbali ili kuweza kuwafikia vijana.

Tunatumia klabu za wapinga rushwa ambazo zinashiriki katika mashindano mbalimbali ili waweze kutambua wajibu wao wa kushiriki katika kuzuia rushwa.

Penye rushwa panapelekea watu wachache tu waweze kufaidika na hivyo kusababisha matabaka.

Na hii inaweza ikasababisha mwisho wa siku nchi isiweze kuwa na amani wala kutawalika. Maana yake ni kwamba Serikali iliyopo madarakani inakosa uhalali.

Tunatarajia kwamba mwana-Dodoma mzalendo anayependa nchi yake anatambua na kuthamini utawala bora, huyu mwana-Dodoma hawezi kukubali kushiriki katika vitendo vya rushwa.

Jackline Kuwanda ni mwandishi wa habari wa The Chanzo anayepatikana mkoani Dodoma. Unaweza kumpata kupitia jackline@thechanzo.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *