The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Barua ya Wazi kwa Wanasiasa Vijana wa CCM Kuhusu Rais Magufuli

Si kweli kwamba wanasiasa vijana wa CCM wanaomsema Magufuli vibaya sasa walikaa kimya wakati yuko hai au walikuwa wanamsifia?

subscribe to our newsletter!

Hayati John Magufuli, Rais wa awamu ya tano aliyefariki Machi 17, 2021, anaendelea kugusa hisia za Watanzania walio wengi kwa namna tofauti. Inaonekana mambo aliyoyafanya Magufuli katika uongozi wake wa miaka mitano – mema au mabaya – yatafanya ichukue muda mrefu sana kwa Watanzania kumsahau.

Sherehe za hivi karibuni za kumpokea rasmi Bernard Membe ndani ya CCM zimeibua tena hisia tofauti walizonazo Watanzania juu ya Magufuli, hususan baada ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye kutamka maneno yaliyozua mjadala mkali.

Akiwa jukwaani, Nape alimsihi Membe asahau machungu ya kufukuzwa kwake CCM kwa kuwa, kwa maneno ya Nape: “Mungu ameamua ugomvi.” Ni sahihi kusema kuwa kauli ya Nape imewagawa Watanzania katika makundi tofauti tofauti kutokana na jinsi wanavyochukulia urithi, au kumbukumbu, aliyoiacha hayati Magufuli.

Ni ngumu kujua kama Nape alitegemea kauli yake ingepokelewa kama ilivyopokelewa. Nadhani alitegemea, kwa sababu yeye ni mwanasiasa mzoefu aliyepitia mambo mengi kama alivyoeleza siku ile ya sherehe za kumkaribisha Membe CCM, na kwa hiyo anajua kuwa kila anachokiongea kinapimwa kwenye mizani na kujadiliwa kwa kina.

Hata hivyo, Mbunge huyo wa Mtama (CCM) siyo mwanasiasa wa kwanza ndani ya CCM kutoa maneno ambayo yanaoneka kumnanga Magufuli. Na wala haionekani kama atakuwa wa mwisho.

Kutoa ya moyoni

Wanasiasa wengi kutoka katika lile kundi lililoguswa kwa namna hasi katika utawala wa Magufuli, na hasa wanasiasa vijana, wamekuwa wakitoa ya moyoni pale wanapopata nafasi, jambo ambalo limekuwa likizua mijadala mikali sana.

Kuna uwezekano wanasiasa hawa wanashangaa na kujiuliza mijadala hii ni ya nini.

Kitu ambacho labda hawakielewi ni kuwa matamshi yao, hasa yale yanayooneka kama vile ni ya kumnanga Magufuli, yanaweza kuwapunguzia kukubalika kwao kwa wananchi, kama wasipokuwa waangalifu.

Katika barua hii ya wazi nataka niwaeleze, na kuwashauri wanasiasa vijana wa CCM, ambao wana mipango ya kufika mbali kisiasa.

Nadhani ni muhimu mtambue kuwa Magufuli bado yuko hai sana katika mioyo ya Watanzania wa kawaida walio wengi ambao ndiyo wapiga kura wenu. Wengi wa wananchi hawa hawajui kiundani kuhusu mapungufu makubwa aliyokuwa nayo Rais Magufuli.

Wananchi hawa hawajui mambo ambayo baadhi yenu mlifanyiwa wakati wa utawala wa Rais Magufuli. Kama wanajua basi hawajali. Ni vizuri mfahamu kuwa kwa wananchi hawa Magufuli alitenda mema zaidi ya mabaya.

Kwao, Magufuli alikuwa mtetezi wa wanyonge aliyepiga vita rushwa na kuwakomesha vigogo wa Serikali waliofuja mali za umma. Wasije wakadhani na nyinyi mnamsema vibaya Magufuli kwa sababu aliwazibia mianya ya rushwa!

Wananchi hawa wanadhani kuwa Magufuli alikuwa ndiyo kiongozi ambaye Tanzania ilikuwa inahitaji kwa wakati ule ili kuikwamua kiuchumi. Kwa kifupi, ni kuwa wananchi hawa bado wanamkubali Magufuli kwa kiasi kikubwa sana na wanamtetea huko vijiweni.

Kwao, Magufuli kaacha pengo ambalo kwao halitazibika hivi karibuni. Wengi wao katika kundi hili huwa wanajisikia vibaya wanaposikia Magufuli anasemwasemwa. Ni vizuri kuelewa kuwa kundi la wananchi hawa linajumuisha watu kutoka makabila na dini mbalimbali, walioko vijijini na mijini.

Kwa uwingi wao, na umuhimu wao, watu wa kundi hili siyo wa kupuuza. Ni vizuri mnapotoa matamko yenu kuhusu Magufuli mlifikirie kundi hili.

Je, Magufuli asisemwe?

Siasa ni sayansi na ni mahesabu. Namba unazojumlisha au kutoa katika hesabu zako za kisiasa leo ndizo zitakazokupa kura kesho. Kama binadam mwingine yeyote, Magufuli alikuwa na sura mbili, ya wema na ubaya.

Ni wazi kuwa mambo mengi mabaya yaliyofanyika katika kipindi cha utawala wake hayakupaswa kufanyika, bila kujali nia yake ilikuwa ni nini.

Lakini je, wananchi walio wengi wanayajua mabaya hayo? Wanajali? Je, siyo kwamba wananchi hawa wanaona kuwa kutangulia mbele za haki kwa Magufuli kumempa  nafasi ya kwenda kujibu mbele ya Mwenyezi Mungu? Na hivyo aachwe apumzike?

Na pia je, nyinyi wanasiasa vijana mliomo ndani ya CCM mnajua kuwa kuna nadharia ya kwamba wote mnaomsema vibaya Magufuli sasa ni wanafiki na waoga kwa kuwa wakati yupo hai mlikaa kimya au mlikuwa mnamsifia?

Swala siyo Magufuli kusemwa au kutokusemwa. Suala ni kuwa kwa nyinyi wanasiasa wenye malengo makubwa ya baadaye kumsema Magufuli kwa namna fulanifulani  kunaweza kuathiri malengo yanu ya kisiasa hapo baadae.

Pili, jifunzeni kutokana na maisha ya Magufuli. Kwenu wanasiasa, na hata kwa sisi watu wa kawaida, maisha mafupi ya kisiasa ya Magufuli yana mafundisho lukuki. Ni wajibu wetu kujifunza.

Wanasiasa mnaochipukia mnapaswa kujifunza jinsi Magufuli alivyopanda ndani ya miaka 20 kutoka Naibu Waziri hadi Rais wa nchi. Somo kubwa hapa ni namna ya kuwa mtu wa vitendo.

Magufuli amewafundisha wanasiasa umuhimu wa kuacha mizaha katika kuwatumikia wananchi. Katika hili, wanasiasa pia wajifunze mapungufu yake na kuyaepuka ili kuwa watu wa vitendo wenye manufaa.

Tatizo bado lipo

Mapungufu karibuni yote katika utawala wa Magufuli, ambayo wanasiasa ndani ya CCM mnayajua vizuri zaidi, yalitokana na Katiba yenye matatizo, Katiba yetu ya mwaka 1977. Katiba hii imefanya Rais wa Tanzania awe na mamlaka makubwa yaliyopitiliza, awe Rais wa Kifalme.

Mamlaka haya ni kishawishi kikubwa kwa Rais kufanya anavyotaka hadi kupitiliza mipaka ya kiutu bila uwoga wa kuwajibishwa wakati akiwa Rais au baada ya kustaafu. Swali ni kuwa je, wanasiasa vijana wa CCM mnayajua haya?

Mnafanya lolote kushawishi chama chenu kibadilishe mfumo huu wa Urais wa kifalme (imperial presidency)? Au mnaona kuondoka kwa Magufuli kumetatua tatizo?

Je, kumnanga Rais Magufuli kwa mambo aliyofanya ambayo yaliwezeshwa na maudhui (spirit) ya Katiba iliyopo bila nia thabiti ya kutaka kubadilisha Katiba hiyo siyo unafiki?

Tatizo bado lipo. Kama mnadhani kuondoka kwa Magufuli kumeondoa tatizo mnajidanganya. Tanzania imefikia kipindi ambacho ni vigumu kuvuka salama bila kuwa na Katiba mpya itakayoondoa mamlaka na madaraka makubwa kwa mtu mmoja.

Majukumu makubwa sana ya kuongoza taifa hayawezi kuachwa kwenye mabega ya mtu mmoja. Akilidondosha taifa halafu tukamlaumu tutakuwa tunamuonea.

Damas Kanyabwoya ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi. Anuwani yake ya barua pepe ni dkanyabwoya@gmail.com. Anapatikana pia Twitter kama @DKanyabwoya. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo Initiative. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

One Response

  1. Unafiki Unafiki Unafiki. Wote hawa wanaojifanya wanamkosoa leo walikuwa wanamlamba na kumuimbia nyimbo na kwaya za kumsifu. Hii ni hatari sana kwa nchi yetu
    Mfano mmoja ni Uviko 19. Kila mmoja alikubaliana naye kuwa hakuna Uviko, hata chama cha madaktari !!!
    Kama sikosei ni chama cha mawakili tu kilijitokeza na kushauri kuwa ni vizuri tufuate ushauri wa wataalamu. Pia kuna askofu ambaye alitofautiana naye
    Waliobaki walikuwa wakimshangilia tu – si mashekhe wala si mapadiri, si mawaziri, si ma DC si ma RC wala si wachungaji WOTE NI WANAFIKI pamoja na Nape. Sina imani nao.
    Katika kesi ya Nuremberg wale wasaidizi na washauri waliokuwa wakitekeleza amri ya Hitler walikutwa na hatia wakafungwa. Hakuna kujidai eti mimi nilikuwa sikubaliani naye, au ilikuwa uamuzi wake si wangu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *