The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Miswada ya Uchaguzi Iliyopitishwa na Bunge Inakinzana na Nia ya Rais Samia ya Kuleta Mageuzi ya Kisiasa Tanzania

Wadau mbalimbali waliotoa mapendekezo yao kuboresha miswada hiyo wamehisi kudharauliwa, wakimtaka Rais Samia asikubali kutia doa mchakato wa mageuzi aliouasisi kwa kusaini miswada hiyo kuwa sheria.

subscribe to our newsletter!

Miswada mitatu inayohusu uchaguzi iliyopitishwa na Bunge hapo Februari 2, 2024, na ambayo inasubiria saini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuifanya iwe sheria, haitaweza kuzaa sheria zitakazotibu matatizo ya uchaguzi yanayoikabili Tanzania, ikiwemo kuziwezesha chaguzi kutoa viongozi bora wa ngazi zote, wanaoweza kubuni na kutekeleza mambo ya maendeleo yatakayoinua ubora wa maisha ya wananchi wote.

Miswada hiyo, ambayo ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, 2023, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, 2023 na Muswada wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, 2023, ilipitishwa licha ya kutozingatia mapendekezo mengi ambayo wadau waliyatoa tangu kusomwa kwao kwa mara ya kwanza bungeni.

Ni muhimu kwa Watanzania kufahamu kwamba duniani kote, nchi zilizopata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii, ziliweka mkazo kwenye suala la uongozi bora unaozingatia jinsia kama rasilimali kuu ya kuchochea maendeleo. Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema ili nchi iendelee inahitaji vitu vinne: uongozi bora, siasa safi, watu na ardhi.

Kwa kulitambua hili, mnamo Septemba 23, 2021, miezi saba tu baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliuambia mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu dhamira yake kama Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania ya kuweka misingi imara itakayohakikisha usawa wa kijinsia katika nyanja zote za maisha, ikiwemo siasa na uongozi.

“[Tu]naboresha mfumo wa sera na sheria ili kuja na mpango unaotekelezeka na kupimika kuhakikisha uchumi wa wanawake unaimarika na kunakuwa na uwiano sawia kati ya wanaume na wanawake katika nyanja zote nyingine,” Rais Samia, aliyeingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli, alihutubia huku akishangiliwa sana.

SOMA ZAIDI: UN Women Yataka Ushiriki Zaidi wa Wanawake Kwenye Siasa, Uchumi

Hata hivyo, dhamira hii haionekani kwenye miswada hiyo mitatu iliyopitishwa na Bunge, ambayo, pamoja na mambo mengine, haitoi dira ya mabadiliko ya msingi aliyoahidi Rais Samia kwani inashindwa kuyapatia ufumbuzi matatizo makuu mawili yanayofanya uchaguzi Tanzania, kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Rais, usitoe viongozi bora: Tume ya Uchaguzi kutokuwa huru na kutokuwepo kwa misingi ya usawa wa jinsia katika mifumo ya uchaguzi.

Kimsingi, miswada hiyo mitatu ilikuwa ni fursa adimu kwa nchi kukarabati tanuru la kuzalisha uongozi bora ambao ni rasilimali nambari moja ya kuharakisha maendeleo ya nchi kwa kutatua matatizo mawili ya kupata Tume Huru ya Uchaguzi na kuweka misingi ya usawa wa jinsia katika uchaguzi ili wanawake na wanaume wawe na fursa sawa ya kupigiwa kura.

Lakini kwa kujuwa au kutokujuwa, Wabunge walipitisha miswada hiyo bila kuingiza mapendekezo ambayo wadau, zikiwemo taasisi za dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia walitoa kwa lengo la kuiboresha miswada hiyo ili iweze kutoa sheria zitakazoweza kutibu matatizo hayo ya uchaguzi.

Asasi za Kiraia, hususan Mtandao wa Wanawake na Katiba, Uchaguzi na Uongozi, walipendekeza Muswada wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani uboreshwe kwa kuhusisha pia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uweke msingi wa kuwezesha mwanamke kugombea kwa kupigiwa kura katika ngazi zote za uongozi wa nchi kuanzia Mwenyekiti wa Kitongozi hadi Rais wa nchi. Pendekezo hili, hata hivyo, halikuingizwa kwenye muswada huo.

Wilaya kama majimbo

Mtandao huo pia, ambao unajumuisha takriban asasi za kiraia 200, ulipendekeza utaratibu wa Viti Maalum ufutwe na badala yake wilaya zigeuzwe kuwa majimbo ambapo kila jimbo litakuwa na Wabunge wawili, mwanamke na mwanaume, hatua ambayo ingepunguza idadi ya sasa ya Wabunge kutoka 393 waliopo sasa hadi 299, na hivyo kuokoa fedha nyingi za walipa kodi.

SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Mikakati Imara Kuongeza Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Pendekezo hili ni la msingi kwani, kama alivyosema Gemma Akilimali, mwanaharakati aliyekuwa mstari wa mbele kwenye harakati za kuitaka Serikali itumie mfumo wa bajeti ya kijinsia kuepusha kodi za wananchi kutumiwa kwa mambo yasiyo ya lazima, “Serikali haipaswi kutumia vibaya kodi za wananchi.”

Kama Wabunge wangezingatia pendekezo hilo, kwa vile kuna wilaya 128 Tanzania Bara na kumi zilizoko Zanzibar, majimbo yangekuwa 138 ambapo kila moja likiwakilishwa na Wabunge wawili, mwanamke na mwanaume, Bunge linakuwa na Wabunge 276 wa majimbo.

Tukitaka pia Bunge liwe shirikishi, ambapo watu wenye ulemavu wanaweza kutengewa mathalan viti 12 Bungeni, sita vya wanawake na sita vya wanaume, na pia mfumo wa Rais kuteua Wabunge kumi kwa kuzingatia usawa wa jinsia uendelee kama ulivyo sasa, na pia kiti kimoja cha Mwanasheria Mkuu, ina maana Bunge litakuwa na Wabunge 299, ikiwa ni Wabunge 94 pungufu ikilinganishwa na Bunge la sasa lenye Wabunge 393.

Kwa kupunguza Wabunge 94, ikizingatiwa kwamba kwa sasa kila Mbunge analipwa mshahara Shilingi milioni 16 kwa mwezi, Serikali ingeweza kuokoa zaidi ya Shilingi bilioni 18 kwa mwaka kutokana na mishahara ya Wabunge hao 94, na kwa miaka mitano, zingeokolewa Shilingi bilioni 90. 

Ukiweka na posho za vikao na mafao, Serikali ingeokoa zaidi ya Shilingi bilioni 200 kwa miaka mitano ambazo zitatosha kabisa kulipia gharama ya bima ya afya kwa watoto wote ambayo, kwa mujibu wa Serikali, haizidi Shilingi bilioni 35 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano. 

Hatua hiyo ingeokoa mamilioni ya watoto kutoka familia maskini kufa kutokana na magonjwa mengi ambayo yanaweza kuzuilika kwa kupata tiba sahihi na kwa wakati.

SOMA ZAIDI: Nini Kitatokea Pale Wanawake Wengi Wakiwemo Kwenye Nafasi za Maamuzi?

Vilevile, wanawake kuchaguliwa kwa kura majimboni kutaleta ukombozi wa wanawake kimapinduzi kwa sababu, kama anavyosema Mary Ndaro, Makamu Mwenyekiti wa Mtandao, “Wabunge wa Viti Maalum huwa wanachukuliwa kama Wabunge wa daraja la pili, hawaruhusiwi kuwa wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, wenyeviti wa Halmashauri au kushika nafasi ya Waziri Mkuu.”

Profesa Ruth Meena, mwanaharakati na mwanamtandao ambaye kwa miaka mingi amepigania haki za wanawake kushiriki katika siasa na vyombo vya maamuzi na uongozi wa nchi, amevieleza vitendo hivi vinavyofanywa dhidi ya Wabunge wa Viti Maalum kama “ubaguzi wa jinsia na ni kinyume na Katiba ya nchi yetu.”

Profesa Meena anasema kwamba Sehemu ya Tatu, kifungu 12(1) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 kinasema, “Binadamu wote huzaliwa huru, na wote ni sawa,” na Kifungu 13 (1-5) kinafafanua zaidi kwa kukataza aina zote za ubaguzi, ikiwa ni pamoja na ubaguzi wa jinsia.

Viti Maalum

Kiukweli, miswada hiyo ilipaswa ifute utaratibu wa Viti Maalum kwa sababu nchi yetu kuendelea kutumia mfumo uliobuniwa miaka ya 1970 kama hatua ya awali kuwezesha wanawake kushiriki katika vyombo vya maamuzi, kumewafanya wanaume viongozi wa vyama vya siasa, na wanaume kwa ujumla katika jamii, kudhani kwamba kwa vile kuna Viti Maalum, wanawake hawana haki wala sababu ya kugombea na kuchaguliwa kuwa Wabunge wa majimbo.

Kwa sababu hiyo, vyama vya siasa huwa vinateua wanawake wachache tu kugombea majimboni na wanapogombea wanakumbana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wakati wa kampeni vyenye lengo la kuwachafua ili wananchi wasiwapigie kura.

SOMA ZAIDI: TGNP Yataka Wanahabari Kuchochea Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Wakati miswada hiyo ikijadiliwa Bungeni kabla ya kupitishwa, wanawake Wabunge kadhaa wa majimbo walipaza sauti, wakitoa ushuhuda wao kuhusu vitendo vya ukatili na udhalilishaji walivyowahi kufanyiwa wakati wa kampeni.

Mmoja kati ya Wabunge hawa, Mbunge wa Same Mashariki (Chama cha Mapinduzi – CCM) Anne Kilango, alisema: “Mimi ni [mwathirika] wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa jinsia. Nimeanza kugombea jimboni tangu 2005. Ninakutana na haya mambo, lakini wengi wanachukulia ni mambo madogo, la hasha, yanaumiza. Makosa ya ukatili yachukuliwe kama makosa ya uchaguzi, kama makosa ya rushwa.”

Jambo jema ni kwamba, vitendo vya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wakati wa kampeni, limeingizwa kwenye Muswada wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani kama kosa la uchaguzi. Hii itasaidia kwa kiasi fulani kuwakinga wanawake dhidi ya vitendo hivi na hivyo kuongeza uwezekano wa wanawake wengi zaidi kuchaguliwa kama Wabunge majimboni, hali ambayo kwa sasa hairidhishi.

Kwa mfano, katika uchaguzi wa 2020, ni wanawake 26 tu ndiyo walichaguliwa kuwa Wabunge wa majimbo, wakati wanaume wakiwa ni 264 na wanawake Wabunge wa Viti Maalum ni 113, hivyo kufanya idadi ya wanawake Bungeni kuwa 142, sawa na asilimia 36, kwa kipindi cha 2020 hadi 2025.

Tume Huru

Kuhusu Tume ya Uchaguzi, Wabunge walipitisha miswada hiyo bila kudai kwanza Serikali ipeleke Bungeni muswada wa marekebisho madogo ya Katiba kama wadau, hasa vyama vya siasa, walivyopendekeza, uamuzi ambao Bob Chacha Wangwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania, ameuelezea kama wa kusikitisha.

SOMA ZAIDI: Tumechelewa Kupata Katiba Mpya Kabla ya Uchaguzi, Basi Tuboreshe Hii Iliyopo

“Muswada wa Tume ya Uchaguzi uliopitishwa na Bunge hauwezi kutupa Tume Huru, kwa sababu, kwa mfano, kifungu cha 12 cha Ibara 74 ya Katiba kinazuia matokeo ya Rais kuhojiwa mahakamani,” alidokeza Wangwe. “Serikali ilipaswa kupeleka kwanza Bungeni Muswada wa marekebisho madogo ya Katiba kufuta kifungu hicho.”

Ili nchi ipate Tume Huru ya Uchaguzi, wadau walipendekeza wakurugenzi wa wilaya, miji na majiji wapigwe marufuku kusimamia uchaguzi kama Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu iliyokuwa imeamua mwaka 2023, badala yake, Tume ya Uchaguzi iwe na afisa wake kila wilaya ambaye ndiye atakuwa msimamizi wa uchaguzi. Mapendekezo hayo, hata hivyo, hayakuingizwa kwenye Muswada husika.

Badala yake, Muswada uliopitishwa ulisema siyo lazima Mkurugenzi kuwa msimamizi na kwamba anaweza kuteuliwa afisa mwingine kufanya kazi hiyo, kitu ambacho Wangwe, ambaye ni wakili kitaaluma, amekitaja kama “mtego,” akifafanua: “Maana, kwa kutumia maneno ‘si lazima’ ni kwamba siyo kosa Wakurugenzi kusimamia uchaguzi, ingawa siyo lazima wasimamie.”

Wapo baadhi ya watu wanaweza kudai kwamba uchaguzi ni tukio linalotokea mara moja katika muda wa miaka mitano, hivyo itakuwa ni kupoteza kodi za wananchi kuajiri maafisa uchaguzi wakati hawatakuwa na kazi yoyote baada ya uchaguzi kumalizika. Hoja hii, hata hivyo, imeonekana kutokuwa na mashiko kwani zipo kazi maafisa hao wanaweza kupangiwa baada ya uchaguzi.

“Kazi zinazohusiana na uchaguzi ni nyingi,” Marjan H. Marjan, Mtendaji Mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya, anafafanua, akizitaja kazi kama vile kuandikisha wapiga kura wapya kila mwaka, kupitia na kuboresha daftari la wapiga kura na kushughulikia kesi za uchaguzi kama baadhi ya kazi zinazoweza kufanywa baada ya uchaguzi.

SOMA ZAIDI: Wadau Wataka Mikakati Imara Kuongeza Ushiriki wa Wanawake Kwenye Uongozi

Wadau pia walikuwa wamependekeza kwamba wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wakishasailiwa na Kamati ya Usaili, majina yao yafikishwe kwanza Bungeni kujadiliwa na kupitishwa na Wabunge ndipo yapelekwe kwa Rais kwa ajili ya uteuzi. Miswada iliyopitishwa, hata hivyo, haikuzingatia pendekezo hilo. Badala yake, imesema Kamati ikishasaili itapeleka majina hayo kwa Rais kwa ajili ya uteuzi.

“Kwa utaratibu huu, kutakuwa hakuna mabadiliko kwenye Tume ya sasa kwa sababu wajumbe watakuwa wateule wa Rais na kwa hiyo hawataweza kuwa huru,” Wangwe ametanabahisha. “Watakuwa wanamtii Rais ambaye naye wakati wa uchaguzi atakuwa ni mgombea.”

Jambo jengine ambalo wadau walipendekeza ni kwamba Mswada wa Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ujumuishe pia ule wa Serikali za Mitaa ili kuhakikisha uchaguzi wa Serikali za Mitaa nao unasimamiwa na Tume, lakini Wabunge wamepitisha miswada hiyo bila kuingizwa pendekezo hilo.

“Mapungufu haya yote yanaonyesha kwamba Serikali haina nia ya dhati ya kutunga sheria za uchaguzi ambazo zitaleta mabadiliko chanya ili kwenye Tume ya Uchaguzi ili uchaguzi uweze kufanyika kwa uhuru na haki kwa lengo la kupata viongozi bora watakaowajibika kwa wananchi,” Wangwe amedokeza.

Dk Ananilea Nkya ni mwanahabari na mwanaharakati wa jinsia na haki za binadamu. Ana Shahada ya Uzamifu kuhusu namna vyombo vya habari Tanzania vinaripoti masuala ya maendeleo. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ananilea_nkya@yahoo.com na @AnanileaN kwenye mtandao wa X.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

2 Responses

  1. asante kwa andiko.lililoshiba na la kitaalam kwa kweli elimu hii inatakiwa iwafikie watanzania walio wengi.

  2. Uchambuzi mzuri. Ila Samia hana nia thabiti ya kuleta mageuzo youote ya maana. Hiyo miswaada ndo taswila ya kile anachokifikiria kuhusu mabadiliko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *