Waziri Mkuu Mstaafu Edward Ngoyai Lowassa (70) amefariki dunia leo Februari 10,2024. Akitoa taarifa cha kifo hicho, Makamu wa Rais, Philip Mpango amesema Lowassa amefariki leo majira ya saa nane mchana katika katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam.
Lowassa alikua akipatiwa matibabu juu ya matatizo ya mapafu,shinikizo la damu, na ugonjwa wa kujikunja utumbo. Mpango ameeleza kuwa Lowassa amekuwa akiuguliwa kwa muda mrefu ambapo alipatiwa matibabu Dar es Salaam na nchini Afrika Kusini.
Serikali pia imetangaza siku tano za maombolezo ambapo bendera itapepea nusu mlingoti.
Akitoa salaam zake za rambirambi katika mtandao wa X, Rais Samia Suluhu Hassan amemuelezea Lowassa kama kiongozi mahiri, aliyejituma na kujitoa kwa ajili ya nchi.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa,” ameandika Rais Samia.
“Mheshimiwa Lowassa ameitumikia nchi yetu katika nafasi mbalimbali kwa zaidi ya miaka 35, akianzia ushiriki wake katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge, Waziri katika wizara mbalimbali na Waziri Mkuu.”
One Response
Kiongozi alie ongoza kwa namna nyepesi na kufanya uongozi ueleweke kwa jamii na vijana kwa ujumla,bila kusahau ajenda yake yenye maneno yanayo jirudia mara tatu ELIMU,ELIMU,ELIMU
Nenda mzee wetu kazi ulifanya tena kwa mfano mzuri.Tutayaenzi mema yako.