Wakati wa uchaguzi mkuu uliopita wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wanafamilia ya mchezo huo walishikwa na butwaa wakati mamlaka zilipoanza kutekeleza kanuni na sheria za uchaguzi huo.
Wengi walijitosa kugombea bila ya kujua mabadiliko makubwa yaliyofanywa mwaka 2020 katika sheria za uchaguzi na kanuni zake hadi walipoanza kuenguliwa ndio wakastuka kwamba mambo yamebadilishwa, wengi wakiona kazi hiyo ilifanyika kinyemela.
Ni mgombea mmoja tu, Ali Saleh ambaye alikwenda Mahakama Kuu kupinga kuenguliwa kwake, akielekeza hoja zake kwenye katiba ya TFF, kwamba haijaijumuisha Zanzibar licha ya shirikisho hilo kuwakilisha taifa la Tanzania na pili suala la wadhamini wa wagombea.
Suala la Zanzibar kutoshirikishwa kwenye katiba hiyo ni la kisiasa, kutokana na ukweli kwamba mambo ya michezo si ya Muungano, lakini ni la utata kutokana na ukweli kwamba TFF ndio mwakilishi wa taifa la Tanzania, lakini viongozi wake wanachaguliwa na wajumbe kutoka Tanzania Bara tu.
Lakini suala la wadhamini ndilo lililokuwa kituko cha mwaka. Kila mgombea urais alitakiwa awe na wadhamini watano, ambao ni vyama wanachama vya mikoa, klabu za Ligi Kuu, na vyama shirikishi kama cha waamuzi, makocha, madaktari na wachezaji.
SOMA ZAIDI: Serikali Itafakari Hili la Mafunzo ya Wachambuzi wa Soka Tanzania
Lakini kanuni hizo zilitaka wadhamini watakaoonekana kwa mgombea mmoja, hatatakiwa kumdhamini mgombea mwingine, na hapo ndipo vituko vilipoanzia.
Wakati kanuni zinataka wadhamini watano, kwa kiwango cha chini, wagombea, hasa waliokuwa madarakani walikusanya wadhamini kadri walivyopatikana na hivyo kusababisha wagombea wengine wasipate.
Yaani kama kuna wanachama 31, ambao ni vyama vya mikoa, klabu 16 za Ligi Kuu na vyama vitano shirikishi, halafu mgombea mmoja akadhaminiwa na vyama 30, waliosalia watagombea vyama 22 vilivyosalia. Na ndivyo ilivyokuwa kwa akina Ali Saleh, Ali Mayay na Oscar Oscar ambao hawakuweza kufikisha idadi hiyo kwa kuwa wale waliotakiwa na mfumo walichukua wajumbe takriban wote.
Yule mmoja aliyepita bila ya kuwa na uhakika na kura za mkutano mkuu, alifarijiwa kwa kupewa ujumbe wa kamati ya utendaji.
Kwa kanuni hizo, ni kama uchaguzi unakuwa umefanyika hata kabla ya kupiga kura. Yaani mgombea atakayekusanya wadhamini wengi ndiye mwenye uhakika wa kushinda na hivyo siku ya kupiga kura ni kwenda kumthibitisha tu.
Kwa nini basi muda upotezwe kupiga kura wakati ili vyama vitoa udhamini mtu vinakuwa vimeshakubaliana ndani kwamba mgombea fulani ndio apite na inabakia suala la kwenda kuthibitisha tu.
Lakini, kwa nini mgombea aende kusomba wadhamini zaidi ya watano? Bila shaka ni kampeni kabla ya muda na njama au hila za kuzuia wengine wasifike kwenye boksi la kura. Huu ni uzandiki.
SOMA ZAIDI: Tumejitahidi AFCON, Lakini Tunajipangaje Upya?
Kwa sheria za vyama vya michezo, vitu muhimu vinavyotakiwa ili viruhusiwe kuendesha shughuli zake, ni katiba na kanuni zilizopitishwa na Msajili wa Vyama vya Michezo. Kwa kanuni kama hizo na kama zilipitishwa na Serikali, basi hilo lilifanyika kimazoea bila ya kuangalia kama masuala ya haki na misingi ya uchaguzi huru yamezingatiwa.
Sitaki kuamini kuwa Msajili wa Vyama vya Michezo alipitisha kanuni hizi zandiki zinazolenga kujenga miungu watu kwenye soka letu baada ya hali hiyo kusumbua kwa muda mrefu hadi mabadiliko yalipofanyika mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Katiba na kanuni kama hizo zilijenga viongozi wenye kiburi, wasio na maono ya maendeleo, wabinafsi na wakorofi kwa kuwa walikuwa na uhakika wa kurejea madarakani kwa kura. Idadi ya wajumbe wakati huo ilikuwa ni ndogo (sabini tu) na hivyo ilikuwa rahisi kuwarubuni na kujenga himaya ya kifalme.
Hayo yamerudishwa kwenye katiba iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2020 na taratibu utawala wa kifalme umeanza kujijenga na unalindwa na kanuni hizo za hovyo.
SOMA ZAIDI: Kamati ya Hamasa Bila ya Mkakati wa TFF
Ziko sheria na kanuni nyingi za uchaguzi na uendeshaji shirikisho zinazolinda viongozi wa sasa na kujenga wigo wa kuzuia walio nje kuingia. Idadi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF imepunguzwa na idadi ya wapiga kura pia imepunguzwa hivyo ni rahisi, hasa kwa mgombea aliye madarakani, kujilinda kwa kurubuni wajumbe wenye haki ya kupiga kura kwa njia nyingi, kama safari, majukumu ya usimamizi bila ya kujali ubora wa mtu, na mambo mengine mengi, achilia mbali fedha ambazo huambatana na hizo fursa.
Katika nchi ya kidemokrasia kama Tanzania na ambayo kilio cha uchaguzi huru na wa haki kinazidi, huku Serikali ikionekana kuchukua hatua kurekebisha sheria, ni muhimu kwa wahusika katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kuanza sasa kurekebisha misingi hiyo ya uchaguzi huru na wa haki katika vyombo vya michezo.
Ni muhimu kwa Msajili wa Vyama vya Michezo kuitisha upya katiba na kanuni za uchaguzi za TFF, kuzitathmini na kuagiza marekebisho pale inapobidi.
Ni muhimu kwa wadau kuanza sasa kupigia kelele kasoro hizo za kisheria na kikanuni kabla ya uchaguzi mpya kutangazwa. Viongozi wa michezo wanatakiwa walindwe na uongozi wao imara na wenye mafanikio katika kuujenga mchezo na shirikisho na si kutafuta mbinu za kujilinda kisheria na kikanuni. Ni ushindani wa haki pekee unaweza kuzaa viongozi wazuri na wawajibikaji.
Ili kuondoa butwaa kama walilokutana nalo akina Ali Saleh na wenzake, ni muhimu kuanza kuangalia sasa sheria za uchaguzi na kanuni zake.
Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.