Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutangaza kupitia Vyombo vya Habari kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi kilichotokea katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es salaam, Februari 29, 2024, tayari Serikali imetoa ratiba ya mazishi.
Katika taarifa ya Serikali iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa usiku wa kuamkia Machi 1, 2024, amesema mwili wa Hayati Ali Hassan Mwinyi utaagwa leo, Ijumaa katika uwanja wa Uhuru kuanzia saa nane mchana baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa BAKWATA ambapo Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakary Zuberi ataongoza dua.
Baada ya kuagwa katika viwanja vya uhuru mwili wa Hayati Ali Hassan Mwinyi utasafirishwa jioni ya leo kuelekea Zanzibar ambapo maombolezo ya kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Amaan Machi 2, 2024 asubuhi.
Mazishi yatafanyika jioni baada ya maombolezo ya kitaifa katika kijiji cha Mangapwani kilichopo kaskazini-magharibi katika kisiwa cha Unga, mahali alichokulia Hayati Ali Hassan Mwinyi.
Hayati Mwinyi alizaliwa Mei 8, 1925 katika kijiji cha Kivule kilichokuwa pembezoni mwa mji wa Dar es Salaam na kisha akiwa na umri wa miaka minne wazazi wake walimpeleka Zanzibar kuishi kwa lengo la kupata elimu.
Katika kipindi cha maisha yake alikuwa rais wa Tanzania katika kipindi cha mwaka 1985 mpaka 1995 ambapo Serikali yake ilitekeleza mageuzi mbalimbali ya kuelekea uchumi wa soko na siasa za vyama vingi.
Amewahi pia kuwa rais wa tatu wa Zanzibar katika kipindi kifupi cha mwaka 1984 mpaka 1985. Kabla ya hapo alihudumu katika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Muungano kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano, Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Afya ma Waziri wa Mambo ya Ndani.
Mwinyi ambaye alisomea ualimu na kufundisha shule mbalimbali visiwani Unguja wakati wa ukoloni, alishika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwanza kama Katibu Mkuu Wizara ya Elimu baada ya mapinduzi Januari 12, 1964 na baadaye kama Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Karuafuu (CGA) Zanzibar mpaka mwaka 1970.