Dar es Salaam. Rais Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki hapo Februari 29, 2024, hakuwahi kujutia uamuzi wake wa kujiuzulu kama Waziri wa Mambo ya Ndani mnamo Januari 22, 1977, uamuzi ambao aliwahi kuuelezea kama “sahihi.”
Mwinyi, aliyekuwa rais wa pili wa Tanzania, alikuwa mmoja kati ya mawaziri wawili wanaohusika na masuala ya usalama wa taifa hilo la Afrika Mashariki waliojiuzulu kufuatia kashfa ya mauaji ya watu waliodaiwa kuhusika na mauaji ya vikongwe katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza chini ya kile kilichojulikana kama ‘Operesheni Mauaji.’
Mbali na Mwinyi, ambaye mwili wake umeagwa leo Ijumaa, Machi 1, 2024, mtu mwingine aliyejiuzulu kufuatia kashfa hiyo ni Peter Siyovelwa ambaye alikuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais yenye dhamana ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Lakini kati ya hawa wawili, ni uamuzi wa Mwinyi, anayetarajiwa kuzikwa huko Zanzibar Jumamosi, Machi 2, ndiyo ambao umebaki kwenye kumbukumbu za Watanzania walio wengi.
Hii inatokana na uamuzi wa makusudi aliouchukua Mwinyi, aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 98, wa kumuandikia barua Julius Nyerere, aliyekuwa rais wakati huo, hapo Januari 22, 1977, akimuomba kiongozi huyo aruhusu kusudio lake la kujiuzulu kufuatia kashfa hiyo iliyokuwa inahusisha maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.
SOMA ZAIDI: Nitakavyomkumbuka Mwinyi, Mzee Rukhsa Asiyekuwa na Tamaa ya Madaraka
“Mwalimu [Nyerere], nakuomba mambo matatu,” Mwinyi, kiongozi pekee aliyepata kuhudumu kama rais wa Zanzibar na Tanzania, aliandika kwenye barua yake hiyo. “Kwanza, naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie nijiuzulu.”
Akiandika kwenye tawasifu yake iliyopewa jina la Mzee Rukhsa: Safari ya Maisha Yangu, Rais Mwinyi, atakayekumbukwa kwa kuitoa Tanzania kwenye changamoto lukuki za kiuchumi, anakumbuka kuhusu uamuzi wake huu maarufu ambapo anaashiria kutokuujutia.
“Bado naamini kuwa uamuzi wangu ulikuwa sahihi na nadhani ulinijengea heshima Serikalini na kwenye jamii kwa kiasi fulani,” Mwinyi anaandika kuhusu uamuzi huo unaotafsiriwa na wengi kama kielelezo cha kiwango cha juu cha uwajibikaji. “Waliohusika moja kwa moja walifikishwa mahakamani, wakawajibika kwa mujibu wa sheria.”
Operesheni Mauaji
‘Operesheni Mauaji’ ilianzishwa kwa nia njema ya kuzuia mauaji holela ya vikongwe katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga kwenye miaka ya 1970 ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakihusiana na imani za kishirikina. Lengo ilikuwa ni kuwasaka wahusika wa mauaji hayo ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Ndani ya wiki tatu watuhumiwa 374 walikuwa wamekamatwa mkoani Mwanza pekee, huku Gereza la Butimba likifanywa ndiyo kituo cha kuhojia watuhumiwa. Maofisa wa Idara ya Usalama ya Taifa na Jeshi la Polisi ndiyo waliiongoza na kuendesha operesheni hiyo.
Mkoani Shinyanga, operesheni ilianza Februari 21, 1976, mpaka Machi 3, 1976, ambapo jumla ya watuhumiwa 524 walikamatwa ndani ya kipindi hicho kifupi. Watuhumiwa hawa walihojiwa katika eneo la Nyang’oha mahali ambapo kulikuwa na kituo cha kununulia pamba kisichotumika.
Hata hivyo, ilikuja kubainika kwamba watuhumiwa hawa wote waliteswa kwa njia mbalimbali, kuanzia matumizi ya nguvu pamoja na kuwadunga sindano za ‘Methedine’ kabla ya kuhojiwa, vitendo ambavyo vilifanywa na madaktari ambao walidai walipokea amri kutoka kwa viongozi.
Katika kipindi hiko kifupi, watu kumi waliuawa Shinyanga na wengine wawili waliuawa Mwanza wakiwa mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama wakihojiwa, huku wengine wengi wakiachwa na ulemavu wa kudumu na vidonda.
Haya yote yaliendelea huku baadhi ya viongozi waliokuwa katika ngazi ya mkoa na wilaya wakijua kilichokuwa kinaendelea na wakati fulani waliwaonya watumishi wa umma kama madaktari walioshirikishwa katika operesheni hiyo wasiseme chochote kwa kile kilichoitwa kutunza siri.
Taarifa zamfikia Nyerere
Taarifa za mauaji na mateso hayo makubwa zilimfikia Nyerere wakati akiwa mapunziko ya mwisho wa mwaka 1976 kijijini kwake Butiama, mkoani Mara. Hii ni baada ya mwanamke mmoja ambaye aliteswa katika operesheni hiyo kwenda Butiama na kutaka kuonana na Nyerere kumuonesha vidonda vilivyotokana na mateso ya vyombo vya dola.
Wasaidizi wa Nyerere walimpeleka mama huyo mbele ya Nyerere, ambaye baada ya kusikia simulizi yake alishituka sana kiasi ya kwamba aliwauliza wasaidizi wake endapo mama huyo ametendewa mambo hayo na askari wa Tanzania ile anayoiongoza yeye.
Nyerere aliunda tume maalumu kuchunguza jambo hilo, ambayo, pamoja na mambo mengine, ilipelekea Mwinyi na Soyovelwa kujiuzulu nafasi zao za uwaziri. Viongozi wengine waliojiuzulu kufuatia kashfa hiyo ni wakuu wa mikoa ya Shinyanga na Mwanza, Marco Mabawa na Peter Kisumo, mtawalia.
Akiandika miaka 43 baada ya matukio haya, Mwinyi, aliyeaga dunia baada ya kupambana na saratani ya mapafu kwa muda mrefu, anasema kwenye tawasifu yake kwamba licha ya kutojutia uamuzi wake huo, alisikitikia sababu iliyomfanya alazimike kuchukua uamuzi huo, akiashiria matamanio yake ya kuchukua uamuzi huo katika mazingira tofauti.
“Ninachosikitika, tena sana, ni kiini cha kilichonifanya nijiuzulu, yaani mauaji ya watu wasio na hatia kwa imani za kishirikina na nyinginezo bado yanaendelea hadi leo, miaka zaidi ya 40 baadaye kwa sura mbalimbali,” anaandika Mwinyi.
“Wengine wanauawa kwa ukongwe wao; wengine kwa rangi ya macho yao au ngozi zao; wengine kwa biashara ya ngozi au viungo vya miili yao; na kadhalika. Tunapaswa kuona aibu kubwa kama taifa! Ni jambo la fedheha mno kwa taifa letu katika karne hii ya sayansi na teknolojia.”