Dar es Salaam. Mahakama Kuu Sumbawanga chini ya Jaji Thadeo Marko Mwenempazi, imefutilia mbali hukumu iliyowafanya watu saba kutumikia kifungo cha mwaka mmoja kila mmoja kwa kugomea watoto wao kupokea chanjo ya surua.
Watu hao walioachiwa huru ni pamoja na Isack Simon Chizu (26), Meshack Isack Yona (28), Yona Simon Chizu (30), Abiniel Isaya Chizu (27), Joshua Meshack (40), Jobo Simon (36) na Efeso Peter (28).
Hukumu ya watu hao kwenda jela mwaka mmoja ilizua gumzo toka Februari 27, 2024, pale ambapo polisi mkoani Rukwa walipotoa taarifa kuhusu watu hao kuanza kutumikia kifungo chao cha mwaka mmoja jela kila mmoja kwa kupinga chanjo, kosa walilofanya Februari 18, 2024.
“Watu hawa saba waliohukumiwa kila mmoja kwenda jela, walitenda kosa la kupinga au kugoma watoto wao wenye umri wa miezi tisa mpaka miezi 59 wasichanjwe ile chanjo ya surua pamoja na rubella,” alieleza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa SACP Shadrack Masija.
Polisi walieleza kuwa sababu ya watu hao kugomea chanjo hiyo ni kwa kuwa “Mungu hajaagiza hilo,” huku polisi ikieleza zaidi kuwa watu hao ni waumini wa dhehebu la Watch Tower.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Ally Chirukile alitembelea kanisa hilo lilopo katika kijiji cha Lula na kulifunga mnamo Februari 18, baada ya kugundua kuwa halina usajili. Askofu wa kanisa hilo alieleza kuwa ni Mungu ameagiza kanisa hilo lisisajiliwe, kanisa hilo pia haliamini katika sensa, kuwa na vitambulisho vya serikali wala kumiliki simu.
Katika kesi ya mapitio ya hukumu hizo ambayo Mahakama Kuu iliitisha, Wakili wa Serikali Godliver Shayo, alieleza kuwa baada ya kupitia nyaraka mbalimbali za mwenendo wa kesi hiyo walijiridhisha kuwa kesi hiyo haikuendeshwa katika usawa na haki.
Wanasheria hao walieleza zaidi kwamba watu hao walifungwa kwa kutokutii amri halali kinyume na kifungu namba 132 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Hata hivyo, wanasheria walieleza kuwa hati ya mashtaka haikuonesha ni amri ipi ambayo watu hao hawakutii na ni nani aliyeitoa amri hiyo na kama aliyeitoa amri alikua na mamlaka ya kutoa amri hiyo.
Wakili kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Peter Kanyamile, alieleza kuwa hakukuwa na ushahidi wa amri iliyotolewa na kupingwa na watuhumiwa hao.
Mahakama ilikubaliana na hoja hii na kueleza, “Jambo lililo wazi katika kesi hii ni kuwa amri halali inayodaiwa kuvunjwa haijaoneshwa, na aliyetoa amri hiyo hajaelezewa vizuri na haijaelezwa alitoa amri hiyo kwa namna gani.”
“Kwa uelewa wangu, Rajab Kwatta alikua anatoa chanjo, hakutoa amri yeyote,” iliendelea kueleza Mahakama. “Ingawa watuhumiwa wamekiri makosa, kosa walilokiri ni kugoma watoto wao kupokea chanjo. Hii inaacha maswali kama walipewa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa chanjo.”
Mahakama ilieleza zaidi kuwa kulikua na makosa katika adhabu iliyotolewa ambapo watuhumiwa walipewa kifungo cha mwaka mmoja katika kosa hilo badala ya miezi sita kama sheria inavyotaka.
Akimalizia hukumu hiyo Jaji Mwenempazi alisema kuwa hukumu na kesi nzima ilijengwa katika msingi usioendana na sheria.
Jaji alihitimisha shauri hilo kwa kutakamka kuwa watuhumiwa hao walifungwa isivyosahihi ambapo alitangaza kufuta mashtaka yote na kuagiza watuhumiwa kuachiwa mara moja.