The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

‘Siyo Uhuni’: Wanawake Jasiri wa Kizanzibar Walioingia Kwenye Sekta ya Uongozaji Watalii

Watu wengi Zanzibar bado wanahusisha suala la wanawake kuongoza watalii na uhuni huku wengine wakisema wanafanya kazi hiyo kujiuza kwa wazungu

subscribe to our newsletter!

Zanzibar. Jua linazama hapa katika fukwe ya Paje iliyopo Wilaya ya Kaskazini, Mkoa Kaskazini  wa Unguja, fukwe hii kwa wakati huu imepambwa na Vishada (Kite) ambavyo watalii wanafundishwa na walimu kutoka katika moja ya shule zilipo karibu na Fukwe hii.

Ayman Mansour, 24, mtoto wa mwisho kwenye  familia yake amekaa pembezoni mwa fukwe hii akiwa anaangalia jinsi wageni wanavyofurahia kujifunza na kuzungumza na walimu, baada ya kumaliza masomo yake ya kidato cha nne Ayman alitamani sana kusoma masuala ya utalii na lugha akitamani kujiajiri kwenye sekta ya Utalii.

“Niliposema tu kuwa nataka kusomea utalii kaka zangu walikataa na hakuna aliyeniunga mkono.” Anaeleza Ayman ambaye anaona fursa ya lugha na ujuzi wa masuala ya utalii yangemuwezesha kuwa mwalimu kwenye kituo hiki cha kurusha vishada.

Ayman anakiri kuwa elimu ndogo juu ya masuala ya utalii kwenye jamii za Kizanzibar zinakwamisha ndoto na fursa zao kama wasichana kusoma. “Nilishapata fursa ya kwenda kusoma mjini lugha ila wazazi wangu wakakataa nami nimekosa nafasi hiyo,” anaeleza Ayman huku tukitembea pamoja katika  fukwe.

Wakati Ayman bado hajafanikiwa kutimiza ndoto zake, hali ni tofauti kwa  Fath-hiya na Asma ambao ni waongozaji maarufu wa watalii.

Mwanangu ni jasiri

Fath-hiya Abdulhamid Ali, 23, alianza kazi ya kutembeza watalii mwaka 2016 akiwa amemaliza elimu ya kidato cha nne. Alipomaliza shule alikuwa ni mwalimu wa somo la Kingereza kwenye vituo vya kuongeza ujuzi wa lugha na hapo ndipo alipoanza kuona fursa ya kuingia kwenye utalii.

“Wakati naanza nilikuwa na miaka 17, sasa huwezi kutambulika na kamisheni ya Utalii mpaka uwe na kitambulisho cha Mzanzibar na mimi umri ulikuwa haujatimia, kwa hiyo sikuweza kupewa kitambulisho,” anaendelea kusema kuwa aliificha kazi yake kwa watu wa karibu hususan baba yake kwa kuogopa familia yake kusemwa na kuonekana hawajamlea vyema.

Mwaka 2017 Fathiya alipata kitambulisho rasmi na alianza kazi akiwa kama muajiriwa, ingawa umahiri wake katika kazi ulimtambulisha bado alikutana na changamoto zilizomkosesha raha.

“Wageni wengi walifurahishwa na kazi yangu ,na bado niko navaa baibui na mtandio wangu, ila njiani kama Darajani na hata Mji Mkongwe watu wanakutazama na hata kusema kuwa mimi ni muhuni sijalelewa vyema,” anaeleza Fath-hiya ambaye kwa sasa amefungua Kampuni yake mwenyewe huku akibeba tuzo nne za mtembezaji bora wa watalii mwanamke.

Fath-hiya ambaye kwa sasa amepanga kutumia kampuni yake kusaidia wanawake wenzake, anaeleza kuwa vikwazo si maneno pekee na udhalilishaji pia. “Pale kwenye kibali ni lazima upate mdhamini wa kampuni, basi kama huna hapo hapo ndio wanatumia mwanya huo kukutaka kimapenzi jambo ambalo linavunja moyo na kuumiza sana,” anaeleza Fath-hiya.

Suala la kuitwa muhuni lilimfikia mpaka mama yake Fath-hiya, Bi Maryam Hamad, “Niliambiwa na wenzangu mtaani kuwa mtoto wangu ni muhuni nilikuwa naumia na nilitaka aache ila baadae nikagundua yeye anafanya kazi hafanyi uhuni,” anaeleza Maryam.

Anaendelea kusema alimficha mume wake juu ya kazi hiyo ila kwa sasa binti yake ndio msaidizi mkubwa wa familia. “ Anasomesha wenzake na anatusaidia sana kwenye maisha licha ya watu wengine wanaovyomuona mimi namuona mwanangu ni jasiri sana na najivunia mtoto wangu.”

Hii kazi inalipa

Asma Mtwana 27, ni mtembeza watalii maarufu Kizimbani. Asma ambaye ni mama wa mtoto mmoja amekuwa akifanya kazi hii toka mwaka 2019. Ni Hodari anayefahamu kila kona ya Kizimbazi, sehemu yenye mashamba mengi ya viungo vya asili.

Asma anaeleza kuwa baba yake amekuwa na mchango mkubwa wa kumsaidia hata hivyo almanusura maneno ya walimwengu yamkatishe tamaa.

“Baba yangu alinisaidia ila maneno ya watu kuwa nataka kujiuza kwa wazungu au natembea na wazungu au nina mahusiano na madereva wa teksi yalikuwa yananiumiza sana hadi nikataka kuacha hii kazi,” anaeleza Asma.

Kazi hii imemwezesha Asma kujenga nyumba yake na anaeleza hii imewezekana kutokana na kuaminika zaidi kwa waongozaji wanawake jambo ambalo linamuwezesha kupata kipato cha kutosha, “Kwa kazi hii kwa mwaka kama ushatumia na umekosa umekosa hapo unaweza kuwa na hata milioni 7 umeweka akiba, hii kazi inapesa na inalipa sana,” anaeleza kwa ujasiri Asma.

Pamoja na changamoto, wanawake wa Zanzibar wameanza kuchangamkia fursa ya kuongoza watalii. Kamisheni ya Utalii Zanzibar inayoratibu vibali vya watembeza watalii wanaeleza kuwa idadi ya wanawake kuomba vibali imeendelea kuongezeka.

Kwa mwaka 2021 waliosajiliwa na kupewa vibali walikuwa 700 kati ya hao wanawake walikuwa 20, na kwa mwaka 2022 waliopata vibali walikuwa 770 huku wanawake wakiwa 40, na mwaka 2023 waliosajiliwa walikuwa 1,405 wanawake ni 79. Hata hivyo idadi hii bado ni ndogo ukilinganisha na soko la watalii ambapo kwa mwaka 2023 pekee watalii 638,498 waliingia visiwani Zanzibar.

Bado elimu inahitajika

Khadija Khamis ni Mwalimu wa Taaluma katika  kituo cha Kawa Training Center ambaye pia ni mwenyekiti wa uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa jamii  kupitia kituo hiki, anaeleza kuwa jamii imeendelea kubadilika ingawa bado safari ni ndefu.

“Mjini ni tofauti na Vijijini kule mila na tamaduni zimeshika kasi ila ukitoa elimu wazazi wengine wanakubali mwanzo baadae unakuta msichana kaacha kuendelea na masomo,” anaeleza Khadija.

“Zamani darasa la wanafunzi 20 wanakuwa wasichana 6 ila sasa hivi wasichana wanaweza kuwa 12 kati 20 darasani, ila sio wote ambao wanamaliza kitu ambacho kinanivunja moyo kama mwalimu,” anafafanua zaidi Khadija wakati akizungumza na The Chanzo ofisini kwake Kiponda Zanzibar.

Amesema Serikali ina jukumu la kuwaelimisha wanajamii juu ya umuhimu wa sekta ya utalii na kuwa sio ya jinsia moja pekee bali ni sehemu ya watu wote kujitafutia riziki halali.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mudrik Soraga amesema jamii ya Kizanzibar inahusianisha utalii na masuala ya uhuni kwa sababu ya kutowepo na wawekezaji wazawa kwenye sekta ya utalii.

”Mfano ni asilimia tano ya wazawa ndio wamewekeza kwenye sekta ya Utalii tofauti na wageni ambao wameona hiyo fursa na wamewekeza, sasa mzawa akiona unaajiriwa na mtu asiyemjua inakuwa ni ngumu na kuweka mawazo hayo,” anafafanua Soraga.

Anaendelea kusema Serikali inampango wa kubadilisha mtaala wa elimu ya masuala ya utalii na kuwasaidia wazawa ambao wamesoma kuwapatia fedha ili waweze kuwekeza kwenye sekta hii kwa ukubwa wake.

Najjat Omar ni mwandishi wa Habari wa The Chanzo kutoka Zanzibar. Kwa mrejesho, unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni najomar@live.com

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *