Mnamo April 04, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Catherine Michael Mashalla ingawa sababu za utenguzi huo hazikubainishwa.
Hata hivyo Mashalla pamoja na watumishi wenzake tayari walikua matatani kufuatia uchunguzi wa TAKUKURU Sumbawanga.
Awali, mnamo tarehe 25 Agosti 2023, TAKUKURU mkoa wa Katavi ilimfikisha mahakamani Mashalla na watumishi wengine sita kwa tuhuma za wizi wa zaidi ya bilioni 1.2 (1,232,408,689/-).
Watuhumiwa hao, wakiwemo Michael Mathew Katanga (muhasibu), Masami Andrew Mashauri (muhasibu), Maira Samson Oluomba (muhasibu) na Juma Motela John Oluomba, walitajwa kuwa sehemu ya genge la watu 15 lililohusika katika wizi huo. Mashalla na wenzake wanashtakiwa kwa kuunda genge la kihalifu, wizi wa fedha za serikali, na utakatishaji wa fedha.
Taarifa ya uchunguzi kutoka takukuru iliyotolewa na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Katavi, Faustine Maijo ya Aug 22, 2023 ilifafanua kuwa uchunguzi wa maafisa wa taasisi hiyo ulibaini kufujwa kwa fedha na watumishi hao kutoka Halmashauri ya Mpimbwe, Manispaa ya Mpanda na ofisi ya Mkuu wa Mkoa Katavi.
Na hapa ikumbukwe kuwa kabla ya kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mashalla alikuwa mkurugenzi wa wilaya ya Mpimbwe kabla ya kuhamishiwa sumbawanga juni 07 2023.
Maijo alieleza kuwa fedha hizo ambazo zilikuwa kwenye akaunti ya halmashauri ya Mpimbwe zilifujwa na watumishi hao huku wakidanganya kuwa walikua wakiwalipa wakandarasi waliofanya shughuli mbalimbali katika halmashauri hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa uchunguzi ulithibitisha kuwa fedha hizo zililipwa kwa watu binafsi ambao hawakua na kazi zozote walizofanya katika halmashauri hiyo na walikuwa ni watu wa karibu na watumishi hao.
Wakati kesi inaendelea, Mashalla na wenzake wanne waliwasilisha maombi ya dhamana mnamo tarehe 25 Machi 2024 katika Mahakama Kuu ya Sumbawanga.
Mahakama iliwapa dhamana tarehe 27 Machi 2024 kwa sharti la kulipa milioni 176 (TZS 176,058,384.1429) kila mmoja au kutoa hati ya umiliki wa mali isiyohamishika yenye thamani sawa.
Aidha pamoja na sharti hilo waombaji katika kesi namba 05 ya uhujumu uchumi ya mwaka 2023 waombaji walitakiwa kuripoti kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi kwenye Kituo cha Polisi cha Katavi.
2 Responses
Mwenye fedha hafungwi. Mtu akistaafu kikokotoo hakimuachi salama hapo ukigawanya fedha hizo mtu ana zaidi ya 200m/= utamfungaje?kesi itapigwa danadana tunasahau maisha yanaendelea..
Issue inakuja kwamba wasaidizi wa Rais ambao wanamsaidia katika kuwachunguza wateule, ni tatizo kubwa haingii akilini mtu ana tuhuma wilaya hii anahamishiwa wilaya nyingine.
Katiba ibadilishwe Makonda awe anateua tu akae ikulu.