Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mwanaume aliyetambulika kwa jina la Abeid Salim Kingazi katika kesi ya jinai namba 59 ya mwaka 2023 iliyohusu mashtaka ya ubakaji na kumpa ujauzito mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17 ambaye imeelezwa kuwa ni shemeji yake.
Mwathirika ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule msingi Lemosho, akiwa anaishi nyumbani kwa mtumhumiwa alikuwa akisumbuliwa na tatizo la kutokwa na damu puani kwa muda mrefu jambo ambalo shemeji yake huyo alimweleza kuwa amerogwa na majirani ili awe tasa.
Aidha imeelezwa kwamba mwanaume huyu alimlaghai kuwa ili kumuokoa na utasa huo aliotupiwa kichawi anatakiwa kufanya naye mapenzi. Baada ya tukio hilo, mshitakiwa alimtishia mwanafunzi huyo kuwa asimwambie mtu yeyote kuhusu kilichotokea.
Kwa kuogopa vitisho kutoka kwa shemeji aliamua kukaa kimya, hata hivyo, aligundua kuwa alikuwa mjamzito mwezi wa Novemba 2022. Hali iliyosababisha kuwaeleza ukweli wazazi wake na ndipo ikabainika kuwa mwanaume huyo alitekeleza tukio hilo mwezi Mei 2022 katika kijiji cha Matadi, Wilaya ya Siha, Mkoa wa Kilimanjaro.
Mtuhumiwa alifikishwa kwenye vyombo vya dola na hatimaye Mahakama ya Wilaya ya Siha, ambapo alipatikana na hatia ya ubakaji na kumpa ujauzito mwanafunzi na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miaka thelathini jela kwa makosa yote mawili.
Hata hivyo mtumhumiwa hakuridhika na maamuzi ya Mahakama ya Wilaya ya Siha, kabla ya kukata rufaa yake kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Moshi ambapo kesi ya jinai namba 59 ya mwaka 2023 ilifunguliwa.
Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote, jana April 15, 2024 Mahakama Kuu ya ilitupilia mbali rufaa ya mshitakiwa huyo na kutoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kama hukumu ya awali iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Siha ilivyokuwa.
Matonyinga Makaro ni mwandishi wa The Chanzo kutoka mkoani Mwanza. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia matonyingamakaro@gmail.com.