The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tujipe Muda Kabla ya Kuanza Kuitumia V.A.R

Ni muhimu kuanza kushughulikia udhaifu wetu katika uamuzi, wakati tukijiandaa kwa teknolojia hiyo.

subscribe to our newsletter!

Kitendo cha Serikali kupendekeza kuondoa kodi kwa vifaa vinavyotumika katika teknolojia ya Refa Msaidizi wa Video (V.A.R) kwa ajili ya kufanikisha uamuzi sahihi katika mechi za mpira wa miguu, kimevutia mashabiki wengi wa mchezo huo maarufu nchini.

Maamuzi mengi katika mechi za Ligi Kuu na zile za chini yamekuwa yakiibua mijadala mikubwa kuhusu usahihi wake kiasi cha kufikia kupoteza ladha ya ushindi kwa timu inayoonekana kunufaika na utata unaoibuliwa na uamuzi wa refa.

Na mechi ya hivi karibuni baina ya Tabora United na Biashara FC ya Shinyanga kuhusu bao pekee katika mchezo wa kwanza inaweza kuwa imechochea zaidi mjadala wa usahihi wa maamuzi. Katika mechi hiyo, refa aliamuru penati katika dakika za majeruhi na mpira wa adhabu hiyo ulionekana kama umepanguliwa na kipa na kutoka nje.

Mwamuzi msaidizi akaonyesha kuwa mpira haukuingia golini na hivyo iwe kona, lakini baada ya kuzongwa, refa akaamua kuwa ni bao, jambo lililosimamisha mchezo kwa dakika kadhaa. 

Yapo matukio mengi mengine kama mpira uliopigwa na Maxi Nzengeli na kugonga mwamba halafu kudunda chini kuonekana haukuvuka mstari wa goli, lakini refa akaamua kuwa ni goli.

SOMA ZAIDI: Simba Inahitaji Kutathmini Safari Yake ya Mabadiliko

Matukio ni mengi kiasi kwamba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likatangaza kuwa Ligi Kuu itatumia teknolojia hiyo ya V.A.R msimu ujao kwa mechi zitakazochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa. Hilo likafuatiwa na pendekezo la Serikali katika bajeti kuu kuhusu kufanikisha matumizi hayo kwa kuondoa kodi katika vifaa vya teknolojia hiyo.

Ni kama vile inaonekana kwamba V.A.R ni suluhisho la matatizo ya uamuzi nchini ambayo kwa misimu kadhaa yamekuwa yakitawala mijadala, hasa timu vigogo za Simba, Yanga na Azam zinapocheza. MIjadala huwa ni kuhusu “goli halali au si halali,” “kulikuwa na kuotea au la” ama “tukio lilistahili kadi nyekundu au la.”

V.A.R

Teknolojia ya V.A.R hutumia kamera takribani 42 kufuatilia matukio kadhaa uwanjani, huku ikiwasiliana na mwamuzi wa kati kuhusu matukio yenye utata ambayo yanastahili ama kuangaliwa marudio yake, kusikiliza ushauri wa wasimamizi wa teknolojia hiyo au kupuuzia.

Kwa hiyo, wasimamizi wa teknolojia hiyo ambayo si lazima wawe kwenye vyumba vya majengo ya uwanja ambao mechi inachezwa, hutakiwa kuhakikisha masuala kama “ni goli au si goli,” “ni penati au siyo,” “ni kadi nyekundu ya moja kwa moja (si ya pili ya njano) au la” au “refa alitoa kadi ya njano au nyekundu kimakosa kwa mchezaji asiyestahili.”

Lakini kanuni kuu ya uamuzi katika mchezo wa mpira wa miguu ni refa wa kati kuwa mwamuzi wa mwisho wa tukio lolote lile. Na kwa sababu hata teknolojia hiyo inasimamiwa na binadamu, bado kunahitajika weledi, ujuzi na ufahamu wa hali ya juu kuwezesha maamuzi kuwa sahihi zaidi.

SOMA ZAIDI: Olimpiki ya Paris Imeshatupita, Tujiandae ya 2028

Nchini England, klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu zililazimika kupiga kura kuamua ziendelee na matumizi ya teknolojia hiyo au la baada ya Wolves kuwasilisha hoja ya kutaka teknolojia hiyo iondolewe msimu wa 2024/25. 

Timu hiyo iliweka mezani hoja tisa za kutaka hatua hiyo, ambazo ni pamoja na athari za V.A.R katika ushangiliaji wa goli, hali ya kuchanganya inayosababishwa na muda unaotumiwa kuangalia marudio ya tukio, hali mbaya ndani ya uwanja, huku mashabiki wakizomea wakati wimbo wa Ligi Kuu ukichezwa na matumizi yaliyopitiliza ya teknolojia hiyo badala yay ale yaliyokusudiwa.

Wolves iliwasilisha hoja hiyo kwenye mkutano mkuu wa klabu za Ligi Kuu uliofanyika mwishoni mwa msimu ambao maamuzi ya kutumia V.A.R yaliyoisha kwa refa kuzawadia bao yalikuwa 33, wakati yaliyoisha kwa refa kukataa mabao yalikuwa 50, likiwemo lililoinyima Manchester City bao la ushindi dhidi ya Liverpool, huku yaliyozawadia penati yakiwa 28 na yaliyopindua penati yakiwa 12. Yapo mengi zaidi yaliyoibua utata.

Nchini Hispania, ushindi wa Real Madrid wa mabao 3-2 dhidi ya Armenia ulitawaliwa na maamuzi tata yaliyowanufaisha mabingwa hao wa Ulaya baada ya Armenia kuushtukiza ulimwengu wa kutangulia kufunga mabao mawili mwanzoni mwa mchezo.

Ligi Kuu ya Hispania imeamua kuwa mazungumzo kati ya refa wa kati na msaidizi wa video yawekwe bayana baada ya mechi kuongeza uwazi, huku Ligi Kuu ya England ikiendesha kipindi kinachoweka bayana mazungumzo hayo ambacho watangazaji wake ni Michael Owen na Howard Webb, ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa Kampuni ya Waamuzi wa Mechi za Kulipwa (PGMOL).

Waamuzi weledi

Kwa hiyo, suluhisho la matatizo ya usahihi katika uamuzi si teknolojia ya V.A.R kwa kuwa bado inaendelea kuibua utata kutokana na ukweli kwamba mpira wa miguu ni mchezo wa tafsiri ya sheria dhidi ya matukio na tafsiri hiyo inafanywa na binadamu ambaye kukosea ni sehemu ya ubinadamu wake.

SOMA ZAIDI: Kwa Hili, Serikali Imeheshimu AFCON 2027

Kitu cha msingi ni kwanza kuwa na waamuzi waliofundishwa vyema wakaelewa tafsiri ya sheria za soka dhidi ya matukio na mazingira yaliyotokea na kupata uzoefu wa kutosha kabla ya kukabidhiwa dhamana ya kusimamia Ligi Kuu. 

Tumeona waamuzi wengi nin vijana ambao hawana hata miaka mitano kwenye ligi za chini ambazo zingewapa uzoefu wa kutosha kuelewa mazingira, sheria na kutoa tafsiri sahihi.

Mazungumzo baina ya mwamuzi wa kati na msaidizi wa video katika mechi baina ya Real Madrid na Armenia yaliibua utata kuhusu weledi wa waamuzi, kitu ambacho ni muhimu sana katika fani hiyo. 

Tumeona mechi za michuano ya klabu ya Afrika zikichezwa bila ya matumizi ya V.A.R licha ya kusimikwa uwanjani, na sababu ikatolewa kirahisi kuwa haikuwa ikifanya kazi na kibaya zaidi kukawa na matukio tata.

Kwa hiyo, iwapo huna waamuzi wenye weledi, walio tayari kuchezesha mechi kwa maagizo, wenye unazi na wasio na upeo mkubwa wa tafsiri ya sheria, teknolojia ni kazi bure na ikitumika itaongeza utata zaidi badala ya kuongeza usahihi katika maamuzi.

SOMA ZAIDI: Ni Muda Makocha Wazawa Tanzania Waanze Kufanya Kazi Kisasa

Nchini England, suala la mwamuzi kushabikia klabu moja au familia yake kuwa na mapenzi na klabu fulani, huzingatiwa sana katika kupanga waamuzi kuchezesha mechi.

Ni kwa kiasi gani tunahangaika kuwapa mafunzo waamuzi wetu ili wawe tayari kwa teknolojia hiyo? Wakati fulani nchini England ilionekana kuwa waamuzi wa V.A.R walifanya kazi wakiwa na uchovu kutokana na idadi yao kuwa ndogo hivyo kuwa kwenye mashine hizo kuanzia Ijumaa hadi Jumapili bila ya mapumziko. 

Kwetu ni wangapi wako tayari kwa teknolojia hiyo na watakidhi mahitaji ya mechi za raundi moja?

Kutokuwa tayari

Pia, kusema kwamba mechi zitakazochezwa Uwanja wa Mkapa ndio zitanufaika na teknolojai hiyo ni kuonyesha kutokuwa tayari kwa matumizi ya V.A.R. Katika Ligi Kuu mechi zote ni sawa na kuna baadhi ambazo zinaweza zisichezwe Uwanja wa Mkapa kama vile Azam FC V Ihefu au Pamba V Polisi Tanzania. 

Mara nyingi, mamlaka hutumia V.A.R kwa mechi chache pale mashindano yanapokuwa ya mtoano. Kwa maana kwamba mechi za kuanzia robo fainali ndiyo zinaweza kutumia teknolojia hiyo na si baadhi ya mechi za Ligi Kuu.

SOMA ZAIDI: Tathmini Inahitajika Kuondoa Mazoea Kwenye Soka la Tanzania

Hali kadhalika, suala la uwazi limeonekana kuwa ni muhimu sana katika matumizi ya teknolojia ya V.A.R na nchi kama Hispania na England zimeamua kushughulikia suala hilo, huku PGMOL ikipania kuanzisha utaratibu ambao refa atalazimika kuwatangazia mashabiki uwanjani kile alichoaamua baada ya kuangalia marudio ya tukio tata.
Pia, ni muhimu kutenganisha wasimamizi wa teknolojia hiyo na kampuni iliyopewa haki ya kutangaza moja kwa moja mechi za Ligi Kuu, kwa hapa Tanzania ni Azam Media. 

Teknolojia ya V.A.R imeweka utaratibu kwamba kunapokuwa na matukio tata yanayohitaji kuangaliwa kwa umakini zaidi, hutuma picha hizo za marudio kwa shirika linalotangaza mechi, na si shirika hilo ndiyo lirekodi matukio hayo na kuyarudia wakati kuna utata.

Kwa hiyo, tunahitaji kutathmini tatizo letu kwenye uamuzi wa mpira wa miguu kabla ya kukimbilia teknolojia wakati hatuko tayari kuitumia. Teknolojia inasaidia tu kuongeza usahihi lakini uamuzi wa binadamu ndio muhimu kuliko vitu vyote.

Bado tuna tatizo la usahihi katika maamuzi ya mechi na bado tunakosa weledi, huku kukiwa na tuhuma nyingi za unazi. Kwa hiyo, ni muhimu kuanza kushughulikia udhaifu wetu katika uamuzi, wakati tukijiandaa kwa teknolojia hiyo. 

Ni muhimu kujipa muda wa kutosha kuandaa rasilimali watu itakayokuwa ina uwezo na ustadi katika uamuzi na utayari wa kutumia teknolojia hiyo muhimu katika uamuzi.

Angetile Osiah ni mwandishi mkongwe wa habari na mchambuzi mashuhuri wa michezo Tanzania. Kwa mrejesho, anapatikana kupitia ngetaiku@yahoo.com. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha kwenye safu hii? Wasiliana na wahariri wetu kupitia editor@thechanzo.com kwa ufafanuzi zaidi.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *