Katika jamii yetu, ukatili dhidi ya watoto ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa kwa haraka na kwa umakini mkubwa. Ukatili huu unaathiri watoto kwa njia nyingi, ikiwemo kisaikolojia, kihisia, kimwili, na kijamii.
Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda haki na ustawi wa watoto ambao ndiyo msingi wa jamii yenye ustawi na maendeleo endelevu.
Watoto hufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ukiwemo wa kijinsia, kimwili, kihisia, kisaikolojia pamoja na ule wa kingono ambao hujumuisha ubakaji, ulawiti, kuoneshwa picha na video za ngono na kushirikisha watoto katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za kingono.
Ukatili kwa watoto husababisha athari kubwa na madhara ya muda mrefu. Watoto wanaokumbwa na ukatili wanaweza kupata matatizo ya kisaikolojia kama vile sonona, wasiwasi, na msongo wa mawazo.
Kimwili, wanaweza kuathirika kwa kuwa na majeraha na magonjwa yasiyopona na hivyo kupelekea ukuaji na ustawi wao kudorora. Watoto hawa hukosa kujiamini na wanaweza kujitenga na jamii, hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi wakiwa wakubwa.
SOMA ZAIDI: Kwa Nini Watoto Wanapaswa Kufahamu Kuhusu Siku ya Mtoto wa Afrika?
Katika jamii nyingi Tanzania, tamaduni na mila ni sehemu kubwa ya maisha ya kila siku na tamaduni hupelekea imani za kishirikina ambazo wakati mwingine zimekuwa chanzo za ukatili dhidi ya watoto wenye ulemavu na wasio na ulemavu.
Kumekua na kesi hivi karibuni za kusikitisha na kukasirisha za vitendo vya kinyama na kikatili dhidi ya watoto kwa sababu ya imani potofu za kishirikina.
Ukatili huu hufanywa na watu ambao hudhani watoto, hasa wadogo, ambao hawajashiriki ngono na wale wenye ulemavu, au magonjwa adimu yasiyo ya kawaida machoni mwa baadhi ya watu, wakiamini kuwabaka, kuwaua na kuwakata baadhi ya viungo vyao itawasaidia kupata maisha mazuri.
Pia, katika baadhi ya jamii, watoto hutolewa kafara au kufanyiwa vitendo vya kikatili kama sehemu ya matambiko ya kimila yanayodhaniwa kuleta utajiri au kuondoa mikosi.
Kama wazazi, au walezi, sisi ndiyo walinzi wa kwanza wa watoto wetu. Tunahitaji kusimama imara katika nafasi zetu kwa kuwa na mahusiano mazuri na watoto ili watueleze pale wanapopitia changamoto, kuwalinda watoto kwa umakini kwa kufahamu sehemu wanazopenda kwenda, watu au marafiki zao, na kadhalika.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwalea Watoto Wetu Kuwa Wenye Furaha?
Jamii ikijumuisha watoto wenyewe ambao ndiyo waathirika, inahitaji kuelimishwa kuhusu haki za watoto na athari za ukatili pamoja na hali halisi ya ukatili katika jamii zetu na ulimwenguni kote.
Hii inaweza kufanyika kupitia vyombo vya habari, mashirika ya kijamii na asasi za kiraia, na taasisi za elimu. Jamii pia inahitaji kuvaa uhusika na kushiriki kikamilifu katika kupinga ukatili kwa watoto kwa kuripoti matukio ya ukatili na kuunga mkono juhudi za kuwalinda watoto.
Serikali inapaswa kusimamia kwa dhati sheria na sera zinazolinda haki za watoto. Adhabu kali zinapaswa kutolewa kwa wale wanaopatikana na hatia ya ukatili dhidi ya watoto. Ni muhimu kuwa na utekelezaji madhubuti wa sheria hizi ili kuhakikisha kuwa wale wanaojihusisha na vitendo hivi wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia, Serikali na wadau wa haki za watoto wanapaswa kuwa na programu endelevu za kuwajengea uwezo maafisa wote wanaohusika na utekelezaji na ushughulikiaji wa kesi nanmatukio ya ukatili kwa watoto.
Ni muhimu pia kuimarisha huduma za ushauri nasaha na matibabu kwa watoto waliokumbwa na ukatili ili kuwasaidia kupona na kurudi katika hali yao ya kawaida kwa ushirikiano kati ya Serikali, jamii na mashirika mbalimbali ili kutoa rasilimali na utaalamu kupitia kampeni za kuondoa ukatili ikiwemo ukatili wa kishirikina dhidi ya watoto.
SOMA ZAIDI: Tunawezaje Kuwajengea Uwezo Thabiti Mabinti Zetu?
Ukatili dhidi ya watoto, iwe kwa sababu za kishirikina au sababu nyingine, ni tatizo kubwa linalohitaji suluhisho la haraka na la pamoja. Kwa pamoja, tunaweza kuelimisha jamii, kuimarisha utekelezaji wa sheria, na kutoa msaada kwa watoto waliokumbwa na ukatili.
Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa watoto wote wanakua katika mazingira salama na yenye upendo, wakipata fursa ya kufikia ndoto zao bila hofu ya ukatili wa aina yoyote. Jamii yenye afya na maendeleo ni ile inayolinda haki na ustawi wa watoto wake.
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.