Nikiwa mtoto, nilikua mpenzi sana wa filamu; nilishinda kwenye vibanda umiza kweli kweli. Moja ya filamu niliyowahi kuiangalia ikanigusa ukiacha Escape From Sobibor ni Shawshank Redemption, filamu kuhusu wafungwa wenye matumaini kuwa siku moja wataiona nuru ya uhuru.
Niwe mkweli, nikiwa mdogo sikuelewa walichokuwa wakiongea , ila mwaka juzi niliirudia tena. Moja ya kipande ambacho kilinigusa sana niliporudia ni pale mwigizaji Morgan Freeman (akienda kwa jina la Red) alipomuambia muigizaji mwenzake Tim Robbins (Andy Dufresne), “Matumaini ni jambo la hatari, matumaini yanaweza kumfanya mtu akawa kichaa.”
Maneno haya yamekua yakijirudia kichwani kwangu toka Juni 27,2024, pale ambapo mtumiaji mwenzetu wa mtandao wa X, Edgar Edson Mwakabela maarufu kwa jina Sativa alipopatikana huko mkoani Katavi baada ya kutupwa na watu waliomteka toka Juni 23,2024. Polisi wameeleza kuwa wameanza uchunguzi juu ya sakata hili na kutoa ulinzi wa karibu mpaka alipoondoka Katavi leo Juni 29,2024.
Utata
Edgar anaelezea kuwa alitekwa maeneo ya Ubungo, majira ya saa moja usiku na kisha kupelekwa katika Karakana iliyopo katika kituo cha Polisi cha Oysterbay. Taarifa kutoka kwa Edgar zinaeleza kuwa watekaji wake walimhoji maswali mbalimbali hasa nini alichokifanya na ikiwa ana ukaribu na wanaharakati mbalimbali.
Edgar ametoa taarifa ambazo kwa kiasi kikubwa inaonekana watekaji wake hawakuzingatia sana kumficha yanayoendelea kwani walikwisha amua kwamba watamtoa uhai wake.
Baada ya kutolewa katika karakana hiyo ya Polisi, anaeleza kuwa walielekea Arusha na kisha kuelekea Katavi, ambapo alipigwa risasi ya kichwa kwa neema za Mungu, risasi ile iliishia kwenye taya, ikiharibu taya na meno yake na kumsababishia maumivu makali.
Eneo alilokutwa Sativa na wasamaria wema ni eneo ambalo kwa kiasi kikubwa linapitiwa na wanyama wakali, hii ikimaanisha kuwa baada ya watekaji wake kuona wameshamuua walimuacha aliwe na wanyama wakali. Tukumbuke hakupigwa risasi ya mguu, wala mkono, ni kichwani, watekaji ambao wanahusishwa na vyombo vya ulinzi waliamua kumuua.
SOMA PIA:Wananchi Waibane Serikali Kukithiri Matukio ya Utekaji Tanzania
Tukio la Sativa linakuwa ni la kipekee, hasa kutokana na kuwepo kwa watu wengi walioendelea kupotea hasa katika siku hizi za karibuni, huku vyombo vya habari mbalimbali ikwepo ITV na Mwananchi wakiripoti matukio hayo. Utofauti wa tukio hili ni kuwa limeonesha mlolongo mzima wa watu kupotea hasa baada ya muathirika kuponea chupu chupu.
Matumaini ni Jambo Hatari
Kwa kiwango kikubwa kama sio juhudi za marafiki wa Sativa na wanasheria wawili Tito Magoti na Miriam Mkanaka walioandaa kampeni #WhereIsSativa, ingewezekana jamii tusingejua au kufuatilia kwa kiwango kikubwa kupotea kwa Sativa.
Nitakuwa mkweli, nilishiriki katika kampeni hii kupitia ukurasa wangu wa X lakini nakiri sikushiriki kama nilivyokuwa nikifanya wakati nchi ilipokua ikipitia majaribu kama haya chini ya Rais Magufuli. Hili ni jambo lililonifanya nishindwe kulala vyema toka majuzi, nikose furaha, hakika najisikia aibu.
Katika tafakari yangu nimegundua sikufanya hivi kwa kiwango kikubwa kwa sababu ya matumaini, matumaini kwamba nchi yetu imetoka kwenye nyakati za giza, matumaini kwamba utekaji haupo, labda kuna mambo madogo hayajakaa sawa, matumaini ya 4R, matumaini kwamba tumerudi kwenye uongozi unaoheshimu ubinadamu na utu, matumaini juu ya kauli za viongozi wetu hasa mheshimiwa Rais.
Na kusema ukweli sikuwa peke yangu, wengi tulikua tumekaa kwenye haya matumaini, matumaini kuwa angepatikana akiwa salama salmini, matumaini yaliyogeuka kuwa jambo la hatari. Kama sio msimamo thabiti wa marafiki zake, wanasheria Tito Magoti na Miriam Mkanaka, inawezekana hata habari yake kupatikana ingebaki kuwa tukio la kawaida wakati ni jambo la kuogofya.
Ishara zote katika tukio hili zinathibitisha kuwa Sativa hakutakiwa kuwa hai, watekaji wake na viongozi wao walishampa adhabu ya kifo. Inwezekana sasa hivi wamekaa mahali wakila nyama choma wakitabasamu na kupanga mtu mwingine au wengine wa kuteka na kuua, wanatuangalia raia kama karatasi za kufuta haja baada ya kujisaidia, maisha yetu ni kama kete kwenye bao, wanaona muda wowote wanaweza kuyatupa.
Nimejiuliza maswali mengi hasa kuhusu mambo yaliyonipa matumaini kuhusu uelekeo wa nchi yangu. Kuna uelewa miongoni mwetu kwamba Rais Samia Suluhu aliamua kurekebisha makosa yaliyofanyika kwenye nchi yetu hasa ukatili, mauaji, kufungwa, upotezwaji, utekaji dhidi ya watu. Na kusema ukweli kuna mambo yaliyotupa matumaini ikiwemo kuachiliwa kwa wafungwa, mikutano ya vyama vya siasa, kufunguliwa kwa vyombo vya habari n.k
Hata hivyo, mambo hayo yamerudi kwa kasi ni kama yalitumiss sana, maana watu wanapotea kiholela holela, na wapotezaji hawajawahi kamatwa wala kujulikana. Najiuliza je Rais anaongea kitu hiki kwetu wananchi na kuagiza kitu kingine? Najiuliza kwa sababu, kwa wengi wetu Rais akiongea tunamuamini, na tunaheshimu kauli yake; hasa kutokana na kuwa yeye ni alama muhimu ya uhai wa taifa letu.
Najiuliza tena au ni sisi raia pekee tunaoamini maneno ya Rais na kuyachukulia kwa uzito au kuna namna watendaji wake wana uhuru wa kuyatafsiri kwa namna wanavyopenda; kwamba kwao zile 4R zinaweza kuwa 4K; Kuteka, Kutesa, Kuua na Kupoteza?
Najiuliza tena au Rais kabadili msimamo wake juu ya kuwa na serikali ya kiungwana inayofuata Katiba na haki za kiasili za binadamu tulizopewa na Mungu?
Dola Yenye Wasiwasi na Uchaguzi wa 2025
Moja ya jambo ambalo lililofanya uongozi wa Rais Magufuli uwe wa kikatili ni pale alipoanza kuwa kiongozi mwenye wasiwasi. Wasiwasi kwamba kila mtu anamhujumu, wasiwasi kwamba kila mtu ana nia mbaya na serikali wake; na wako watu makatili hii ndio hali ambayo wakiiona toka kwa viongozi mioyo yao hufurahi sana, wengi wao katika mazingira mengine wangekuwa magaidi au majambazi, wana shetani ndani yao.
Historia inatufundisha dola yenye wasiswasi ni dola ambayo lazima izae ukatili na mauaji. Hii tuliona kwa Stalin huko Usovieti akiua watu zaidi ya milioni mbili, yaani serikali inaamua kuua tu, wala hakuna vita, ikafika mahali mpaka mwenyewe akahofia anaweza asiwe na nchi ya kuongoza. Hii tuliiona Kenya enzi za Utawala wa Daniel Arap Moi, na jumba lake la mateso la Nyayo House, sehemu ambayo kila aliyeingia basi ndio ulikua mwisho wake.
SOMA PIA: Serikali Ysema Matukio 21 Ya Watu Kutekwa na Kupotea Yamepatiwa Ufumbuzi
Siamini kama Rais Samia, ana uelekeo wa kutaka kufanya mambo mabaya ila pia ninaamini dola inaweza kuwa ovu kiasi kwamba ikaharibu taifa zima. Ni muhimu wanasiasa wakaelewa kuwa wakati wao wanaangalia 2025 maisha yetu yapo sasa, hatutaki kupotea, hatutaki kuuliwa, hatutaki kutekwa.
Sio wote ambao tupo katika familia zenu tuhakikishiwe kwamba watekaji wakiangalia majina yetu watasema huyu ni mtoto wa fulani, huyu ni kaka, mjomba, shangazi wa fulani. Na sisi tunataka kuwa salama kama watoto wenu, tunataka kuwa salama kama waume na wake zenu, tunataka kuwa salama kama marafiki zenu.
Lakini, mnadhani mnajenga taifa la namna gani? Sijui mnachokiwaza ila Watanzania tunastahili kuwa na uhakika wa kesho yetu na sio mtekaji mmoja kutueka kwenye ratiba ya kutufanya kuwa chakula cha jioni cha papa, simba au fisi.
Lakini najiuliza, katika mambo yote hayo watu wote mliopewa dhamana juu ya maisha yetu, ubinadamu wenu uko wapi? Kweli hakuna watu wema miongoni mwenu?
Nimeandika haya kwa matumaini kwamba labda tunaweza badili uelekeo wetu, lakini naelewa matumaini ni jambo la hatari, na sina namna nyingine.
Kwenu ndugu watekaji, imani yetu juu ya taifa letu ni kubwa, nchi yetu itavuka hapa. Ninajuwa kwa sasa inawezekana mmekaa mahali mkipata sharubati baridi, au bia moja mbili huku mkiangalia ni nani kati yetu mkamteke tena, yatafika mwisho haya. Niwaachie maneno ya Mwalimu Nyerere, naamini mkitoka katika kazi zenu za utekaji na kuharibu taifa letu manapata muda wa kujisomea:
“Juu ya uhuru wa watu hatuwezi kubishana, watu hawawezi kusema kwamba wana maendeleo na katika nchi yao hawawezi kutembea kwa uhuru wana ogopa, wana hofu, wanadhani asubuhi yeyote wakisikia mlangoni [mtu akigonga] kwa! Kwa! Kwa! anafikiri kaja mtu kuwapeleka kwenda kuwafunga, sasa nchi ya namna hiyo hauwezi kusema ina maendeleo nchi haina uhuru wa watu,” Mwalimu Julius Nyerere.
Tony Alfred K ni mchambuzi na mwandishi anayefanya kazi na The Chanzo. Unaweza kumpata kupitia anuani yake ya barua pepe ambayo ni tony@thechanzo.com au unaweza kumfuatilia Twitter kupita @tonyalfredk. Haya ni maoni binafsi ya mwandishi na si lazima yaakisi mtazamo wa The Chanzo. Ungependa kuchapisha katika safu hii? Wasiliana na mhariri wetu kupitia editor@thechanzo.com.
One Response
Nimependa mtiririko wa mwandishi. Hata mimi niliangukia katika mtego huo wa matumaini. Sikutegemea kabisa kama Sativa angekuwa anapitia hayo. Nilijulishwa tu kuwa haonekani, na kwa utaratibu wangu ambao nimeshindwa kuubadili, naweza kutokuwa katika mawasiliano hata wiki nzima kwa maamuzi tu ya “kupumua”.
Nimeelewa hatari hii. Sitarudia.
Mwisho niseme tu, hakuna marefu yasiyo na ncha; vilevile WAKATI UKUTA.