The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on April 20, 2024. Register Here

Search
Close this search box.

Tunawezaje Kuwafanya Watoto Wetu Wapende Kunywa Maji?

Maji hupoza mwili na husaidia kulinda joto la mwili, huzuia kuvimbiwa na maambukizi ya njia ya mkojo.

subscribe to our newsletter!

Sote tunajua kuwa maji ni muhimu kwa afya zetu na haswa kwa afya ya mtoto. Maji hupoza mwili na husaidia kulinda joto la mwili, huzuia kuvimbiwa na maambukizi ya njia ya mkojo.

Lakini, tunafanyaje pale ambapo mtoto hapendi kunywa maji? Leo, tujaribu kujadili njia wanazotumia wazazi wengine kuwapa watoto wao maji kama walivyonukuliwa na mtandao wa Baby Centre.

Maji yawepo muda wote, kama mzazi mmoja anavyoeleza hapa: “Kila wakati napohisi mwanangu ana kiu, mimi humpa maji. Mara nyingi atanijibu kuwa hana kiu, lakini ninamuomba walau kumnywesha matone matano. Mara nyingi mbinu hii humsaidia kunywa zaidi ya ninavyotaka. Mara tu anapoanza kunywa maji mtoto hugundua kumbe alikuwa na kiu, hivyo hunywa maji mengi zaidi ya yale matone matano.”

Hivyo, tujitahidi kuweka kikombe cha maji ya kunywa karibu na mahala mtoto anapopenda kucheza. Mahala anapoweza kuyafikia wakati wowote hivyo atashawishika kunywa maji apatapo kiu.

Mzazi mwingine alisema: “’Chezeni mkinywa maji. Watoto wengi hupenda kushindana na wazazi wao kufanya mambo kadha wa kadha. Fanya unywaji wa maji sehemu ya mashindano hayo. Unaweza kujaza glasi ya maji baada ya chakula na kumtaka mtoto kushindana nawe kumaliza glasi yake. Namna hii atakunywa maji pasi kujua lengo lako la kumjenga kupenda maji ya kunywa. Watoto, hasa wa mijini, unaweza kumwekea mrija katika glasi yake na kumruhusu kunywa maji kwa mrija. Haka ka-mchezo katamsaidia kujenga tabia ya kunywa maji. Unaweza pia kujaribu kukamua limao ama chungwa na kuongeza kidogo katika maji unayompatia mtoto.”

SOMA ZAIDI: Jinsi ya Kuwasaidia Watoto Kuepuka Vishawishi vya Makundi-Rika

“Tumia kikombe maalum,” mwingine alisema. “Wakati binti yangu alikuwa na umri wa miaka miwili alipenda sana umalkia. Hivyo, kuendana na matakwa yake tulimtafutia kikombe cha plastiki chenye mahadhi ya kimalkia-malkia na kumshawishi kukinywea ‘maji ya malkia.’ Mara zote alipenda mbwembwe hizi hivyo ilimwia vigumu kukataa kuyanywa ‘maji ya malkia.’ Zoezi hili bado linafanya kazi ingawa ameshakuwa mkubwa kiasi.”

Hivyo, tuwaruhusu watoto kuchagua kikombe maalumu cha kunywea maji iwapo inawezekana. Kadiri wanavyoona ‘umilikishwaji’ katika zoezi zima ndivyo mafanikio yetu katika unywaji wa maji utakavyoongezeka. Tuungane nao katika zoezi hili, yaani tuongoze kwa vitendo. Tukitoka kazini tuwashawishi kunywa maji pamoja na pia kila baada ya chakula.

Wape uhuru wao. Watoto wadogo mara tu wanapohisi ‘kujitegemea’ hutaka uhuru kufanya ‘watakavyo’ katika ulaji, uvaaji na hata unywaji. Mtoto anataka afanye mwenyewe. 

Tujitahidi kuwatafutia glasi, ama kikombe, anachoweza kunywa maji bila ya msaada pasi na madhara. Ila, tusiwaache kunywa maji katika glasi ya udongo iwapo bado hawawezi kuishika pasi ajali pekee yao.

Zoezi la kunywa maji kama mazoezi mengine katika malezi huhitaji subira. Malezi ya watoto kwa ujumla wake ni kazi ya masaa 24 kwa siku miaka yake yote hadi atakapokua mtu mzima. 

SOMA ZAIDI: Mambo Muhimu Wazazi Tunapaswa Kuwafundisha Vijana Wetu

Hivyo, tunatiana moyo kama wazazi, bahati mbaya huwa katika safari ya malezi tunajifunza kwa ‘mafunzo-kazini.’ Hakuna mahala katika ukuaji wetu na utafutaji elimu au pesa tuliandaliwa kimahususi kwa ajili ya kuingia katika biashara ya uzazi, hasa malezi ya watoto. 

Sote tupo darasani tukijifunza. Yataka moyo!
Makala hizi za malezi huandaliwa na C-Sema, shirika lisilo la kiserikali linalojikita katika kuendeleza na kulinda haki za watoto Tanzania. Kwa maoni na ushauri, wapigie kwenye simu namba 116, ambayo ni maalumu kwa huduma za mtoto. Huduma hii haitozi malipo toka mitandao yote nchini. Vilevile, unaweza kuwapata kupitia kurasa za Facebook: Sema Tanzania, X: @SemaTanzania, na kupitia tovuti yao www.sematanzania.org.

Digital Freedom and Innovation Day
The Chanzo is hosting Digital Freedom and Innovation Day on Saturday April 20, 2024 at Makumbusho ya Taifa.

Register to secure your spot

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *